TAKRIBANI WATOTO 14 WAMETEKETEA WAKIWA HOSPITALINI, NCHINI PAKISTAN

 

Takriban watoto wachanga 14 wamefariki baada ya moto kuteketeza wodi ya watoto katika hospitali moja mjini Islamabad, nchini Pakistan.

Moto huo unasemekana kusababishwa na hitalafu ya mfumo wa kiyoyozi.

Moto huo ulianza mapema leo asubuhi katika Taasisi ya Sayansi za Tiba ya Pakistan (PIMS), kwenye ghorofa la tatu lenye wodi ya mama na mtoto.

Tukio hilo ni miongoni mwa matukio mabaya zaidi ya moto kuwahi kutokea katika hospitali nchini Pakistan.

Kulikuwa na watoto wachanga 16 katika wodi hiyo wakati moto huo ulipozuka, mmoja aliokolewa.

Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, amezitaka mamlaka husika kufanya uchunguzi wa haraka kuhusu tukio hilo.

“Wahusika wanapaswa kutambuliwa na hatua kali zaidi zichukuliwe,”

MWANAMUZIKI DOLLY PARTON AFARIKI AKIWA NA MIAKA 80

 

Mwanamuziki mashuhuri wa muziki wa country, Dolly Parton, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 80, familia yake imetangaza kupitia mitandao yake ya kijamii.

“Maumivu yako kwetu, si kwa Dolly,” alisema mpwa wake, Brian Seaver, katika video iliyotangaza kifo chake.

Parton, aliyekulia katika Milima ya Smoky katika jimbo la Tennessee, atakumbukwa kwa nyimbo zake zilizokuwa zikisimulia hadithi za maisha, zikiwemo Coat of Many Colors, Jolene na I Will Always Love You.

Gwiji huyo wa muziki wa country aliuza zaidi ya rekodi milioni 100 duniani kote na aliandika zaidi ya nyimbo 3,000.

Parton aliuchukulia uandishi wa nyimbo kwa uzito mkubwa na alijitambulisha zaidi kama mtunzi wa nyimbo.

“Ni njia yangu ya kujieleza. Ni tiba yangu,” aliwahi kusema.

Mbali na muziki, Parton alikuwa mfanyabiashara mahiri. Ucheshi na haiba yake vilimsaidia kudumu katika tasnia ya burudani kwa zaidi ya miaka 60.

“Dolly aliishi katika mwanga na sasa yuko mikononi mwa Yesu, bila shaka,” alisema mpwa wake.

Dolly Parton alizaliwa mwaka 1946 katika familia maskini ya wakulima iliyokuwa ikiishi katika nyumba ndogo yenye chumba kimoja kando ya Mto Little Pigeon huko Tennessee.

Alikuwa wa nne kati ya watoto 12. Baba yake, Robert Lee Parton, alikuwa mkulima wa tumbaku na alilipa misionari kwa gunia la unga wa mahindi ili amsaidie kumleta duniani.

Parton alisema mama yake, Avie Lee, alikuwa akiimba nyimbo za jadi mara kwa mara. Pia alipewa msukumo na shangazi yake, aliyekuwa akipiga gitaa na kutunga nyimbo.

Mradi wa maji wa miji 28 Geita wafikia 80% – HabariLeo

GEITA: MRADI mkubwa wa maji wa miji 28 unaotekelezwa kwa gharama ya Dola za Marekani Milioni 53.463 ndani ya Manispaa ya Geita umefikia asilimia 80 ya utekelezaji.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mjini Geita (GEUWASA) Mhandisi Frank Changawa ametoa taarifa hiyo kwa viongozi wa mbio za Mwenge mwaka 2026 walipotembelea kituo cha kusukuma maji.

Mhandisi Changawa alisema mkandarasi wa mradi huo tayari amelipwa Dola za Kimarekani Milioni 37.47 ambapo mradi umesanifiwa kuhudumia wakazi zaidi ya 700,000 kwa asilimia 100 katika ata zote 13 za Manispaa ya Geita.

Amesema mkataba wa mradi huo wa Maji wa Miji 28 ulisaniwa mwezi Juni 2022 huku utekelezaji wa mradi ukianza rasmi Aprili 11 na awali ulipangwa kutekelezwa kwa miezi 32 na kukamilika ifikapo Disemba 2025.

