Makonda: Timu ya Taifa ni Mali Ya Nchi, Si Kampuni ya Mtu Binafsi

Global Publishers
September 24, 2026
0 views
0 Comments

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema Timu ya Taifa ni mali ya Nchi na si kampuni inayomilikiwa na mtu binafsi.

 

Akizungumza leo Septemba 24, jijini Dar es Salaam, Makonda amesema mamlaka ya Waziri katika kusimamia Sekta ya Michezo yanaongozwa na Sheria, Sera na Kanuni, huku akisisitiza kuwa Timu ya Taifa inawakilisha Nchi kila inaposhiriki mashindano ndani na nje ya Tanzania.

 

“Timu ya Taifa ni mali ya Nchi, si kampuni ya mtu. Ndiyo maana tumeikasimu na kuihudumia. Timu ikienda popote pale, ni Nchi inaenda,” amesema Makonda.

 

Aidha, Makonda amekosoa mtazamo wa baadhi ya watu wanaodharau mamlaka ya Waziri katika utekelezaji wa majukumu yake, akisisitiza kuwa Waziri ni mteule wa Rais na anawajibika kusimamia sekta aliyopewa kwa mujibu wa sheria.

 

“Wanamfanya kama Waziri wanamdharau, lakini huyo ni mteule wa Rais anayesimamia Wizara ambayo inakupa mkate,” amesema Makonda.

 

FAHAMU LISHE BORA NA MAKUNDI SITA YA VYAKULA


Na Bibi Maendeleo, Irene Samora

Lishe bora ni ulaji wa mlo kamili unaotokana na makundi yote sita ya vyakula. Mlo kamili huupatia mwili virutubisho vinavyohitajika kwa ajili ya kutoa nguvu, kujenga mwili, kuimarisha kinga na kuuwezesha kufanya kazi zake vizuri.

Makundi sita ya vyakula ni haya yafuatayo:

1. Vyakula vya nafaka, mizizi na ndizi

Vyakula hivi ni chanzo kikubwa cha wanga, ambao huupa mwili nguvu na nishati. Mifano yake ni mahindi, ndizi mbichi na za kupikwa, mihogo, ngano, mchele na viazi.

Ili mwili uweze kufanya shughuli mbalimbali za kila siku, unahitaji kupata vyakula vya kundi hili kwa kiwango kinachofaa.

2. Vyakula vya asili ya wanyama

Vyakula hivi ni chanzo muhimu cha protini, ambayo husaidia kujenga mwili, kutengeneza seli mpya na kukarabati tishu zilizoharibika.

Mifano ya vyakula vya kundi hili ni nyama ya ng’ombe, kuku, samaki, mayai, senene, kumbikumbi na maziwa.

3. Vyakula vya jamii ya mikunde na mbegu

Kundi hili linajumuisha maharage, kunde, mbaazi, choroko, dengu na njegere. Vyakula hivi vina protini pamoja na madini mbalimbali yanayohitajika katika mwili.

Virutubisho vinavyopatikana katika vyakula hivi husaidia kujenga mwili, kutengeneza seli na kuimarisha afya kwa ujumla.

4. Mboga

Mboga ni chanzo muhimu cha vitamini na madini ambayo husaidia kuulinda mwili dhidi ya magonjwa.

Mifano yake ni tembele, mchicha, spinachi, mlenda, majani ya maboga, kisamvu, kabichi, majani ya kunde, bamia, nyanya chungu, mashona-nguo, karoti, hoho na bilinganya.

Mboga zinapaswa kuandaliwa kwa usafi na zisipikwe kwa muda mrefu sana, kwa sababu kufanya hivyo kunaweza kupunguza baadhi ya virutubisho vyake.

5. Matunda

Matunda ni chanzo cha vitamini na madini ambayo husaidia kuimarisha kinga ya mwili na kuukinga dhidi ya magonjwa mbalimbali.

Mifano ya matunda ni tikitimaji, maembe, zabibu, nanasi, parachichi, mapera, ndizi mbivu na papai. Pia yapo matunda ya porini, kama vile furu, ukwaju, ubuyu na embe ng’ongo.

Ni muhimu kula matunda mbalimbali mara kwa mara ili kuupatia mwili virutubisho vinavyohitajika.

