
Habari Mpya Kilasiku
Naibu Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko amesema kuwa mashindano ya ngalawa race ni miongoni mwa matukio makubwa ya kiburudani yanayoipamba Kizimkazi Festival 2026.
Mashindano hayo yamefanyika Kizimkazi, Kusini Unguja Agosti 12, 2026 yaliyokuwa na ushindani mkubwa ambapo Nassor Pandu wa Mkunguni ameibuka mshindi wa mashindano ya ngalawa ikiwa ni sehemu ya shughuli mbalimbali zinazoendelea katika Tamasha la Kizimkazi.
“ Ni dhahiri kwamba mashindano haya yamekuwa muhimu kwa vijana na jamii kwa ujumla. Tukio hili limewaleta pamoja wadau mbalimbali na kuchangia kwa kiasi kikubwa juhudi za kuboresha mazingira ya michezo na burudani,” amesema Dkt. Biteko.
Dkt. Biteko ameongeza kuwa mashindano ya Ngalawa race Kizimkazi Festival yameendelea kutoa fursa za kiuchumi kwa vijana mbalimbali katika kushindana hadi kupata timu mbili bora za Mchangamle na Mkunguni ambapo kila timu imehusisha manahodha 10.
Mwisho.
Na Matukio Matukio Daima Media
WANANACHI Mkoani Mtwara wameishukuru Serikali kwa kuendelea kujenga na kuboresha miundombinu ya huduma za afya, hatua iliyowarahisishia upatikanaji wa huduma hizo bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.
Hayo yamejiri, katika siku ya tatu ya ziara ya kikazi ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), mkoani humo, yenye lengo la kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita.
Wananchi hao wamesema wanapata huduma za afya kwa wakati na kwa urahisi, jambo walilolieleza kuwa limepunguza changamoto ya kufuata matibabu katika maeneo ya mbali.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Waziri Kapinga amesema Serikali inalenga kuboresha huduma za afya ili wananchi wapate matibabu kwa urahisi na kuendelea na shughuli zao za uzalishaji, hivyo kuimarisha uchumi wa familia na Taifa.
Amesema kusogeza huduma za afya karibu na wananchi ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu kwa wakati.
Aidha, amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akisisitiza kuwa ushirikiano ni msingi wa maendeleo.
Katika siku ya tatu ya ziara hiyo, Waziri Kapinga ametembelea miradi mbalimbali katika Majimbo ya Nanyamba, Mtwara Mjini na Mtwara Vijijini, ikiwemo kuzindua Kituo cha Afya Msangamkuu, kuzindua mabweni mawili na kutoa taulo za kike kwa wanafunzi wa Shule ya Wasichana Mtwara, kukagua ujenzi wa Shule ya Amali Chikota, pamoja na kutembelea Wodi ya Wazazi katika Hospitali ya Wilaya ya Tandahimba.
Elisante John, Singida,
Hatua ya Serikali kupanua Uwanja wa Ndege wa Singida imeibua ombi kutoka kwa wananchi, kuondolewa kwenye maeneo yao, wakiomba thamani ya ardhi inayotumika katika fidia, ipandishwe kutoka Sh. 8,000 hadi Sh.10,000, kwa mita ya mraba.
Mthamini wa Ardhi Mkoa wa Singida, Zablon Mwalyasi, amesema upanuzi huo unahusisha kuongeza ekari 316.6 kutoka maeneo ya wananchi yaliyo pembezoni mwa uwanja. Amesema lengo ni kuboresha huduma za usafiri wa anga, kwa kuwa uwanja uliopo hautoshelezi mahitaji ya sasa.
Mwalyasi amesema kila mwananchi atakayepitiwa na zoezi hilo atalipwa fidia kwa kuzingatia thamani halisi ya ardhi na mali zilizopo. Amesema mali hizo ni pamoja na majengo, miti na maendeleo mengine yanayotambuliwa kisheria.
Ameongeza kuwa wananchi watastahili pia posho mbalimbali, ikiwamo ya usumbufu, makazi, upangaji na gharama za kuhamisha mali. Amewataka wananchi kuwa wazi wakati wa uthamini na kuwaruhusu wataalamu kukagua mali zote ili kuhakikisha thamani halisi inapatikana.
Baadhi ya wananchi, akiwamo Charles Rwegoshora, Shabani Nyuda, Karani Kisuke, Hassan Irunde na Diwani wa Kata ya Mandewa, Yusufu Makera, wameomba thamani hiyo ipandishwe kutoka Sh. 8,000 hadi Sh10,000, kwa mita ya mraba. Mwalyasi amesema atalifikisha ombi hilo kwa mamlaka husika kwa ajili ya uamuzi.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Singida, Bornege Tatwebwa, amesema upanuzi wa uwanja huo utaongeza fursa za usafiri wa anga na kuchochea maendeleo ya kiuchumi. Pia amewapongeza wananchi kwa ushirikiano wanaouonesha katika kuunga mkono zoezi hilo.
