Na Matukio Daima Media, Kilosa
VURUGU zinazohusishwa na mgogoro kati ya wakulima na wafugaji wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro, zimesababisha vifo vya watu wawili katika matukio tofauti, kujeruhiwa kwa askari watatu na kuharibiwa kwa mali za Jeshi la Polisi.
Taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro inaeleza kuwa tukio linaanzia Septemba 23, 2026, saa 7 mchana katika Mashamba ya Bondeni, Kitongoji cha Legeza Mwendo, Kijiji na Kata ya Tindiga, Tarafa ya Masanze, ambako Festo Selias Chaula maarufu kwa jina la Walter Mkulima alijeruhiwa vibaya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro ACP Andrew Kantimbo akasema kuwa Festo alikatwa kichwani kwa kitu chenye makali na kupigwa kwa vitu butu sehemu mbalimbali za mwili wake na kupata majeraha makubwa yanayosababisha kifo chake katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa wakati akiendelea kupatiwa matibabu.
Baada ya tukio hilo, Polisi lilifanya ufuatiliaji na kuwakamata Seletwi Samiji Mdamanya na Paulo Lukas Sumai, likiwatuhumu kuhusika na mauaji hayo.
Wawili hao wanaelezwa kuwa ni wafugaji na wakazi wa Kijiji cha Malangali, Kata ya Tindiga.
Hata hivyo, wakati askari wakiwa wanawapeleka watuhumiwa Kituo cha Polisi Kilosa, kundi la watu linalodaiwa kuwa wakulima na kukadiriwa kufikia 200 lilidaiwa kufunga barabara na kuanza kuwashambulia askari waliokuwa wamewabeba watuhumiwa hao.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kantimbo, kundi hilo lilikuwa na silaha mbalimbali za jadi likilenga kuwadhuru watuhumiwa hao jamii ya wafugaji.
Askari Polisi ikadaiwa walitumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi hao waliokuwa na visu, mapanga, mishale, mikuki, marungu na mawe.
Baada ya kundi hilo kutawanyika, Polisi walifanya ukaguzi na kumkuta mmoja wa wananchi, Kelvin Mhagama, mkulima na mkazi wa Kichangani, akiwa amejeruhiwa kwa kitu chenye makali sehemu mbalimbali za mwili wake.
Majeruhi huyo alipelekwa hospitali ya wilaya ya Kilosa, lakini alifariki Dunia akiwa anapatiwa matibabu.
Kamanda huyo wa Polisi amethibitisha licha ya kifo hicho, katika vurugu hizo, askari watatu walipata madhara ikiwemo kujeruhiwa maeneo mbalimbali ya mwili baada ya kushambuliwa kwa silaha za jadi na wanaendelea na matibabu.
Vurugu hizo pia zimesababisha pikipiki ya Polisi yenye namba PT 3131 aina ya SANLG kuteketea kwa moto, huku gari la Polisi PT 5877 Toyota Hilux likiharibiwa baada ya kupigwa kwa mawe.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limewataka wakulima, wafugaji na wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na kutumia njia rasmi za kisheria katika kushughulikia migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Polisi pia wanaendelea na msako wa kuwakamata wote waliohusika na vurugu hizo na kujichukulia sheria mkononi katika tukio hilo.

