TBS yasisitiza upimaji bidhaa za ujenzi – HabariLeo

DAR ES SaLAAM: SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewasihi wahandisi na watumiaji wa bidhaa na malighafi za ujenzi kutumia huduma ya Upimaji wa Hiari (Type Testing) ili kujiridhisha kuhusu ubora wa bidhaa hizo kabla ya kuzitumia katika miradi ya ujenzi.

Wito huo umetolewa na Yona Afrika wa TBS wakati wa Maonesho ya Wahandisi yaliyofanyika Mlimani City, Dar es Salaam, ambapo alieleza kuwa ubora wa bidhaa na malighafi za ujenzi ni msingi muhimu wa kuhakikisha usalama, uimara na ustahimilivu wa majengo na miradi mbalimbali.

Alisema TBS inatoa huduma ya Upimaji wa Hiari (Type Testing – TT) inayowawezesha wazalishaji, waagizaji, wasambazaji na watumiaji kujiridhisha kuhusu ubora na utendaji wa bidhaa na malighafi mbalimbali kabla ya matumizi.

Kwa mujibu wa Yona, huduma hiyo inafanywa na wataalamu wenye weledi kwa kutumia maabara zenye vifaa na mitambo maalumu, huku vipimo vikizingatia viwango na taratibu zinazotambulika kitaifa na kimataifa.

Alisema matokeo ya vipimo husaidia kutoa taarifa muhimu kuhusu sifa na utendaji wa bidhaa au malighafi zinazokusudiwa kutumika, hatua inayoweza kusaidia watumiaji kufanya maamuzi sahihi kabla ya kuanza matumizi.

TBS imewataka watumiaji wa bidhaa na malighafi za ujenzi kuchukua hatua mapema kwa kupima bidhaa hizo badala ya kusubiri changamoto za ubora kujitokeza baada ya matumizi.

“Usisubiri changamoto ijitokeze ndipo uchukue hatua. Kama wewe ni mtumiaji wa bidhaa na malighafi za ujenzi, fika TBS na tumia huduma ya Type Testing ili kujiridhisha kuhusu ubora kabla ya matumizi,” alisema.

Huduma hiyo inalenga kuongeza uelewa na matumizi ya bidhaa zinazokidhi viwango, hivyo kuchangia katika ujenzi wa majengo na miradi yenye usalama, uimara na ubora unaokubalika.

Haaland Afikisha Mabao 64 Katika Mechi 56 za Norway

Global Publishers
September 25, 2026
0 views
0 Comments

Mshambuliaji wa Manchester City, Erling Haaland, ameendelea kuonyesha uwezo wake wa kufunga mabao katika soka la kimataifa baada ya kuifungia Norway mabao mawili katika ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Denmark.

Haaland alianza kuandika jina lake kwenye ubao wa matokeo dakika ya 18, kabla ya kuongeza bao la pili dakika ya 74 na kuisaidia Norway kupata ushindi katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa.

Mabao hayo mawili yameifikisha jumla ya mabao yake akiwa na timu ya taifa ya Norway kuwa 64 katika mechi 56, akifikisha wastani wa zaidi ya bao moja kwa kila mchezo.

Kwa idadi hiyo, Haaland amevuka rekodi ya mabao ya kimataifa ya mastaa wawili wakubwa wa soka duniani, Ronaldo Nazário na Zlatan Ibrahimović, ambao kila mmoja alifunga mabao 62 katika mechi za kimataifa.

Haaland pia anaendelea kufanya vizuri kwenye UEFA Nations League, akiwa amefikisha mabao 21 katika mechi 17 katika mashindano hayo.

Kwa sasa, kasi yake ya kufunga mabao akiwa na Norway imeendelea kuvutia, hasa ikizingatiwa kuwa bado ana umri wa miaka 26 na ana miaka mingi mbele ya kuendelea kuongeza idadi hiyo.