Mhandisi Changawa amesema kutokana na changamoto za upatikanaji wa eneo la kujenga chanzo cha maji, mradi umeongezewa muda wa utekelezaji na sasa unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 30 Septemba 2026.

“Ujenzi wa chanzo chenye ukubwa wa lita milioni 46 kwa siku kwenye ziwa Viktoria katika eneo la Senga umefikia asilimia 80 huku Ujenzi wa Kituo cha kusukuma Maji chenye ukubwa wa lita milioni tatu umefikia asilimia 85.

“Ujenzi wa chujio lenye ukubwa wa lita milioni 45 kwa siku umefikia asilimia 75 huku ujenzi wa Matenki matano ya kuhifadhia maji umefikia wastani wa asilimia 95”, amesema.

Mhandisi Changawa ameongeza kuwa kazi ya ulazaji wa bomba kuu lenye kipenyo cha 150mm hadi 800mm urefu wa km 76.47 kutoka kwenye chujio hadi kwenye matanki matano ya kuhifadhia maji umefikia asilimia 95

“Aidha uazaji wa mabomba ya usambazaji wa maji yenye kipenyo cha milimita 75 hadi 400 urefu wa kilometa 30 umefikia asilimia 10”, amesema Mhandisi Changawa.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2026, Wazo Michael Mwang’oda amesifu maendeleo ya mradi na huo na kuwaomba wananchi kulinda miundombinu ya mradi ili kusaidia kufikiwa lengo la serikali kupunguza changamoto ya maji.

Aishi na Uvimbe Miaka 20 Aomba Msaada wa Matibabu, Afunguka Mazito -Video

Global Publishers
August 26, 2026
1,242 views
0 Comments

Usemi wa Kiswahili “Kabla hujafa hujaumbika” unaakisi kwa kiasi kikubwa maisha ya Ester Juma, mwenye umri wa miaka 32, mkazi wa Tabata Barakuda jijini Dar es Salaam, ambaye kwa zaidi ya miaka 20 amekuwa akiishi na uvimbe mkubwa usoni.

Ester anapitia wakati mgumu huku akihangaika kutafuta fedha kwa ajili ya matibabu na upasuaji wa kuondoa uvimbe huo ambao umeathiri kwa kiasi kikubwa maisha yake ya kila siku.

Akizungumza kuhusu hali yake, Ester amesema amekuwa akikumbana na changamoto mbalimbali anapokuwa katika maeneo ya umma. Anaeleza kuwa baadhi ya watoto humkimbia wanapomuona, huku wakati mwingine hata mtoto wake mwenyewe akimuogopa kutokana na mabadiliko ya sura yake.

Changamoto hiyo, amesema, imemfanya kuishi maisha yenye maumivu na msongo mkubwa huku akiwa na matumaini ya kupata msaada wa matibabu.

Ester amesema aliwahi kufika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kupata matibabu, lakini hakufanikiwa kuanza mchakato huo baada ya kushindwa kupata Shilingi 450,000 zinazohitajika kwa ajili ya vipimo.

Kwa sasa, Ester anaendelea kuomba msaada kutoka kwa wasamaria wema ili aweze kupata fedha za vipimo na hatimaye kufanyiwa upasuaji.

Mtu yeyote aliyeguswa na hali ya Ester na angependa kumsaidia anaweza kuchangia kupitia namba 0760 780914, jina Magoli Juma.

Stamico yawekeza Sh milioni 40 mkaa mbadala Geita – HabariLeo

GEITA: SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limetoa ufadhili wa jumla ya Sh milioni 40 kwa wazalishaji wa mkaa mbadala mkoani Geita ambao ni Taasisi ya Wanawake na Samia ili kuongeza matumizi ya nishati safi nchini.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Samia mkoani Geita, Adelina Kabakama ametoa taarifa hiyo mbele ya viongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa kwa Mwaka 2026.

Kabakama amesema kupitia mradi huo Taasisi ya Wanawake na Samia Geita itashirikiana na STAMICO kuunga mkono jitihada za kuzalisha na kuuza mkaa wa nishati safi.

Amesema hatua hiyo inalenga kutekeleza mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati safi ya kupikia kwa mwaka 2024/34 kwa kuhakikisha asilimia 80 ya watanzania wanatumia Nishati safi ifikapo 2034.

