Saratani ya mlango wa kizazi yaongoza kwa vifo Tanzania
Dodoma. Saratani ya mlango wa kizazi imeendelea kuwa tishio kubwa kwa wanawake nchini, ikiongoza kwa idadi ya wagonjwa na vifo vinavyotokana na saratani, huku wataalamu wakisisitiza umuhimu wa uchunguzi wa mara kwa mara ili ugonjwa huo ugundulike mapema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dk Diwani Msemo, amesema leo Jumatano, Agosti 19, 2026, kuwa saratani hiyo inachangia asilimia 34 ya wagonjwa wote wa saratani nchini, akiwataka wanawake kutopuuza uchunguzi wa afya.
Amesema ugonjwa huo unaweza kutibika endapo utagundulika katika hatua za awali, tofauti na wagonjwa wanaofika hospitalini wakiwa katika hatua za juu, ambapo nafasi za tiba huwa ndogo zaidi.
“Ugonjwa wa saratani unapona kama ukigundulika kwa hatua za awali, lakini ukigundulika kwenye hatua za juu tunachokifanya ni kumpa mgonjwa shufaa ya kumpunguzia maumivu makali wakati akisubiri siku yake, na ndiyo maana tunasisitiza uchunguzi wa mara kwa mara,” amesema Dk Msemo.
Amesema changamoto ya wagonjwa kufika hospitalini wakiwa katika hatua za juu inachangiwa na mambo kadhaa, yakiwamo uwezo mdogo wa kiuchumi, umbali wa vituo vya huduma na ukosefu wa elimu kuhusu saratani.
Amesema Serikali imeendelea kusogeza huduma za uchunguzi na matibabu karibu na wananchi kupitia hospitali za kanda na mikoa ili kupunguza changamoto ya wagonjwa kulazimika kufika Taasisi ya Saratani Ocean Road kwa huduma zote.
“Kwa kuliona hilo, ndiyo maana Serikali imeamua kusogeza huduma za matibabu karibu na wananchi kwenye hospitali za kanda na mikoa na siyo mpaka wafike Ocean Road, ili kuwarahisishia huduma ya vipimo na matibabu kwa wale watakaogundulika na dalili za mapema kabla ya kufikishwa kwetu kwa hatua kubwa zaidi,” amesema.
Dk Msemo amesema kutokana na ukubwa wa tatizo hilo, Serikali imeendelea kutoa chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka tisa hadi 14 bila malipo.
Amesema hatua hiyo inalenga kuwakinga wasichana dhidi ya ugonjwa huo ambao mara nyingi hujitokeza zaidi wanapokuwa watu wazima.
Kwa mujibu wa Dk Msemo, kuwekeza katika kinga na uchunguzi wa mapema ni muhimu kwa sababu ugonjwa huo unaweza kumpata mwanamke katika umri wa utu uzima, ambao ni muhimu katika familia, jamii na uchumi wa Taifa.
Akizungumzia saratani ya matiti, Dk Msemo amesema unyonyeshaji ni miongoni mwa mambo yanayoweza kupunguza baadhi ya vihatarishi vya ugonjwa huo, lakini si kinga ya moja kwa moja.
Amesema hata wanawake wanaonyonyesha wanaweza kupata saratani ya matiti, huku wanaume pia wakiwa miongoni mwa wanaoweza kuugua.
Kwa upande wake, mtaalamu wa Idara ya Kinga wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dk Kandali Samwel, amekanusha taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba mwanaume kunyonya matiti ya mwanamke kunaweza kumkinga mwanamke dhidi ya saratani ya matiti.
Amesema hakuna ushahidi wa kitabibu unaothibitisha madai hayo, akieleza kuwa unyonyeshaji unaoweza kuwa na mchango katika kupunguza baadhi ya vihatarishi ni wa mtoto kunyonya maziwa ya mama.
“Mtoto anaponyonya maziwa ya mama anapunguza kasi ya uzalishaji wa homoni ya estrojeni, lakini si baba. Hivyo, ili kuzuia au kuondoa hatari ya kupata saratani ya matiti kwa mwanamke, anatakiwa kumyonyesha mtoto na si mwenza wa kiume, kama ambavyo wengi wanasema,” amesema.
Dk Samwel amesema mabadiliko ya homoni yanayotokea wakati wa kunyonyesha hupunguza uzalishaji wa estrojeni na shughuli nyingine za uzazi kwa kipindi fulani, jambo linaloweza kupunguza baadhi ya vihatarishi vya saratani ya matiti.
Pia amewashauri wanawake wenye historia ya saratani katika familia zao kufanya uchunguzi wa afya mapema kutokana na uwezekano wa kuwa katika hatari kubwa zaidi.
“Hatari inaongezeka kutokana na ukaribu, hivyo tunashauri wanaotoka katika familia zenye historia ya tatizo hili kufanya uchunguzi mapema ili kubaini iwapo wana matatizo hayo na waanze tiba mapema, kwa sababu kinga ni bora kuliko tiba,” amesema.
Mkazi wa Dodoma, Neema Kajange, amesema jamii inahitaji kupewa elimu zaidi kuhusu saratani ili wanawake na wanaume wafahamu njia sahihi za kujikinga, kufanya uchunguzi na kutafuta matibabu.
Amesema kampeni za kupambana na saratani ya matiti zinapaswa pia kuwahusisha wanaume kwa kuwa baadhi yao hujinyanyapaa wanapogundulika kuwa na ugonjwa huo kutokana na dhana kwamba saratani ya matiti ni ugonjwa unaowapata wanawake pekee.
Kajange amewataka wananchi kuwa makini na taarifa za afya zinazotolewa kwenye mitandao ya kijamii, kuzihakiki na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya badala ya kutumia taarifa zisizothibitishwa katika kufanya maamuzi kuhusu afya zao.