Na Matukio Daima Media
NAIBU Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Salome Makamba, amehimiza umma kupata taarifa sahihi kuhusu hali ya sekta ndogo ya umeme nchini, huku akitoa wito kwa Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuendelea kutoa elimu na taarifa kwa wananchi kuhusu jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kuboresha huduma za umeme.
Mhe. Makamba ametoa wito huo leo, tarehe 13 Agosti 2026, alipotembelea banda la EWURA katika Maonesho ya Kizimkazi yanayoendelea katika Viwanja vya Dimbani, Kizimkazi, Zanzibar.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, amesema ni muhimu wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu kuongezeka kwa uzalishaji na upatikanaji wa umeme nchini na hivyo kukidhi mahitaji tuliyonayo.
“Gharama ya umeme nchini Tanzania ni nafuu ikilinganishwa na nchi jirani, na Serikali inaendelea na juhudi za kuboresha na kuimarisha miundombinu ya umeme ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa uhakika, hatua itakayochochea maendeleo ya kiuchumi nchini,” aliongeza.
Katika banda la EWURA, Mhe. Makamba alifahamishwa Mamlaka imetumia fursa ya Maonesho hayo kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya udhibiti ikiwemo mikataba ya huduma kwa wateja, matumizi sahihi na salama ya huduma za bidhaa za gesi ya mitungi, gesi asilia, umeme na maji, fursa za uwekezaji katika sekta na mengineyo.
Serikali wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, imemuokoa mtoto mwenye umri wa miaka 10, jina limehifadhiwa, aliyekuwa ameachishwa shule na familia yake na kupelekwa kwa mwanaume kwa lengo la kumuozesha.
Mtoto huyo, mwanafunzi wa Darasa la Pili katika Shule ya Msingi Jiungeni, iliyopo Kata ya Ruvu wilayani Same, aliokolewa baada ya Serikali kupata taarifa kutoka kwa raia mwema kuhusu tukio hilo.
Akizungumza Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, alisema baada ya kupokea taarifa hiyo alielekeza maafisa wa Serikali kufanya uchunguzi, ambapo walibaini kuwa mtoto huyo alikuwa akiishi na kijana anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 18 na 20 katika mazingira ya ndoa.
“Serikali inalaani vikali kitendo hiki cha kikatili cha kumnyima mtoto haki zake za msingi, ikiwemo haki ya kupata elimu na kukua katika mazingira salama,” alisema Kasilda.
Alisema watuhumiwa wamefikishwa mikononi mwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa ajili ya hatua za kisheria, huku akiwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa Serikali kuhusu vitendo vya aina hiyo.
Aidha, Kasilda alisema Shule ya Msingi Jiungeni ilijengwa mahususi kusaidia watoto kutoka jamii ya wafugaji wanaoishi katika eneo hilo kupata elimu.
Alisema kuna uwezekano wa kuwepo kwa wanafunzi wengine walioacha shule kutokana na ndoa za utotoni au kwenda kuchunga mifugo, hivyo Serikali itaendelea kufanya ufuatiliaji kuhakikisha watoto wote wanapata haki yao ya elimu.
“Msimamo wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha watoto wanakwenda shule na sisi tutapambana na wazazi wanaokiuka maelekezo ya Serikali,” alisema.
Kasilda aliwapongeza maafisa wa Serikali pamoja na wananchi waliofanikisha zoezi la kumuokoa mtoto huyo, akisema walilazimika kufanya uchunguzi katika mazingira magumu ya porini ambako mtoto huyo alikuwa akiishi na kijana huyo.
Pia aliwaonya watu wanaojaribu kutoa rushwa kwa lengo la kuwaachia watuhumiwa, akisema watakaobainika kufanya hivyo watakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Alisema vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kufuatilia suala hilo kwa karibu na kwamba Serikali haitamvumilia mtu yeyote anayehatarisha usalama, elimu na ustawi wa watoto.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema mtoto huyo atarejeshwa shuleni ili kuendelea na masomo yake.
Ndoa za utotoni zinaweza kuwanyima watoto fursa ya kupata elimu na kuwaweka katika mazingira hatarishi ya ukatili na unyanyasaji, pamoja na changamoto za kiafya na kisaikolojia.
Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa jamii kulinda haki za watoto, kuhakikisha wanapata elimu na kukua katika mazingira salama yanayozingatia maslahi na mustakabali wao.
NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA.
KAMPUNI ya VEROTAS PLUMBING imeendelea kutoa suluhisho katika ujenzi na uboreshaji wa mifumo ya maji kwa wananchi, kwa kutoa bidhaa zenye ubora zinazolenga kuhakikisha mifumo hiyo inakuwa safi, salama na yenye kudumu.