Stori na Tereza Muga | GPL -TUDACO

MITIHANI YA TAIFA YASOGEZWA KUEPUKA ATHARI ZA EL NINO

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imefanya marekebisho ya ratiba ya upimaji na mitihani ya Taifa kwa mwaka 2026, kwa lengo la kuzuia athari zinazoweza kujitokeza kutokana na uwezekano wa mvua kubwa za El Nino zinazotarajiwa katika baadhi ya maeneo nchini.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam, Septemba 25, 2026, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, amesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya Serikali kufuatilia kwa karibu taarifa za hali ya hewa na kutathmini athari zinazoweza kujitokeza katika uendeshaji wa upimaji na mitihani ya Taifa.

Amesema kwa mujibu wa utabiri rasmi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, kuna uwezekano wa kutokea kwa El Nino yenye nguvu, huku mvua zikitarajiwa kuanza katika baadhi ya maeneo mwezi Oktoba 2026 na kuwa nyingi zaidi mwezi Novemba 2026, hali ambayo inaweza kuathiri usafiri na kufikika kwa baadhi ya vituo vya mitihani.

Ameeleza kuwa kwa kuzingatia jiografia ya nchi na uwezekano wa baadhi ya maeneo kukumbwa na mafuriko, changamoto za usafiri na athari nyingine zinazoweza kusababishwa na hali ya hewa, Wizara kwa kushirikiana na Baraza la Mitihani la Tanzania imefanya marekebisho ya ratiba ya upimaji na mitihani ya Taifa.

Kwa mujibu wa ratiba iliyorekebishwa, Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Pili Ngazi ya Shule utafanyika Oktoba 7 hadi 8, 2026, wakati Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne utafanyika Oktoba 5 hadi 6, 2026.

Aidha, Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili utafanyika Oktoba 12 hadi 23, 2026, huku Mitihani ya Kidato cha Nne ikifanyika kuanzia Oktoba 19 hadi Novemba 6, 2026.

Amesema marekebisho hayo yanalenga kuhakikisha usalama wa wanafunzi, walimu, wasimamizi, maafisa na wadau wengine wanaohusika na uendeshaji wa mitihani, pamoja na kulinda mitihani, vifaa na nyaraka muhimu.

Ameongeza kuwa iwapo ratiba ya awali ingeendelea na mvua kubwa zikajitokeza mwezi Novemba 2026, changamoto zingeweza kujitokeza katika usafirishaji na ufikishaji wa mitihani, vifaa na nyaraka muhimu katika vituo, huku wanafunzi na wasimamizi wakikabiliwa na ugumu wa kufika kwa wakati kutokana na mafuriko na uharibifu wa barabara.

Wizara imeendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa hali ya hewa na kuchukua hatua stahiki kwa kushirikiana na mamlaka na taasisi husika, ili kuhakikisha upimaji na mitihani ya Taifa inafanyika kwa utaratibu unaofaa, huku usalama wa wanafunzi, walimu, wasimamizi na wadau wengine ukipewa kipaumbele.

Dk Samia atekeleza ahadi, Tarsila apokea Mil 20/- – HabariLeo

DAR ES SALAAM: BINTI aliyebuni na kutengeneza ndege nyuki (drone), Tarsila Mellita, amepokea Sh milioni 20 kutoka kwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan, fedha zilizowasilishwa na Msaidizi wa Rais Maendeleo ya Jamii, Jacqueline Kawishe.

Fedha hizo ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Rais Dk Samia wakati wa kilele cha Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nane Nane 2026 yaliyofanyika jijini Dodoma, baada ya kukagua banda la vijana aliloshiriki Tarsila wakati wa maonesho hayo.

Tarsila amebuni ndege nyuki inayotumika kusambaza viuatilifu kwenye mashamba, ubunifu unaolenga kuongeza ufanisi katika shughuli za kilimo kupitia matumizi ya teknolojia.

Binti huyo na vijana wenzake wanamiliki kampuni ya Nyika Ventures, ambayo itatumia fedha hizo kuendeleza na kuboresha teknolojia ya drone inayotengenezwa nchini.

Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuongeza matumizi ya teknolojia katika kilimo na kuwawezesha vijana kutumia ubunifu kutatua changamoto zinazowakabili wakulima na kuongeza ufanisi katika uzalishaji.
–

WANANCHI NDUNGU WAMLILIA MWANRI: “TUNATESWA NA KILIO CHA MAJI”

Ashrack Miraji Matukio Daima 

WANANCHI wa Kata ya Ndungu, Jimbo la Same Mashariki, Wilaya ya Same, Mkoa wa Kilimanjaro, wameangua kilio mbele ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Aggrey Mwanri, wakieleza namna ukosefu wa huduma ya maji safi na salama unavyowaathiri.

Wananchi hao wamesema kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji, hali inayowalazimu kutumia maji yasiyo salama kwa matumizi ya binadamu na hivyo kuongeza hofu kuhusu afya zao.

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Jana tarehe 24/9/2026 Kata ya Ndungu, mbele ya Naibu Katibu Mkuu huyo, wananchi walisema eneo hilo halina miundombinu ya kutosha ya maji, licha ya changamoto hiyo kuendelea kwa muda mrefu bila kupata ufumbuzi wa kudumu.

Walisema wamekuwa wakifikisha kilio chao kwa viongozi mbalimbali waliowahi kutembelea kata hiyo, lakini hadi sasa hawajaona suluhisho la kudumu la tatizo hilo.

Diwani wa Kata ya Ndungu alisema changamoto ya maji imekuwa ni tatizo kubwa kwa wananchi, akieleza kuwa wamekuwa wakitoa kilio hicho mara kwa mara kwa viongozi mbalimbali bila kupata majibu ya uhakika kuhusu lini tatizo hilo litapatiwa ufumbuzi.

Kutokana na hali hiyo, wananchi hao walimuomba Naibu Katibu Mkuu huyo kusaidia kufikisha kilio chao kwa Serikali ili hatua zichukuliwe za kuhakikisha wanapata huduma ya maji safi na salama.

Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Aggrey Mwanri, alikiri kupokea na kuelewa changamoto hiyo, akisema atawasilisha suala hilo kwa Waziri wa Maji, Juma Aweso, ili hatua za kulitatua ziweze kuchukuliwa.

Mwanri alisema changamoto hiyo inahitaji kufanyiwa kazi ili wananchi wa Ndungu waweze kupata huduma ya maji safi na salama, huku akieleza kuwa atahakikisha kilio hicho kinawafikia wahusika katika Serikali kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi.

Marekani Yakataa Viza ya Mkuu wa Jeshi la Sudan Mkutano wa UN

Global Publishers
September 25, 2026
0 views
0 Comments

Marekani imezuia viza ya mkuu wa jeshi la Sudan, Abdel Fattah al-Burhan, kabla ya safari yake iliyopangwa kwenda New York kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), hatua inayoongeza mvutano kati ya Washington na jeshi la Sudan.

Kwa mujibu wa Reuters, chanzo cha ngazi ya juu nchini Sudan kimesema Burhan ameahirisha safari yake kwenda New York, ingawa bado hajapokea taarifa rasmi kuhusu kukataliwa kwa viza. Serikali ya Sudan imeelezea hatua hiyo kama ukiukaji wa Mkataba wa UN na sheria za kimataifa, ikisisitiza kuwa iko tayari kwa amani.

Balozi wa Sudan katika UN amemwomba Katibu Mkuu wa Umoja huo, Antonio Guterres, kuingilia kati suala hilo. Katika barua yake, balozi huyo amesema kumzuia Burhan kuhudhuria Mkutano Mkuu wa UN kunakiuka wajibu wa Umoja huo kwa nchi wanachama.

Chanzo cha kidiplomasia cha Sudan kimeiambia Reuters kuwa maafisa wa Marekani wameweka sharti kwamba Burhan akubali kusitisha mapigano kwa siku 90 ili kuhudhuria mkutano huo.

Pendekezo hilo linahusishwa na Mshauri Mkuu wa Marekani anayehusika na Masuala ya Waarabu na Afrika, Massad Boulos. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani haikutoa maoni kuhusu viza hiyo.

