WANANCHI wa Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera wamepata elimu kuhusu umuhimu wa uwekezaji kupitia mifuko ya pamoja, huku wahitimu wa Shule ya Msingi Rwambaizi waliomaliza masomo miaka 50 iliyopita wakirejea shuleni na kuchangia maendeleo ya taasisi hiyo.
Wahitimu hao wameungana na wahitimu wa Darasa la Saba mwaka 2026 kufanya ibada ya pamoja na kuchangia maendeleo ya shule hiyo, hatua inayosisitiza umuhimu wa wahitimu kukumbuka walikotoka na kushiriki katika kuboresha mazingira ya elimu kwa kizazi cha sasa.

Zoezi la kuwaunganisha wahitimu hao limeongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Pamoja wa Uwekezaji nchini UTT AMIS, Profesa Faustine Kamzora. Katika tukio hilo, wahitimu pamoja na UTT AMIS wamechangia Sh milioni 10 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Shule ya Msingi Rwambaizi.
Mchango huo unalenga kusaidia shule hiyo kuwa na mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia, huku ukiwa mfano kwa jamii kwamba mafanikio anayopata mtu baada ya kumaliza masomo yanaweza kutumika kurudisha fadhila kwa jamii na taasisi zilizomjenga.

Ibada hiyo imeongozwa na Padre Edward Rwechungura, ambaye ni miongoni mwa wahitimu wa shule hiyo miaka 50 iliyopita. Ushiriki wake pamoja na wahitimu wenzake umeonyesha namna kumbukumbu ya shule inaweza kubaki kuwa sehemu muhimu ya maisha ya mtu hata baada ya miongo kadhaa kupita.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Vincent Edward, amesema Shule ya Msingi Rwambaizi ilianzishwa mwaka 1946, huku tukio hilo likiwa funzo kwa wahitimu wapya wa Darasa la Saba kwamba safari ya elimu haiishii katika kuhitimu, bali mafanikio yao ya baadaye yanaweza kuwa fursa ya kurejea na kusaidia jamii.

Baada ya ibada, Profesa Kamzora alitoa semina kwa mamia ya wananchi waliohudhuria Misa na mahafali ya Darasa la Saba kuhusu umuhimu wa kuwekeza fedha zao kupitia mifuko ya pamoja ya uwekezaji, ikiwemo UTT AMIS.
Alisema wananchi wengi huwa na hofu kuhusu namna salama ya kuhifadhi fedha, hivyo akawataka kufanya maamuzi sahihi ya kifedha kwa kuchagua maeneo yenye fursa ya kukuza fedha zao badala ya kuzitumia zote bila mpango.
Profesa Kamzora amewataka wananchi wa Karagwe kutumia vizuri mapato wanayoyapata kutokana na kilimo na mazao mbalimbali kwa kutenga sehemu ya fedha hizo kwa ajili ya uwekezaji.

Amesema wananchi wanaopata fedha kwa misimu tofauti baada ya kuuza mazao wanaweza kutenga sehemu ya mapato yao na kuiwekeza kwa muda ili fedha hizo ziweze kukua na kuleta faida badala ya kutoweka katika matumizi ya muda mfupi yasiyokuwa na mpango mzuri wa kifedha.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa wananchi kujenga utamaduni wa kupanga matumizi ya fedha, kutenga fedha kwa mahitaji muhimu na kuweka sehemu kwa ajili ya uwekezaji wa baadaye.
Amesema uwekezaji unahitaji uvumilivu na maamuzi yenye malengo, hivyo wananchi wanapaswa kuelewa aina ya mfuko wanaochagua, masharti yake, kiwango cha hatari na matarajio ya faida kabla ya kuwekeza fedha zao.

Kwa upande wake, Padre Rwechungura amesema tukio la Rwambaizi limekuwa ujumbe mpana kwa jamii kuhusu umuhimu wa “kukumbuka nyumbani” na kurudisha mchango kwa jamii baada ya kufanikiwa.
Amesema wananchi wanaweza pia kuwekeza katika maisha yao ya baadaye na kutumia sehemu ya mafanikio yao kusaidia familia, shule na jamii kwa ujumla.
Ameongeza kuwa kwa kufanya hivyo, uwekezaji unakuwa siyo tu njia ya kukuza fedha, bali pia sehemu ya kujenga maisha yenye mipango na kuacha alama chanya kwa vizazi vinavyofuata.
