PANGANI NA NEEMA YA UWEKEZAJI WA KIWANDA CHA KUCHAKATA MADINI YA MCHANGA WA BAHARINI

Sekta vya viwanda ni injini ya maendeleo ya uchumi kutokana na kufungamanishwa kwake na fursa mbalimbali za maendeleo.

Katika jitihada za kuinua maendeleo ya watu na ya uchumi, viwanda havipaswi kuachwa nyuma kwani vina mchango mkubwa katika kufanikisha azma hiyo.

Nchi nyingi zilizoendelea zilifanikiwa katika mipango ya maendeleo kutokana na kuipa msukumo mkubwa sekta ya viwanda.

Katika mikakati ya kujenga na kuinua uchumi wa Tanzania, serikali imeweka mazingira bora na wezeshi kwa ajili ya uwekezaji za viwanda huku seta binafsi ikipewa nafasi kubwa ya kuwekeza katika viwanda.

Mkoa wa Tanga umekuwa na historia kubwa nchini kwa kuwa na maendeleo makubwa ya viwanda, lakini katika miaka ya nyuma viwanda vingi vilikufa.

Juhudi za makusudi zimekuwa zikifanywa na serikali kwa kuhakikisha viwanda vilivyokufa vinafufuliwa huku ujenzi wa viwanda vipya ukifanyika kwa kuishirikisha kikamilifu sekta binafsi.

Sasa ni dhahiri maamuzi ya kuurejesha mkoa wa Tanga katika hadhi yake ya maendeleo ya viwanda yanaendelea kutekelezwa kwa vitendo na matunda yake yameanza kuonekana kwa macho ya damu na nyama.

Katika wilaya ya Pangani mkoani Tanga, neema ya maendeleo imeshuka. Hii ni baada ya kampuni ya Shenghe Resource ya nchini China kuamua kuwekeza kiwanda kikubwa cha kuchakata madini ya mchanga mzito wa baharini (Heavy Mineral Sands).

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, akiwa ziarani China, amehakikishiwa mradi huo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Shenghe, Xie Bing.

Kimsingi, utekelezaji wa mradi huo unafungua na kuongeza fursa za ajira, jambo litakalochochea ustawi wa maisha ya wananchi.

Aidha, kupitia mradi huo, mapato ya serikali yataongezeka kupitia ulipajikodi serikalini, ambapo kodi hizo zitasaidia uboreshaji wa sekta nyingine kama elimu, afya, maji, kilimo, uvuvi na miundombinu.

Vilevile, kuongezeka kwa fursa za biashara. Sekta binafsi itanufaika kwa uanzishwaji wa shughuli za biashara kama migahawa, hoteli na maduka ya bidhaa mbalimbali.

Ni kwamba, ujenzi wa kiwanda hicho cha kuchakata mchanga wa bahari barani Afrika kinachojengwa katika ardhi ya Pangani itachangia kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi Pangani na Tanzania kwa ujumla. 

Pamoja na hayo, Pangani pia kuna mradi mkubwa wa mashamba ya miwa pamoja na ujenzi wa kiwanda cha sukari kinachogharimu zaidi ya shingi bilioni 900 za Kitanzania. 

Kwa hakika, hadhi ya Tanga ya viwanda na maendeleo ya viwanda nchini inazidi kukua kwa kasi zaidi kutokana na utashi mkubwa wa kisiasa wa serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya viwanda na maendeleo ya kiuchumi kwa ujumla.

DKT. MWIGULU AIPONGEZA TANESCO KUTUMIA WATAALAMU WA NDANI

*_▪︎ Asisitiza GRID IMARA Simiyu ikamilike kwa wakati_*

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amewapongeza viongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kuhakikisha Kituo cha Kupokea, Kupooza na Kusambaza Umeme cha Imalilo pamoja na njia ya kusafirisha umeme kutoka Shinyanga hadi Simiyu vinaendelea kujengwa kwa kutumia wataalamu wa ndani.

“Hongereni sana TANESCO kwa uamuzi wenu wa kutekeleza ujenzi wa kituo hiki kwa kutumia wataalamu wa ndani baada ya changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa mkataba na mkandarasi wa awali lakini pia niwapongeze na kazi mnayofanya. Ni nzuri. Ina standard na ubora,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa pongezi hizo leo (Jumanne, Septemba 15, 2026) baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Imalilo na kupokea taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, na kuongeza kuwa hatua hiyo imeonesha uwezo wa wataalamu wa Kitanzania katika kutekeleza miradi mikubwa kwa viwango vinavyostahili.

