ASKOFU MIHALI AWATAKA WAZAZI KUENDANA NA DIRA 2050 KWA KUWEKEZA KATIKA ELIMU

 

NA MATUKIO DAIMA MEDIA IRINGA 

Askofu wa Jimbo Katoliki Iringa Romanus Elamu Mihali amewataka wazazi na walezi kuendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 kwa kuwekeza zaidi katika elimu ya watoto akisema elimu ni msingi muhimu wa maendeleo ya mtoto, familia na taifa kwa ujumla.

Askofu Mihali ametoa wito huo alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali ya Shule ya St. Dominic Savio, ambapo amesisitiza kuwa elimu ni urithi mkubwa ambao mzazi anaweza kumuachia mtoto wake.

Alisema wazazi na walezi wanapaswa kutambua umuhimu wa elimu katika kuwaandaa watoto kwa maisha ya baadaye na kuchangia katika ujenzi wa taifa.

“Ili kuendana na Dira yetu ya 2050 inayolenga malezi bora kwa vijana wetu, ningependa kuwasihi wazazi na walezi kuweza kuacha urithi wa elimu kwa watoto wao ili kusaidia kuchochea maendeleo ya Taifa kwa sababu elimu ni maisha.”

Aidha Askofu Mihali amewahimiza wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao katika Shule ya St. Dominic Savio alisema shule hiyo inatoa elimu pamoja na malezi yenye kuzingatia maadili.

Alisema mafanikio yaliyooneshwa na wanafunzi katika mahafali hayo, ikiwemo katika elimu, michezo na nidhamu, ni sehemu ya ushahidi wa ubora wa malezi na elimu inayotolewa shuleni hapo.

“Shule za St. Dominic ni shule bora na nzuri sana kwa watoto wetu Kama ambavyo wao wenyewe watakuwa wameshuhudia kwa yale yaliyotolewa kwa muhtasari katika mahafali haya  ikiwemo michezo, kauli zao na upande wa elimu inaonesha kuwa katika shule hii elimu inayotolewa ni njema na nzuri.”

Hatahivyo Mwenyekiti wa Mtaa wa Mkimbizi A, Aghata Kasisi amepongeza uongozi wa Shule za St. Dominic kwa kutoa elimu bora na malezi yanayojenga nidhamu na kujiamini kwa watoto, akisema shule hizo zimekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya elimu Manispaa ya Iringa.

“Leo nimeshuhudia mahafali ya wanafunzi  wa darasa la saba wanaomaliza masomo yao katika Shule hii nimefurahishwa na kiwango cha elimu kinachotolewa shuleni hapa pamoja na juhudi zinazofanywa na walimu katika kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa na uwezo wa kuwasiliana kwa ujasiri”

Naye Diwani wa Kata ya Gangilonga, Kenyata Likotiko  amelipongeza Kanisa Katoliki kwa uwekezaji katika sekta ya elimu kupitia shule za St. Dominic, akisema uwekezaji huo umekuwa chachu ya maendeleo ya elimu katika Manispaa ya Iringa na umeongeza imani ya wazazi katika shule hizo.

“Nampongeza Padre Ulungi kwa kutimiza miaka 30 ya huduma katika Jimbo la Iringa katika kipindi hicho amekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya elimu na jamii,kuanzia kuanzishwa na kuendelezwa kwa shule za St. Dominic ikiwemo matawi yaliyopo maeneo mbalimbali kumechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya elimu katika Manispaa ya Iringa na Mkoa wa Iringa kwa ujumla”

Aidha kwa upande wake Mchungaji  wa kanisa la kiinjilisti la kilutheri Dayosisi ya Iringa Yusto Jaffet Kinyowa  amewataka wazazi na walezi nchini kuendelea kuziamini shule  hizo  kwa kuwa ni sehemu muhimu ya kuwajengea vijana maarifa na msingi mzuri wa maisha alisema elimu inayotolewa katika shule hizo huwasaidia wanafunzi kuendeleza maarifa waliyoyapata katika elimu ya msingi na kuwaandaa kwa masomo ya juu na maisha ya baadaye.

