Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limeimarisha ulinzi na usalama katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mwanza kuelekea sherehe ya harusi ya Isaya Yunge na Charlene Ruto inayotarajiwa kufanyika leo, Novemba 6, 2026, katika Hoteli ya Malaika Beach Resort.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafungwa, amesema jeshi hilo limeweka mikakati madhubuti ya kiusalama kutokana na umuhimu wa tukio hilo litakalohudhuriwa na viongozi wa kitaifa na kimataifa pamoja na wageni kutoka ndani na nje ya nchi.

Amesema hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuimarisha doria katika maeneo ya nchi kavu, hoteli zitakazotumiwa na wageni pamoja na doria za boti katika Ziwa Victoria na maeneo mengine yanayozunguka jiji hilo.
Kwa mujibu wa Kamanda Mutafungwa, hatua hizo zinalenga kuhakikisha sherehe hiyo inafanyika katika mazingira ya amani, utulivu na usalama, huku watu na mali zao wakiendelea kuwa salama.

Aidha, amewatahadharisha watumiaji wa barabara kuhusu ongezeko la magari na matumizi makubwa ya barabara mbalimbali za jiji hilo, hususan Barabara ya Makongoro, barabara inayounganisha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwanza na katikati ya jiji, pamoja na njia zinazoelekea Malaika Beach Resort.
Barabara nyingine zilizotajwa ni Barabara ya Nyerere kuelekea Kisesa, ambapo amewataka madereva na wananchi kufuata sheria za usalama barabarani na kutii maelekezo yatakayotolewa na askari wa usalama barabarani ili kupunguza msongamano na kuhakikisha safari zinaendelea kwa usalama.

Vilevile, Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuendelea kudumisha amani na utulivu kwa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola, ikiwemo kutoa taarifa mapema kuhusu viashiria vyovyote vinavyoweza kuhatarisha usalama wa watu na mali zao.
Uimarishaji huo wa ulinzi unafanyika huku Jiji la Mwanza likijiandaa kupokea wageni mbalimbali wanaotarajiwa kuhudhuria sherehe hiyo ya harusi katika Hoteli ya Malaika Beach Resort.