6. Mafuta

Mafuta yanayotokana na mimea, kama vile ufuta na alizeti, ni muhimu kwa kuupa mwili nguvu na nishati. Mafuta pia husaidia mwili kufyonza baadhi ya vitamini, ikiwemo vitamini A, D, E na K.

Hata hivyo, licha ya umuhimu wake, mafuta yanapaswa kutumiwa kwa kiasi kidogo. Matumizi ya mafuta mengi yanaweza kuchangia kuongezeka kwa uzito wa mwili na hatari ya kupata shinikizo la damu pamoja na magonjwa mengine.

Faida za lishe bora

Lishe bora ina faida nyingi kwa afya ya binadamu. Baadhi ya faida hizo ni:

1:Hutengeneza seli mpya za mwili.

2:Hukarabati tishu zilizoharibika.

3:Husaidia kutengeneza vichocheo vya mwili.

4:Huchangia ukuaji mzuri wa akili na mwili.

5:Huupa mwili nguvu na joto.

6:Husaidia kuzuia baadhi ya magonjwa, ikiwemo saratani.

7:Husaidia umeng’enyaji wa chakula na kudhibiti kiwango cha sukari mwilini.

8:Husaidia mwili kupata nguvu za kufanya shughuli mbalimbali.

9:kutengeneza baadhi ya vichocheo muhimu mwilini.

10:Husaidia ufyonzwaji wa vitamini A, D, E na K.

11:Hulinda mwili dhidi ya magonjwa.

12:Husaidia kuimarisha mifupa na meno.

13:Husaidia kupambana na upungufu wa damu kupitia madini ya chuma.

14:Huimarisha kinga na afya ya mwili kwa ujumla.

Madhara ya kukosa lishe bora

Mtu asipopata lishe bora anaweza kukabiliwa na madhara mbalimbali ya kiafya, yakiwemo:

1:Mwili kudhoofika.

2:Kupoteza nguvu mwilini.

3:Kuongezeka kwa hatari ya kupata magonjwa sugu na maambukizi.

4:Udhaifu na uchovu wa mara kwa mara.

5:Kudhoofika kwa kinga ya mwili.

6:Kudumaa kwa watoto kimwili na kiakili.

7:Magonjwa ya mifupa na misuli.

8:Matatizo ya afya ya akili.

Lishe bora na afya njema

Lishe bora ni moja ya nguzo muhimu za afya njema. Mbali na kula chakula bora, mtu anatakiwa kufanya mazoezi ya viungo, kunywa maji safi na salama, kupata mwanga wa jua, kuvuta hewa safi na kupata muda wa kutosha wa kupumzika.

Binadamu anahitaji chakula ili aweze kuishi, kukua na kufanya shughuli zake za kila siku. Hata hivyo, chakula kinapaswa kuchaguliwa, kuandaliwa na kuhifadhiwa kwa usafi na umakini mkubwa.

Kwa hiyo, chakula kiwe dawa kwa mwili. Kisipochaguliwa na kuandaliwa vizuri kinaweza kuwa chanzo cha matatizo ya kiafya. Tafiti zinaonyesha kuwa takribani asilimia 35 ya visa vya saratani vinaweza kuhusishwa na ulaji usiofaa.

Kila mtu anapaswa kuhakikisha anakula mlo kamili wenye vyakula kutoka katika makundi yote sita kwa kiasi kinachofaa. Lishe bora ni msingi wa ukuaji mzuri, nguvu, kinga imara na maisha yenye afya.

Fuatilia kipindi cha bibi Maendeleo kila siku kupitia matukio Daima Tv kwa mawasiliao piga 0656285926/0754026299                     

WHI YAFUNGUA FURSA ZA NYUMBA NA UWEKEZAJI ARUSHA

Na.Matukio Daima Media.

Watumishi Housing Investments (WHI) inaendelea kuwafikia na kutoa elimu kwa wananchi mbalimbali wanaotembelea banda lake lililopo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wakaguzi wa Ndani unaofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 21 hadi 25 Septemba, 2026.

Kupitia banda hilo, wananchi wanapata fursa ya kuzungumza moja kwa moja na wataalamu wa WHI na kupata maelezo kuhusu huduma na fursa mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo, ikiwemo fursa za kumiliki nyumba, uwekezaji kupitia Faida Fund na huduma ya e-Wekeza, pamoja na huduma za ujenzi na ushauri elekezi.