“Mradi huu unanufaisha wananchi kwani gharama za mkaa huu ni nafuu, pia mkaa huu ni nishati rafiki kwa mazingira kwani hupunguza matumizi ya kuni na kupunguza ukataji wa miti ili kutengeneza mikaa.

“Kwa sasa tunasambaza wastani wa tani 03 kwa mwezi, na tumenuwia kupeleka kwenye taasisi mbalimbali za umma na kulingana na ongezeko la mahitaji”, amesema Kabakama.

Amesema ili kukidhi mahitaji, STAMICO imepanga kujenga kiwanda cha mkaa mbadala mkoani Geita ili kusogeza huduma kwa wateja na kuendelea kuweka ukaribu kwa watanzania kupata nishati safi kwa ukaribu”, amesema.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa kwa Mwaka 2026, Wazo Michael Mwang’oda amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia inapaswa kuungwa mkono na kila mtu kwani inalenga kuimarisha usalama wa afya za binadamu na mazingira.

OUT na Mzumbe Watangaza Nafasi 6 za Kazi, Mwisho wa Maombi Agosti 31

Kwa niaba ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na Chuo Kikuu cha Mzumbe (MU), Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma anawakaribisha Watanzania wenye sifa, uwezo, ari ya kufanya kazi, uadilifu na wanaolenga kupata matokeo bora kuomba nafasi sita (6) za kazi zilizoainishwa hapa chini.

CHUO KIKUU HURIA CHA TANZANIA (OUT)

1.0 MKUFUNZI DARAJA LA II – ELIMU MAALUMU

Nafasi 2

1.1 Majukumu ya Kazi

i. Kusaidia katika kutekeleza majukumu yote ya kitaalamu yanayohitaji uwezo mkubwa wa kupanga na kubuni katika maeneo ya mafunzo kwa vitendo na miradi ya wanafunzi.
ii. Kusaidia katika shughuli za utafiti na maendeleo.
iii. Kusaidia katika kutunza na kufanya matengenezo ya vifaa vya TEHAMA vinavyotumika kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
iv. Kusaidia katika kuandaa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi.
v. Kutekeleza majukumu mengine yanayohusiana na kazi atakayopewa na msimamizi.

1.2 Sifa na Uzoefu

Mwombaji awe na Shahada ya Kwanza ya Elimu Maalumu katika Lugha ya Alama (Sign Language) au sifa inayolingana na hiyo kutoka katika taasisi inayotambuliwa. Mwombaji lazima awe na ujuzi wa matumizi ya kompyuta.

1.3 Mshahara

PUSS 4.1

2.0 FUNDI DARAJA LA II – MIFUMO YA VIYOYOZI NA MAJOKOFU

Nafasi 1

2.1 Majukumu ya Kazi

i. Kukagua mifumo na vipengele vya vifaa vya kupooza.
ii. Kukagua ufungaji wa mifumo na kutoa mapendekezo kuhusu matengenezo ya mifumo ya umeme.
iii. Kuondoa kimiminika cha zamani na kilichochafuliwa cha kupooza na kuweka kimiminika kipya.
iv. Kusaidia katika ukarabati na matengenezo ya mifumo ya umeme katika maabara au karakana.
v. Kusaidia watumishi wakuu katika shughuli zinazohusiana na taaluma yake.
vi. Kutekeleza majukumu mengine atakayopewa na msimamizi.

2.2 Sifa na Uzoefu

Mwombaji awe na Stashahada ya NTA Level 6 au Full Technician Certificate (FTC) katika Uhandisi wa Baharini na Majokofu (Marine and Refrigeration Engineering) au sifa inayolingana na hizo kutoka katika chuo kikuu kinachotambuliwa.

