JALSA YA 55 AHMADIYYA KUFANYIKA DAR SEPTEMBA 25

 

Na Matukio DaimaMedia 

Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya Tanzania inatarajia kufanya Mkutano Mkuu wa mwaka (Jalsa Salana) wa 55, Septemba 25 hadi 27, 2026 katika eneo la Kitonga, Kata ya Msongola, Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam.

Zaidi ya washiriki 5,500 kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo wenye kaulimbiu “Taqwa (Uchamungu) Ndiyo Msingi wa Kila Wema.”

Akizungumza na waandishi wa habari, Amiri na Mbashiri Mkuu wa Jumuiya hiyo, Sheikh Khawaja Muzaffar Ahmad, amesema Jalsa hiyo inalenga kuwaimarisha waumini kiroho kwa kuongeza hofu ya Mwenyezi Mungu, uchamungu, huruma na upendo, huku wakijiepusha na mambo mabaya.

Amesema mkutano huo pia utajadili changamoto zinazoikabili dunia, ikiwemo migogoro na vita, huku waumini wakipata fursa ya kushiriki ibada, mihadhara na mafundisho ya dini, pamoja na Sala ya usiku (Tahajjud).

Aidha, amesema waumini wamehimizwa kushiriki shughuli za kijamii, ikiwemo kuwasaidia wenye mahitaji na kuchangia damu kwa ajili ya wagonjwa, huku Jumuiya hiyo ikisema ina uwepo katika nchi 212 duniani.

Kwa upande wake, Naibu Amir wa Ahmadiyya Muslim Jamaat Tanzania, Abdurahman Mohamed Ame, amesema maadili ni msingi muhimu wa maisha ya mwanadamu na Uislamu unasisitiza kuishi kwa maadili mema katika kila hatua ya maisha.

Amesema mafundisho ya Uislamu yanamtaka mtu kusema ukweli, kuheshimu haki za wengine na kutambua kuwa katika kudai haki zake anapaswa pia kutekeleza wajibu wake bila kuvunja haki za wengine.

“Ni kweli kudai haki zetu, lakini tukumbuke wajibu wetu na tuhakikishe kwamba wakati tunadai haki, tusije tukateleza, tukavunja haki au wajibu wetu, au tukavunja haki za wengine kwa kisingizio cha kudai haki zetu,” amesema.

Ameongeza kuwa maadili mema katika familia na jamii ni msingi wa amani, akisema dunia ikiheshimu haki za wengine na kuzingatia maadili, migogoro na matatizo yanaweza kupungua.