Mashabiki Kukutana Uso Kwa Uso na Wachezaji wa Taifa Stars

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limezindua tukio la ‘Mashabiki Open Day’, litakalowapa mashabiki na wadau wa soka nchini fursa ya kukutana kwa karibu na wachezaji pamoja na benchi la ufundi la Timu ya Taifa, Taifa Stars.

Tukio hilo linatarajiwa kufanyika kesho Jumatano, Septemba 23, 2026, kuanzia saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa TFF, hatua hiyo inalenga kuwawezesha mashabiki kushuhudia kwa karibu mazoezi ya Taifa Stars, huku ikiwa sehemu ya maandalizi ya timu kuelekea michezo ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 pamoja na mchezo wa kirafiki.

Mashabiki watakaohudhuria watapata fursa ya kuona maandalizi ya timu kwa karibu, huku pia wakipewa nafasi ya kupiga picha na kujipiga selfie pamoja na wachezaji na benchi la ufundi.

TFF imeeleza kuwa tukio hilo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha uhusiano kati ya Taifa Stars na mashabiki wake, pamoja na kuongeza morali kwa wachezaji na benchi la ufundi kuelekea michezo ijayo.

Stori na Peter Jinanai| GPL -TUDACO

The post Mashabiki Kukutana Uso Kwa Uso na Wachezaji wa Taifa Stars appeared first on Global Publishers.

OMDTZ YAFANIKISHA MIPANGO YA KUKABILIANA NA MAFURIKO DAR ES SALAAM

 

Na, Matukio Daima Media- Dar es Salaam

Taasisi ya OpenMap Development Tanzania (OMDTZ), kwa kushirikiana na Serikali, imekamilisha zoezi la kukabidhi Mipango ya Maandalizi na Kukabiliana na Mafuriko kwa jamii katika kata tano za Jiji la Dar es Salaam.

Zoezi hilo limewezesha zaidi ya washiriki 1,345 kutoka katika kata za Keko, Mabibo, Ubungo, Makurumla na Tabata kupata mipango, elimu na taarifa muhimu za maandalizi na mwitikio wa mafuriko.

Aidha utekelezaji wa zoezi hilo umepitia Mradi wa “Ramani Zetu, Sauti Zetu”, unaofadhiliwa na Zayed Sustainability Prize, kwa lengo la kuhakikisha jamii na viongozi wa kata hizo wanakuwa na taarifa sahihi kuhusu maeneo yao ili kuwawezesha kujiandaa kabla ya mafuriko, kuchukua hatua wakati wa hatari na kuendelea kuwa salama baada ya tukio.

Katika kata hizo wananchi walipatiwa taarifa kuhusu maeneo hatarishi, njia salama za uhamishaji, maeneo ya mikusanyiko na maeneo yanayohitaji uangalizi zaidi wakati wa mafuriko.

Aidha, walipata elimu kuhusu hatua za kuchukua kabla na wakati wa mafuriko, matumizi ya Mifumo ya Tahadhari za Mapema, hatua za msingi za uokoaji na taarifa kuhusu mwenendo wa mvua za El Niño.

Akifunga rasmi zoezi hilo katika Kata ya Tabata, Diwani wa Kata hiyo, Mheshimiwa Masudi Masudi, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya jamii, viongozi na wadau katika kukabiliana na changamoto za mafuriko.

“Ushirikiano kati ya OMDTZ, viongozi na jamii umetusaidia kutambua changamoto na kuchukua hatua katika maeneo yetu. Mfano ni eneo la Mtaa wa Msimbazi Magharibi ambapo hatua zimechukuliwa na OMDTZ kwa kujenga mfereji wa kupokea maji. Tunahitaji kuendelea na ushirikiano huu ili kuhakikisha maandalizi yanaendelea kuwa sehemu ya maisha ya jamii,” amesema Mhe. Masudi

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa OpenMap Development Tanzania, Bw. Innocent Maholi, amesema kukamilika kwa zoezi hilo ni hatua muhimu katika kuhakikisha mipango na taarifa zilizotengenezwa kwa kushirikisha wananchi zinarejeshwa kwa jamii na kutumika katika kuchukua hatua.