Waziri Mkuu ambaye yuko katika ziara ya kikazi mkoani Simiyu, ameiagiza TANESCO iongeze kasi ya utekelezaji wa Mradi wa Gridi Imara mkoani Simiyu na kuhakikisha Kituo  cha Imalilo pamoja na njia ya kusafirisha umeme kutoka Shinyanga hadi Simiyu vinakamilika kwa wakati.

Amesema Serikali itahakikisha mtiririko wa fedha unaendelea ili kukamilisha njia hiyo ya kusafirisha umeme, akisisitiza kuwa kukamilika kwa kituo cha Imalilo bila kukamilika kwa njia ya kuleta umeme hakutatatua changamoto ya upatikanaji wa umeme mkoani Simiyu. “Fedha zipo, kazi ifanyike. Fanyeni kazi mchana na usiku ili kazi hii iishe kwa wakati,” amesisitiza.

Waziri Mkuu amesema eneo linalohitaji msukumo mkubwa sasa ni kukamilika kwa njia ya kusafirisha umeme kutoka Ibadakuli, Shinyanga hadi Imalilo yenye urefu wa kilomita 110, ili kituo hicho kiweze kuanza kutoa huduma iliyokusudiwa. “Tutasukuma fedha kwenye njia ya kuleta umeme ili seti yote iweze kukamilika. Tukiweka tu transforma hapa bila kuwa na njia ya kuleta umeme tutakuwa bado hatujamaliza,” amesema.

Amesema Simiyu ni mkoa wa kimkakati kwa uwekezaji katika viwanda kutokana na nafasi yake kijiografia na rasilimali zilizopo, hivyo kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuimarisha upatikanaji na ubora wa umeme pamoja na kuwezesha shughuli za kiuchumi.  “Kilio cha kukatika katika umeme ni kikubwa sana. Na Simiyu ni mkoa wa kimkakati kwenye viwanda,” amesema.

Waziri Mkuu amesema baada ya kurejea Dodoma atafanya kikao na Wizara ya Nishati na Wizara ya Fedha ili kuhakikisha mtiririko wa fedha haukwamishi utekelezaji wa mradi huo, huku akiwaagiza wakandarasi waongeze kasi ya kazi na kuhakikisha timu nzima inakuwa eneo la mradi wakati wote.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Lazaro Twange amesema Kituo cha Imalilo kinajengwa kwa fedha za ndani kwa gharama ya sh. bilioni nane na hadi Septemba 13, 2026 utekelezaji wake umefikia asilimia 82.

Bw. Twange amesema TANESCO iliamua kutekeleza mradi wa kituo hicho chenye uwezo wa MVA 60, kV 220/33, kwa kutumia wataalamu wake wa ndani baada ya kutokukubaliana na masharti ya utekelezaji ya kampuni ya Xian Electric Engineering Company Limited iliyokuwa imepewa kazi hiyo awali.

Amesema njia ya kusafirisha umeme kutoka Ibadakuli, Shinyanga hadi Imalilo yenye urefu wa kilomita 110 na msongo wa kV 220 inagharimu sh. bilioni 48.7, huku utekelezaji wake ukiwa umefikia asilimia 60 na unatarajiwa kukamilika Februari, 2027.

Bw. Twange amesema mkandarasi ameshapeleka eneo la mradi takribani asilimia 90 ya vifaa vinavyohitajika na kazi za ujenzi wa misingi zimefikia zaidi ya asilimia 50, huku changamoto kubwa ikiwa ni upatikanaji wa fedha za kumlipa mkandarasi na wakandarasi wadogo.

Akizungumza kuhusu utekelezaji wa njia hiyo, mwakilishi mkazi wa kampuni ya Kalpataru Project International ya India, Bw. Ashish Tehran alisema ujenzi wa misingi umefikia asilimia 50 na ujenzi wa minara umeanza, huku vifaa vya mradi vikiwa vimewasili eneo la kazi.