Ushiriki wa WHI katika mkutano huo ni sehemu ya jitihada za taasisi hiyo za kuendelea kusogeza huduma na taarifa karibu na wananchi, sambamba na kuongeza uelewa kuhusu fursa za makazi na uwekezaji zinazopatikana kupitia WHI.

Wananchi waliopo Arusha wanakaribishwa kutembelea banda la WHI katika AICC hadi tarehe 25 Septemba, 2026, ili kupata maelezo zaidi na kuzungumza moja kwa moja na wataalamu kuhusu huduma na fursa zinazotolewa na taasisi hiyo.

 

Jaji Aamuru Rais Trump Kurejesha Vibali vya Kazi Waandishi wa CNN

Global Publishers
September 24, 2026
0 views
0 Comments

Jaji wa Mahakama ya Shirikisho nchini Marekani, Timothy Kelly, ameamuru utawala wa Rais Donald Trump kurejesha mara moja vibali vya waandishi wa habari kutoka CNN, MS NOW na Politico vya kuingia na kufanya kazi katika Ikulu ya Marekani, White House.

Uamuzi huo umetolewa baada ya vyombo hivyo kufungua kesi kupinga hatua ya utawala wa Trump kuviondoa katika shughuli za White House.

Jaji Kelly ametoa amri ya muda ya siku 14, huku akisema marufuku hiyo inaonekana kuwa na matatizo ya kikatiba na kwamba waandishi hawakupewa utaratibu unaostahili kabla ya vibali vyao kufutwa.

Tukio hilo lilianza baada ya Trump kutangaza Septemba 18, 2026 kuwa CNN, MS NOW na Politico havitaruhusiwa tena kupata huduma ya kawaida ya waandishi ndani ya White House.

Utawala wake ulidai kuwa baadhi ya taarifa zilizochapishwa na vyombo hivyo zilihusisha masuala ya usalama wa taifa, huku vyombo hivyo vikidai kuwa hatua hiyo ilikiuka haki zao za kikatiba.

Kwa mujibu wa uamuzi wa jaji, utawala wa Trump unatakiwa kurejesha press passes za waandishi wa vyombo hivyo na kusitisha utekelezaji wa marufuku hiyo kwa kipindi cha siku 14 wakati mchakato wa kesi ukiendelea.

Na Ashura Karimu

 

MJUMBE WA KAMATI YA SIASA SAME MARIAM MJEMA ASHIRIKI MAPOKEZI YA NAIBU KATIBU MKUU BARA NDUGU AGGREY MWANRI

Na Ashrack Miraji, Same – Kilimanjaro

Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Same, Mariam Mjema, ameshiriki katika mapokezi ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, Ndugu Aggrey Mwanri, aliyewasili wilayani Same kuanza ziara ya kikazi.

Ndugu Mwanri amewasili katika Ofisi za CCM Wilaya ya Same, ikiwa ni sehemu ya ziara yake inayolenga kutembelea maeneo mbalimbali ya Majimbo ya Same Mashariki na Same Magharibi.

Katika ziara hiyo, Naibu Katibu Mkuu huyo anatarajiwa kukutana na viongozi na wanachama wa CCM, pamoja na wananchi, kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali yanayohusu shughuli za chama na maendeleo ya wananchi.

Mariam Mjema, akiwa miongoni mwa viongozi walioshiriki katika mapokezi hayo, amekuwa sehemu ya viongozi wa CCM wa Wilaya ya Same waliokuwepo kumpokea Naibu Katibu Mkuu huyo wakati wa kuwasili kwake.

Ziara hiyo inatarajiwa kuhitimishwa kwa mkutano wa hadhara, ambapo Ndugu Mwanri atazungumza na wananchi pamoja na wanachama wa CCM wa Wilaya ya Same kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu chama na maendeleo ya jamii.

 

UEFA Nations League Kuanza leo Klopp Uso Kwa Uso Na Xavi

Global Publishers
September 24, 2026
0 views
0 Comments

Mashindano ya UEFA Nations League 2026/27 yanaanza leo, Alhamisi Septemba 24, huku macho yakielekezwa kwenye mchezo wa Kundi A2 kati ya Uholanzi na Ujerumani.