Amehimiza viongozi na wananchi kuendelea kutumia zana zilizotolewa na OMDTZ katika shughuli za usafi wa mazingira, hususan usafishaji wa mifereji na maeneo yanayoweza kuziba na kusababisha maji kutuama.

“Mradi wa Ramani Zetu, Sauti Zetu unalenga kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya mafuriko kupitia matumizi ya ramani shirikishi, taarifa za jamii, mipango ya maandalizi na mwitikio wa maafa pamoja na uhamasishaji wa hatua za mapema,” alisema Maholi

Aliongezea kuwa kupitia mradi huo, OMDTZ itaendelea katika Mikoa ya Pwani na Morogoro  kushirikiana na Serikali na jamii katika kutumia taarifa za maeneo husika kuimarisha maandalizi, kupunguza vihatarishi na kuongeza uwezo wa jamii kukabiliana na athari za mafuriko.

Cédric Kaze Atangazwa Kocha Mkuu Mpya wa Kagera Sugar

Global Publishers
September 22, 2026
492 views
0 Comments

Klabu ya soka ya Kagera Sugar imemtangaza rasmi kocha mzoefu Cédric Kaze kuwa Kocha Mkuu mpya wa timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.

Kaze, raia wa Burundi, anachukua nafasi hiyo baada ya Juma Kaseja kuondolewa kwenye nafasi ya Kocha Mkuu kufuatia mwenendo usioridhisha wa timu katika michezo ya mwanzo ya msimu.

Kaseja aliondolewa baada ya Kagera Sugar kuanza vibaya msimu huu, ikikusanya alama mbili pekee katika michezo sita ya kwanza bila kupata ushindi.

Kaze anajiunga na Kagera Sugar akitokea nchini Afrika Kusini, ambako alikuwa akiifundisha klabu ya Sekhukhune United.

Uongozi wa Kagera Sugar umeamua kumpa nafasi Kaze kutokana na uzoefu wake katika soka la Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Kabla ya kujiunga na Kagera Sugar, Kaze amewahi kuifundisha Yanga SC, huku pia akiwa amefanya kazi kama Kocha Mkuu na Kocha Msaidizi katika klabu za Kaizer Chiefs na Sekhukhune United za Afrika Kusini.

Akizungumza mara baada ya kutambulishwa, Kaze ameahidi kufanya kazi kwa bidii na kutumia kila jitihada kuhakikisha anairejesha Kagera Sugar kwenye mstari wa ushindi na kuipa mafanikio katika michezo ijayo.

Stori na Peter Jinanai | GPL -TUDACO

Yanga Yaipiga Bao Simba Ufungaji Shalulile Ampoteza Doumbia

Global Publishers
September 22, 2026
0 views
0 Comments

Kikosi cha Yanga SC chini ya Kocha Mkuu, Manqoba Mngqithi ni namba moja eneo la ufungaji safu hiyo ya ushambuliaji inayoongozwa na Peter Shalulile imeipoteza ile ya Simb SC inayoongozwa na Ibrahim Doumbia.

Yanga SC baada ya mechi 6 ambazo ni dakika 540, safu ya ushambuliaji imefunga mabao 16,ina wastani wakufunga bao moja kila baada ya dakika 16 msimu wa 2026/27.

Ni Singida Black Stars yenye Jonathan Sowah, hii ni namba mbili kwa safu kali za ushambuliaji ikiwa imetupia mabao 13 baada ya mechi 6 ikiwa na wastani wakufunga bao moja kila baada ya dakika 41.

 

Simba SC ni namba tatu kwa timu zenye mabao mengi ikiwa imetupia mabao 11 ina wastani wakufunga bao 1 kila baada ya dakika 49.

Timu hii inanolewa na Kocha Mkuu, Steve Barker imefunga mabao sawa na Azam FC iliyocheza mechi 7 ikiwa na wastani wakufunga bao moja kila baada ya dakika 57.

Azam FC kwenye msimamo ni nafasi ya 3 imecheza mechi 7 ambazo ni dakika 630 imekusanya jumla ya pointi 14 huku Simba SC ikiwa na pointi 18 nafasi ya pili vinara ni Yanga SC wenye pointi 18.