Amesema pamoja na changamoto zilizopo katika baadhi ya misingi, wanaendelea na kazi na wanaamini watakamilisha mradi kwa wakati. Mradi huo pia unatarajiwa kutoa ajira kwa wananchi wa maeneo yanayotekelezwa, ikiwemo takribani ajira 200 kwa wakazi wa eneo la Bunamhala.

*DKT. MWIGULU: TUTENGENEZE MABILIONEA WATANZANIA KUPITIA MADINI*

*_▪︎ Aagiza leseni zisizoendelezwa zipewe vijana_*

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka vijana wa Kitanzania wachangamkie fursa zilizopo katika sekta ya madini ili wanufaike na utajiri wa rasilimali hizo na kujenga biashara kubwa za Kitanzania.

Amesema Serikali inalenga kuwawezesha wachimbaji wadogo kukua na kuwa wawekezaji wakubwa, akisisitiza kuwa rasilimali za madini zinapaswa kuwanufaisha Watanzania.

“Tunataka wachimbaji hawa wadogo nao wakue, tutengeneze mabilionea wa Kitanzania; ndiyo maana rasilimali hizi zililetwa hapa Tanzania ziwanufaishe Watanzania,” amesema.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Septemba 15, 2026) wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Sapiwi, katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Mkoa wa Simiyu, katika ziara yake ya kikazi mkoani humo.

Waziri Mkuu amesema baadhi ya watu wamekuwa wakishikilia idadi kubwa ya leseni za madini kwa miaka mingi bila kuziendeleza, huku vijana wakikosa maeneo ya kufanya shughuli za uchimbaji.

“Mtu mmoja anakuwa na leseni nyingi, ameshikilia miaka 10, vijana wanatafuta pa kuchimba… hili nimemwelekeza Waziri wa Madini afanye tathmini, aliye na leseni asiyoifanyia kazi, apewe vijana wapate pa kuchimba,” amesema.

Ametoa agizo kwa Waziri wa Madini afanye tathmini ya leseni zinazoshikiliwa kwa muda mrefu bila kuendelezwa na, pale zinapobainika kutotumika kwa mujibu wa masharti, kuchukua hatua stahiki ili maeneo hayo wapatiwe vijana wenye nia ya kufanya shughuli za uchimbaji.

Kuhusu barabara, Waziri Mkuu amemwelekeza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu kuhakikisha barabara ya Somanda–Nkololo–Matongo–Igegu inapandishwa hadhi kuwa ya Mkoa ili iende kuhudumiwa na TANROADS.

“Hii barabara pandisheni, iende ihudumiwe na TANROADS, ipandisheni kwenye hadhi ya mkoa ili ipate uamuzi wa mwisho lakini kabla ya hapo, madaraja lazima yajengwe, wananchi wasikwame na wakati huo huo tusiwe tunapoteza maisha ya watu kwa kusombwa na maji,” amesema.

Katika sekta ya afya, Waziri Mkuu amekemea vitendo vya kuwatoza wagonjwa wanaohitaji huduma za rufaa fedha za mafuta ya ambulance, akisisitiza kuwa magari hayo yanapaswa kuwa na mafuta na dereva wakati wote.

“Mgonjwa ameshapewa rufaa anatakiwa apelekwe hospitali ya rufaa, anatakiwa apelekwe kwa haraka. Ambulance ipo, mara zote ambulance iwe na mafuta na iwe na dereva,” amesema.

Ameagiza pia watumishi wanaobainika kuwachangisha wagonjwa fedha kwa ajili ya mafuta wachukuliwe hatua za kinidhamu.

Waziri Mkuu amesema Serikali imeondoa utaratibu wa kutaifisha mifugo ya wananchi na kwamba sheria nyingine zinazohusiana na mifugo, wanyamapori na hifadhi zitaendelea kufanyiwa mapitio.

Aidha, amewaagiza viongozi na watendaji kuacha tabia ya kukamata vitendea kazi vya wananchi, ikiwemo pikipiki, bajaji, baiskeli na mikokoteni, kwa makosa yanayoweza kushughulikiwa kwa kutoza faini.

