WANANCHI BUKOBA WAFUNGULIWA HUDUMA JANJA YA MAJI, MWANG’ONDA ATOA WITO.

Na Matukio Daima Media -BUKOBA, KAGERA 

Wananchi zaidi ya 700 wa Kata ya Ijuganyondo, Halmashauri ya Bukoba, wameanza kunufaika na huduma ya maji safi na salama kufuatia uzinduzi wa Mradi wa Kituo Janja, huku Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Michael Wazo Mwang’onda, akiwataka wananchi kulinda na kutunza miundombinu hiyo ili iendelee kutoa huduma kwa muda mrefu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Mwang’onda amesema upatikanaji wa maji safi na salama ni sehemu muhimu ya kuboresha maisha ya wananchi, kwa kuwa unasaidia kuimarisha afya, usafi wa mazingira na kupunguza muda unaotumika kutafuta maji.

Amesema huduma hiyo pia itawawezesha wananchi kutumia muda wao katika shughuli za kiuchumi na kijamii, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kaya na jamii kwa ujumla.

“Ni jukumu la wananchi kuhakikisha miundombinu hii inalindwa na kutunzwa ili iweze kudumu na kuendelea kutoa huduma kwa jamii kwa muda mrefu,” amesema Mwang’onda.

Kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa na Mhandisi kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA), Edmund Deus, ujenzi wa Kituo Janja umetokana na upanuzi wa mtandao wa mradi wa maji unaohudumia Kata za Ijuganyondo na Karabagine.

Deus amesema uzinduzi wa kituo hicho ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na muhimu za kijamii, sambamba na kuimarisha miundombinu inayolenga kuboresha ustawi wa wananchi na kuchochea maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa upande wao, wananchi wa Kata ya Ijuganyondo wameeleza kufurahishwa na ujio wa mradi huo, wakisema huduma ya maji inayopatikana karibu na makazi yao itawasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji iliyokuwa ikiikabili jamii hiyo.

Wamesema upatikanaji wa maji karibu utawapunguzia muda na nguvu zinazotumika kutafuta maji, huku ukitoa fursa kwa jamii kuelekeza muda zaidi katika shughuli za uzalishaji na maendeleo.

Uzinduzi wa Kituo Janja unaongeza kasi ya jitihada za Serikali za kusogeza huduma muhimu za kijamii karibu na wananchi, hasa katika maeneo ambayo yamekuwa yakikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama.

Wakati huo huo, Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026 zinaendelea katika Mkoa wa Kagera, zikiwa na kauli mbiu:

“Tanzania ni yetu sote, Tushikamane.”

Kupitia kauli hiyo, Mwenge wa Uhuru unaendelea kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo, kutunza miradi ya Serikali na kuimarisha mshikamano katika jamii