“Shule hizi zinatoa mafunzo ya ziada yanayowajengea wanafunzi uwezo wa kuwasiliana na kujifunza lugha mbalimbali, ikiwemo lugha ya Kichina, stadi hizi ni muhimu kwa vijana katika dunia ya sasa na zinaweza kuwasaidia kupata fursa mbalimbali za kielimu na kiuchumi pia niwashukuru wazazi, walezi, walimu na wanafunzi kwa mchango wao katika kufanikisha elimu, akisisitiza kuwa kuwekeza katika elimu ya msingi na sekondari ni kuwekeza katika taifa la kesho”

Ziara ya Rais Tshisekedi kufungua ukurasa mpya wa biashara, amani

Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Felix Tshisekedi, amewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia leo Agosti 17 hadi kesho Agosti 18, 2026, ikiwa ni mara yake ya tatu kutembelea Tanzania tangu alipochaguliwa kuwa Rais mwaka 2018.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imeeleza kuwa Rais Tshisekedi atafanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan, Zanzibar, kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya nchi hizo.

Ajenda hiyo inatarajiwa kugusa biashara na uwekezaji, kilimo, madini, nishati, utalii, elimu, afya, miundombinu na usafirishaji, pamoja na amani, usalama na utangamano wa kikanda.

Ziara hiyo inafanyika wakati uhusiano wa Tanzania na DRC ukiendelea kupanuka kutoka uhusiano wa kisiasa na kihistoria hadi kwenye masuala ya uchumi, biashara na uwekezaji.

Ziara ya kwanza ya Tshisekedi Tanzania ilikuwa Juni 2019, alipofanya ziara ya kitaifa ya siku mbili kwa mwaliko wa Rais wa wakati huo, Dk John Magufuli.

Viongozi hao walijadili amani, biashara, miundombinu na ushirikiano wa kiuchumi. Tshisekedi pia alitembelea Bandari ya Dar es Salaam, ambayo ni njia muhimu ya kusafirisha mizigo kwenda DRC.

Ziara yake ya pili ilikuwa Oktoba 2022, alipokutana na Rais Samia kujadili namna ya kuongeza ushirikiano katika miundombinu, usafiri, biashara, uwekezaji, teknolojia, ulinzi na usalama, pamoja na masuala ya kijamii.

Katika ziara ya sasa, viongozi hao wanatarajiwa kutoa taarifa kwa waandishi wa habari kesho kuhusu maazimio na makubaliano yatakayofikiwa.

Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Denis Konga, amesema ziara hiyo inapaswa pia kuangazia usalama Mashariki mwa DRC na changamoto za kiafya, ikiwamo milipuko ya magonjwa, ili kuweka mazingira bora ya mwingiliano wa kibiashara.

“Kongo ni Taifa kubwa, matatizo ya kiusalama na kiafya yakishughulikiwa, fursa za kiuchumi na uwekezaji zinaweza kufunguka zaidi. Haya ni maeneo ambayo yanapaswa kuzingatiwa katika mazungumzo ya ushirikiano,” amesema.

Kwa upande wa uchumi, Tanzania imeendelea kuimarisha miundombinu inayolenga kuongeza uwezo wa kuhudumia masoko ya nchi jirani. Kwa DRC, Bandari ya Dar es Salaam, reli, barabara na miundombinu ya Ziwa Tanganyika ni muhimu katika kurahisisha usafirishaji wa bidhaa.

Takwimu zilizopo zinaonesha mauzo ya bidhaa kutoka Tanzania kwenda DRC yaliongezeka kutoka Dola milioni 150.75 za Marekani (Sh343.02 bilioni) mwaka 2018 hadi Dola milioni 312.8 (Sh749.40 bilioni) mwaka 2023.

Mtaalamu wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Hamphrey Moshi, amesema ongezeko hilo linaonesha umuhimu wa kuimarisha zaidi uhusiano wa kiuchumi baina ya nchi hizo.

Amesema Tanzania na DRC zinapaswa kuboresha mikataba ya uwekezaji, hasa katika sekta ya madini, ili kuhakikisha rasilimali zinawanufaisha wananchi.

“Siyo kuwa na sera tu, tuwe na uwezo mzuri wa kujadili na wawekezaji ili kuhakikisha nchi zetu zinanufaika na madini yetu. Hii si kwa Tanzania na Kongo tu, bali Afrika nzima tuna hili tatizo,” amesema.