Kuhusu zao la pamba, Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Kilimo akutane na wadau ndani ya mwezi mmoja na kuwasilisha mapendekezo ya mfumo bora wa ununuzi wa pamba utakaowanufaisha wakulima na kuongeza uzalishaji.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew, amesema Serikali imetumia zaidi ya Shilingi bilioni 10 kutekeleza miradi 22 ya maji katika Jimbo la Bariadi Vijijini, huku Shilingi bilioni 3.2 zikitengwa kwa ajili ya kukamilisha miradi mitatu.

Naye, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Chande, amesema Serikali imepokea madai 516 ya madhara yatokanayo na wanyamapori katika mwaka wa fedha 2024/2025 hadi 2025/2026, ambapo 469 yamelipwa na yaliyobaki yanaendelea kushughulikiwa.

Pia, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI, Mhe. Dkt. Festo John Dugange, amesema Serikali imetenga Shilingi milioni 40 kwa ajili ya usanifu wa madaraja mawili ya Duma na Gambosi, huku barabara ya Dutwa kuelekea Hospitali ya Wilaya ikiwa tayari ina mkandarasi.

Lissu Ataka Kukutana na IGP Wambura, CDF Mkunda na Kingai Kupanga Mkakati wa Ushahdi Wa Kesi

Global Publishers
September 15, 2026
0 views
0 Comments

Mhe. Tundu Lissu ameieleza Mahakama kuwa John Heche ndiye shahidi wake wa mwisho ambaye ni raia, akisema anaamini re-examination yake itakamilika kesho kwa muda usiozidi saa moja.

Aidha, Lissu aliomba mashahidi wake wengine waliobaki wafike ili aweze kukutana nao na kupanga namna ya kuendelea na ushahidi uliosalia ambapo kauli hiyo ilizua vicheko ndani ya ukumbi wa Mahakama baada ya kutoa hoja hiyo.

Awali, Jaji Ndunguru alimweleza Lissu kuwa bado ana mashahidi watatu na kwamba Mahakama ilitarajia upande wa utetezi kuwasilisha final submissions siku ya Ijumaa.

Hata hivyo, Lissu alieleza kuwa anahitaji kwanza kukutana na mashahidi hao ili kupanga mkakati wa kesi.

Mashahidi hao ni IGP Camillius Wambura, Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania; CDF Jenerali Jacob John Mkunda, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Wananchi wa Tanzania; pamoja na DCI Ramadhan Kingai, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai.

Baada ya maelezo hayo, Jaji Ndunguru aliahirisha shauri hadi kesho saa tatu kamili asubuhi, huku akibainisha kuwa shahidi John Heche bado hajamaliza kutoa ushahidi wake.

Binti wa Miaka 24 Afariki Akidaiwa Kuamulia Ugomvi wa Rafiki Zake Arusha – Video

Arusha. Binti mwenye umri wa miaka 24, Irene Mallya, mkazi wa Mtaa wa Lemara, Kata ya Lemara jijini Arusha, amefariki dunia baada ya kudaiwa kujeruhiwa wakati akijaribu kuamulia ugomvi kati ya rafiki zake.

Kwa mujibu wa mama mzazi wa marehemu, Mariam Selemani, tukio hilo lilitokea Septemba 14, 2026, majira ya saa 12 asubuhi, baada ya baadhi ya marafiki wa Irene kufika nyumbani na kumtaarifu kuwa binti yake alikuwa amejeruhiwa na kukimbizwa hospitalini.

Mariam amesema taarifa alizopewa kuhusu mazingira ya tukio hilo zilikuwa zikitofautiana, akieleza kuwa awali aliambiwa Irene alikuwa akihusika katika ugomvi huo, kabla ya baadaye kupewa taarifa kwamba alikutwa amelala nje huku akitokwa na damu muda mfupi baada ya kujaribu kuamulia ugomvi.

Kutokana na taarifa hizo zinazotofautiana, familia bado inasubiri uchunguzi wa mamlaka kubaini mazingira halisi yaliyopelekea Irene kujeruhiwa na hatimaye kufariki dunia.

Wakati huo huo, watu wawili waliokuwa karibu na marehemu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya mahojiano, huku uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo cha tukio hilo na iwapo kuna mtu anayehusika na kifo hicho.

The Hub yakanusha kuhusishwa na tukio

Katika hatua nyingine, uongozi wa The Hub Arusha umekanusha taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinazohusisha eneo hilo na tukio la kifo cha Irene Mallya.