Huduma hiyo inalenga kuwasaidia wananchi kupata mifumo bora ya maji katika maeneo mbalimbali, ikiwemo majumbani, maliwatoni na kwenye majengo ya biashara, huku wakizingatia matumizi ya bidhaa zinazokidhi viwango vya ubora.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa VEROTAS PLUMBING, Veronica Mwita, amesema kampuni hiyo imejikita katika kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa na huduma zinazowawezesha kuwa na mifumo bora ya maji katika mazingira yao.
Amesema matumizi ya bidhaa bora katika mfumo wa maji ni muhimu katika kuhakikisha maji yanapitishwa katika mazingira salama, huku yakipunguza changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya vifaa visivyo na ubora.
“Tunatoa suluhisho kwenye mifumo ya maji kwa kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa zenye ubora ambazo zitawasaidia kuwa na mfumo mzuri, salama na wa kudumu. Tunazingatia mahitaji ya wananchi kuanzia kwenye maliwato hadi kwenye mfumo mzima wa maji wa nyumba,” amesema Mwita.
Aidha, amesema VEROTAS PLUMBING inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuchagua bidhaa sahihi wakati wa kujenga au kuboresha mifumo ya maji, ili kuepuka gharama zinazoweza kujitokeza kutokana na uharibifu wa mifumo.
Amesema wananchi wanapaswa kuzingatia ubora wa bidhaa wanazonunua na kuhakikisha zinafaa kwa matumizi yanayokusudiwa, kwani mfumo bora wa maji una mchango mkubwa katika usafi, afya na ustawi wa familia.
VEROTAS PLUMBING imeendelea kuwahimiza wananchi wanaojenga nyumba mpya au kufanya maboresho katika nyumba zao kutumia wataalamu na bidhaa bora ili kuhakikisha mifumo ya maji inakuwa salama, imara na yenye kudumu kwa muda mrefu.
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na Kituo cha Umahiri cha Afya Moja (SACIDS Foundation for One Health) na wadau wengine wa utafiti, imeendelea kuimarisha juhudi za kuhakikisha matokeo ya tafiti yanawafikia wananchi na watumiaji wa mwisho. Hayo yameelezwa wakati wa Warsha ya Mkakati wa Ushirikishwaji wa Utafiti ya Vigoda vya Utafiti vya OR. Tambo, iliyofanyika SUA, Morogoro, 13 Agosti, 2026 ikilenga kuwajengea watafiti uwezo wa kuwasilisha kwa ufanisi tafiti zao ili kuongeza athari zake katika jamii.
Akizungumza katika warsha hiyo, Prof. Gerald Misinzo, Mwenyekiti wa Kigoda cha Utafiti Barani Afrika cha OR Tambo cha Magonjwa ya Kuambukiza ya virus, amesema mawasiliano ya kisayansi ni nyenzo muhimu katika kubadilisha matokeo ya utafiti kuwa maarifa yanayoeleweka na kutumika katika jamii. Amesema watafiti wanapaswa kuwasilisha taarifa za kisayansi kwa lugha na njia zinazolingana na mahitaji ya walengwa, ili kuongeza uelewa, ushiriki na matumizi ya matokeo ya tafiti.
Prof. Misinzo amesema tafiti zinazofanywa na Kigoda hicho kwa kushirikiana na SACIDS na wadau wengine zinahusu magonjwa mbalimbali yanayoathiri wanyama na binadamu, yakiwemo homa ya nguruwe ya Afrika, Newcastle na magonjwa ya samaki. Amesema ni muhimu matokeo ya tafiti hizo kuwafikia wafugaji, wataalamu, watunga sera na wananchi kwa wakati, ili kusaidia kuchukua hatua stahiki na kupunguza madhara ya milipuko ya magonjwa.
Aidha, Prof. Misinzo amesisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia na majukwaa mbalimbali ya mawasiliano katika kufikisha taarifa za utafiti kwa hadhira pana. Amesema mawasiliano ya kisayansi yanapofanyika kwa ubunifu na kuzingatia mahitaji ya walengwa, yanaweza kuongeza uelewa wa jamii, kuimarisha ushirikiano na kujenga uaminifu katika taarifa za kisayansi.
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam wa SUA, Prof. Maulid Mwatawala, amesema utafiti haupaswi kuishia katika machapisho ya kitaaluma pekee, bali unapaswa kuwafikia watumiaji wa mwisho. Amesema mafunzo ya mawasiliano ya kisayansi ni muhimu katika kuwajengea watafiti uwezo wa kueleza matokeo ya tafiti kwa lugha rahisi na inayoeleweka, kushirikisha wadau na kuhakikisha utafiti unaleta suluhisho na mchango chanya katika maendeleo ya jamii.