2.3 Mshahara

PGSS 5.1

CHUO KIKUU CHA MZUMBE (MU)

1.0 AFISA TEHAMA DARAJA LA II – VIFAA VYA SAUTI NA PICHA

Nafasi 2

1.1 Majukumu ya Kazi

i. Kusaidia kutunza kumbukumbu sahihi za matokeo yote ya mitihani, mihutasari ya vikao, kanuni na taratibu.
ii. Kusaidia kutunza chumba cha televisheni.
iii. Kutunza kumbukumbu za vifaa vya sauti na picha (Audio-Visual) vinavyohitajika.
iv. Kusaidia katika ukarabati wa vifaa vya sauti na picha pamoja na vifaa vya kituo cha televisheni.
v. Kusaidia katika upigaji wa video kwa kutumia kamera kulingana na matukio mbalimbali.
vi. Kusaidia katika kufunga, kuweka na kurekebisha vifaa vya sauti na picha.
vii. Kutekeleza majukumu mengine atakayopewa na msimamizi.

1.2 Sifa na Uzoefu

Mwombaji awe na Shahada ya Kwanza katika mojawapo ya fani zifuatazo:

  • Teknolojia ya Multimedia na Uhuishaji (Multimedia Technology and Animation);
  • Uendelezaji wa Maudhui ya Multimedia (Multimedia Content Development);
  • Ubunifu wa Mafunzo (Instructional Design);
  • Ubunifu wa Mafunzo na Teknolojia ya Habari (Instructional Design and Information Technology);

au sifa inayolingana na hizo kutoka katika taasisi inayotambuliwa.

1.3 Mshahara

PGSS 7.1

2.0 MHUSIKA WA USAFISHAJI WA NGUO DARAJA LA II

Nafasi 1

2.1 Majukumu ya Kazi

i. Kukusanya mashuka na neti za vitanda zilizotumika kutoka wodini.
ii. Kuhakikisha vifaa vya kufulia vinawekwa katika hali safi na salama ya kufanya kazi.
iii. Kuhakikisha eneo la kufulia linakuwa katika hali salama.
iv. Kuwapatia idara mbalimbali mashuka na neti za vitanda zilizo safi.
v. Kufua na kupiga pasi nguo za hospitali.
vi. Kuripoti nguo, mashuka na neti za vitanda zilizochakaa au kuharibika.
vii. Kutekeleza majukumu mengine atakayopewa na msimamizi.

2.2 Sifa na Uzoefu

Mwombaji awe amehitimu Kidato cha Nne na awe na Cheti cha Usimamizi wa Huduma za Ukarimu (Hospitality Management) au fani inayolingana na hiyo kutoka katika taasisi inayotambuliwa.

2.3 Mshahara

PMOSS 1.1

MASHARTI YA JUMLA YA MAOMBI

  1. Waombaji wote lazima wawe raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wasiwe na umri unaozidi miaka 45. Hata hivyo, kwa nafasi zilizo katika taasisi za kijeshi/paramilitary, waombaji wa nafasi zisizohitaji shahada hawapaswi kuzidi miaka 25, na waombaji wa nafasi zinazohitaji shahada hawapaswi kuzidi miaka 30.
  2. Waombaji wanapaswa kuomba kwa kuzingatia sifa na taarifa zilizotolewa katika tangazo hili.
  3. Waombaji wanapaswa kuambatanisha nakala zilizothibitishwa za vyeti vifuatavyo:
    • Vyeti vya Uzamili/Shahada/Stashahada ya Juu/Stashahada/Vyeti;
    • Nakala za matokeo ya masomo (transcripts);
    • Vyeti vya usajili wa kitaaluma na mafunzo kutoka katika mamlaka husika za usajili au udhibiti, pale inapohitajika;
    • Cheti cha kuzaliwa.
  4. Hairuhusiwi kuwasilisha:
    • Karatasi za matokeo (results slips) za Kidato cha Nne na Kidato cha Sita;
    • Testimonials;
    • Nakala za matokeo ambazo hazijakamilika (partial transcripts).
  5. Mwombaji anatakiwa kupakia picha yake ya hivi karibuni ya ukubwa wa passport katika Mfumo wa Ajira.
  6. Watumishi walioajiriwa katika Utumishi wa Umma hawaruhusiwi kuomba nafasi hizi. Wanapaswa kuzingatia Waraka Na. CAC.45/257/01/D/140 wa tarehe 30 Novemba, 2010.
  7. Mtumishi aliyestaafu katika Utumishi wa Umma kwa sababu yoyote ile haruhusiwi kuomba.
  8. Kila mwombaji anatakiwa kutaja wadhamini (referees) watatu wenye sifa nzuri pamoja na mawasiliano yao yanayoweza kupatikana.
  9. Vyeti vyote vya elimu vilivyotolewa nje ya Tanzania lazima vitambuliwe na mamlaka husika, ambazo ni TCU, NECTA na NACTVET. Waombaji wa nafasi zinazohitaji GPA wanapaswa kuambatanisha cheti cha ukokotoaji wa GPA kutoka TCU.
  10. Barua ya maombi iliyosainiwa inaweza kuandikwa kwa Kiswahili au Kiingereza na ielekezwe kwa:

