WAISLAM KIGOMA WAJITOKEZA KUPIMA AFYA, KUCHAGIA DAMU

 

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

WAUMINI wa kiislam Zaidi ya 200 wamejitokeza kupima afya huku uniti 61 za damu zikikusanywa kutoka kwa waumini wa kiislam waliohudhuria Hauli ya kumbukumbu ya miaka 70 ya kifo cha Mwanazuoni na Mwalim Mkubwa wa dini mkoani Kigoma Marehemu Shekhe Mohamed Ibrahim Kabeka iliyofanyika Ujiji mjini Kigoma.

Kiongozi wa timu ya Madaktari waliokuwa wakisimamia zoezi hilo, Shaban Magorwa alisema kuwa zoezi hilo liliendeshwa kwa siku mbili katika msikiti wa Kabondo Ujiji Mjini Kigoma na kwamba zoezi hilo limekuwa na mafanikio makubwa.

Magorwa alisema kuwa mikusanyiko ya kidini na shughuli nyingine za kijamii ni vizuri zikafanyika na kufanyika kwa matukio hayo ya uchangiaji damu na kupima afya hasa kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo Presha na kisukari.

Akizungumza kufanyika kwa maadhimisho hayo kwa niaba ya Familia ya Shekhe Ibrahim kabeke, Shekhe wa mkoa Mwanza, Hassan Kabeke alisema kuwa maadhimisho hayo (Hauli) imefanyika miaka yote tangu kifo cha Mwanzuoni huyo na kwamba hilo linafanyika kuenzi mchango wake mkubwa katika mafundisho ya dini ambayo yametoa wahadhiri, walimu wa dini na Mashekhe mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Pamoja na kupima afya, kuchangia damu, dua na shughuli mbalimbali za kidini pia Shekhe Kabeke alisema kuwa kumefanyika makongamano ya kufundisha elimu ya ujasiliamali na masuala ya uchumi na biashara sambamba na kufundisha elimu ya kujikinga na magonjwa ikiwemo magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Akitoa mada ya elimu ya fedha na ujasiliamali katika maadhimisho hayo Imam wa Masjidi Maamur Upanga jijini Dar es Salaam na Mjumbe wa baraza la Ulamaa Taifa la Baraza kuu la Waisalm Tanzania (BAKWATA), Shekhe Issa Othman amewataka waumin wa dini ya kiislam nchini kujifunza masuala ya elimu ya fedha na biashara na kuanzisha shughuli za ujasiliamali kwani zina mchango mkubwa katika kuendesha maisha yao ya kila siku na kuwaondoa kwenye kashfa ya kuwa ombaomba.

Shekhe Othman alisema kuwa mkoa Kigoma umepata bahati ya kuteuliwa na serikali kuwa mkoa wa kimkakati wa masuala ya uchumi na biashara hivyo waumin wa kiislam wanapaswa kutumia fursa hiyo kuchukua maeneo kuanzisha shughuli za kiuchumi ambazo kwa sasa zinatija kubwa mkoani humo.