BRELA YATOA WITO KWA WAFANYABIASHARA GEITA KUSAJILI BIASHARA KUEPUKA MIGOGORO YA MAJINA

 

Na Matukio Daima  Geita

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umewataka wafanyabiashara na wachimbaji madini mkoani Geita kutumia fursa ya maonesho ya madini kutembelea banda la BRELA na kupata elimu kuhusu umuhimu wa kusajili biashara na kampuni zao.

Wito huo umetolewa wakati BRELA ikishiriki katika Maonesho ya Tisa ya Madini mkoani Geita, ambapo wananchi wanapata fursa ya kujifunza kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo, ikiwemo usajili wa majina ya biashara na kampuni.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Geita, Afisa kutoka  BRELA Athumani Makuka  amewataka wafanyabiashara, wachimbaji na wajasiriamali kuhakikisha wanasajili majina ya biashara zao na kampuni ili kuepuka changamoto na migogoro inayoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya jina moja la biashara na watu tofauti.

Amesema usajili wa jina la biashara ni hatua muhimu kwa mfanyabiashara, kwani humsaidia kutambulika kisheria na kulinda jina alilolijenga kupitia shughuli zake za biashara.

Kwa mujibu wa BRELA, baadhi ya wafanyabiashara huanza kutumia majina ya biashara bila kuyasajili, na baadaye mfanyabiashara mwingine anaweza kusajili jina hilo na kuanza kulitumia kisheria, jambo ambalo linaweza kusababisha migogoro na changamoto kwa mwanzilishi wa biashara hiyo.

“Ni muhimu mfanyabiashara kuhakikisha jina la biashara limesajiliwa mapema ili kulinda utambulisho wa biashara yake na kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza baadaye,” amesisitiza.

Aidha, BRELA imesema inatumia maonesho hayo kuwaelimisha wananchi kuhusu huduma zake pamoja na kuwafikishia huduma karibu na maeneo yao.

Katika maonesho hayo, BRELA pia inatoa baadhi ya huduma bila malipo, ikiwemo huduma zinazohusiana na usajili wa biashara, leseni pamoja na huduma kwa viwanda vidogo na vya kati.

BRELA imewahimiza wananchi wanaoshiriki maonesho hayo, hususan wafanyabiashara na wachimbaji madini, kutumia fursa hiyo kutembelea banda la taasisi hiyo na kupata elimu pamoja na ufafanuzi kuhusu taratibu za usajili wa biashara na kampuni.

Maonesho hayo yanaendelea mkoani Geita yakilenga, miongoni mwa mambo mengine, kuwaunganisha wadau wa sekta ya madini, wafanyabiashara na taasisi mbalimbali za serikali ili kutoa elimu na huduma zinazohusiana na shughuli za kiuchumi.