NA HADIJA OMARY
LINDI
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeanzisha mpango wa bima ya afya kupitia vikundi, unaolenga kuwawezesha wananchi kupata huduma za matibabu kwa kuchangia shilingi elfu 60 kwa mwaka kwa kila mwanachama. Akizungumza kuhusu mpango huo,
Meneja wa Bima ya Afya wa NHIF Mkoa wa Lindi Radhia Makono amesema mpango huo unalenga kuongeza wigo wa wananchi wanaonufaika na bima ya afya, ambapo mwanachama anatakiwa kuwa sehemu ya kikundi chenye wanachama wasiopungua 10, kiwe rasmi au kisicho rasmi mradi kitimize masharti.
Meneja huyo amesema kila mwanachama atatakiwa kuchangia shilingi elfu 60 kwa mwaka, na baada ya kukamilisha taratibu za uanachama ataweza kupata huduma za afya katika vituo na hospitali zilizosajiliwa na NHIF kwa kufuata mfumo wa rufaa kuanzia ngazi ya zahanati, kituo cha afya, hospitali ya wilaya na hatimaye hospitali ya mkoa pale huduma inayohitajika inapokosekana ngazi ya chini.
Amesema mpango huo ni fursa kwa wananchi, hususan wanaojishughulisha na shughuli za kiuchumi kupitia vikundi, kuwa na ulinzi dhidi ya gharama za matibabu ambazo wakati mwingine huwa mzigo kwa mtu mmoja au familia, hivyo amewataka wananchi kuunda au kujiunga na vikundi na kutumia fursa hiyo.
Baadhi ya wananchi mkoani Lindi wamepongeza kuanzishwa kwa mpango huo wakisema kiwango cha shilingi elfu 60 kwa mwaka kinawapa nafasi watu wengi wakiwemo wafanyabiashara wadogo, wakulima na wajasiriamali kumudu gharama za bima na kinawapa matumaini ya kupata matibabu bila kulazimika kutafuta fedha nyingi pindi wanapougua.
Hata hivyo, wananchi hao wameiomba Serikali na NHIF kuhakikisha huduma zinapatikana kwa ufanisi katika vituo vilivyosajiliwa ikiwemo upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, na kuwataka viongozi kuendelea kutoa elimu kuhusu namna ya kuunda vikundi, kujiandikisha na kutumia huduma kwa mfumo wa rufaa ili wananchi wengi waelewe manufaa ya mpango huo.