Katika taarifa iliyotolewa Septemba 15, 2026, uongozi wa The Hub umesema tukio hilo halikutokea ndani ya The Hub wala ndani ya eneo lao la biashara.

Uongozi huo umesema umesikitishwa na taarifa zisizo sahihi zinazosambazwa na kuhusisha eneo hilo na tukio hilo, huku ukitoa pole kwa familia ya Irene, ndugu, marafiki pamoja na wote walioguswa na msiba huo.

“Tukio hilo halikutokea ndani ya The Hub wala ndani ya eneo letu la biashara,” uongozi huo umesisitiza katika taarifa yake.

The Hub imesema inaendelea kuheshimu uchunguzi unaofanywa na mamlaka husika na iko tayari kutoa ushirikiano pale itakapohitajika.

Aidha, uongozi huo umesisitiza kuwa usalama na ustawi wa wateja pamoja na wafanyakazi ni miongoni mwa vipaumbele vyao.

The Hub imeviomba vyombo vya habari, waendeshaji wa kurasa za mitandao ya kijamii na wananchi kwa ujumla kuhakikisha wanathibitisha taarifa kabla ya kuzichapisha au kuzisambaza, ili kuepusha kuenea kwa taarifa potofu zinazoweza kulihusisha eneo hilo na tukio la kifo cha Irene Mallya.

Uchunguzi wa Jeshi la Polisi unaendelea ili kubaini kwa undani mazingira ya tukio hilo.

Tanzania Yaweka Lengo la Kuwa Kitovu cha Tiba ya Saratani Afrika

Global Publishers
September 15, 2026
6 views
0 Comments

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kinga, uchunguzi na matibabu ya saratani kutokana na uwekezaji unaofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akihutubia Jukwaa la Kisayansi la IAEA mjini Vienna, Austria, amesema Tanzania inalenga kuwa kitovu cha utaalamu na mafunzo ya tiba ya saratani kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni ongezeko la chanjo ya HPV kwa wasichana wenye miaka 9–14 kutoka asilimia 58 mwaka 2018 hadi asilimia 98 mwaka 2026, huku vituo vya tiba ya saratani kwa mionzi vikiongezeka kutoka vitatu mwaka 2020 hadi sita mwaka 2026. Serikali pia imeongeza teknolojia za kisasa za uchunguzi na matibabu, ikiwemo PET-Scan, MRI, LINAC, CT Scan na mammography, na inalenga kuwa na vituo tisa vya huduma jumuishi za saratani katika kanda sita za kimkakati Tanzania Bara na Zanzibar ifikapo 2030.

Makamu wa Rais ametoa wito kwa IAEA na washirika wa kimataifa kuendelea kuiunga mkono Tanzania kupitia mpango wa Rays of Hope, pamoja na kuiteua Taasisi ya Saratani Ocean Road kuwa Kituo cha Umahiri cha Saratani kwa ajili ya mafunzo na kujenga uwezo wa wataalamu wa Afrika.

Hatua hiyo inalenga kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha huduma, utaalamu na teknolojia za kisasa za tiba ya saratani katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Kwa Tanzania, mkutano huo unatoa fursa ya kuunganisha hatua ambazo tayari zimepigwa na mahitaji ya awamu inayofuata ya kuongeza vituo vya saratani, kujenga uwezo wa wataalamu, kupata teknolojia zaidi na kuimarisha ushirikiano wa kisayansi na kifedha.

Jukwaa hilo la siku mbili linafanyika chini ya kaulimbiu “Rays of Hope: Delivering on the Promise of Cancer Care,” likiwakutanisha viongozi, wanasayansi, wataalamu wa afya na wadau wengine kujadili namna ya kupunguza pengo la upatikanaji wa huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani duniani.

Sokabet Yatumia Sh44.7 Bilioni Kuwazawadia Washindi Wa Mwezi Agosti

Dar es Salaam. Kampuni ya michezo ya kubashiri ya Sokabet imetumia jumla ya Sh44, 658,787,637 kuwazawasia washindi mbalimbali kwa mwezi Agosti.