Katibu,
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma,
S.L.P. 2320,
Mtaa wa Mahakama, Tambukareli,
Dodoma.

  1. Mwisho wa kutuma maombi ni tarehe 31 Agosti, 2026.
  2. Waombaji watakaofaulu katika hatua ya usaili wa awali pekee ndio watakaotaarifiwa kuhusu tarehe ya usaili.
  3. Kuwasilisha vyeti vya kughushi au taarifa za uongo kutasababisha hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya mwombaji.
  4. Maombi yote yanapaswa kutumwa kupitia Mfumo wa Ajira (Recruitment Portal) kwa kutumia anwani: http://portal.ajira.go.tz. Anwani hii pia inaweza kupatikana kupitia tovuti ya PSRS kwa kubofya sehemu ya “Recruitment Portal.”
  5. Maombi yatakayotumwa kwa njia nyingine yoyote hayatapokelewa au kuzingatiwa.

Imetolewa na:
KATIBU
SEKRETARIETI YA AJIRA KATIKA UTUMISHI WA UMMA

SAFARI YA MIONGO MITATU YA BALOZI DKT NCHIMBI NA KUJIUZULU KWAKE

Na Matukio Daima Media 

BALOZI Dk. Emmanuel Nchimbi amefunga ukurasa wa zaidi ya miongo mitatu katika siasa na utumishi wa umma, baada ya kutangaza kujitenga na nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kustaafu siasa pamoja na utumishi wa umma.

Balozi Dk. Nchimbi alitangaza uamuzi huo jana, Jumatano Agosti 25, 2026, akisema amemwandikia Rais Samia Suluhu Hassan barua ya kumjulisha uamuzi wake. Kujizulu kwake kutaanza kutumika Septemba 4, 2026.

Katika ujumbe wake, Balozi Dk. Nchimbi amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya kujiridhisha kuwa Rais Samia anahitaji mabadiliko katika nafasi hiyo, akieleza ahadi aliyopewa Mkuu wa Nchi wakati akiingia katika nafasi ya Makamu wa Rais.

Alisema Agosti 27, 2025 aliwahidi Rais kuwa angeendelea kwa uwezo wake wote na kwa uaminifu, lakini pia akamhakikishia kuwa angeachia nafasi hiyo endapo angehitaji Makamu mwingine.

“Nimejiridhisha pasipo shaka kuwa Mheshimiwa Rais anatamani mabadiliko, hivyo nimeamua kujitenga ahadi yangu,” alisema katika taarifa yake ya jana.

Uamuzi huo unamfanya Balozi Dk. Nchimbi kuondoka katika nafasi ya pili kwa ukubwa wa kikatiba nchini akiwa ametumikia kwa kipindi kifupi, licha ya kuwa na historia ndefu ya utumishi wa umma na siasa.

UVCCM HADI IKULU

Kumbukumbu kwa Balozi Dk. Nchimbi hakumaanishi tu mwisho wa kipindi chake kifupi katika nafasi ya Makamu wa Rais, bali pia kunafunga safari ndefu ya mwanasiasa aliyeanzia ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Balozi Dk. Nchimbi aliteguliwa katika shughuli za kisiasa akiwa kijana kupitia Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), ambako mwaka 1998 alichaguliwa kuwa mwekezaji wa jumuiya hiyo.

Kabla ya hapo, alikuwa amehamia safari yake ya utumishi wa umma na kufanya kazi katika Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Baadaye alijenga taaluma ya kisiasa na kiutawala, akihudumu katika nafasi mbalimbali za serikali, Bunge na diplomasia.

Balozi Dk. Nchimbi amewahi kuwa Mbunge wa Songea Mjini, Waziri wa Mambo ya Ndani na balozi, kabla ya kufikia nafasi ya Makamu wa Rais.

