Waziri Mkuu Ahimiza Nchi Za Afrika Ziongeze Mapambano Dhidi Ya Sotoka

Global Publishers
September 21, 2026
0 views
0 Comments

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amezitaka nchi za Afrika na washirika wa kimataifa ziweke kipaumbele kwenye ajenda ya kutokomeza ugonjwa wa sotoka kwa mbuzi na kondoo (Peste des Petits Ruminants-PPR) kwa kuimarisha misaada ya kifedha na ya kiufundi.

“Mpango wa kutokomeza PPR si uwekezaji katika afya ya mifugo pekee, bali pia ni uwekezaji katika usalama wa chakula, kupunguza umaskini, kukuza biashara ya mifugo na kuimarisha ustahimilivu wa kiuchumi kwa wananchi. Tunatakiwa kuhakikisha ajenda hii inaendelea kupewa kipaumbele katika ngazi za kitaifa, kikanda na kimataifa ili kufikia lengo hili,” amesema.

Ametoa wito huo leo (Jumatatu, Septemba 21, 2026) wakati akitoa hotuba kuu kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi wa mkutano wa siku tatu wa Kimataifa wa Kujadili Afya Moja na Mifumo ya Chakula na Kilimo ulioanza leo katika Makao Makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), jijini Roma, Italia.

Akielezea mafanikio ya Tanzania katika kutokomeza ugonjwa wa sotoka, Waziri Mkuu amesema Serikali ililifanya suala hilo kuwa jambo kitaifa na inaendelea kutetea jitihada za kutokomeza ugonjwa huo barani Afrika.

“PPR si tu tatizo la afya ya wanyama. Kwa mamilioni ya kaya za wafugaji, hasa zile zinazotegemea kondoo na mbuzi, ni tishio kwa usalama wa chakula, mapato ya kaya, biashara na maisha,” amesema.

Katika mwaka wa fedha 2025/2026, Dkt. Mwigulu amesema Tanzania ilichanja kondoo na mbuzi milioni 16.8 dhidi ya sotoka na ilifanikiwa kufikia sehemu kubwa ya wanyama 17.2 waliolengwa kupata chanjo katika maeneo hatarishi.

“Kwa mwaka 2026/2027, zaidi ya sh. bilioni 30.8 (takriban dola milioni 11.6) zimetengwa kuendeleza awamu ya pili ya kampeni. Uzoefu wetu umetupa somo rahisi kwamba sotoka haiwezi kuondolewa kwa chanjo pekee bali kunahitajika jitihada zaidi. Inahitaji uchunguzi, utambuzi na ufuatiliaji wa wanyama, huduma sahihi kwa mifugo, ushirikiano baina ya nchi na nchi, na ufadhili endelevu.”