Hayo yalisemwa na Meneja Msaidizi wa Huduma kwa Wateja wa Sokabet Tanzania, Lazaro Mduma, wakati wa wa zoezi la kumkabidhi fedha mmoja wa washindi, Alisema R. Likwawa ambaye alishindi Sh Sh143.1 milioni kuoitia mchezo wa Shining Crown

Mduma alisema kuwa Likwawa ni moja ya washindi walishinda fedha nyingi katika michezo yao mbalimbali na kushika nafasi ya pili huku A. Mwakalinga akishika nafasi ya kwanza kwa kupata Sh180 milioni.

Mwakalinga alishinda fedha hizo kupitia mchezo wa slot wa mtandaoni unaofahamika kama 20 Burning Hot unaotolewa na kampuni ya michezo ya kubashiri ya Sokabet Tanzania.

Mduma alisema kuwa nafasi ya tatu imechukuliwa na B. Mushi akipata Sh109m katika mchezo wa 40 Extra Crown Buy Bonus huku F. Mwasumbi alishinda Sh98.48 milioni na E. Kessy alipata Sh82.8 milioni kwa mchezo wa 40 Super Hot.

Washindi wengine ni H. Omary aliyepata Sh80 milioni, G. Nkya Sh50.3 milioni, M. Mbwambo Sh24.2 milioni na E. Shirima aliyeshinda Sh24 milioni Walishinda kupitia mchezo wa Live Casino Crazy Time

Pia katika orodha hiyo ni Asha Kimaro alijinyakulia Sh21.53 milioni, D. Massawe akipata Sh21.29 milioni na N. Mgaya alipata Sh20 milioni katika mchezo wa Monopoly. Washindi wengine waliotajwa katika matokeo hayo ni H. Chande aliyeshinda Sh19.6 milioni, G. Mwakasege Sh18.76 milioni na K. Lyimo Sh17.34 milioni.

Mduma alisema Sokabet Tanzania inatoa michezo ya slot mtandaoni katika makundi mbalimbali, yakiwamo video slots, classic slots, jackpot, free spins na michezo yenye chaguo la kununua bonansi ambapo wateja wanaweza pia kutumia huduma ya USSD kwa kubonyeza *149*35#, www.sokabet.co.tz au kupiga simu 0800 784242 kwa maelezo Zaidi

“Mbali na michezo ya slot, jukwaa hilo pia linatoa huduma za Live Casino, Virtual Games, Crash Games na sports na bidhaa nyingine za michezo ya mtandaoni,” alisema. Pia Sokabet inamchezo wa Zeppelin ambao wenye mfanano na aviator ambao umetoa zaidi ya kiasi 3,837,558,164 kwa mwezi agosti.

Kwa upande wake, Mwakalinga alisema amefurahishwa na ushindi huo mkubwa, akisema hakutarajia kupata kiasi hicho cha fedha.

“Nina furaha sana kushinda kiasi hiki cha fedha. Sikuwa na fikra za siku moja kupata ushindi huu mnono kwa kutumia kiasi kidogo tu katika kucheza michezo ya mtandaoni ya kampuni ya Sokabet,” alisema.

Alisema anapanga kutumia kwanza kukaa na familia yake wapange kwa pamoja sehemu ya fedha hizo katika uwekezaji ili kuboresha maisha yake na ya familia yao kwa ujumla.

“Nitatumia fedha hizo kwa kufanya mambo mbaimbali ya maendeleo yangu na familia yangu. Nawashauri vijana wenye umri zaidi ya miaka 18 kuendelea kubashiri na Sokabet ambao wana michezo mbalimbali ya mitandaoni ambayo inakupa chaguo kubwa katika kucheza,” alisema.

Watuhumiwa 37 Wahukumiwa Kwa Makosa Mbalimbali Ya Jinai Kilimanjaro

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linaendelea kutekeleza majukumu yake ya kikatiba ya kuhakikisha ulinzi na usalama wa wananchi pamoja na mali zao, huku likiendelea kuchukua hatua dhidi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu na uvunjifu wa sheria.

Katika kipindi cha mwezi Agosti 2026, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro lilifanya operesheni mbalimbali za kukabiliana na makosa ya jinai na makosa mengine yanayohatarisha usalama na ustawi wa jamii.

Operesheni hizo zimewezesha kukamatwa kwa jumla ya watuhumiwa 242 wa makosa mbalimbali ya jinai, ambapo baadhi ya kesi zao zimefikishwa Mahakamani baada ya kukamilika kwa taratibu za uchunguzi na upelelezi.

