SERIKALI IMEENDELEA KUCHUKUA ATUA ZA KUIMARISHA SEKTA YA ELIMU

Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha sekta ya elimu kwa kuongeza miaka ya elimu ya lazima, kupanua fursa za elimu ya sekondari na kuimarisha mafunzo ya ufundi ili kuwapa vijana uwezo wa kushiriki kikamilifu katika soko la ajira.  

Akizungumza Septemba 02, 2026 jijini Dodoma na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema maandalizi ya utekelezaji wa miaka 10 ya elimu ya lazima kuanzia mwaka 2028 yanaendelea, hatua itakayohitaji miundombinu, walimu na nafasi za kutosha katika shule za sekondari.  

Prof. Mkenda amebainisha kuwa mpango huo utasababisha ongezeko kubwa la wanafunzi watakaoingia sekondari, hivyo Serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha wanafunzi wote wanaostahili wanapata nafasi ya kuendelea na masomo.  

Aidha, ameongeza kuwa  Serikali inaendelea kuimarisha mfumo wa elimu wenye mikondo ya elimu ya jumla na elimu ya amali, ili wanafunzi wapate maarifa na stadi zinazowawezesha kuajirika au kujiajiri.  

Katika mazungumzo hayo, Prof. Mkenda ameeleza kuwa Serikali inajenga vyuo vya ufundi katika maeneo mbalimbali na kuimarisha mafunzo ya ufundi ili kukidhi mahitaji ya vijana na uchumi wa Taifa.  

Prof. Mkenda ameongeza kuwa Serikali inawekeza katika masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati pamoja na teknolojia mpya kama akili bandia (AI), ujifunzaji wa mashine na usalama wa mtandao, ili kuandaa wataalamu wa kisasa.  

Amesisitiza  umuhimu wa ushiriki wa sekta binafsi katika kupanua fursa za elimu, hususan katika ujenzi wa miundombinu na utoaji wa elimu ya amali.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Carolyne Nombo, amesema kuwa Serikali inatazama uwezekano wa kuboresha vivutio vya kisera vitakavyoongeza uwekezaji wa sekta binafsi katika elimu.  

Naye Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Mhe. Marianne Young, amepongeza juhudi za Tanzania na kuahidi kuendeleza ushirikiano katika elimu na na mafunzo ya  ufundi, ikiwemo kuunganisha taasisi za Tanzania na vyuo vikuu vya Uingereza katika maeneo ya teknolojia ya kisasa na mazingira.