Marekani imesema Jeshi la Sudan (SAF), kikosi cha Rapid Support Forces (RSF) na viongozi wao “hawawakilishi utawala halali wa kikatiba nchini Sudan.” Burhan alitarajiwa kuhutubia Mkutano Mkuu wa UN leo, lakini hotuba hiyo itatolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan, Mohieldin Salem hatua hiyo inatokea wakati vita vya Sudan vilivyoanza Aprili 2023 vikiendelea.



MHE. MBUNGE DAVID MATHAYO AMPOKEA NAIBU KATIBU MKUU BARA NDUGU AGGREY MWANRI

Same Kilimanjaro 

Mbunge wa Jimbo la Same Magharibi, Mhe. David Mathayo, amempokea Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Ndugu Aggrey Mwanri, aliyewasili katika Ofisi za CCM Wilaya ya Same kwa ajili ya kuanza ziara ya kikazi katika wilaya hiyo.

Ndugu Mwanri amewasili Same jana ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi, ambapo a alitembelea Majimbo ya Same Mashariki na Same Magharibi kwa ajili ya kukutana na viongozi, wanachama wa CCM pamoja na wananchi katika maeneo mbalimbali.

Katika ziara hiyo, Naibu Katibu Mkuu huyo  alisikiliza na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu shughuli za Chama Cha Mapinduzi, pamoja na changamoto na maendeleo ya wananchi wa Wilaya ya Same.

Ziara hiyo hili hitimishwa kwa mkutano wa hadhara, ambapo Ndugu Mwanri atazungumza na wananchi pamoja na wanachama wa CCM kuhusu masuala mbalimbali ya chama na maendeleo ya jamii.

Judith Aonyesha Gari Jipya la Sh Milioni 160, Asema “Nililipa Cash”

Mwanadada muigizaji Judith.

Muigizaji Judith amewapa mashabiki wake jambo jipya la kuzungumza baada ya kuonyesha gari lake jipya, huku akifichua kuwa gari hilo limemgharimu Sh milioni 160 na kwamba hakulinunua kwa kudunduliza fedha.

Judith ametoa ufafanuzi huo baada ya kuwapo kwa taarifa zilizokuwa zikidai kuwa gari hilo lina thamani ya Sh milioni 90. Muigizaji huyo amekanusha taarifa hizo na kusema yeye alilinunua kwa Sh milioni 160, huku akisisitiza kuwa alilipa fedha hizo taslimu.

Judith amesema mafanikio hayo ni sehemu ya matokeo ya kazi yake, akieleza kuwa amekuwa akifanya kazi kwa bidii usiku na mchana.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Judith aliweka picha za gari hilo na kuandika ujumbe huu:

“Baraka zinazovaliwa kwa uzuri. 🥷
Gari hili ni kwa ajili ya wanawake warembo pekee. 😎

Sura mpya. Moyo uleule.
Bado najifunza, bado nakua na bado nimeweka miguu yangu chini.

Kumbuka: Aina hii ya gari ni kwa ajili ya wanawake warembo tu, na si kwa wanaume 😂

Uzuri, kujiamini na kusudi — taji limevalishwa. 👑✨
Hongera kwa malkia wote wa Miss Grand! ”

Baada ya ujumbe huo, mashabiki walijitokeza kwa wingi kumpongeza Judith, huku baadhi yao wakimtania kuwa gari hilo ni mwanzo wa kupata magari makubwa zaidi.

Nana Dollz alimpongeza huku akisema: “Range Rover mwakani , mambo mengi mazuri zaidi yanakuja .”

Shabiki mwingine alitania kuhusu kauli yake ya kwamba gari hilo si la wanaume, akisema: “Naondoka na sentensi ya mwisho  ‘si kwa wanaume’. Hongera babe .”

Wengine waliendelea kumpongeza kwa ujumbe mbalimbali kama “Hongera tajiri,” “Msichana wangu,” “Hongera mama,” huku wakitumia emoji za moto na moyo kuonyesha furaha yao.

Wakati huohuo, Judith amekuwa akitajwa kwenye mitandao kufuatia tetesi za kuachana na mpenzi wake ambaye awali alikuwa akihusishwa naye.

