Wizara ya Nishati yatwaa Tuzo Utendaji MEL 2026 – HabariLeo

ARUSHA; Wizara ya Nishati imeibuka kinara kwa kutwaa Tuzo ya Wizara Bora kwa Utendaji (Best Performing Ministry Award) katika eneo la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza (MEL), katika Kongamano la Tano la Kitaifa la MEL 2026 linaloendelea jijini Arusha.

Tuzo hiyo imekabidhiwa  Septemba 23, 2026 na Naibu Spika wa Bunge, Daniel Sillo, wakati wa ufunguzi rasmi wa Kongamano la MEL 20260.

Tuzo hiyo inaitambua Wizara ya Nishati kwa utendaji na matumizi ya mifumo ya ufuatiliaji na tathmini katika kuimarisha utekelezaji wa mipango, programu na miradi ya sekta ya nishati.

Akizungumza kuhusumafanikio hayo, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara ya Nishati, Anitha Ishengoma, amesema wizara inajivunia kutambuliwa kwa juhudi na mafanikio yake katika eneo la ufuatiliaji na tathmini, jambo linalodhihirisha dhamira ya wizara katika kuimarisha utendaji unaozingatia ushahidi na matokeo.

“Tunajivunia kuona juhudi na mafanikio ya sekta ya nishati katika ufuatiliaji na tathmini yakitambuliwa kwa kutunukiwa Tuzo ya Sekta Bora kwa Utendaji 2026.

“Tuzo hii ni matokeo ya kazi ya pamoja, uwajibikaji, ushirikiano na kujituma kwa Wizara ya Nishati pamoja na Taasisi zilizo chini yake,” amesema Ishengoma.

Amefafanua kuwa mafanikio hayo yanaakisi dhamira ya wizara ya kuendelea kutumia ufuatiliaji na tathmini kama nyenzo muhimu ya kusimamia utendaji, utekelezaji wa mipango, programu na miradi, pamoja na kuwezesha ufanyaji wa maamuzi unaozingatia ushahidi na matokeo.

“Tunatoa shukrani kwa uongozi, watumishi na wadau wote waliochangia kufanikisha mafanikio haya. Tuzo hii si mwisho wa safari, bali ni chachu ya kuongeza kasi, ubora, uwajibikaji na kuleta matokeo yenye tija katika sekta ya nishati kwa manufaa ya wananchi,” amesisitiza Ishengoma

Mizigo yawaweka matatani madereva bajaji 72 Mwanza – HabariLeo

MWANZA; Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza limekamata madereva 72 wa bajaji pamoja na vyombo vyao vya usafiri kwa kosa la kubeba mizigo kwa njia hatarishi.

Akizungumza leo jijini Mwanza, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa, alisema madereva hao wamekamatwa wakiwa wamejaza mizigo katika bajaji zao na kutumia barabara bila kujali usalama wa watumiaji wengine.

Ameeleza kuwa bajaji zimekuwa zikitumika kubeba mizigo hatarishi, jambo ambalo linaweza kuhatarisha usalama wa watumiaji wa barabara.

Alisema amekuwa akipokea maoni mbalimbali kuwa makosa yanayolalamikiwa ni ubebaji hatarishi wa mizigo katika bajaji, hali ambayo imekuwa ikihatarisha usalama wa abiria, mizigo na madereva.

Wanawake tutafute elimu tujenge uchumi – HabariLeo

DODOMA: Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima, amewataka wanawake kutafuta elimu na kujiimarisha kiuchumi, ili waweze kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika familia na malezi ya watoto.
‎
‎Dk Gwajima amesema wanawake wanapaswa kuweka mkazo katika kupata elimu na kujenga uwezo wa kiuchumi, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu kukabiliana na changamoto za maisha.
‎
Amesema hayo leo Septemba 23, 2026, jijini Dodoma, wakati wa Mkutano wa Nusu Mwaka wa Tathmini ya Utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto.

Mkutano huo umefanyika ukiwa na kaulimbiu ‘Malezi Bora kwa Watoto: Msingi wa Kufikia Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050’.