Alikuwa pia miongoni mwa wanasiasa waliopata nafasi ya kushika nyadhifa za uwaziri katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, akihudumu katika wizara mbalimbali zikiwamo Habari, Utamaduni na Michezo, Kazi, Ajira na Vijana, Ulinzi na Kujenga Taifa, kabla ya kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

SIASA ZA KITATIPA

Balozi Dk. Nchimbi aliingia kwenye siasa za kitaifa kupitia nafasi mbalimbali ndani ya CCM na Serikali, huku akijijengea jina katika mijadala na shughuli za chama.

Safari yake haikuepukana na misukosuko ya kisiasa, ikiwamo vipindi tofauti vya mabadiliko ya nafasi na majukumu ndani ya chama na serikali.

Baadaye akawa mwanadiplomasia na kuiwakilisha Tanzania katika vituo mbalimbali nje ya nchi.

Mikusanyiko hiyo ya uzoefu ulimweka katika nafasi kubwa ya kisiasa na utumishi wa umma kabla ya kufikia nafasi ya juu kabisa ya Makamu wa Rais.

KATIBA MPYA

Katika miezi ya mwisho ya utumishi wake kama Makamu wa Rais, Balozi Dk. Nchimbi alijikita katika shughuli na mijadala mbalimbali ya kitaifa, ikiwamo suala la Katiba Mpya na utawala bora.

Katika mwaka huu, aliyekuwa mgeni rasmi katika Mkutano Mkuu wa 15 wa Tanzania Human Rights Defenders Coalition (THRDC), alisema serikali ina nia ya kuendelea na mchakato wa Katiba Mpya.

Alisisitiza umuhimu wa Katiba Mpya na kuwataka watetezi wa haki za binadamu kuendelea kusimamia haki kwa njia zinazozingatia sheria na misingi ya utawala bora.

DIPLOMASIA

Mbali na siasa za ndani, Balozi Dk. Nchimbi pia alijenga uzoefu mkubwa katika diplomasia baada ya kuteuliwa kuiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali.

April mwaka huu, alihitimisha shughuli zake katika nafasi mbalimbali za kidiplomasia kabla ya kurejea katika majukumu ya juu serikalini.

Uzoefu wake katika diplomasia ulimpa nafasi ya kuifahamu Tanzania kwenye mahusiano ya kimataifa na kuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa nchi na mataifa mengine.

SIASA ZA MWISHO

Uamuzi wa Balozi Dk. Nchimbi kujizulu unafunga wakati ambao kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusu nafasi yake ndani ya Serikali na CCM.

Ripoti za vyombo vya habari na mijadala ya mitandaoni zilikuwa zimeeleza madai kuhusu mustakabali wake kisiasa, ingawa mengi ya madai hayo hayakuwa yamethibitishwa rasmi.

Kwa sasa, jambo lililo wazi ni kwamba Balozi Dk. Nchimbi ameamua kuweka pembeni siasa na utumishi wa umma.

Akizungumza na Rais Samia na CCM kwa imani yao kwake, Balozi Dk. Nchimbi katika taarifa yake ya jana pia amewashukuru Watanzania kwa ushirikiano waliompa katika kipindi chote cha utumishi wake.

Alisema ataendelea kuwa raia mwema wa Tanzania.

Safari yake ya zaidi ya miongo mitatu ya siasa, utumishi wa umma na diplomasia imefikia mwisho, ikiacha historia ya mwanasiasa aliyepitia UVCCM, Bunge, Baraza la Mawaziri, diplomasia hadi kufikia nafasi ya Makamu wa Rais.

Karol G atoa Bilioni 3.1 Kusaidia Waathirika wa Tetemeko Colombia

Msanii mkubwa wa muziki kutoka Colombia, Karol G, ameonyesha mshikamano na wananchi walioathiriwa na tetemeko kubwa la ardhi nchini humo baada ya kutoa mchango wa dola milioni 1.2 kupitia taasisi yake ya Con Cora Foundation.

Kwa thamani ya takribani TSh bilioni 3.1, mchango huo unalenga kusaidia waathirika wa tetemeko hilo pamoja na juhudi za kurejesha na kujenga maeneo yaliyoathirika.

