Skip to content
-
Subscribe to our newsletter & never miss our best posts. Subscribe Now!
Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

  • Home
  • Sample Page
  • Home
  • Sample Page
Close

Search

  • https://www.facebook.com/
  • https://twitter.com/
  • https://t.me/
  • https://www.instagram.com/
  • https://youtube.com/
Subscribe
Habari

Sababu wanaume kuvutiwa na wanawake wenye maumbo makubwa

By admin
August 18, 2026 4 Min Read
Comments Off on Sababu wanaume kuvutiwa na wanawake wenye maumbo makubwa

Dar es Salaam. Mjadala kuhusu aina ya mwili unaovutia zaidi umeibua mitazamo tofauti huku baadhi ya wanaume wa Kiafrika wakisema wanapendelea wanawake wenye maumbo makubwa, hasa wenye makalio na nyonga pana.



Tafiti zinaeleza kuwa mvuto wa makalio unaweza kuhusishwa na jinsi ubongo unavyotambua umbo la mwili kwa ujumla pamoja na ishara zinazoweza kuhusishwa na afya na uwezo wa uzazi.

Hata hivyo, watafiti wanaonya kuwa hakuna sababu moja inayoweza kueleza mapendeleo hayo, kwa kuwa mvuto huathiriwa na utamaduni, mazingira, malezi na ladha binafsi. Mvuto hauwezi kuelezwa na uwiano wa kiuno na nyonga au ukubwa wa makalio pekee, kwa kuwa ukubwa wa mwili, umbo lote na mazingira ya kitamaduni pia vina mchango.

Mazingira na tafsiri ya uzuri

Kwa baadhi ya jamii za Afrika, mwili mkubwa kihistoria umehusishwa na afya, uwezo wa kuzaa na hali nzuri ya maisha. Mtazamo huo unaweza kuhusishwa na mazingira ambayo upatikanaji wa chakula haukuwa wa uhakika, hivyo mtu mwenye mwili mkubwa alionekana kuwa na uwezo wa kupata lishe ya kutosha.

Brian Geofrey, mmoja wa wachangiaji wa mjadala uliofanyika katika mtandao wa kijamii wa X hivi karibuni, anasema mazingira yanaweza kuathiri namna jamii inavyotafsiri uzuri.

“Katika maeneo ambako lishe imekuwa changamoto, mwili wenye unene unaweza kuonekana kama ishara ya mtu anayepata chakula cha kutosha na mwenye afya,” anasema.

Mtazamo huo haupo Afrika pekee. Katika baadhi ya jamii duniani, miili mikubwa imewahi kuhusishwa na afya na ustawi, ingawa mitazamo ya uzuri imebadilika kadiri mazingira, uchumi na mitindo ya maisha ilivyobadilika.

Mkazi wa Tegeta jijini Dar es Salaam, Said Seif anasema anavutiwa zaidi na wanawake wenye maumbo makubwa.

“Napenda wanawake wenye maumbo makubwa kwa sababu naona wana mvuto wa asili. Makalio na umbo la mwili ni sehemu ninayoangalia na kunivutia, ingawa kila mwanaume ana ladha yake,” anasema Said.

Paul Beda, mkazi wa Tabata jijini humo anasema kwake mwanamke mwenye maumbo makubwa anaonekana mwenye mvuto na kujiamini.

“Ni aina ya mwonekano ambao nimeuzoea na kuupenda tangu zamani. Hata hivyo, si lazima kila mwanaume awe na mtazamo huo, kwa sababu uzuri na mvuto hutofautiana kati ya mtu na mtu,” anasema.

Andu Mwakalyelye anaona mvuto huo unaweza pia kuhusishwa na namna jamii inavyotafsiri afya na uzuri.

“Kwa sisi ni ishara ya afya na uzazi,” anasema, akisisitiza kuwa kila mtu ana mapendeleo yake.

Hata hivyo wapo baadhi ya wanaume ambao hawavutiwi na ukubwa wa umbo la mwanamke.

“Mimi napenda mwanamke asiye na mwili mkubwa, huyu ninamfurahia zaidi kuliko mwenye umbo kubwa na mnene,” anasema mkazi wa Morogoro Jafari Juma.

Utafiti uliohusisha wanaume 221 uliochapishwa mwaka 2009 na jarida la PubMed la nchini Uingereza, uliangalia uhusiano kati ya uwiano wa kiuno na nyonga, ukubwa wa matiti na mvuto.

Ulibaini kuwa mapendeleo ya umbo la mwanamke yanaweza kutofautiana kulingana na utamaduni na mazingira, hivyo hakuna kipimo kimoja cha mwili kinachopendwa na wanaume wote.

Matokeo ya utafiti huo ulioongozwa na Profesa wa Saikolojia ya Kijamii kutoka Chuo Kikuu cha Anglia Ruskin (ARU) Uingereza, Viren Swami yalionyesha kuwa wanaume wa makundi tofauti hawakuwa na mtazamo mmoja kuhusu umbo la mwanamke.