‎
‎“Wamama mnakwama wapi? Wamama tutafute elimu kwanza, wamama tutafute kuimarisha kiuchumi kwanza,” amesema Dk Gwajima.
‎
‎Amesema baadhi ya wanaume na wanawake hukutana mtaani, kuanzisha mahusiano na kupata watoto bila kuwapelekea wazazi wao au kufuata taratibu za kifamilia na kuongeza kuwa wanaposhindwana katika mahusiano, baadhi ya wanawake huachwa na changamoto za malezi ya watoto, huku wazazi hao kushindwa kutatua changamoto zinazowakabili watoto.
‎
‎Ametoa kauli hiyo wakati akizungumzia umuhimu wa wanawake kujenga uwezo wao, ili kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika familia na malezi ya watoto.

Waajiri wapewa somo kuboresha mifumo ya taarifa – HabariLeo

MWANZA; Waajiri wametakiwa kuhakikisha wanaweka mifumo madhubuti ya kuzuia na kushughulikia udhalilishaji, unyonyaji na ukatili wa kingono katika maeneo ya kazi, ikiwemo kuweka sera, kamati maalumu na njia salama za kutoa taarifa.

Wito huo umetolewa leo, Septemba 23, 2026, mkoani Mwanza, wakati mashirika yasiyo ya kiserikali yakijengewa uwezo kuhusu namna ya kuzuia udhalilishaji, unyonyaji na ukatili wa kingono, kuboresha mifumo ya utoaji taarifa, kuhimiza uwajibikaji na kuwezesha manusura kupata huduma na msaada.

Akizungumza baada ya elimu hiyo, Mtaalamu wa Jinsia kutoka Tanzania Bora Initiative, Sima Bateyunga, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mradi wa maonesho ya sanaa shirikishi unaolenga kutoa elimu kuhusu namna ya kuzuia udhalilishaji wa kingono mahali pa kazi.

Sima amesema sheria za Tanzania zinaelekeza kuwepo kwa mazingira salama ya kazi, hivyo kila mwajiri anapaswa kuhakikisha watumishi wanafanya kazi katika mazingira yasiyo na vitendo vya udhalilishaji.

Ameshauri waajiri kuweka mifumo rafiki ya utoaji taarifa, ikiwemo sera, kanuni na kamati maalumu zitakazoshughulikia malalamiko ya udhalilishaji katika maeneo ya kazi.

Amesema elimu hiyo imetolewa kupitia sanaa shirikishi, iliyoandaliwa na Tanzania Bora Initiative (TBI), kwa kushirikiana na Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania na Kuckuck Production.

Amesema wameamua kutumia sanaa shirikishi kwa kuwa suala hilo ni nyeti na mara nyingi halitambuliki kwa urahisi, hali inayosababisha watu wengi kuathirika.

CCM Kigoma yataka hatua miradi iliyokwama – HabariLeo

KIGOMA; Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa Kigoma, imeitaka serikali ya Mkoa Kigoma kuchukua hatua kwa Halmashauri za Wilaya za mkoa Kigoma, ili kuhakikisha miradi ya wananchi iliyokwama inakamilishwa na kuanza kutoa huduma.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa Kigoma, Jamal Tamim, alipoongiza Kamati ya Siasa ya Mkoa Kigoma kukagua ujenzi wa Kituo cha Afya Rukoma, Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma,  ambapo alisema mwaka 2023 aliyekuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitoa maelekezo kituo hicho kikamilike na kianze kutoa huduma, lakini hadi sasa hakuna utekelezaji.

Tamim alisema kuwa kiasi cha Sh milioni 546 kimetumika hadi sasa, kiasi ambacho pia kimetolewa kwa vituo vingine vya afya, ambavyo vimekamilika na kuanza kutoa huduma, lakini kituo hicho kilipoanza kupokea fedha mwaka 2021 hadi sasa kimefikia aslimia 85 na hakuna dalili zozote kuanza kutoa huduma karibuni.