Baadhi ya watu wamekuwa wakidai kuwa uhusiano huo umefikia mwisho, ingawa madai hayo bado ni tetesi.

Pamoja na gumzo hilo, Judith kwa sasa ameendelea kuonyesha mafanikio yake, huku gari hilo jipya likiwa miongoni mwa vitu vilivyoibua gumzo kubwa kwa mashabiki wake.

Haaland wa Moto Afikisha Goli 64 Kwenye Uzi wa Norway

Global Publishers
September 25, 2026
0 views
0 Comments

Mshambuliaji wa Manchester City na timu ya taifa ya Norway Erling Haaland, ameendelea kuweka rekodi ya kuvutia katika soka la kimataifa baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa Norway wa 3-2 dhidi ya Denmark kwenye mchezo wa UEFA Nations League.

Haaland alifunga bao lake la kwanza dakika ya 18 kabla ya kuongeza la pili dakika ya 74, na kuifanya Norway kupata ushindi katika mchezo huo wa kusisimua.

Mabao hayo mawili yameifanya rekodi yake ya kimataifa kufikia mabao 64 katika mechi 56 akiwa na timu ya taifa ya Norway, wastani wa zaidi ya bao moja kwa kila mchezo.

Kwa kufikisha mabao hayo 64, Haaland amevuka idadi ya mabao ya kimataifa iliyowahi kufungwa na Ronaldo Nazario na Zlatan Ibrahimovic, ambao kila mmoja alifunga mabao 62 katika maisha yake ya kimataifa.

Haaland pia anaendelea kuwa miongoni mwa wafungaji bora wa UEFA Nations League, akiwa tayari amefikisha mabao 21 katika mechi 17 kwenye mashindano hayo.

Kwa sasa, rekodi yake inaendelea kuvutia kutokana na kasi ambayo amekuwa akifunga mabao akiwa na Norway, huku akiwa bado ana umri wa miaka 26.

Na Tereza Muga



Rayvanny Kutumbuiza Afro Nation Portugal 2027

 

 

Msanii wa Tanzania, Rayvanny, ametangazwa kuwa miongoni mwa wasanii watakaotumbuiza katika tamasha kubwa la Afro Nation Portugal 2027, nchini Ureno.

Jina la Rayvanny limeonekana katika orodha ya kwanza ya wasanii iliyotangazwa na waandaaji wa tamasha hilo Septemba 23, 2026, hatua inayomweka tena msanii huyo wa Tanzania kwenye jukwaa kubwa la muziki wa Afrika kimataifa.

Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika kuanzia Juni 9 hadi 11, 2027, katika ufukwe wa Praia da Rocha, Portimão, nchini Portugal, likiwa na lengo la kuunganisha muziki, utamaduni na burudani kutoka Afrika na maeneo mbalimbali duniani.

Rayvanny atashiriki jukwaa hilo pamoja na baadhi ya majina makubwa katika muziki wa Afrika na kimataifa, akiwemo Davido, Rema, Fally Ipupa, Omah Lay, Victony na Shenseea.

Davido, Rema na Fally Ipupa wametajwa miongoni mwa wasanii wakuu watakaotumbuiza katika tamasha hilo.

Kwa upande wa muziki wa Amapiano, jukwaa la Piano People Stage linatarajiwa kuwakutanisha wasanii mbalimbali, akiwemo Kabza De Small, TxC na Dlala Thukzin.

Waandaaji wa Afro Nation wamesema orodha hiyo bado haijakamilika, huku wasanii wengine wakitarajiwa kutangazwa katika awamu zijazo kuelekea tamasha hilo.

Kwa Rayvanny ushiriki huo unampa nafasi ya kuwakilisha muziki wa Tanzania katika moja ya matukio ya kimataifa yanayolenga Afrobeats, Amapiano na muziki wa Afrika. Tamasha hilo limekuwa likifanyika Portugal tangu mwaka 2019 na limeendelea kuwaleta pamoja wasanii na mashabiki kutoka maeneo mbalimbali duniani.

Na Anifa Mwegelo