Mchezo huo utakuwa wa kwanza kwa Jürgen Klopp kuiongoza Ujerumani tangu alipoteuliwa kuwa kocha mwezi Julai, huku Uholanzi ikianza rasmi kipindi kipya chini ya Xavi Hernández.

Katika michezo mingine ya League A, Serbia itakutana na Ugiriki, wakati Norway itamenyana na Denmark katika Kundi A4. Mabingwa watetezi, Ureno, wataanza kampeni yao dhidi ya Wales.

Ureno inaingia kwenye mashindano hayo ikiwa na dhamira ya kutetea taji ililolitwaa mwaka 2025. Taifa hilo tayari limetwaa Nations League mara mbili.

Kwa upande wa League B, Austria itacheza dhidi ya Israel, huku Kosovo ikiwa mwenyeji wa Jamhuri ya Ireland.

Katika League D, Andorra itakutana na Malta, wakati Liechtenstein itapambana na Lithuania.

Hatua ya ligi ya UEFA Nations League 2026/27 itaendelea hadi Novemba 17, huku timu za League A, B na C zikicheza jumla ya mechi sita kila moja.

Na Erick Elibariki

 

Pezeshkian Amjibu Trump: Iran Haiwezi Kulazimishwa Kusalimu Amri

Global Publishers
September 24, 2026
0 views
0 Comments

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amemjibu Rais wa Marekani, Donald Trump, kufuatia kauli za Trump kuhusu Iran, akisisitiza kuwa Tehran haitasalimu amri wala kukubali kushinikizwa kupitia vitisho.

 

Katika hotuba yake, Pezeshkian alisema Iran iko tayari kwa mazungumzo na diplomasia, lakini haitakubali mazungumzo yanayoambatana na vitisho au shinikizo “Hatutainamisha kichwa wala kupiga goti.”

Pezeshkian pia alisisitiza kuwa shinikizo, vikwazo na vitisho havitabadilisha msimamo wa Iran. Alisema Iran iko tayari kushirikiana na mataifa mengine, lakini mazungumzo yanapaswa kufanyika bila kutumia lugha ya nguvu.

Kauli hiyo ilikuja siku moja baada ya Trump kuhutubia Mkutano Mkuu wa UN na kutoa kauli kali kuhusu Iran, huku akieleza kuwa Marekani ilikuwa ikikabiliwa na chaguo kati ya diplomasia na hatua kali zaidi dhidi ya Tehran.

Katika hotuba yake, Pezeshkian pia alitetea haki ya Iran ya kutumia teknolojia ya nyuklia kwa madhumuni ya amani, huku akisema nchi yake haitafuti silaha za nyuklia.

Wakati Pezeshkian akianza kuhutubia, wajumbe wa Marekani waliondoka ukumbini. Tukio hilo lilitokea katika kipindi ambacho mvutano kati ya Washington na Tehran umeendelea kuwa mkubwa, huku pande hizo zikijadili uwezekano wa kurejea kwenye diplomasia.

NA TEREZA MUGA



JNIA, KIA zang’ara tuzo za ACI AFRICA Nigeria – HabariLeo

ABUJA: VIWANJA vya Ndege vya Kimataifa vya Julius Nyerere (JNIA) na Kilimanjaro (KIA) vimeipa Tanzania heshima katika sekta ya usafiri wa anga barani Afrika baada ya kutwaa tuzo tatu zinazotolewa na Baraza la Viwanja vya Ndege Afrika (ACI Africa).

Katika tuzo hizo, JNIA imetwaa tuzo mbili, ikiwemo nafasi ya pili katika kipengele cha Utawala Bora upande wa Uwezeshaji na Utayari wa Huduma kwa Abiria 2026 (Runner-Up of Passenger Facilitation and Readiness Excellence Awards 2026 – Governance Category).

JNIA pia imepata nafasi ya pili katika kipengele cha Ubunifu na Mageuzi ya Kiteknolojia (Innovation & Transformation Category) katika kundi la viwanja vya ndege vinavyohudumia kati ya abiria milioni mbili na milioni tano kwa mwaka.

Kwa upande wake, KIA imeibuka mshindi wa kwanza katika Tuzo ya Uwezeshaji na Utayari wa Huduma kwa Abiria 2026, katika kipengele cha Ushirikishwaji wa Wadau (Stakeholder Engagement), kwa kundi la viwanja vya ndege vinavyohudumia chini ya abiria milioni mbili kwa mwaka.