Ameongeza kuwa usalama nchini DRC ni muhimu katika kuvutia uwekezaji wa kimataifa.

Wizara ya Mambo ya Nje imesema Tanzania na DRC tayari zinashirikiana katika miundombinu, nishati, utalii, elimu, afya, huduma za kifedha, biashara, uwekezaji, kilimo, maliasili na ufugaji.

Uhusiano huo pia una umuhimu kutokana na DRC kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Nchi hiyo ilikubaliwa kuwa mwanachama wa saba wa EAC Machi 29, 2022, na kuwa mwanachama kamili baada ya kuwasilisha hati ya kuridhia Mkataba wa EAC Julai 11 mwaka huo.

Kwa DRC, Tanzania ni lango muhimu la biashara kuelekea Bahari ya Hindi kupitia Bandari ya Dar es Salaam, wakati Tanzania ikinufaika na soko kubwa la DRC.

Uhusiano wa nchi hizo una historia ndefu, ukiwa umejengwa katika misingi ya ujirani, biashara, historia ya ukombozi wa Afrika na ushirikiano wa amani na usalama katika eneo la Maziwa Makuu.

Tanzania pia imekuwa ikishiriki katika juhudi za kikanda za kutafuta amani Mashariki mwa DRC, eneo ambalo limekuwa likikabiliwa na migogoro ya silaha na changamoto za kibinadamu.

SEKTA YA MADINI YAVUTIA UWEKEZAJI WA TRILIONI 9 NDANI YA MIAKA MINNE*

▪️Mikataba ya Msingi 14 ya Madini Yasainiwa

▪️Serikali yasaini Mkataba wa Bilioni 265 na Kampuni ya Henan Yudi Mining ya Mradi wa Graphite Morogoro

▪️Tanzania yawa kivutio kikubwa cha uwekezaji sekta ya Madini Afrika

▪️Rais Samia apongezwa kwa mazingira wezeshi ya uwekezaji

📍MOROGORO: 

Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema ndani ya kipindi cha Miaka Minne, (4)  Sekta ya Madini imevutia uwekezaji wa Shilingi trilioni 9, hatua inayoiweka Tanzania kuwa kivutio cha uwekezaji wa Madini Barani Afrika.

Amesema hayo leoAgosti 15, 2026, Mkoani Morogoro wakati wa hafla ya utiaji saini wa Mikataba ya Ubia wa Uchimbaji wa Madini ya Kinywe baina ya Serikali na Kampuni ya Henan Yudi Mining na kuongeza kuwa, hadi sasa tayari jumla ya mikataba ya Msingi 14 imekwisha sainiwa.

Amesema kuwa mradi huo una mashapo yaliyothibitishwa ya takribani tani milioni 104.28 za kinywe, na unatarajiwa kuwekeza takribani Dola milioni 100 (Shilingi bilioni 265) huku uzalishaji wa kiwango kamili ukilenga kufikia tani 50,000 za kinywe kwa mwaka na kwamba mradi unatakuwa na uwezo wa kuchakata tani milioni moja kwa mwaka wakati huohuo zaidi ya Watanzania 600 wakitarajiwa kupata ajira za moja kwa moja.

Mavunde amesema Serikali inaendelea kuimarisha nafasi yake katika sekta ya madini kutoka kuwa mwenyeji wa uchimbaji hadi kuwa mshiriki wa thamani inayozalishwa, ambapo katika mradi huo Serikali inamiliki asilimia 17 ya hisa.

Amesema kinywe ni madini muhimu katika teknolojia za kisasa, ikiwemo utengenezaji wa anode za betri, hivyo mradi huo una nafasi ya kuchangia katika azma ya Tanzania kushiriki zaidi kwenye mnyororo wa thamani wa kinywe duniani.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, amesema Serikali ya Wilaya inashukuru juhudi zilizofanyika kufanikisha makubaliano hayo, akieleza kuwa mradi unatarajiwa kufungua fursa za kiuchumi na ajira, kuongeza uzalishaji wa madini na kuchochea maendeleo ya sekta ya madini na uchumi wa Taifa.