Wanaume 51 wa Afrika Kusini walionyesha upendeleo zaidi kwa michoro ya wanawake Waafrika wenye uwiano wa mzunguko wa kiuno na nyonga ya 0.75 na matiti makubwa, huku kwa wanawake weupe wakiwa na uwiano huohuo wakipendelea zaidi matiti madogo.

Kwa upande mwingine, Waafrika 56 wanaoishi Uingereza na wanaume 114 weupe wa Uingereza walionyesha upendeleo tofauti, wakivutiwa zaidi na wanawake Waafrika wenye uwiano wa mzunguko wa kiuno na nyonga ya 0.75 na matiti madogo, huku kwa wanawake weupe wakipendelea uwiano huo ikiwa imeambatana na matiti makubwa.

Watafiti walihitimisha kuwa mvuto wa umbo la mwili hauwezi kuelezwa kwa kipimo kimoja pekee, kwa kuwa mazingira ya kitamaduni na asili ya mwanamke vinaweza kuathiri mapendeleo ya wanaume.

Utafiti pia ulibaini uhusiano mkubwa kati ya mvuto na mtazamo wa afya kwa ujumla, michoro ya wanawake iliyotathminiwa kuwa ya kuvutia zaidi pia ilionekana kuwa ya afya zaidi.

Hata hivyo, watafiti walionya dhidi ya kutafsiri uwiano wa 0.75 moja kwa moja kama “makalio makubwa”, kwa kuwa kipimo hicho kinaonyesha uwiano kati ya kiuno na nyonga, si ukubwa wa makalio pekee.

Utafiti mwingine ulipendekeza kuwa mwonekano wa mwili wenye curves, ikiwamo ukubwa wa makalio, unaweza kuwa na mchango mkubwa katika mvuto kuliko kuangalia uwiano wa kiuno na nyonga pekee.

Utafiti huu ulioandikwa na Ronald Hübner na Emily Sophie Ufken na kuchapishwa katika jarida la Scientific Reports Oktoba 4, 2024, ulishirikisha watu 98, wakiwemo wanaume 33, ambao walipewa michoro ya miili ya wanawake yenye tofauti katika upana wa mwili na kiwango kikubwa cha mikunjo ya mwili kwa maana ya umbo.

Matokeo yalionyesha kuwa umbo ilikuwa kiashiria bora zaidi cha mvuto wa mwili kuliko uwiano wa kiuno na nyonga. Watafiti walibaini kuwa umbo pamoja na upana wa mwili vilieleza takribani asilimia 92 ya tofauti katika alama za mvuto, wakati kiuno na nyonga pamoja na upana wa mwili vilieleza takribani asilimia 63.

Hata hivyo, utafiti haukupima moja kwa moja ukubwa wa makalio, bali umbo na mikunjo ya mwili kwa ujumla.

Mwili mkubwa si kipimo cha afya

Hata hivyo, wataalamu wa afya wanatahadharisha dhidi ya kuhusisha moja kwa moja ukubwa wa mwili na afya.

Mtaalamu wa afya ya jamii, Jane Solomon, anasema mwili mkubwa si ushahidi wa moja kwa moja kwamba mtu ana afya njema.

“Ni muhimu kutenganisha suala la mvuto na afya. Mtu anaweza kuwa na mwili mkubwa na akawa na afya njema, lakini pia uzito uliopitiliza unaweza kuongeza hatari ya magonjwa mbalimbali,” anasema.

Anataja shinikizo la damu, kisukari na magonjwa ya moyo kuwa miongoni mwa matatizo yanayoweza kuhusishwa na unene uliopitiliza, ingawa hatari hutofautiana kati ya mtu na mtu. Kwa upande mwingine, anasema kuwa mwembamba pia hakumaanishi mtu hana afya.

“Afya ya mtu haiwezi kuamuliwa kwa kumtazama tu. Tunahitaji kuangalia hali yake kwa ujumla na, inapohitajika, kufanya vipimo vinavyoweza kutoa picha sahihi zaidi,” anasema.

Author

admin

Follow Me
Other Articles
Previous

Hatari iliyofichika kumrusha mtoto hewani wakati wa kumbembeleza

Next

KANISA LA EBENEZER MBALIZI LAGEUKA FARAJA KWA WAZEE WASIOJIWEZA

Recent Posts

  • Hichilema ashinda tena urais Zambia, Mundubile aibua shaka
  • Bado kiza kimetanda mtoto wa siku moja aliyeibwa Dareda
  • Dola ya Marekani yadhoofika, wawekezaji wakisubiri uamuzi wa Fed
  • Wafugaji walalamikia operesheni za usiku, Serikali yajibu
  • Tanzania, DR Congo kuimarisha ushirikiano, kuondoa vikwazo

Recent Comments

  1. A WordPress Commenter on Hello world!

Archives

  • August 2026

Categories

  • Habari
  • Magazeti
  • Michezo
Copyright 2026 — Habarimpya. All rights reserved. Blogsy WordPress Theme