Kwa upande wa Katibu wa CCM Mkoa Kigoma, Christopher Pallangyo alisema kuwa vituo vilivyopata fedha kama hicho vimenza kutoa huduma, lakini wanashangazwa na kituo hicho kushindwa kutoa hata huduma za nje wakati taratibu nyingine zikisubiri, hivyo watatoa taarifa kwa mamlaka za serikali zichukue hatua.

Akizungumza katika ziara hiyo Mkuu wa Wilaya Uvinza, Dinna Mathaman alioneshwa kusikitishwa na utoaji huduma kituoni hapo kutoanza hadi sasa, wakati aliwaahidi wananchi hao huduma kuanza kutolewa Septemba Mosi mwaka huu na kwamba watalifanyia kazi suala hilo kwa mamlaka zinazohusika, ili mradi ukamilike na utoaji huduma uanze.

Waziri Makonda Kuzungumza na Waandishi wa Habari Kesho

Global Publishers
September 23, 2026
0 views
0 Comments

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Christian Makonda (Mb), kesho, Septemba 24, 2026, atakutana na Waandishi wa Habari ambapo atazungumzia masuala mbalimbali yanayohusu Wizara hiyo, ikiwemo matukio makubwa ya Kitaifa na Kimataifa yanayotarajiwa kufanyika nchini katika mwaka 2026/2027.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, mkutano huo utafanyika katika Hoteli ya Hyatt iliyopo Posta, Jijini Dar es Salaam, kuanzia saa 4:00 asubuhi.

Waandishi wa Habari wote wamealikwa kuhudhuria mkutano huo ambao utatoa fursa ya kumuuliza Waziri Makonda maswali mbalimbali na kupata ufafanuzi kuhusu masuala yatakayojadiliwa.

Usajili wa Waandishi wa Habari utaanza saa 2:00 asubuhi katika hoteli hiyo.

Taarifa hiyo imetolewa leo, Septemba 23, 2026, na Zaituni Mkwama, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.



Lamine Yamal: Sitaki Kuwa Bora Zaidi ya Pele na Messi

Global Publishers
September 23, 2026
0 views
0 Comments

Nyota wa FC Barcelona, Lamine Yamal, amesema hataki kujilinganisha na magwiji wakubwa wa soka kama Pele na Lionel Messi, bali anatamani kujenga historia yake mwenyewe na kukumbukwa kwa jina lake.

Akizungumza na gazeti la L’Équipe, Yamal amesema lengo lake ni kuandika historia yake katika soka bila kujaribu kuwa kama wachezaji waliomtangulia.

“Ninacheza ili kuandika historia. Sitaki kuwa bora kuliko Pele au Messi. Nataka kuwa Lamine Yamal na nikumbukwe kama Lamine Yamal. Natumaini nitakuwa miongoni mwa wachezaji wakubwa,” amesema Yamal.

Yamal tayari ameshinda mataji matatu ya La Liga akiwa na Barcelona, lakini amesema bado ana kiu kubwa ya mafanikio na angependa kuongeza idadi hiyo hadi kufikia mataji saba, nane au hata zaidi.

Kuhusu Ligi ya Mabingwa Ulaya, Yamal amesema bado hajafanikiwa kutwaa taji hilo na ana hamu kubwa ya kulibeba. Ameeleza kuwa endapo Barcelona itashinda, angependa kuendelea kupambana hadi kufikia hatua za mwisho na kushinda mataji matatu mfululizo, hasa akiwakabili wapinzani kama Paris Saint-Germain.

Kwa upande wa Ballon d’Or, Yamal amesema bado hajafikia malengo yake katika tuzo hiyo na anaamini mwaka unaofuata anaweza kuwa na nafasi kubwa zaidi. Endapo atashinda, amesema hilo litaongeza motisha kwake kutafuta mafanikio mengine.

Kwa ujumla, Yamal ameweka wazi kuwa hataki kuishi chini ya kivuli cha Messi au Pele bali anataka kujenga urithi wake mwenyewe na kuacha alama katika historia ya soka.