Aidha, Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Chen Mingjian, amezipongeza pande zote zilizoshiriki katika majadiliano hayo, akisema mradi huo utaongeza uwekezaji wa kibiashara nchini, kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na China.

Balozi Chen amesema China ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa uwekezaji wa moja kwa moja nchini Tanzania, huku akieleza kuwa mradi huo unaongeza eneo jingine la ushirikiano wa kibiashara kati ya mataifa hayo na kufungua fursa za ajira na maendeleo ya kiuchumi kwa eneo la mradi na Taifa kwa ujumla.

VETA YAANDAA MTAALA WA MAFUNZO YA MUDA MFUPI WA FANI YA RECYCLING

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeandaa mtaala maalum wa kozi fupi za recycling kwa lengo la kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika sekta ya taka na kuongeza thamani ya taka zinazoweza kurejelewa.

Hayo yameelezwa Agosti 15, 2026 jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hussein Mohammed Omari, wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo katika Chuo cha VETA wilaya ya Bahi.

Amesema hatua hiyo imekuja baada ya tafiti kubaini kuwa baadhi ya vijana wanaojihusisha na shughuli za taka wanakabiliwa na changamoto za kiafya na kiusalama, hivyo kuhitajika kwa mtaala mahsusi utakaowawezesha kukabiliana na mazingira ya kazi.

Dkt. Omari amesema mtaala huo umeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya wadau katika mnyororo wa thamani wa taka, kuanzia ukusanyaji hadi uchakataji, kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais, sekta binafsi, vyuo vya walimu na waajiri.

Aidha, amesema VETA inaendelea kushirikiana na wataalamu wa sekta mbalimbali kuunganisha ujuzi wa vitendo na mafunzo ya vyuoni. Ametolea mfano ushirikiano na mtaalamu wa samani, Edo Sama, anayerejeleza zaidi ya asilimia 50 ya mbao zilizokuwa zikitupwa na kuzitumia kutengeneza samani, hivyo kuongeza thamani ya taka na kupunguza upotevu wa rasilimali.

Ameongeza kuwa VETA inaendelea kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi, ikiwemo kampuni ya Hans Paul ya Arusha inayotengeneza magari ya utalii, ili kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi wa vitendo. Amesema hatua hiyo inaendana na msisitizo wa Serikali wa kushirikisha sekta binafsi katika kukuza ujuzi na ajira kwa vijana.

VETA IMETAKIWA KUENDELEA KUWASHIRIKISHA WATAALAMU WALIOBOBEA FANI MBALIMBALI

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imetakiwa kuendelea kuwashirikisha wataalamu waliobobea katika fani mbalimbali zinazotolewa vyuoni, ili kuwezesha mafunzo kwa vitendo na kujenga umahiri kwa vijana.

Rai hiyo imetolewa Agosti 15, 2026 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mhe. Husna Sekiboko, akisema ushirikishwaji huo utawawezesha vijana kupata ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na jamii.

Amesema vyuo vya VETA havipaswi kujifungia kama kisiwa, wataalamu kutoka Jeshi la Zimamoto, maafisa biashara na sekta nyingine zinaweza kushirikishwa kulingana na mahitaji ya fani.

Mhe. Sekiboko ameipongeza Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi kupitia ujenzi na uimarishaji wa vyuo vya VETA, hatua inayolenga kuwawezesha vijana kupata ujuzi na fursa za ajira na kujiajiri.

Aidha, Mwenyekiti huyo amepongeza uanzishwaji wa kampuni tanzu za VETA zinazolenga kuongeza uzalishaji wa bidhaa halisi badala ya vielelezo pekee hatua itawawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo, kuongeza mapato ya vyuo na kuwajengea vijana uwezo wa kibiashara.

 

BAHI IMETENGA MILLION 100 KUTOKA MAPATO YAKE YA NDANI KUSAIDIA VIJANA WA WILAYA KUPATA ELIMU VETA

Halmashauri ya Wilaya ya Bahi imeonyesha mfano wa namna halmashauri zinavyoweza kutumia mapato ya ndani kuwekeza katika elimu ya Amali (ufundi na ufundi stadi) kuwaandalia vijana fursa za ajira kupitia Mfuko wa Elimu. Bahi inatenga shilingi milioni 100 kutoka mapato yake ya ndani kusaidia vijana wa wilaya hiyo kupata elimu na ujuzi katika Chuo cha Ufundi Stadi VETA Bahi.  