Na Lunyamadzo Mlyuka



KIGAILA APOKEA WANACHAMA WAPYA ZAIDI YA 300 CHAUMMA BAHI

 

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Basi

KATIBU Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Benson Kigaila, amepokea wanachama wapya zaidi ya 300 kutoka Wilaya ya Bahi, mkoani Dodoma, walioamua kujiunga na chama hicho.

Wanachama hao wamekabidhiwa kadi za uanachama na Kigaila leo Septemba 22,2026  katika Kijiji cha Mpinga, Kata ya Mpinga, Wilaya ya Bahi.

Kigaila alikuwa ameambatana na Mkurugenzi wa Bunge, Halmashauri na Tawala za Mikoa wa Chaumma, Kayombo Kabutal, pamoja na Katibu wa Chaumma Mkoa wa Dodoma, Mathias Nyakapala.

Akizungumza na wananchi waliohudhuria hafla hiyo, Kigaila amesema hali ya umaskini inayowakabili baadhi ya wananchi wa Bahi imesababishwa na kuendelea kukichagua Chama cha Mapinduzi (CCM).

Amesema wakati umefika kwa wananchi hao kufanya mabadiliko ya kisiasa kwa kuondoa CCM madarakani na kukipa nafasi Chaumma, akieleza kuwa chama hicho kinaamini kinaweza kuleta maendeleo ambayo wananchi wa Bahi wamekuwa wakiyahitaji kwa muda mrefu.

“Nyinyi ni maskini wa kutupa kwa sababu ya kuichagua CCM. Wamewatelekeza na ninyi mpo tu, maisha yenu hayaeleweki. Hebu jitathmini, achaneni na CCM sasa, chagueni Chaumma,” amesema Kigaila.

Kwa upande wake, Kabutal alisema pamoja na Wilaya ya Bahi kuwa na utajiri wa rasilimali za madini ikiwemo Uranium, wananchi wake bado wameendelea kukabiliwa na hali ya umaskini.

Kutokana na hali hiyo, amewaomba wananchi wa Bahi kukiamini Chaumma na kukipa nafasi ya kushiriki katika uongozi ili kutekeleza sera na mipango yake ya maendeleo.

Naye Novatus Madanya, mmoja wa wanachama wapya waliojiunga na Chaumma, alisema ameamua kuunga mkono chama hicho kutokana na kuridhishwa na sera zake.

Amesema anaamini sera hizo zinaweza kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi wa Bahi.

Kwa upande wake, Neema Mlay alisema wananchi wa Bahi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa maji kwa muda mrefu.

Mlay amesema hali hiyo imewafanya baadhi ya wananchi kuhisi kama wametelekezwa na kunyanyaswa licha ya kuwa sehemu ya nchi yenye rasilimali mbalimbali.

Amesema wananchi wanahitaji kuona mabadiliko katika huduma za msingi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuboresha maisha yao.

Aliyekuwa Mtayarishaji wa Fox News Jennifer Eckhart Afariki

Jennifer Eckhart, aliyewahi kufanya kazi kama mtayarishaji msaidizi katika kituo cha televisheni cha Fox News nchini Marekani, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 36.

Kwa mujibu wa taarifa ya TMZ, Jennifer amefariki katika jimbo la Florida, huku ofisi ya Martin County Medical Examiner ikithibitisha kifo hicho. Vyanzo vya vyombo vya sheria vimeeleza kuwa kifo chake kimeainishwa kuwa kujiua.

Jennifer alikutwa amefariki katika nyumba yake iliyopo Hobe Sound, Florida, Jumamosi asubuhi, huku uwepo mkubwa wa polisi ukiripotiwa katika eneo hilo.

Jennifer alifahamika zaidi mwaka 2020 baada ya kumfungulia mashtaka aliyekuwa mtangazaji wa Fox News, Ed Henry, akimtuhumu kwa kumbaka wakati wote wawili walipokuwa wakifanya kazi katika kituo hicho.

