NG’OMBE WAINGIA MIWA MTIBWA, WALINZI WAWILI WASHAMBULIWA

 

Na Matukio Daima, Mvomero.

Kundi la ng’ombe linalodaiwa kuingizwa katika mashamba ya miwa ya Kiwanda cha Sukari Mtibwa, Mvomero, limeibua vurugu baada ya walinzi wawili wa kiwanda hicho kushambuliwa na kujeruhiwa wakati wakijaribu kuwaondoa mifugo hiyo katika mashamba.

Tukio hilo limetokea Septemba 23, 2026 majira ya saa sita mchana katika eneo la D6, ndani ya mashamba ya miwa ya Kiwanda cha Sukari Mtibwa, Kata ya Mtibwa, Tarafa ya Turiani, Wilaya ya Mvomero.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, amesema walinzi hao walifanikiwa kulikata kundi la ng’ombe na kuanza kuwaswaga kuelekea Kambi ya Dumila One inayomilikiwa na kiwanda hicho kwa ajili ya utambuzi na hatua zaidi.

Hata hivyo, amesema zoezi hilo lilikumbana na upinzani kutoka kwa wafugaji waliodaiwa kuzuia walinzi na kuanza kuwashambulia kwa visu aina ya sime, marungu na fimbo.

Mashambulizi hayo yalisababisha walinzi Sayuni Ndika Nemes (25) na Sanula Masaga Msabila (36) kujeruhiwa. Wote ni walinzi wa Kiwanda cha Sukari Mtibwa.

Katika tukio hilo.

Jeshi la Polisi limewakamata Sisone Lugaso Ndabali (20), Taturo Tetetea Shangalima (28) na Likua Kaika Ndikila (21), wote wakazi wa Kijiji cha Kambala, Kata ya Mkindo, Mvomero.

Polisi Mkoa wa Morogoro limewataka wafugaji kuacha kuingiza mifugo katika mashamba ya wakulima na kuacha kujichukulia sheria mkononi, likisisitiza matumizi ya taratibu na sheria katika kudai haki

Mwisho