ZANZIBAR: Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Afrika haiwezi kuendelea kubaki kuwa soko la teknolojia zinazozalishwa na mataifa mengine, bali inapaswa kujenga uwezo wa kuzalisha teknolojia na bunifu zake, kukuza vipaji na kujipambanua kuwa kitovu cha ushindani katika ubunifu na uwekezaji.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, Septemba 29, 2026, wakati akifungua Maonesho ya Teknolojia na Akili Unde (Tech and AI Expo Zanzibar 2026) katika Hoteli ya Golden Tulip Airport, Zanzibar, sambamba na uzinduzi wa Sera ya Kidijitali ya Zanzibar 2026 (Zanzibar Digital Policy 2026) inayolenga kutoa mwelekeo wa mageuzi ya mageuzi ya kidijitali Zanzibar.

Amesema mageuzi ya teknolojia yanatoa fursa kubwa kwa Afrika kukabiliana na changamoto za maendeleo, kuboresha huduma za umma, kupanua upatikanaji wa elimu na afya, kuongeza uzalishaji, kuimarisha biashara na kufungua fursa mpya za ajira.
Rais Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanza kuweka mazingira na miundombinu yatakayowezesha wananchi, wafanyabiashara na taasisi kutumia teknolojia kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Amesema Serikali inalenga kuunganisha kaya 100,000 na huduma za intaneti za uhakika kupitia mfumo wa Fibre-to-the-Home (FTTH) ndani ya miaka mitatu, sambamba na kuimarisha mawasiliano kupitia nyaya za chini ya bahari (Submarine Cable) na kuendeleza miundombinu ya vituo vya kuhifadhi na kuchakata taarifa (Data Centers).

Akizungumzia Akili Unde (Artificial Intelligence – AI), Rais Mwinyi amesema teknolojia hiyo ina uwezo mkubwa wa kuongeza tija katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, afya, elimu, utalii, huduma za Serikali na biashara.
Hata hivyo, amesema matumizi ya AI yanahitaji miundombinu imara, taarifa sahihi na za kuaminika, wataalamu wenye ujuzi, usimamizi wenye uwajibikaji pamoja na imani ya wananchi katika matumizi ya teknolojia hiyo.

Amesema Serikali inaandaa Mfumo Mkakati wa Akili Unde (AI Strategy Framework) utakaosaidia kuhakikisha matumizi ya teknolojia hiyo yanafanyika kwa usalama na kwa kuzingatia uwajibikaji katika uchumi na huduma za umma, huku ikilinda faragha, usalama na haki za msingi za wananchi.
Aidha, Rais Mwinyi amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuweka mfumo bora wa kisheria na kisera kwa kampuni changa, wabunifu na wawekezaji wa teknolojia, sambamba na kuimarisha ulinzi wa taarifa binafsi na uwajibikaji katika mazingira ya kidijitali.

Amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuimarisha ushirikiano katika miundombinu ya kidijitali, usalama wa mtandao, usimamizi wa taarifa, utafiti, ubunifu na uhamishaji wa teknolojia ili kuiwezesha Afrika kuwa na uwezo mkubwa wa kutatua changamoto zake.
Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga, amesema Serikali inalenga kujenga mazingira yatakayowawezesha vijana kutumia teknolojia na ubunifu kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali na kutengeneza bidhaa na huduma zenye uwezo wa kushindana katika masoko ya kimataifa.

Katika maonesho hayo, Rais Dkt. Mwinyi pia ameshuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) baina ya Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar na Huawei Technologies Tanzania Limited, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika sekta ya teknolojia.
Maonesho hayo yamewakutanisha wadau mbalimbali wa teknolojia, wakiwemo wataalamu wa Akili Unde, wawekezaji, watafiti, kampuni changa, washirika wa maendeleo na vijana wabunifu kutoka ndani na nje ya nchi, kwa lengo la kubadilishana maarifa, kuimarisha ushirikiano na kujadili nafasi ya teknolojia katika maendeleo ya Afrika.