Tuzo hizo zimepokelewa na Mkurugenzi wa Biashara na Maendeleo wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mzee Kilele, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Abdul Mombokaleo, katika hafla iliyofanyika wakati wa Mkutano Mkuu wa 35 wa ACI Africa unaoendelea jijini Abuja.

Mkutano huo umeanza Septemba 19 na unatarajiwa kufungwa Septemba 25, 2026, ukiwa na kaulimbiu “Next-Gen Airports: Driving Performance and Resilience”, inayolenga kujadili namna ya kuimarisha utendaji, ubunifu, matumizi ya teknolojia na ustahimilivu wa viwanja vya ndege barani Afrika.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hizo, Mkurugenzi wa Biashara na Maendeleo, Mzee Kilele, amesema tuzo hizo ni uthibitisho wa juhudi zinazofanywa na TAA katika kuboresha huduma, kuimarisha ushirikiano na wadau na kuweka mazingira bora ya kukuza shughuli za kibiashara na kiutendaji katika viwanja vya ndege nchini.

“Tuzo hizi ni matokeo ya kazi kubwa inayofanywa na TAA kwa kushirikiana na wadau. Tunatambua kuwa ukuaji wa viwanja vya ndege unaenda sambamba na ubora wa huduma, ubunifu na uwezo wa kujenga mahusiano imara na wadau. Utambuzi huu unatupa nguvu zaidi ya kufanya kazi kwa bidii, kuongeza ubunifu na kuhakikisha tunapata matokeo yanayoonekana,” amesema Kilele.

Ameongeza kuwa TAA itaendelea kutumia fursa mbalimbali za kibiashara na ubunifu katika sekta ya usafiri wa anga ili kuongeza ushindani wa viwanja vya ndege vya Tanzania na kuvifanya kuwa vituo vinavyokidhi mahitaji ya abiria, mashirika ya ndege na wadau wengine wa sekta hiyo.

Mafanikio ya JNIA na KIA yanaongeza mwonekano wa Tanzania katika sekta ya usafiri wa anga barani Afrika, wakati Serikali ikiendelea na juhudi za kuboresha miundombinu, huduma na mazingira ya biashara katika viwanja vya ndege nchini.

Rukwa kuunganishwa Gridi ya Taifa kupitia TAZA – HabariLeo

IRINGA: Wananchi wa Mkoa wa Rukwa wanatarajiwa kuanza kunufaika na huduma ya umeme wa uhakika baada ya kukamilika kwa Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa Kilovoti 400 wa Iringa–Kisada–Mbeya–Tunduma–Sumbawanga (TAZA), hatua inayotarajiwa kuchochea maendeleo ya kiuchumi, uwekezaji na utoaji wa huduma bora za kijamii mkoani humo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange, amesema kukamilika kwa mradi huo kutawezesha Rukwa kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa kwa mara ya kwanza, jambo litakaloongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi, taasisi za umma, viwanda na wafanyabiashara.

Akizungumza Oktoba 24, 2026 wakati wa kikao na wakandarasi wa mradi huo, Twange amewataka kuhakikisha mradi unakamilika ifikapo Novemba 15, 2026 ili wananchi waanze kupata manufaa yaliyokusudiwa.

“Huu ni mradi mkubwa wa kimkakati wenye urefu wa kilomita 616 na gharama ya takribani Shilingi trilioni 2. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji huu mkubwa katika sekta ya nishati. Kukamilika kwa mradi huu kutawapatia wananchi wa Rukwa umeme wa uhakika na kufungua fursa mpya za maendeleo ya kiuchumi,” amesema Twange.

Amesema hadi sasa mradi huo umefikia asilimia 96.57 ya utekelezaji na utakapokamilika utaongeza uwezo wa Gridi ya Taifa kusafirisha umeme, kupunguza changamoto za upatikanaji wa umeme katika maeneo ya Kusini Magharibi mwa Tanzania na kuweka mazingira bora ya uwekezaji katika viwanda, madini, biashara na kilimo.

Kwa wananchi wa Rukwa, mradi huo unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma bora katika hospitali, shule na taasisi nyingine za kijamii zinazotegemea umeme, huku ukiimarisha shughuli za uzalishaji mali na ajira kupitia uwekezaji unaotegemea nishati ya uhakika.