Na Tereza Muga



Makamu wa Rais Atoa Msimamo wa Tanzania Kuhusu Israel na Palestina

Global Publishers
September 23, 2026
0 views
0 Comments

Tanzania imetoa wito wa kulindwa kwa raia, kuruhusiwa kwa misaada ya kibinadamu bila vikwazo na kuhuishwa kwa juhudi za kidiplomasia zenye lengo la kufikia amani ya kudumu katika Ukanda wa Gaza na Mashariki ya Kati.

Akihutubia Kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Septemba 22, 2026, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, amesema Tanzania inaendelea kusisitiza umuhimu wa kupatikana kwa suluhisho la kudumu la mgogoro kati ya Israel na Palestina.

Ndejembi amesema Tanzania inaunga mkono suluhisho la nchi mbili, ambapo Israel na Palestina zitaishi pamoja kwa amani na usalama, kwa kuzingatia sheria za kimataifa na maazimio husika ya Umoja wa Mataifa.

Amesema Tanzania pia inatambua haki ya watu wa Palestina ya kujitawala, akisisitiza kuwa amani ya kudumu inapaswa kuzingatia utu, usalama na matarajio halali ya pande zote mbili.

Katika hotuba hiyo, Ndejembi ameeleza pia msimamo wa Tanzania kuhusu umuhimu wa kuheshimu mamlaka ya nchi na sheria za kimataifa, huku akipinga hatua za upande mmoja zinazoweza kuathiri uchumi na ustawi wa wananchi wa nchi zinazolengwa.

Amesema Tanzania inaunga mkono ushirikiano wa kimataifa unaozingatia mamlaka ya kila nchi, huku ikihimiza kuondolewa kwa hatua zinazoweza kuwa kikwazo kwa maendeleo na utekelezaji kamili wa haki za binadamu.



Serikali yajivunia ongezeko bajeti mikopo elimu ya juu – HabariLeo

MWANZA; Serikali imeongeza bajeti ya mikopo na ruzuku kwa wanafunzi wa elimu ya juu hadi Sh 1.06 trilioni kwa mwaka wa masomo 2026/2027, fedha zinazotarajiwa kuwezesha wanafunzi wasiopungua 292,463.

Hayo yamesemwa leo Septemba 23 na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Dk Bill Kiwia, wakati akizungumza katika kikao kazi cha maofisa mikopo wa vyuo vya elimu ya juu na vya kati jijini Mwanza.

Amesema ongezeko hilo linaifanya miaka miwili mfululizo kuwa ya kuvunja rekodi katika bajeti na idadi ya wanufaika wa mikopo na ruzuku.

Dk Kiwia amesema katika mwaka wa masomo 2025/2026 zilitengwa Sh 916.7 bilioni, zilizowanufaisha wanafunzi 252,773.

Amesema mwaka wa masomo 2026/2027, serikali imetenga Sh1.06 trilioni, huku idadi ya wanufaika ikitarajiwa kufikia wasiopungua 292,463.

“Miaka hii miwili 2025/2026 na huu tunaelekea kuanza wa 2026/2027, imevunja rekodi kwa bajeti na wanufaika,” amesema Dk Kiwia.

Kwa mujibu wa Dk  Kiwia, ongezeko hilo linaonesha jitihada za serikali katika kuwezesha vijana wenye sifa kumudu gharama za elimu ya juu na kupata taaluma mbalimbali kwa ajili ya kulitumikia Taifa.

DKT. MWIGULU AHIMIZA USHIRIKIANO WA KIKANDA KUDHIBITI MAGONJWA YA MIFUGO

*_▪︎ EU kuwekeza Euro milioni 50 kusaidia kutokomeza sotoka barani Afrika_*

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na FAO, Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (WOAH), Umoja wa Afrika, jumuiya za kikanda, na wadu wengine katika kuimarisha uwekezaji na mifumo ya kudhibiti magonjwa ya mifugo kwa lengo la kuchangia kutokomeza Sotoka ifikapo mwaka 2040.

“Tunataka kuona uwekezaji wenye nguvu zaidi, unaotabirika na endelevu. Umiliki wa kitaifa na ufadhili wa ndani lazima viwe msingi, vikisaidiwa na FAO, WOAH, Umoja wa Afrika, jumuiya za kikanda, taasisi za fedha za kimataifa, washirika wa maendeleo na sekta binafsi.”