Katika madai yake, Jennifer alisema Henry alimgusa kingono bila ridhaa yake na kwamba aliogopa kuwa alikuwa na mamlaka ya kuharibu taaluma yake. Henry alikanusha madai hayo na kusema uhusiano wao ulikuwa wa makubaliano.

Fox News ilimfuta kazi Henry mwezi Julai 2020 baada ya kupokea malalamiko ya Jennifer na kufanya uchunguzi wa ndani.

Mapambano ya kisheria kati ya Jennifer na Henry yaliendelea kwa miaka kadhaa, kabla ya wawili hao kufikia makubaliano ya kisheria mwaka 2024, muda mfupi kabla kesi hiyo kufikishwa mahakamani kwa ajili ya kusikilizwa.

Jennifer pia aliishtaki Fox News, akiishutumu kampuni hiyo kwa kushindwa kumlinda dhidi ya Henry na kutomchukulia hatua ipasavyo kutokana na madai ya mwenendo wake.

Hata hivyo, madai hayo dhidi ya Fox News yalitupiliwa mbali, na Mahakama ya Rufaa ya Shirikisho iliunga mkono uamuzi huo mwezi Aprili 2025, ikisema Fox News haikuwa na taarifa kuhusu madai ya mwenendo wa Henry kabla Jennifer hajatoa malalamiko yake.

Baadaye Jennifer alizungumza hadharani kuhusu madai hayo, akieleza kuwa kipindi alichokuwa akifanya kazi Fox News kilimfanya kuishi katika hali ya hofu.

Waziri wa Mambo ya Nje Iran Awasili Marekani Kwa Mkutano wa UN

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amewasili mjini New York, Marekani, akiwa anaongoza ujumbe wa kidiplomasia wa Iran katika Mkutano Mkuu wa 81 wa Umoja wa Mataifa (UNGA) unaofanyika wiki hii.

Araghchi amekuwa afisa wa ngazi ya juu zaidi kutoka Iran kuingia nchini Marekani tangu kuanza kwa vita kati ya Marekani na Iran, hali inayofanya ziara yake kufanyika katika mazingira ya mvutano mkubwa wa kidiplomasia.

Marekani imeidhinisha ujumbe wa msingi wa Iran, ukiwemo Rais Masoud Pezeshkian na Waziri Araghchi, kuhudhuria Mkutano Mkuu wa UN, lakini imeweka masharti kuhusu safari na matumizi yao wakiwa New York. Miongoni mwa masharti hayo ni marufuku ya kununua bidhaa za kifahari, huku pia harakati za wajumbe hao zikiwa zimewekewa mipaka katika maeneo maalumu.

Baada ya kuwasili New York, Araghchi alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ambapo walibadilishana maoni kuhusu ajenda ya Mkutano Mkuu wa UN na masuala yanayohusiana na mkutano huo.

Awali, Iran ilikuwa imetangaza kuwa ujumbe wake ungeongozwa na Rais Pezeshkian. Hata hivyo, ripoti kutoka Iran zilisema baadhi ya wajumbe, wakiwemo watu katika timu ya mawasiliano ya Rais, walikumbana na changamoto za kupata visa vya kuingia Marekani.

Rais Pezeshkian pia anatarajiwa kwenda New York kuhudhuria Mkutano Mkuu wa UN na kutoa hotuba, huku Araghchi akitarajiwa kushiriki katika vikao mbalimbali na kufanya mazungumzo na mawaziri wa mambo ya nje pamoja na maafisa kutoka mataifa mbalimbali watakaohudhuria mkutano huo.

Kwa mujibu wa taarifa za sasa, ziara hiyo inafanyika wakati ambapo mvutano kati ya Washington na Tehran bado ni mkubwa, huku Mkutano Mkuu wa UN ukiwa moja ya majukwaa muhimu kwa pande mbalimbali kueleza misimamo yao kuhusu masuala ya kimataifa.

TBS yatoa somo ubora wa bidhaa Kanda ya Magharibi – HabariLeo

KIGOMA; Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Magharibi, limetoa wito kwa wazalishaji, wafanyabiashara pamoja na wananchi kutumia fursa za kuthibitisha ubora wa bidhaa zao, ili kuweza kupata nafasi ya kushiriki katika soko Afrika Mashariki linalokuwa kwa kasi.

