
Mahakama nchini Marekani imemkuta na hatia Duane “Keffe D” Davis kwa kosa la mauaji ya mwanamuziki maarufu wa Hip Hop, Tupac Shakur, katika tukio lililotokea takribani miaka 30 iliyopita huko Las Vegas, Nevada.
Davis amepatikana na hatia baada ya kesi hiyo iliyohusu kifo cha Tupac, ambaye alipigwa risasi mjini Las Vegas mwaka 1996 na kufariki siku chache baadaye kutokana na majeraha aliyoyapata.
Katika hoja za kuhitimisha kesi hiyo, upande wa mashtaka ulidai kuwa Davis alikuwa mmoja wa viongozi wa kundi la South Side Compton Crips na kwamba alihusika katika kupanga na kusimamia tukio lililosababisha kifo cha Tupac Shakur.

Mwendesha mashtaka pia alikitaja kitabu cha kumbukumbu za maisha ya Davis kama sehemu muhimu ya ushahidi uliowasilishwa mahakamani.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, maelezo yaliyomo katika kitabu hicho kuhusu tukio hilo yanaweza kuchukuliwa kama kukiri kwa Davis kuhusu kile alichokijua na nafasi yake katika tukio lililosababisha kuuawa kwa Tupac.
UTETEZI WAPINGA USHAHIDI
Kwa upande mwingine, mawakili wa Davis walipinga hoja za upande wa mashtaka, wakisema maelezo yaliyotolewa na mteja wao kuhusu tukio hilo katika kitabu chake yalikuwa “hadithi ya kubuni.”
Utetezi pia ulieleza kuwepo kwa mapungufu katika uchunguzi wa kesi hiyo, ukiwemo upotevu wa baadhi ya kumbukumbu muhimu za uchunguzi.
Aidha, mawakili hao walidai kuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaomuunganisha Davis na mauaji ya Tupac Shakur.
Baada ya kupatikana na hatia, Davis anatarajiwa kurejea mahakamani Oktoba 13 kwa ajili ya kusomewa hukumu yake.
Davis tayari ameeleza kuwa ana mpango wa kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.
Kifo cha Tupac Shakur kimeendelea kuwa miongoni mwa matukio makubwa na yenye utata katika historia ya muziki wa Hip Hop, huku uchunguzi wa mauaji yake ukiendelea kwa miongo kadhaa kabla ya Davis kukabiliwa na mashtaka.
