IRINGA: Baadhi ya wananchi mkoani Iringa wameeleza uelewa wao kuhusu mvua za El Niño na madhara yake, huku wakisema mvua hizo zinaweza kusababisha mafuriko, kuharibu mazao, madaraja na miundombinu mingine endapo tahadhari hazitachukuliwa mapema.
Maoni hayo yametolewa na wananchi wa maeneo mbalimbali waliohojiwa na Matukio Daima Media, akiwemo Simon Msele, Marvin Fabian, Yohana Mhinga na Akolinari Kiungo.
Wananchi hao wameeleza namna wanavyozielewa mvua hizo pamoja na hatua wanazochukua au wanazopaswa kuchukua ili kukabiliana na madhara yanayoweza kujitokeza.
“Mvua za El Niño ni mvua kubwa zinazozidi kiwango cha mvua za kawaida ambazo tumekuwa tukizipata,” alisema Simon Msele, akieleza uelewa wake kuhusu mvua hizo.
Msele alisema moja ya hatua muhimu za kukabiliana na mvua hizo ni kuhakikisha mazingira yanakuwa safi, hususan kwa kusafisha mitaro iliyoziba ili kuruhusu maji kupita vizuri na kupunguza uwezekano wa mafuriko.
Alisema wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi, hasa mabondeni, wanapaswa kuchukua tahadhari mapema kwa kuhama kwenda maeneo salama ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na mafuriko.
Kwa upande wake, Marvin Fabian alisema anaelewa mvua za El Niño kuwa ni mvua zinazoweza kunyesha kwa muda mrefu bila kukatika, tofauti na mvua za kawaida.
Alitolea mfano mvua zinazoweza kuanza kunyesha asubuhi na kuendelea hadi jioni au usiku.
“Kwa kweli, sijajipanga kukabiliana nazo. Labda tutapokea tu hali itakapokuja,” alisema Marvin.
Wananchi wengine walisisitiza umuhimu wa kuhifadhi chakula, kusafisha mifereji na kujiweka katika maeneo salama ikiwa ni sehemu ya tahadhari dhidi ya madhara yanayoweza kujitokeza.
Akolinari Kiungo, mkazi wa Ilala, alisema wananchi katika eneo lake wameanza kuchukua tahadhari kwa kuandaa mifereji ya kupitisha maji na kuhifadhi chakula ndani ya nyumba.
Alisema hatua hizo ni muhimu kwa kuwa muda ambao mvua zinaweza kuendelea kunyesha hauwezi kujulikana ila mvua zikianza watajihami na kujilinda zaidi.
Tayari Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua za Vuli (Oktoba – Desemba) 2026, ikitoa angalizo la msimu huo kuathiriwa kwa kiwango kikubwa na hali ya El Niño yenye nguvu kubwa iliyotokana na joto la bahari kuwa Juu ya Wastani katika Bahari ya Pasifiki, hali itakayochagiza ongezeko la Mvua za Vuli 2026 kuwa za Juu ya Wastani hadi Wastani katika maeneo mengi ya Ukanda wa Pwani ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Ukanda wa Ziwa Viktoria na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.

