Global Publishers
September 24, 2026
0 views
0 Comments

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amemjibu Rais wa Marekani, Donald Trump, kufuatia kauli za Trump kuhusu Iran, akisisitiza kuwa Tehran haitasalimu amri wala kukubali kushinikizwa kupitia vitisho.
Katika hotuba yake, Pezeshkian alisema Iran iko tayari kwa mazungumzo na diplomasia, lakini haitakubali mazungumzo yanayoambatana na vitisho au shinikizo “Hatutainamisha kichwa wala kupiga goti.”
Pezeshkian pia alisisitiza kuwa shinikizo, vikwazo na vitisho havitabadilisha msimamo wa Iran. Alisema Iran iko tayari kushirikiana na mataifa mengine, lakini mazungumzo yanapaswa kufanyika bila kutumia lugha ya nguvu.
Kauli hiyo ilikuja siku moja baada ya Trump kuhutubia Mkutano Mkuu wa UN na kutoa kauli kali kuhusu Iran, huku akieleza kuwa Marekani ilikuwa ikikabiliwa na chaguo kati ya diplomasia na hatua kali zaidi dhidi ya Tehran.
Katika hotuba yake, Pezeshkian pia alitetea haki ya Iran ya kutumia teknolojia ya nyuklia kwa madhumuni ya amani, huku akisema nchi yake haitafuti silaha za nyuklia.
Wakati Pezeshkian akianza kuhutubia, wajumbe wa Marekani waliondoka ukumbini. Tukio hilo lilitokea katika kipindi ambacho mvutano kati ya Washington na Tehran umeendelea kuwa mkubwa, huku pande hizo zikijadili uwezekano wa kurejea kwenye diplomasia.
NA TEREZA MUGA
