Na Matukio Daima Media, Morogoro
Hali ya usafiri katika Kituo Kikuu cha Mabasi Msamvu mkoani Morogoro leo ilikuwa tete, huku mabasi mengi yanayoanzia safari kituoni hapo yakishindwa kuanza safari na kusababisha abiria waliokuwa wakielekea mikoa mbalimbali nchini kusubiri kwa muda mrefu bila kujua hatma yao.
Baadhi ya abiria waliokuwa wamefika kituoni hapo tangu saa 12 kamili alfajiri waliendelea kusubiri, huku wengine wakilazimika kurejea nyumbani baada ya kukosa uhakika wa kuondoka.
Miongoni mwa waliokumbwa na hali hiyo ni Harold Jackson, Anold Munuo na Hemedi Michael waliokuwa wakielekea Arusha na Moshi ambao walilalamikia muda walioupoteza kituoni hapo.
Mwenyekiti wa Wasafirishaji Kituo Kikuu cha Mabasi Msamvu, Aziz Kapilima, akaishauri Serikali kukutana na madereva na kusikiliza malalamiko yao ili kupata ufumbuzi wa haraka.
Kapilima alisema kuendelea kwa mgomo huo kutaathiri abiria, wamiliki wa mabasi, madereva na Serikali kwa ujumla kiuchumi na kijamii.
Dereva mwingine ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema moja ya mambo yaliyowakwaza madereva ni kutoshirikishwa katika maamuzi yanayowahusu, huku akilalamikia faini, kufungiwa leseni na kupunguziwa pointi wanapokutwa na makosa barabarani.
Alisema hali hiyo inaweza kuathiri ajira zao na maisha ya familia zinazowategemea hasa pale wanapokuwa hawana Leseni za kufanya kazi tofauti na madereva wa Serikali walioajiriwa ambao hata wakipata Ajali wakaumia na wasifanye kazi watalipwa.
Katika hatua nyingine, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, ametembelea maeneo mbalimbali ya usafirishaji, ikiwemo Mikumi na Kituo cha Mabasi Msamvu, na kutoa onyo kwa watu watakaowabughudhi madereva pamoja na vyombo vya usafiri vilivyoamua kuendelea kutoa huduma.
Wakati huohuo, baadhi ya mabasi yalianza kutoa huduma kwa uchache majira ya mchana tofauti na awali ambapo yale yaliyotokea safari za masafa marefu ndio yaliyooendelea kupita kituoni hapo.
Mwisho