Jumla ya watuhumiwa 69 walikamatwa kwa makosa ya maadili dhidi ya jamii.

– Watuhumiwa 17 walikamatwa kwa kosa la kupatikana na dawa za kulevya aina ya bhangi, ambapo jumla ya gramu 722 zilikamatwa na kesi 22 zilifunguliwa.

– Watuhumiwa 28 walikamatwa kwa kosa la kupatikana na/kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi, ambapo jumla ya kilo 95.2 zilikamatwa na kesi 46 zilifunguliwa.

– Watuhumiwa 23 walikamatwa kwa kosa la kupatikana na pombe haramu aina ya gongo, ambapo jumla ya lita 420.5 zilikamatwa na kesi 36 zilifunguliwa.

– Mtuhumiwa mmoja alikamatwa baada ya kupatikana na mitambo miwili ya kutengenezea pombe haramu aina ya gongo, ambapo kesi moja ilifunguliwa.

– Watuhumiwa wawili walikamatwa wakiwa na nyara za Serikali, ambapo jumla ya kilo 16 za nyama ya wanyamapori aina ya swala na nyumbu zilikamatwa na kesi tatu zilifunguliwa.

Kwa upande wa uhamiaji haramu, kesi mbili zilifunguliwa dhidi ya raia wa nchi jirani waliokutwa wameingia nchini bila kibali.

Katika makosa yanayohusiana na mazao ya misitu, kesi 10 zilifunguliwa na watuhumiwa wanane walikamatwa wakiwa na jumla ya magogo 13.

WATUHUMIWA 37 WAHUKUMIWA MAHAKAMANI
Kwa upande wa kesi zilizofikishwa Mahakamani ndani ya Mkoa wa Kilimanjaro, jumla ya kesi 37 zilisikilizwa na mashauri yake kukamilika, ambapo Mahakama zilitoa hukumu mbalimbali dhidi ya watuhumiwa waliopatikana na hatia, ikiwemo hukumu ya kifungo cha maisha jela kwa makosa dhidi ya binadamu.

 

MIL.71 KUONDOA MSONGAMANO KITUO CHA AFYA NGURUKA

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

 

Halmashauri ya wilaya uvinza mkoani Kigoma imetumia  kiasi cha shilingi milioni 71.6 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba sita vya kujifungua wajawazito na wodi yenye vitanda 15 kwenye kituo cha afya Nguruka ili kukabiliana na wimbi kubwa la mama wajawazito wanaojifungulia kwenye kituo hicho.

Sambamba na ujenzi wa wodi hizo pia halmashauri imekarabati jengo lililokuwa likitumika awali katika kituo hicho kilichoanza kutumika  mwaka 1976 na kwamba mradi huo unatokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya mama wajawazito wanaojifungulia kwenye kituo hicho cha afya.

Mganga Mfawidhi wa kituo cha Afya Nguruka, Joseph George akitoa taarifa kwa kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru, Wazo Mwang’onda alisema kuwa WATOTO 400 wanazaliwa kila mwezi kwenye kituo hicho  kikiwa ni moja ya vituo vinavyokabiliwa na idadi kubwa ya mama wajawazito wanaofika kituo hapo kujifungua.

 

George alisema kuwa hali hiyo ilikifanya kituo hicho kuzidiwa na idadi kubwa ya watu ambayo ilikuwa haiendani na hali halisi ya utoaji huduma hasa majengo na ndipo halmashauri iliamua kutumia mapato ya ndani kujenga wodi ya kujifunguliwa wajawazito na kulaza wagonjwa.

 

Akizungumza katika uzinduzi huo Mkuu wa wilaya Uvinza, Dinna Mathamani alisema kuwa idadi kubwa ya watu katika eneo hilo linachangia pia idadi kubwaya watu wanaojifungua lwenye kituo hicho ambapo hata maboresho yamekuwa yakifanyika kila wakati hali ya majengo,idadi ya watu viwe na uwiano katika utoaji huduma.

Akizindua kituo hicho kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru, Wazo Mwang’onda alisema kuwa serikali imedhamiria kuboresha utoaji huduma za afya ikiwemo ya Mama mjamzito na watoto ili kupata mtoto isiwe adhabu kwa Mtanzania.