Hayo yameelezwa Agosti 15, 2026 na Katibu Tawala wa Wilaya ya Bahi, Mwanamvua Muyonga, wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo katika chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Bahi.

Amesema kati ya wanafunzi 90 waliodahiliwa chuoni hapo, 45 wanalipiwa ada na halmashauri hiyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa shughuli za Mfuko wa Elimu na juhudi za kuhakikisha vijana wanapata elimu inayowawezesha kushiriki katika shughuli za kiuchumi.  

“Halmashauri yetu haiishii kwenye kulipa ada tu, tumejenga mfumo wa kuunganisha mafunzo, uwezeshaji na fursa za kiuchumi. Kupitia ushirikiano na VETA, vijana 127 wamepatiwa mafunzo ya udereva na baadaye kuwezeshwa mikopo yenye thamani ya takribani shilingi milioni 210, pamoja na kukabidhiwa pikipiki kwa ajili ya kujiajiri,” amesema DAS Muyonga.  

Ameeleza kuwa mfumo huo pia unaonekana katika mafunzo ya muda mfupi yanayotolewa kulingana na mahitaji ya jamii, ambapo vijana wa Bahi wamepatiwa mafunzo katika fani mbalimbali ikiwemo uchomeleaji na upishi. Baadhi ya waliohitimu mafunzo ya uchomeleaji wameunda vikundi na kuanza kushiriki katika shughuli za kiuchumi.  

Aidha, juhudi hizo zimeenda sambamba na kuwaunganisha vijana wenye ujuzi na fursa za manunuzi ya umma. Baadhi ya vikundi vya vijana vilivyopata mafunzo na mikopo kutoka halmashauri vimeanza kupata kazi katika miradi inayotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, ikiwamo ujenzi wa madarasa, uchomeleaji, utengenezaji wa milango na madirisha. Hatua hiyo imewezesha fedha zinazotengwa kurejea tena katika uchumi wa eneo kupitia shughuli za uzalishaji.  

“Halmashauri ya Wilaya ya Bahi imeendelea kuwa na ushirikiano na VETA katika kuangalia mahitaji ya vijana kabla ya kuamua aina ya mafunzo yanayohitajika. Pale inapobainika kuwa kundi la vijana linahitaji ujuzi fulani, halmashauri hushirikiana na chuo kuwezesha mafunzo hayo. Tunaweza kuona kwa vijana wetu waliohitaji mafunzo ya ulishi, chuo kiliandaa mafunzo hayo kuhakikisha vijana wanapata ujuzi katika eneo hilo,” amesisitiza Muyonga.

 

*WAKULIMA WA KITOMONDO WANUFAIKA NA HUDUMA YA MAWASILIANO*

Wakulima katika Kijiji cha Kitomondo wamenufaika na kuimarika kwa huduma za mawasiliano ambayo imeondoa changamoto kubwa ya ugawaji dawa, pembejeo na upatikanaji wa masoko kupitia mfumo wa kidijitali.

 

Akizungumzia mafanikio hayo, Katibu wa Chama cha Ushirika – Kitomondo (AMCOS) Yusuf Mansouri amesema hapo awali walikuwa wanapata changamoto kubwa kwa wakulima kuchelewa kupata huduma lakini baada ya Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kuwawezesha mnara wa mawasiliana changamoto hizo zimemalizika.

Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imetekeleza mradi wa ujenzi wa Minara 768 ya kimkakati ya mawasiliano wenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa huduma ya mawasiliano kwa wananchi waishio yasiyo maeneo machache ya mjini na vijijini yenye yasiyo na mvuto wa kibiashara kwa watoa huduma.

 

DCEA YATEKETEZA EKARI 603 ZA BANGI MVOMERO

 

Matukio Daima Media, Morogoro

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeteketeza ekari 603 za mashamba ya bangi na kukamata magunia 49 ya bangi katika operesheni maalum iliyofanyika Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro, huku watuhumiwa 13 wakikamatwa  kuhusisiana na mashamba hayo. 