“Tunapaswa kuondoka katika hatua zilizotawanyika na kuelekea kwenye mifumo ya kudumu; kutoka mipango ya kitaifa pekee kwenda ushirikiano wa kikanda; na kutoka ahadi kwenda kwenye matokeo yanayoweza kupimika,” alisisitiza Waziri Mkuu.

Alisema hayo jana, (Jumanne, Septemba 22, 2026) jijini Roma, Italia, wakati akishiriki mjadala wa ngazi ya juu kuhusu uwekezaji katika kutokomeza Sotoka na kudhibiti Ugonjwa wa Miguu na Midomo kwenye Mkutano wa Kimataifa ulioandaliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kuhusu utekelezaji wa Afya Moja katika mifumo ya chakula na kilimo.

Alisema chanjo pekee haitoshi, bali Tanzania inahitaji maabara zinazofanya kazi, mifumo madhubuti ya ufuatiliaji, usambazaji wa chanjo wa uhakika, utambuzi wa mifugo, wataalamu wenye ujuzi na ushirikiano baina ya nchi na nchi hasa kwenye maeneo ya mipakani.

Akizungumzia umuhimu wa ushirikiano wa kikanda, Dkt. Mwigulu alisema magonjwa ya mifugo hayaheshimu mipaka ya nchi, na kubainisha kuwa wakati nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zikijadili hatua za kuelekea shirikisho, wanyama tayari wameungana kwa kasi zaidi.

“Wakati nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zikiendelea kujadili namba ya kuingia katika mfumo wa shirikisho, wanyama tayari wameungana haraka kuliko sisi,” alisema.

Akifungua mlango wa kuchangia mada kwenye mjadala huo, Balozi wa Umoja wa Ulaya jijini Roma na Mwakilishi wa Kudumu wa Umoja huo katika Mashirika ya Umoja wa Mataifa ya Roma, Dkt. Martin Selmayr, alisema Umoja wa Ulaya unaandaa uwekezaji mpya wa Euro milioni 50 kwa ajili ya awamu ya pili ya mpango wa kutokomeza Sotoka barani Afrika.

Balozi Selmayr alisema uwekezaji huo unalenga kuongeza nguvu katika juhudi za kutokomeza ugonjwa huo na kuwa kichocheo kwa nchi husika, taasisi za fedha za maendeleo, sekta binafsi na washirika wengine kuongeza uwekezaji katika programu za kitaifa za kutokomeza sotoka.

“Umoja wa Ulaya unaamini kuwa uwekezaji huo haupaswi kuishia katika kampeni nyingine ya chanjo pekee, bali unapaswa kusaidia pia kuimarisha huduma za mifugo, uzalishaji na ubora wa chanjo, ushirikiano wa sekta binafsi pamoja na hatua za pamoja za kukabiliana na magonjwa yanayovuka mipaka,” alisisitiza.

Naye, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Godfrey Magwenzi, alisema afya ya wanyama ni uwekezaji wa kimkakati katika usalama wa chakula, maendeleo ya uchumi na ustahimilivu, akisisitiza umuhimu wa uwekezaji wa muda mrefu katika kutokomeza sotoka.

Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uzalishaji wa Wanyama wa Chad, Prof. Abderrahim Awat Atteib, alisema juhudi za kutokomeza ugonjwa huo zinahitaji ufadhili endelevu na unaotabirika ili kuzuia ugonjwa huo kurejea katika maeneo ambayo tayari yamedhibitiwa.

Naye, Dkt. Samuel Thevasagayam, Mkurugenzi wa Timu ya Mifugo wa Taasisi ya The Gates Foundation, alisema mafanikio ya kutokomeza sotoka yanahitaji umiliki wa Serikali, ushiriki wa wafugaji na sekta binafsi, pamoja na matumizi ya sayansi na ushahidi katika kupanga na kutekeleza hatua za kudhibiti ugonjwa huo.