Madereva wagoma, abiria wakwama Moshi – HabariLeo

MOSHI: Baadhi ya madereva wa mabasi katika Stendi Kuu ya Mabasi Moshi, mkoani Kilimanjaro, wamegoma kutoa huduma za usafiri kwa saa kadhaa kupinga mfumo wa kukatwa pointi za leseni kwa makosa ya barabarani, wakidai kuwa utaratibu huo unawaongezea mzigo wa kiuchumi licha ya baadhi ya makosa hayo kutozwa faini.

Madereva hao pia wanaitaka Serikali kuweka wazi mgawanyo wa uwajibikaji kati yao na wamiliki wa magari, wakieleza kuwa baadhi ya makosa yanayosababisha kukatwa pointi yanahusiana na hali na vifaa vya magari ambavyo viko chini ya dhamana ya wamiliki.

Mgomo huo umesababisha baadhi ya safari kusitishwa na abiria waliokuwa tayari wamekata tiketi kukosa usafiri, hali iliyolazimu uongozi wa kituo kushirikiana na wadau wengine kutafuta usafiri mbadala.

Akizungumza kuhusu sababu za mgomo huo, dereva wa mabasi, Emmanuel Singine, amesema mfumo wa faini na kukatwa pointi unawaweka madereva katika mazingira magumu kiuchumi, hasa wale wenye majukumu ya kifamilia.

Singine amesema dereva anapokosea na kutozwa faini ya Sh30,000, bado hukatwa pointi, hali ambayo amesema inaongeza gharama kwa dereva ambaye tayari ana majukumu ya kugharamia familia na elimu ya watoto.

“Nina mke na watoto na nasomesha. Nakosea unanipa fine ya 30 elfu, halafu bado unanikata pointi. Nikikatwa pointi zikifika 15, natakiwa kurudi tena shule na kulipa ada. Kwa mtindo huu nitaweza kulipa pointi, fine na kulipa ada ikiwemo kusomesha watoto?” amehoji Singine.

Amesema madereva wanahitaji maelezo ya wazi kuhusu namna mfumo wa pointi unavyotekelezwa, huku akitaka uwajibikaji ugawanywe kati ya dereva na mmiliki wa gari kulingana na aina ya kosa.

Ametoa mfano wa makosa yanayohusu vifaa vya gari, kama matairi na vioo, akisema yanapaswa kuwajibishwa zaidi kwa mwenye gari, wakati makosa yanayotokana moja kwa moja na mwenendo wa dereva, kama kuzidisha abiria, yawajibishwe kwa dereva.

“Kama watatukata pointi kulingana na makosa tushirikiane. Kama ni vifaa kama matairi, kioo na kadhalika, alipishwe mwenye gari, lakini kama ni kuhusu kuzidisha abiria basi mimi kama dereva niwajibishwe,” amesema.

Kwa upande wake, Shadrack Kaaya, dereva wa kampuni ya Masalu, amesema malalamiko yao yanahusu namna sheria zinavyotekelezwa dhidi ya madereva, akidai kuwa baadhi ya makosa, yakiwemo ya kupita magari mengine (overtaking), yanaweza kusababisha kukatwa pointi.

Kaaya amesema hali hiyo inazidishwa na ukweli kwamba madereva wengi hawana mikataba ya ajira inayowalinda ipasavyo, hivyo ameiomba Serikali kuangalia upya mfumo huo na kuhakikisha majukumu yanagawanywa kwa kuzingatia aina ya kosa.

“Madereva wengi hawana mikataba. Serikali itusaidie kwa sababu hizi sheria zinambana dereva peke yake wakati mengine yanamhusu mwenye gari. Asilimia 99 dereva ndiye anabanwa na hizi sheria,” amesema Kaaya.

Akizungumzia athari za mgomo huo, Samuel Mlay, msimamizi wa Kituo cha Mabasi Moshi, amesema baadhi ya mabasi yaliyokuwa tayari yameuza tiketi yalishindwa kuondoka kutokana na kukosekana kwa madereva.

Mlay amesema uongozi wa kituo ulihusika kutafuta usafiri mbadala kwa abiria waliokwama ili kuwawezesha kuendelea na safari zao na kupunguza usumbufu uliotokana na hali hiyo.

Wakati huo huo, Afisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Mkoa wa Kilimanjaro, Paul Nyelo, alikuwa katika kituo hicho na kushirikiana na uongozi wa stendi kuhakikisha abiria waliokosa usafiri wanapata usafiri mbadala na kuendelea na safari zao.

Hata hivyo, Nyelo hakutaka kuzungumzia zaidi sababu za mgomo huo wala kutoa maelezo kuhusu hatua zinazochukuliwa na mamlaka kukabiliana na malalamiko ya madereva.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani (RTO), Nassoro Sisiwaya, ambaye pia alikuwepo katika kituo hicho, hakutoa maelezo kuhusu mgomo huo na hatua zinazochukuliwa.

Hadi wakati wa taarifa hii, baadhi ya mabasi yalikuwa yakiendelea na safari, huku mengine yakiwa yamesitisha huduma kutokana na mgomo huo.

Madereva hao wanataka mamlaka husika kuangalia upya utekelezaji wa mfumo wa faini na pointi za leseni, pamoja na kuweka utaratibu unaotambua wajibu wa dereva na mmiliki wa gari kulingana na aina ya kosa.