TAASISI YA OMDTZ YAWEZESHA KATA TANO KUWA NA MIPANGO YA KUKABILI MAFURIKO DAR ES SALAAM

 

Na Matukio Daima Dar es Salaam

Taasisi ya OpenMap Development Tanzania (OMDTZ) kwa kushirikiana na Serikali imeanza zoezi la kukabidhi Mipango ya Kata ya Kujiandaa na Kukabiliana na Mafuriko kwa jamii katika kata tano za Jiji la Dar es Salaam. 

Zoezi hilo la siku tano kuanzia tarehe 14 hadi 18 Septemba 2026 ambalo litaziwezesha Kata kupokea mpango na elimu kwa lengo la kuzijea uwezo wa kukabiliana na mafuriko endapo yatatokea katika maeneo yao.

Zoezi hilo linalotekelezwa kupitia Mradi wa “Ramani Zetu, Sauti Zetu”, unaofadhiliwa na Zayed Sustainability Prize, linahusisha Kata za Keko, Makurumila, Mabibo, Ubungo na Tabata, na linalenga kuwezesha jamii na viongozi kuwa na mipango na taarifa sahihi za maeneo yao kwa ajili ya maandalizi na mwitikio wa mafuriko.

Akifungua rasmi zoezi hilo katika Kata ya Keko, Diwani wa Kata hiyo Mheshimiwa Ismail Amanzi alieleza umuhimu wa mipango hiyo kutumika kama nyenzo ya vitendo katika kuimarisha maandalizi ya jamii na kupunguza athari za mafuriko.

“Zoezi hili limekuja wakati sahihi hivyo, ni vyema tukaitumia fursa hii kwa kuhakikisha elimu tunayopewa inafanyiwa kazi kwa vitendo ili kuleta matokeo yaliyokusudiwa kwa kuzingatia athari za mafuriko katika maeneo yetu”, alisema mhe. Amanzi

Kwa upande wake Mkurugenzi wa OpenMap Development Tanzania, Bw. Innocent Maholi, amesema ushirikishwaji wa jamii katika kutambua maeneo hatarishi na kuweka taarifa hizo kwenye ramani ni hatua muhimu ya kuhakikisha wananchi wanakuwa sehemu ya kwanza ya maandalizi ya maafa.

“Lengo letu si kutengeneza ramani pekee, bali kuhakikisha taarifa hizo zinatumika na jamii katika kufanya maamuzi na kuchukua hatua kabla ya mafuriko kutokea,” amesema Maholi.

Alifafanua kuwa, kupitia mipango hiyo, wananchi wamewezeshwa kutambua maeneo hatarishi, njia salama za uhamishaji, maeneo ya mikusanyiko na hatua muhimu za kuchukua kabla na wakati wa mafuriko. Zoezi hilo pia linahusisha elimu kwa jamii kuhusu tahadhari za mapema, usafi wa mifereji na hatua za msingi za uokoaji.

Mradi wa “Ramani Zetu, Sauti Zetu” unalenga kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya mafuriko kupitia ramani shirikishi, mipango ya maandalizi ya maafa na matumizi ya taarifa za ndani za jamii katika kuchukua hatua za kupunguza vihatarishi.

Ikumbukwe kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu yenye dhamana ya kuratibu shughuli za Serikali ikiwemo ya masuala ya maafa nchini imeendelea kusisitiza umuhimu wa maandalizi ya mapema na ushirikiano kati ya Serikali na jamii katika kupunguza madhara yatokanayo na majanga, hususan wakati wa misimu ya mvua hasa kipindi hiki cha mvua za El Nino.

Hata hivyo OpenMap Development Tanzania (OMDTZ) ni taasisi inayolenga kutumia teknolojia ya ramani, taarifa za kijiografia na ushirikishwaji wa jamii katika kutambua na kupunguza vihatarishi vya majanga. Kupitia Mradi wa “Ramani Zetu, Sauti Zetu”, OMDTZ inashirikiana na Serikali na wadau mbalimbali kuwezesha jamii kutambua maeneo hatarishi, njia salama na rasilimali muhimu, pamoja na kuandaa mipango ya maandalizi na kukabiliana na mafuriko ili kuimarisha ustahimilivu wa jamii.