Aidha, Twange amesema mradi huo una umuhimu wa kikanda kwa kuwa utakamilisha maandalizi ya kuunganisha mifumo ya umeme ya Tanzania na Zambia, hatua itakayowezesha biashara ya umeme kati ya nchi hizo mbili na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi ndani ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Akizungumzia changamoto zilizochelewesha mradi huo, amesema ni pamoja na usafirishaji wa vifaa vikubwa, hususan transfoma zenye uzito wa zaidi ya tani 200, zilizohitaji maandalizi maalum ya miundombinu ya barabara kabla ya kusafirishwa.

Hata hivyo, TANESCO inaendelea kushirikiana na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuhakikisha vifaa vilivyosalia vinafikishwa salama katika maeneo ya mradi ili kazi zote zikamilike ndani ya muda uliokubaliwa.

Mradi wa TAZA, ambao awali ulitarajiwa kukamilika Mei 2026, sasa unatarajiwa kukamilika Novemba 15, 2026, ukiwa sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa.

Marekani Yatoa Onyo Baada ya Mashambulizi Dhidi ya Saudi Arabia

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio.

Marekani imesema itatekeleza kikamilifu ahadi zake za ulinzi kwa Saudi Arabia, huku kukiwa na ongezeko la mvutano wa kiusalama katika Mashariki ya Kati na mashambulizi yanayohusishwa na Wahouthi dhidi ya Saudi Arabia.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, Jumatano, Septemba 23, 2026, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini New York.

Rubio alisema Marekani ina mkataba madhubuti wa ulinzi na Saudi Arabia na kwamba Washington itaendelea kutimiza majukumu yake chini ya makubaliano hayo.

“Tuna makubaliano madhubuti ya ulinzi na Saudi Arabia, na tutatimiza ahadi zetu katika makubaliano hayo,” Rubio alisema.

Alipoulizwa iwapo Rais wa Marekani, Donald Trump, alikuwa tayari kuchukua hatua zaidi dhidi ya Wahouthi, Rubio hakutaja aina ya hatua za kijeshi zinazoweza kuchukuliwa. Hata hivyo, alisema rais huyo ana chaguo mbalimbali alizonazo.

Rubio pia alisisitiza kuwa Saudi Arabia ni mshirika muhimu wa kimkakati wa Marekani katika masuala ya ulinzi.

Kauli hiyo inakuja wakati Saudi Arabia ikikabiliwa na wasiwasi wa kiusalama kufuatia mfululizo wa mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani yanayohusishwa na Wahouthi katika wiki za hivi karibuni.

 Makubaliano ya Ulinzi

Saudi Arabia na Marekani zilitia saini makubaliano ya kimkakati ya ulinzi wakati wa ziara ya Mwanamfalme Mohammed bin Salman mjini Washington, Novemba 2025.

Makubaliano hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na uwezo wa kuzuia vitisho katika Mashariki ya Kati.

Wakati wa ziara hiyo, Trump pia aliitangaza Saudi Arabia kuwa mshirika mkuu wa Marekani asiye mwanachama wa NATO.

Rubio alisema Washington inaendelea kufuatilia kwa karibu mashambulizi ya hivi karibuni nchini Saudi Arabia, huku akielezea mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati katika eneo hilo kuwa jambo la kutia wasiwasi.

Pia alikaribisha kuanza tena kwa shughuli za bomba la mafuta la Saudi Arabia lililokuwa limefungwa kwa muda baada ya mashambulizi mapema mwezi huu.

Kwa mujibu wa Rubio, miundombinu hiyo ni muhimu si kwa uchumi wa Saudi Arabia pekee, bali pia kwa biashara ya kimataifa.

Marekani Yaituhumu Iran

Katika taarifa zake, Rubio pia aliishutumu Iran kwa kuunga mkono makundi yanayolenga miundombinu ya nishati na raia katika eneo la Mashariki ya Kati.

Alisema wanamgambo wa Kishia nchini Iraq wanaoungwa mkono na Tehran huenda walihusika katika baadhi ya mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya miundombinu ya nishati.

Marekani, hata hivyo, haijaweka wazi hadharani hatua zaidi za kijeshi ambazo Trump anaweza kuchukua, huku Washington ikiendelea kusisitiza kuwa itatimiza ahadi zake za ulinzi kwa Saudi Arabia.