
Doha, Qatar – Waziri Mkuu wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameipongeza Serikali ya Qatar kwa matumizi makubwa ya teknolojia na nishati safi katika kuimarisha huduma za usafiri wa umma nchini humo.
Dkt. Mwigulu alitoa pongezi hizo Jumamosi, Septemba 26, 2026, jijini Doha, baada ya kupokea taarifa kuhusu uendeshaji wa kampuni ya usafirishaji ya MOWASALAT kutoka kwa Waziri wa Uchukuzi wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdullah bin Mohammed Al Thani.
Waziri Mkuu yupo nchini Qatar kwa ziara ya kikazi ya siku tatu, ambapo amesema Tanzania inaweza kujifunza kutokana na mfumo wa usafiri wa umma unaotumiwa nchini humo, hususan katika matumizi ya teknolojia na nishati safi.
Dkt. Mwigulu amesema moja ya changamoto zinazoikabili Tanzania ni msongamano wa magari, hivyo uzoefu wa Qatar unaweza kusaidia katika kutafuta njia za kuboresha usafiri wa umma na kupunguza msongamano barabarani.

“Nyumbani tunalo tatizo la msongamano wa magari na kupitia teknolojia mnazotumia, Tanzania inaweza kujifunza mbinu mlizotumia ili nasi tuweze kukabiliana nalo,” amesema Dkt. Mwigulu.
Dkt. Mwigulu pia amepongeza hatua ya Qatar kutumia nishati safi katika sehemu kubwa ya magari yake ya usafiri wa umma.
Amesema matumizi hayo yanaendana na juhudi za Tanzania katika kukuza nishati safi, akimtaja Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kama kinara wa kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo barani Afrika.

Amesema uzoefu huo unaweza kuwa na umuhimu zaidi kwa Tanzania kutokana na maandalizi ya kuwa mwenyeji wa AFCON 2027.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kinara wa nishati safi barani Afrika, na hii ni hatua nzuri kwetu. Tunatarajia kuwa wenyeji wa AFCON 2027, kwa hiyo itatufaa sana,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameishukuru kampuni hiyo kwa kutoa ajira kwa Watanzania 722 katika nafasi mbalimbali.
Kwa mujibu wa Dkt. Mwigulu, ajira hizo zinatoa fursa kwa vijana wa Tanzania kupata uzoefu, kukuza ujuzi na kujifunza teknolojia zinazotumika katika sekta ya usafirishaji.

“Ni fursa kwa vijana wetu kukuza ujuzi na kujifunza teknolojia mbalimbali,” amesema.
Akitoa taarifa kuhusu shughuli za kampuni hiyo, Waziri wa Uchukuzi wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdullah bin Mohammed Al Thani, amesema MOWASALAT inatoa huduma mbalimbali za usafiri wa abiria.
Huduma hizo zinahusisha mabasi, teksi, usafiri wa wanafunzi pamoja na usafiri kwa ajili ya matukio binafsi, kitaifa na kimataifa.

Amesema katika mwaka 2025, kampuni hiyo ilitoa huduma kwa takribani watu milioni 42, huku ikiwa na magari 1,200 na njia 128 za usafiri.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, takribani asilimia 70 ya magari ya kampuni yanatumia umeme, hatua inayosaidia kuongeza matumizi ya nishati safi katika usafiri wa umma.
Aidha, amesema ubora na uhakika wa huduma zinazotolewa na kampuni hiyo umechangia kupunguza matumizi ya magari binafsi barabarani, ambapo takribani magari 12,363 yameondolewa kwenye matumizi ya barabara kutokana na wananchi kutumia huduma za usafiri wa umma.
Waziri huyo pia ameeleza kuwa MOWASALAT inatumia teknolojia katika kufuatilia na kukagua hali ya magari yake.
Amesema magari yamewekewa mfumo wa kielektroniki unaowezesha kubaini changamoto mapema, badala ya kusubiri gari lifikishwe kwa mafundi baada ya kupata hitilafu.
Mfumo huo, amesema, unasaidia kampuni kutambua changamoto kwa haraka na kuchukua hatua stahiki ili kuhakikisha huduma za usafiri zinaendelea kuwa salama na zenye uhakika.

Ziara ya Dkt. Mwigulu nchini Qatar inaendelea huku Tanzania ikitarajia kutumia fursa hiyo kujifunza uzoefu wa nchi hiyo katika maeneo mbalimbali, ikiwemo usafiri wa umma, matumizi ya teknolojia na nishati safi.