Operesheni hiyo iliyofanyika katika vijiji vya Misengele, Lugenge, Kisaki na Nyarutanga, pia ilibaini na kuharibu kambi 21 zilizokuwa zikitumiwa na wakulima wa bangi.

Akizungumza kuhusu operesheni hiyo, Kamishna Jenerali wa DCEA Aretas Lyimo, amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati endelevu wa Serikali wa kudhibiti uzalishaji wa dawa za kulevya nchini, hususan bangi, ambayo imeendelea kuzalishwa katika baadhi ya maeneo ya nchi.

Amesema operesheni hizo zimebaini mabadiliko katika mbinu zinazotumiwa na baadhi ya wakulima wa bangi, ambapo wanahamisha shughuli zao kutoka maeneo yaliyofikiwa na operesheni na kuingia ndani zaidi ya maeneo ya hifadhi.

“Tumebaini kuwa baadhi ya wakulima wamehamishia shughuli zao ndani zaidi ya maeneo ya hifadhi ili kukwepa hatua za kisheria. Hali hii inachangia uharibifu mkubwa wa mazingira kupitia ukataji wa miti ovyo, uvamizi wa vyanzo vya maji na kuathiri mfumo wa ikolojia,” amesema Lyimo.

Kwa mujibu wa Lyimo, tathmini ya operesheni zilizotekelezwa na DCEA tangu mwaka 2023 imeonyesha kuwa, licha ya mashamba mengi ya bangi kubainika na kuteketezwa katika Mkoa wa Morogoro, baadhi ya wahusika wameendelea kubadilisha maeneo ya uzalishaji na kujificha ndani ya maeneo ya hifadhi.

Amesema hali hiyo inahitaji ushirikiano wa karibu zaidi kati ya DCEA, vyombo vya ulinzi na usalama, mamlaka zinazosimamia maeneo ya hifadhi na wananchi ili kuzuia maeneo hayo kutumiwa kwa uzalishaji wa dawa za kulevya.

Lyimo amewataka wasimamizi wa maeneo ya hifadhi kuhakikisha maeneo wanayoyasimamia hayatumiki kwa kilimo cha bangi, akisisitiza kuwa mapambano dhidi ya uzalishaji wa dawa za kulevya yanahitaji ushirikiano wa taasisi na jamii.

DCE itaendelea kufanya operesheni jumuishi katika maeneo mbalimbali nchini kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, mamlaka za uhifadhi na wananchi ili kudhibiti kilimo na biashara haramu ya bangi.

Sambamba operesheni hizo, Lyimo amesema Mamlaka itaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya dawa za kulevya na kuhamasisha wananchi kutoa taarifa kuhusu watu wanaojihusisha na uzalishaji, usafirishaji na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Kinachosubiriwa Ijumaa kesi ya Lissu

Dar es Salaam. Hatima ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, katika kesi ya uhaini inayomkabili imeingia katika hatua muhimu, baada ya Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam kupanga Ijumaa, Agosti 21, 2026, kutoa uamuzi mdogo wa kubaini kama ana kesi ya kujibu au la.

Uamuzi huo unakuja baada ya upande wa Jamhuri kufunga ushahidi wake jana Jumatatu, Agosti 17, baada ya kuwaita mashahidi 17 kati ya 30 walioorodheshwa.

Lissu, anafikisha siku 495 akiwa kizuizini hadi leo Agosti 17, 2026, alikamatwa Aprili 9, 2025 katika Wilaya ya Mbinga, Mkoa wa Ruvuma, kwenye mkutano wa hadhara wa Chadema.

Kesi hiyo inatokana na shtaka moja la uhaini chini ya Kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, likihusishwa na maneno aliyodaiwa kuyatamka Aprili 3, 2025 kuhusu kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Leo Agosti 17, 2026 Jamhuri imeeleza haitaita mashahidi   wote 30 waliokuwa kwenye orodha ikifafanua kuwa baada ya kupitia ushahidi uliowasilishwa na kuangalia wa mashahidi waliobaki, umeona uliopo unatosheleza. Hivyo uamuzi wa Agosti 21, 2026 utakaoweka mwelekeo wa hatua inayofuata.

