Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imeibuka mshindi wa kwanza katika mchezo wa mpira wa wavu kwa wanaume kwenye mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Serikali za Mitaa Tanzania (SHIMISEMITA) yaliyofanyika jijini Mbeya mwaka 2026.
Ushindi huo umekuwa sehemu ya mafanikio makubwa kwa Manispaa ya Iringa baada ya kushindana na Halmashauri 177 kutoka maeneo mbalimbali nchini, huku timu hiyo ikifanikiwa kuibuka kidedea katika mchezo wa voliboli kwa wanaume.
Akizungumza baada ya ushindi huo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Zaina Mlawa, amesema mafanikio hayo yameipa heshima Manispaa hiyo na Mkoa wa Iringa kwa ujumla.
“Iringa Manispaa tumeweza kuupa heshima kubwa Mkoa wetu wa Iringa. Kati ya Halmashauri 177 zilizoshiriki SHIMISEMITA 2026 tumeweza kuibuka kidedea kwa kupata ushindi wa kwanza katika mchezo wa voliboli kwa wanaume,”
Mbali na juhudi za wanamichezo, Mlawa amesema Manispaa ya Iringa iliweka mazingira mazuri kwa timu zake kwa kuhakikisha wanamichezo wanapata sare pamoja na vifaa muhimu kwa ajili ya mashindano hayo.
“Tulianza maandalizi mapema, tukawapa t-shirt zenye nembo ya Manispaa lakini pia tukawaandalia t-shirt nyingine kwa ajili ya kubadilisha wanapokuwa kwenye mazoezi. Lakini kikubwa zaidi kilikuwa ni maandalizi na mazoezi,”
Pia ameongeza kuwa mafanikio hayo yametokana na maandalizi na juhudi za wanamichezo huku akieleza kuwa Manispaa hiyo itaendelea kujipanga vizuri kwa ajili ya mashindano yajayo.
“Tuko imara na tunaendelea kujipanga vema kwa ajili ya SHIMISEMITA 2027.
Mbali na ushindi wa voliboli Manispaa ya Iringa pia ilishiriki katika michezo mingine ambapo timu ya netiboli ilifika hatua ya robo fainali kabla ya kutolewa kwenye mashindano hayo.
Timu ya mpira wa miguu nayo ilifanikiwa kufanya vizuri katika baadhi ya michezo ya hatua za awali kabla ya kuondolewa na wenyeji wa mashindano.
“Nawapongeza sana timu zetu zote zilizoshiriki kwa sababu haikuwa kazi ndogo Wachezaji walipambana katika michezo mbalimbali na tutaendelea kujipanga vizuri zaidi kwa mashindano yanayofuata,”
Ushindi huo wa voliboli umeifanya Manispaa ya Iringa kubeba kombe la ubingwa wa wanaume katika SHIMISEMITA 2026 huku matumaini yakiwa ni kuendelea kufanya vizuri zaidi katika mashindano yajayo.










