Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media Dodoma
Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) imeanzisha huduma maalum ya kutibu kiharusi (stroke), ikiwa ni sehemu ya hatua za kupanua huduma za kibingwa na ubingwa bobezi nchini.
Huduma hiyo ni miongoni mwa huduma mpya zilizoanzishwa na Taasisi hiyo, pamoja na upasuaji wa ubongo kupitia tundu la pua, tiba ya maumivu sugu ya mgongo na upasuaji wa magoti kwa njia ya matundu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya, amesema kuanzishwa kwa huduma hizo kumesaidia kupunguza wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
Amesema huduma za kibingwa zilizoanzishwa na Taasisi hiyo zimewezesha kupunguza rufaa za wagonjwa wa mifupa kwa asilimia 98 na wagonjwa wa ubongo kwa asilimia 97.
Kwa mujibu wa Dkt. Ulisubisya, MOI imeendelea kuimarisha huduma za uchunguzi na matibabu kwa kutumia vifaa vya kisasa, ikiwamo MRI, CT Scan, Digital X-Ray, Ultrasound, Brain Lab na vifaa vya kisasa vya upasuaji wa ubongo na mgongo.
“Katika mwaka wa fedha 2025/2026, MOI ilihudumia wagonjwa 211,359, ambapo 202,000 walikuwa wagonjwa wa nje na 9,359 walilazwa ,” Amesema.
Aidha, Taasisi hiyo imeendelea kutoa huduma za fiziotherapia kwa wagonjwa wenye changamoto mbalimbali za kiafya, ikiwamo waliopata majeraha, kufanyiwa upasuaji na wenye matatizo ya mifupa na mishipa ya fahamu.
“Katika kipindi hicho, wagonjwa 71,819 walipatiwa huduma za fiziotherapia kwa lengo la kurejesha nguvu za misuli, uwezo wa kutembea na utendaji wa viungo vya mwili, ” Amesema.
Dkt. Ulisubisya amesema MOI itaendelea kuanzisha huduma mpya za kibingwa na ubingwa bobezi kwa kutumia teknolojia za kisasa, pamoja na kusogeza huduma karibu na wananchi kupitia programu za outreach na vituo vya satellite katika mikoa mbalimbali.