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, akizungumza na wafuasi wa chama hicho waliojitokeza katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo, Agosti 17, 2026, kufuatilia kesi ya uhaini inayomkabili. Picha na Said Powa

Iwapo mahakama itaona Jamhuri imefeli kujenga kesi, Lissu hatalazimika kuingia katika hatua ya kujitetea na anaweza kuachiwa kwa mujibu wa uamuzi wa mahakama. Lakini iwapo majaji wataona kuna ushahidi unaomtaka ajibu mashtaka, kesi itaingia katika hatua ya utetezi na Lissu atalazimika kujibu ushahidi uliowasilishwa dhidi yake.

Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu, Dunstan Ndunguru, James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.

Safari ya Lissu mahakamani

Katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja akiwa mahabusu, Lissu amekutana na vikwazo kadhaa vya kisheria, huku baadhi ya mapingamizi yake yakikubaliwa na mengine yakitupiliwa mbali.

Miongoni mwa hatua kubwa ilikuwa Septemba 22, 2025, Mahakama Kuu ilipotupilia mbali mapingamizi yake kuhusu uhalali wa hati ya mashtaka.

Mahakama ilisema hati hiyo ilikuwa inakidhi matakwa ya kisheria, huku suala la nia ya kutenda uhaini likielezwa kuwa ni jambo la ushahidi litakaloamuliwa wakati wa usikilizwaji wa kesi.

Oktoba 2025, Lissu aliwasilisha mapingamizi manne kupinga kupokelewa kwa vielelezo vya video na vifaa vya kuhifadhia taarifa vilivyowasilishwa na upande wa Jamhuri.

Baadaye, katika hatua nyingine ya kesi, aliwasilisha mapingamizi matano kuhusu masuala yanayohusiana na shahidi wa siri na kizimba kilichotengenezwa mahakamani kwa ajili ya mashahidi hao.

Februari 11, 2026, Mahakama Kuu ilitupilia mbali mapingamizi manne kati ya matano, lakini ikakubali moja lililohusu kizimba cha shahidi wa siri.

Mahakama iliamuru kifanyiwe marekebisho ili majaji waweze kumuona shahidi wakati akitoa ushahidi.

Kwa maana hiyo, katika hatua hizo mbili zinazojulikana wazi, Lissu aliwasilisha jumla ya mapingamizi tisa, ingawa si yote yalikuwa na mada moja.

Kati ya mapingamizi hayo, mahakama ilikubali mawili huku moja likihusu kielelezo cha video na jingine kuhusu kizimba cha shahidi wa siri, wakati mengine yalitupwa.

Katika hoja zake Lissu ameieleza mahakama hiyo kuwa Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki iliweka msingi wa uthibitishaji wa kosa la uhani ili mshtakiwa awe na kesi ya kujibu kupitia kesi za Grey Likungu Mataka na wenzake dhidi ya Jamhuri na  Hatibu Gandhi na wenzake dhidi ya Jamhuri.

Amesema kuwa mahakama hiyo iliweka masharti matatu ambayo ni mshtakiwa awe na utiifu kwa Jamhuri ya Muungano, nia ya kutenda kosa la uhaini, uthibitisho wa nia hiyo kwa maandishi au kwa matendo ya wazi.

Mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, akiwasili katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo, Agosti 17, 2026, kufuatilia kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu. Picha na Said Powa.

Pia, amedai kuwa mahakama hiyo ilisema maneno matupu hayatengenezi kosa la uhaini isipokuwa kama yataendana na kosa la uhaini, hata hivyo msimamo huo unatumika pale ambapo mshtakiwa wa uhaini ni mmoja.

Kuhusu utiifu amesema kuwa halina mjadala kwani ni  raia wa Tanzania.

Ameeleza kuwa kosa linalotajwa katika kifungu anachoshtakiwa ni kuitishia Serikali, Bunge au Mahakama na lazima nia hiyo idhihirishwe kwa kuchapisha maandishi au kwa kuonesha matendo ya wazi ni kosa la uhaini.

Amesema kuwa kwa kurejea hati ya mashtaka maneno aliyoyatamka ya kuzuia uchaguzi si miongoni mwa makosa  kwa mujibu wa kifungu hicho cha  Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2025 au sheria yoyote nchini.