Karol G alishiriki kwa njia ya mtandao katika tamasha maalum la hisani lililopewa jina la “Colombia: Voces por la Vida”, lililofanyika katika ukumbi wa Vive Claro Distrito Cultural jijini Bogotá. Tamasha hilo liliwakutanisha zaidi ya wasanii 30 walioungana kuchangisha fedha kwa ajili ya wananchi walioathiriwa.

Msanii huyo, ambaye alikuwa California, Marekani wakati wa tukio hilo, alitumbuiza nyimbo zake “Coleccionando Heridas” na “Milagros”, huku akitoa ujumbe wa kugusa moyo kuhusu hali inayowakabili wananchi wake.

Karol G alisema ilikuwa vigumu kwake kushuhudia kwa mbali mateso yanayowakabili Wacolombia kutokana na madhara ya tetemeko hilo. Hata hivyo, alieleza kuguswa na namna wananchi walivyoonyesha mshikamano, upendo na kujitolea kusaidiana wakati wa kipindi hicho kigumu.

Msanii huyo alisisitiza kuwa mshikamano wa wananchi haupaswi kuonekana wakati wa maafa pekee, bali unapaswa kuwa sehemu ya maisha ya kila siku kwa watu kusaidiana na kulindana.

Tetemeko hilo lilitokea Agosti 10, 2026, likiwa na ukubwa wa 7.4 kwa mujibu wa Servicio Geológico Colombiano (SGC), huku kitovu chake kikiwa karibu na San José del Palmar katika eneo la Chocó, kwa kina cha takribani kilomita 103.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, SGC imelielezea tetemeko hilo kuwa miongoni mwa matetemeko makubwa zaidi kuwahi kurekodiwa nchini Colombia katika karne ya 21.

Tamasha la “Colombia: Voces por la Vida” liliwakutanisha baadhi ya wasanii maarufu wa Colombia na Amerika Kusini, akiwemo Maluma, Sebastián Yatra, Greeicy, Eladio Carrión, Miguel Bosé, Draco Rosa, Manuel Turizo na Grupo Niche.

Taarifa za baada ya tamasha zinaeleza kuwa fedha zilizokusanywa zilifikia zaidi ya peso bilioni 11.2 za Colombia, kiasi kinachokadiriwa kuwa zaidi ya TSh bilioni 9.

Hatua ya Karol G imeongeza msukumo katika kampeni ya kuwasaidia wananchi waliopoteza makazi na mali kutokana na tetemeko hilo, huku wasanii mbalimbali wakitumia umaarufu wao kuhamasisha jamii kushiriki katika juhudi za uokoaji na ujenzi upya.

Serayah Aachana na Mchumba wake Joey, Afichua Madai ya Usaliti

Global Publishers
August 26, 2026
42 views
0 Comments

Muigizaji wa filamu na mwanamitindo Serayah ametangaza kuachana na mchumba wake, rapa Joey Bada$$, huku akidai kuwa msanii huyo alikuwa akimsaliti mara kwa mara katika kipindi cha uhusiano wao.

Serayah, anayefahamika pia kwa nafasi yake katika tamthilia Empire, amedai kuwa usaliti huo uliendelea kujitokeza katika vipindi mbalimbali vya uhusiano wao, ikiwemo wakati alipokuwa akipitia changamoto za maisha.

Wawili hao walikutana mwaka 2021 kupitia sherehe ya siku ya kuzaliwa ya rafiki yao na baadaye wakaanza uhusiano wa kimapenzi.

Uhusiano wao uliendelea kwa miaka kadhaa, ambapo mwaka 2025 walipata mtoto pamoja na kutangaza uchumba wao.

Hata hivyo, uhusiano huo umefikia mwisho huku Serayah akieleza madai ya kutoridhishwa na mwenendo wa Joey Bada$$ katika kipindi walichokuwa pamoja.

Taarifa kuhusu kuvunjika kwa uhusiano wao zimeibua hisia mbalimbali miongoni mwa mashabiki, hasa kutokana na wawili hao kuwa wamekuwa wakionekana pamoja hadharani na kushirikiana katika malezi ya mtoto wao.

Hadi sasa, Joey Bada$$ hajatoa maelezo ya kina kuhusu madai yaliyotolewa na Serayah.