Dkt. Mwigulu Awataka Watanzania Qatar Kutunza Jina la Tanzania

Global Publishers
September 28, 2026
54 views
0 Comments

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania wanaofanya kazi nje ya nchi watunze uaminifu na wafanye kazi kwa bidii ili wasiliharibu jina zuri la Tanzania.

Alitoa kauli hiyo Jumamosi, Septemba 26, 2026 wakati akizungumza na madareva wa Kitanzania zaidi ya 500 walioajiriwa na kampuni ya usafirishaji ya MOWASALAT kwenye kikao kifupi kilichofanyika kwenye ofisi za kampuni hiyo, zilizoko Lusail Depot nje kidogo ya Jiji la Doha, Qatar.

Dkt. Mwigulu ambaye yuko nchini Qatar kwa ziara ya siku tatu kwa mwaliko wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Abdulrahman bin Jassim Al Thani alisema: “Fanyeni kazi kwa bidii ili muwe mabalozi kwa wenzenu walioko nyumbani. Kuweni waaminifu, tunzeni jina la nchi yetu ili wenzenu waweze kupata fursa za ajira katika nchi mbalimbali. Mkiaminiwa inakuwa rahisi kufungua milango kwa wenzenu.”

Waziri Mkuu alitumia fursa kuwapa picha halisi ya maendelea yaliyofikiwa nchini Tanzania katika sekta za elimu, afya, maji, miundombinu na akawasihi waendelee kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa amedhamiria kuwahudumia Watanzania.

Akijibu hoja za madereva hao kuhusu kutotambuliwa kwa vyeti vyao pindi wanaporudi nyumbani, Dkt. Mwigulu Nchemba alimwagiza Waziri wa Mambo ya Ndani afuatilie suala hilo kwa kushirikiana na wizara husika.

“Fuatilia uwezekano wa kulink vyeti vyao wanapohitimu mafunzo yao. Wale wanaopata distinction na wanahitajika nyumbani, tuwe na database yao ili watambuliwe kwa urahisi.

Utambuzi wa elimu inayopatikana hapa unaweza kutambuliwa endapo mtu ameamua kurejea nyumbani. Kama tatizo ni sheria, basi iangalieni hiyo sheria. Mheshimiwa Rais alishasema sheria isiwe kikwazo cha Watanzania kujiletea ustawi,” alisema na kuamsha shangwe kubwa moingoni mwa madereva hao.

Kuhusu usumbufu wa kudaiwa vibali vya kazi na ushuru wa vyakula wanavyotaka kuondoka navyo, ambao wanaupata kwenye uwanja wa ndege wa Dar es Salaam wanapokuwa wanarejea kutoka likizo, Waziri Mkuu aliwahakikishia kwamba litafanyiwa kazi mara moja.