Akizungumza katika maonesho ya Lake Tanganyika Expo 2026 yaliyoanza Septemba 16 na yanatarajiwa kumalizika leo Septemba 22, 2026 Viwanja vya Community Center mkoani Kigoma, Meneja wa TBS Kanda ya Magharibi, Hamisi Seleleko alisema kuwa kanda hiyo inajumuisha mikoa mitatu ambayo ni Kigoma, Katavi, na Tabora.

Alisema kuwa lengo kuu la kushiriki katika maonesho hayo ni kutangaza huduma mbalimbali zinazotolewa na TBS na kuwaonesha wajasiriamali na wazalishaji fursa zinazopatikana kupitia udhibitisho wa ubora wa bidhaa.

“Uthibitishaji wa ubora unampa mzalishaji fursa ya kuingiza bidhaa yake kwenye soko la ndani na nchi wanachama wa Afrika Mashariki, ambalo hadi sasa linajumuisha nchi nane,” alisema.

Aisema katika maonesho hayo, TBS imeweka dawati maalumu la kutoa huduma za papo kwa papo kwa wananchi na wadau wanaotembelea banda lao na kutaja huduma hizo kuwa ni pamoja na usajili wa bidha,a kutoa elimu na usajili wa bidhaa za chakula na vipodozi.

Alisema usajili huo ni kigezo cha msingi kinachoonesha kuwa bidhaa hizo ni salama kwa matumizi ya jamii.

Pia alisema wanatoa elimu juu ya bidhaa zilizopigwa marufuku na kuwaonesha wananchi na wafanyabiashara mifano ya vipodozi na bidhaa zisizokidhi viwango au vyenye viambata hatari ambavyo vimepigwa marufuku, ili kuepuka madhara ya kiafya.

Aidha alitoa wito kwa wazalishaji wote kutumia fursa ya maonesho hayo kuwasilisha maombi yao kupitia mtandao na kukidhi vigezo ili maofisa wa TBS waweze kukagua maeneo yao ya uzalishaji, kupima bidhaa, na kuwapatia leseni ya kutumia alama ya ubora.

 

TBS YATUMIA LAKE TANGANYIKA EXPO 2026 KUWAJENGEA WADAU UELEWA WA VIWANGO NA UTHIBITISHO WA UBORA

  Na Mwandishi Wetu.

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Magharibi limetoa wito kwa wazalishaji, wafanyabiashara pamoja na wananchi kutumia fursa za kuthibitisha ubora wa bidhaa zao ili kuweza kupata nafasi ya kushiriki katika soko linalokua kwa kasi la Afrika Mashariki. 

 

Akizungumza katika maonesho ya Lake Tanganyika Expo 2026 ambayo yalianza Septemba 16 hadi 22 yanayofanyika katika viwanja vya Community Center mkoani Kigoma, Meneja wa TBS Kanda ya Magharibi, Hamisi Simon Seleleko alisema kuwa shirika hilo linahudumia mikoa mitatu ambayo ni Kigoma, Katavi, na Tabora.  

Alisema kuwa lengo kuu la kushiriki katika maonnesho hayo ni kutangaza huduma mbalimbali zinazotolewa na TBS na kuwaonesha wajasiriamali na wazalishaji fursa zinazopatikana kupitia udhibitisho wa ubora wa bidhaa.  

 

“Uthibitishaji wa ubora unampa mzalishaji fursa ya kuingiza bidhaa yake kwenye soko la ndani na nchi wanachama wa Afrika Mashariki, ambalo hadi sasa linajumuisha nchi nane,” alisema.  

Aidha alisema katika maonesho hayo, TBS imeweka dawati maalum la kutoa huduma za papo kwa papo kwa wananchi na wadau wanaotembelea banda lao. 

Alitaja huduma hizo kuwa ni pamoja na 

usajili wa bidhaa kutoa elimu na usajili wa bidhaa za chakula na vipodozi. 