Amesisitiza kuwa katika maneno hayo hakuna mahali alikotamka Serikali, Bunge wala mahakama, rais, waziri mkuu au mkuu wa mkoa lakini mashahidi hawakuthibitisha akisisitiza kuwa uchaguzi husimamiwa na Tume ya Uchaguzi na si Serikali.

Kuhusu kuchapisha au kuonesha  matendo ya wazi, amedai kuwa Jamhuri haikuweza kuthibitisha kuwa ni yeye aliyechapisha maneno hayo kwenye mtandao wa Youtube wa  Jambo TV na   hata hiyo video hawakuiwasilisha mahakamani.

Badala yake amesema kuwa shahidi wa 17 ambaye ndiye alikuwepo katika mkutano wake alieleza kuwa yeye, shahidi huyo na wenzake watano ndio waliorekodi na kuchapisha video hiyo.

“Kwa hiyo kudhihirisha nia ya uhaini kama ilivyowekwa kwenye  kesi ya Grey na Gandhi haupo na hakuna ushahidi wa nia ya kutenda kosa lolote kwa mujibu wa sheria za Tanzania zinazojulikana”, amesema Lissu.

Amesisitiza kuwa ameshtakiwa kwa kosa lisilokuwepo kisheria kwa mujibu wa Sheria za Uchaguzi na kwamba amekaa gerezani kwa siku 496 kwa kitendo ambacho si kosa la uhaini wala kosa kwa mujibu wa sheria yoyote nchini bali kwa mashtaka ya uonevu na ya kijinga.

Hivyo, ameiomba mahakama iamuru alipwe fidia kwa uonevu huo wa kukaa gerezani kwa muda wote huo kwa mujibu wa kifungu cha 367 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Jamhuri katika hoja zake kupitia Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, ameieleza mahakama kuwa kwa kuzingatia ushahidi uliowasilishwa wamethibitisha viini vyote vya kosa la uhaini na kwamba kwa mshtakiwa anapaswa kujitetea.

“Sisi Jamhuri tunaona mshtakiwa ana kesi ya kujibu katika mashtaka alivyoshtakiwa nayo chini ya kifungu  cha 39(2) (d) cha Penal code.

Akichambua hati ya mashtaka, Katuga alidai kuwa kiini cha kwanza cha nia ya kutenda kosa mshtakiwa huyo ni kwamba yeye ni raia wa Tanzania,  anawajibu wa kutii sheria kwa mujibu wa katika ya Muungano wa Tanzania, kiini hicho kina thibitisha kuwa mshtakiwa anakiri kuwa yeye ni Mtanzania.

Baadhi ya wanachama na wafuasi wa Chadema wakifanya maombi ndani ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo, Agosti 17, 2026, kabla ya kuanza kwa usikilizwaji wa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu. Picha na Said Powa.

Kiini cha pili, cha nia ya uhaini amesema kuwa maneno aliyoyasema  mshtakiwa ya kukinukisha na kuvuruga uchaguzi yalilenga kuchochea umma  kwa nia ya kuitishia Serikali.

Alidai kiini hicho kimedhibitisha na shahidi wa kwanza, wa 16 na wa tatu, ambapo kwa pamoja walisema maneno ya mshtakiwa ya kwamba watavuruga uchaguzi, yalitishia Serikali kwani ndio ina jukumu la kulinda sheria.

Amesisitiza kuwa kuitishia Serikali lazima mpaka iwe imetishika bali hata kuonesha nia hiyo ni kosa la uhaini chini ya kifungu hicho.

“Tunaomba mahakama ione ushahidi ulitolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka, mshtakiwa anao wajibu wa kujitetea, hivyo anatakiwa aletwe mahakamani kwa ajili ya kujitetea,” amesema  Katuga

Kuhusu ombi la mshtakiwa kulipwa fidia, amesema kuwa hoja hiyo hawataijibu kwa sasa mpaka ambapo Mahakama itamkuta na kesi ya kujibu.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote Jaji Ndunguru amesema kwa kuwa mashahidi ni wengi na hoja ni nyingi wanahitaji kupata muda wa kupitia ushahidi na hoja hizo na Mahakama itatoa uamuzi wake Agosti 21, 2026.