Na Lilian Kasenene, Morogoro
Morogoro.FUNDI cherehani Jovita Bategeuye Budyo (30), mkazi wa Mafisa, anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro kwa tuhuma za kumuua mumewe, Abeli Charles (44), mfanyabiashara na mkazi wa Mafisa, Manispaa ya Morogoro.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, tukio hilo lilitokea usiku wa Agosti 31, 2026, katika eneo la Mafisa, Kata ya Mafisa.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa mtuhumiwa na marehemu walikuwa wakiishi pamoja.
Aidha alisema wakati wakiwa wanajiandaa kula, kulitokea mgogoro ambao, kwa mujibu wa taarifa ya polisi, ulihusishwa na madai ya marehemu kunyimwa unyumba.
Mgogoro huo ulizua ugomvi mkubwa na inadaiwa mtuhumiwa alimpiga/kumkata marehemu kwa kitu chenye makali katika maeneo ya shingoni na kichwani, hali iliyosababisha majeraha makubwa na hatimaye kupelekea kifo chake.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limeendelea na uchunguzi wa tukio hilo na linamshikilia mtuhumiwa kwa hatua zaidi za kisheria.
Kamanda Kantimbo ametoa wito kwa wananchi kuepuka kutumia nguvu katika kutatua migogoro ya kifamilia na kijamii, badala yake kutumia njia salama za kumaliza tofauti na changamoto za mahusiano.
Pia amewataka wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuhakikisha usalama unadumishwa, hasa kwa kuwalinda watoto, wazee, watu wenye ulemavu na makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi.
Taarifa hiyo imetolewa Septemba 1, 2026, na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro. ACP Kantimbo.
Mwisho