Alisema usajili huo ni kigezo cha msingi kinachoonesha kuwa bidhaa hizo ni salama kwa matumizi ya jamii.  

Pia alisema wanatoa elimu juu ya bidhaa zilizopigwa marufuku na kuwaonesha wananchi na wafanyabiashara mifano ya vipodozi na bidhaa zisizokidhi viwango au vyenye viambata hatari ambavyo vimepigwa marufuku ili kuepuka madhara ya kiafya.  

Aidha alitoa wito kwa wazalishaji wote kutumia fursa ya maonyesho hayo kuwasilisha maombi yao kupitia mtandao na kukidhi vigezo ili maofisa wa TBS waweze kukagua maeneo yao ya uzalishaji, kupima bidhaa, na kuwapatia leseni ya kutumia alama ya ubora.  

Pia, alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wafanyabiashara wa chakula na vipodozi kufika katika banda la TBS ili kupata usaidizi wa ukaguzi na usajili katika kipindi hiki cha maonyesho.

Filamu yaonyesha juhudi kulinda faru – HabariLeo

ARUSHA: Juhudi zinazofanyika kuhakikisha faru wanaendelea kuishi katika mazingira yao ya asili zimeangaziwa kupitia filamu mpya ya “The Rhinos of Ngorongoro – A Conservation Story”, iliyoandaliwa na Ngoteya Wild kwa kushirikiana na Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).

Filamu hiyo imezinduliwa leo Septemba 22, 2026, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Faru Duniani, huku ikitoa fursa kwa watazamaji kuona kwa karibu kazi zinazofanyika kulinda faru na kuhakikisha ustawi wao katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.

Tofauti na filamu nyingi zinazolenga kuonyesha wanyamapori pekee, The Rhinos of Ngorongoro inaangazia pia watu wanaobeba jukumu la kuhakikisha faru wanaendelea kuwepo, wakiwemo askari wa uhifadhi, wafuatiliaji na madaktari wa wanyamapori.

Kupitia simulizi hiyo, filamu inaonyesha kazi ya kuwafuatilia faru, kutambua mienendo yao, kuchunguza afya zao na kuchukua hatua za kuhakikisha usalama wao katika mazingira ya asili.

Kazi hiyo inahitaji ujuzi, uzoefu na uvumilivu, huku wafuatiliaji wakitumia alama za nyayo na viashiria vingine vya mazingira kufahamu mienendo ya faru na maeneo wanayopita.

Ngorongoro ni eneo muhimu katika uhifadhi wa faru, likiwa na faru weusi na faru weupe, jambo linalofanya ulinzi na ufuatiliaji wa wanyama hao kuwa sehemu muhimu ya shughuli za uhifadhi katika eneo hilo.

Filamu hiyo pia inaonyesha kuwa uhifadhi wa faru hauwezi kufanywa na kundi moja pekee, bali unahitaji ushirikiano wa askari wa uhifadhi, wafuatiliaji, madaktari wa wanyamapori, wataalamu wa ikolojia, viongozi, jamii na wadau wengine.

Kwa mtazamo huo, The Rhinos of Ngorongoro inaweka mbele mchango wa binadamu katika kuhakikisha wanyamapori wanaendelea kuwepo, ikionyesha kazi zinazofanyika kila siku ambazo mara nyingi hazionekani kwa watalii na umma.

Ngoteya Wild imesema uhifadhi wa faru ni wajibu wa kizazi cha sasa kwa vizazi vijavyo, huku matumizi ya utaalamu, teknolojia, ufuatiliaji na ushirikishwaji wa jamii yakiendelea kuwa muhimu katika kulinda urithi huo.

Filamu hiyo imeongozwa na Hans Cosmas Ngoteya kwa kushirikiana na NCAA na timu nzima ya Ngoteya Wild.

The Rhinos of Ngorongoro – A Conservation Story sasa inapatikana kupitia akaunti ya Ngoteya Wild kwenye YouTube, ikiwaalika watazamaji kujionea kwa karibu maisha ya faru na juhudi zinazofanyika kuhakikisha wanaendelea kuwa sehemu ya urithi wa Ngorongoro na dunia.