Israel Yaamuru Ubalozi Mdogo wa Uingereza Jerusalem Kufungwa

Global Publishers
September 9, 2026
84 views
0 Comments

Israel imeuambia ubalozi mdogo wa Uingereza uliopo Jerusalem Mashariki kwamba unatakiwa kufungwa, huku wanadiplomasia waliopangiwa katika eneo hilo wakitarajiwa kupoteza vibali vyao ndani ya siku 30.

Kwa mujibu wa afisa wa Israel na chanzo kinachofahamu suala hilo, wawakilishi wa Uingereza waliopangiwa katika ujumbe wa kuratibu masuala ya Gaza unaoongozwa na Marekani nchini Israel, pamoja na wanadiplomasia wa Uingereza walioko Ramallah, wanatakiwa kuondoka ndani ya siku saba.

Hatua hiyo imekuja baada ya Israel Jumanne kuamuru kufungwa kwa ubalozi mdogo wa Uingereza mjini Jerusalem, ikiwa ni hatua ya kulipiza kisasi kufuatia Uingereza kuongoza vikwazo vilivyowekwa na mataifa ya Magharibi dhidi ya baadhi ya walowezi wa Israel wanaotuhumiwa kufanya vitendo vya vurugu dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Uamuzi huo umeongeza mvutano wa kidiplomasia kati ya Israel na Uingereza kuhusu sera za Israel katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na hali ya usalama katika Ukingo wa Magharibi.

Mtanzania Neema Kengere Arejeshwa Tanzania Leo Kutoka Oman – Video

Global Publishers
September 9, 2026
6 views
0 Comments

Mtanzania Neema Anthony Kengere, aliyekuwa amelazwa katika Wodi ya Wagonjwa Mahututi (ICU) katika Hospitali ya Sohar nchini Oman, anatarajiwa kurejeshwa Tanzania leo, Septemba 9, 2026, kwa ajili ya kuendelea na matibabu.

Neema alipata matatizo ya kiafya akiwa nchini Oman, alikokwenda kufanya kazi. Hali yake ilizidi kuwa mbaya hadi kulazwa katika ICU akiwa hajitambui.

Jitihada za kuhakikisha Neema anarudishwa nchini zimefanywa kwa ushirikiano wa Ubalozi wa Tanzania nchini Oman, huku mtangazaji wa Kipindi cha Mapito, @zali_mapito, akisafiri hadi Oman kujionea hali ya Mtanzania huyo na kufuatilia hatua za kurejeshwa kwake nyumbani.

Safari hiyo imewezesha kukamilika kwa taratibu muhimu za kumsafirisha Neema kurejea Tanzania, kama ilivyokuwa ombi la familia yake.

Baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, Neema atapelekwa moja kwa moja katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kuendelea na matibabu.

Hospitali ya Taifa Muhimbili tayari imethibitisha kuwa imeandaa taratibu zote muhimu za kumpokea mgonjwa huyo. Gari la wagonjwa, daktari pamoja na nesi watakuwa wakimsubiri uwanjani ili kumpokea na kumpeleka hospitalini kwa haraka kwa ajili ya kupata huduma zaidi.

Taarifa zaidi kuhusu hali ya Neema na hatua zinazofuata zitakujia kupitia Global TV.

Stori na  ZALI MAPITO, GPL

KUPIGA KURA ZA SKA2026 KUIPATIA USHINDI MATUKIO DAIMA MEDIA BONYEZA HAPA

 

KUPIGA KURA KWA TOVUTI BONYEZA HAPA KISHA PIGIA KURA TUZO ZOTE NNE

 MATUKIO DAIMA MEDIA IMETEULIWA KUWANIA TUZO ZA SAMIA KALAMU AWARDS (SKA2026) TUNAOMBA KURA YAKO WAWEZA KUPIGA KURA KILA BAADA YA MASAA 24 UNARUDIA KUPIGA KURA  NA UNAWEZA KUPIGA KWA LINK KUINGIA KWENYE TOVUTI HAPO KUU AMA KUPIGA KAWAIDA KUPITIA UJUMBE MFUPI KAMA INAVYOELEKEZA KWENYE POSTA HAPO JUU ZOEZI LITAFUNGWA SEPT 30

Job na Mzize Kuongeza Nguvu Yanga Baada ya Kufanyiwa Vipimo Afrika Kusini

Global Publishers
September 9, 2026
24 views
0 Comments

Beki wa kati ndani ya kikosi cha Yanga SC, Dickson Job na mshambuliaji Clement Mzize wanatarajiwa kurejea uwanjani hivi karibuni baada ya kufanyiwa vipimo nchini Afrika Kusini.

Wachezaji hao wa Yanga SC walikosekana kwenye mechi 5 za ligi 2026/27 kutokana na kutokuwa fiti tayari walianza mazoezi chini ya uangalizi wajopo la madaktari la Yanga SC. Nyota hao walikosekana kwenye mchezo dhidi ya Gaborone United walipotoshana nguvu kwa kufungana 1-1 Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ali Kamwe, Menej awa Idara ya Habari na Mawasiliano Yanga SC amesema wachezaji hao tayari wamefanyiwa vipimo wanajiandaa kurejea uwanjani kuendelea na majukumu ya kazi.

“Kuna habari njema kutoka kwa wataalamu wetu wa masuala ya kitabibu wanasema kuwa wachezaji wetu Dickson Job na Clement Mzize, ambao walisafiri kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya vipimo, wapo salama na wanajiandaa kurejea uwanjani.

“Kimsingi, wachezaji hawa wawili ni kama usajili mpya kwetu, wale ambao mmecheza na Yanga na hamkukutana na Clement Mzize Bull Striker basi niwaambie tu kwamba Mzize na Job wamerudi,” alisema Kamwe.

Yanga SC kwenye msimamo wa ligi inaongoza ikiwa na pointi 15 baada ya kucheza mechi 5 imeshinda zote msimu wa 2026/27. Mchezo wa kwanza ilipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Namungo FC.

Mchezo ujao kwa Yanga SC ni dhidi ya Gaborone United ya Botswana mechi ya  mkondo wa pili Ligi ya Mabingwa Afrika unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Azam Complex, Septemba 12, 2026 saa 1:00 usiku umepewa jina la Sele Day mfungaji wa bao pekee dhidi ya Gaborone, ugenini.

Stori na Lunyamadizo Mlyuka | GPL

Kesi ya Lissu Yaendelea, Upande wa Utetezi Kuwasilisha Ushahidi

Global Publishers
September 9, 2026
42 views
0 Comments

Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, inaendelea leo, Septemba 9, 2026, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, huku upande wa utetezi ukiendelea kuwasilisha ushahidi.

Kesi hiyo imefikia hatua hiyo baada ya Mahakama Kuu kuamua kuwa Lissu ana kesi ya kujibu, hivyo kuufungulia upande wa utetezi nafasi ya kuanza kutoa ushahidi wake.

Katika hatua ya hivi karibuni, shahidi wa utetezi, Brenda Rupia, ameendelea kutoa ushahidi na kujibu maswali kutoka upande wa Jamhuri.

Usikilizwaji wa kesi hiyo umeendelea kwa siku kadhaa, huku Mahakama ikiongeza muda wa kusikiliza shauri hilo kwa siku 14.

Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini linalohusishwa na kauli anazodaiwa kutoa katika mkutano wa CHADEMA mwaka 2025 kuhusu uchaguzi mkuu.

 



Madrid, Man City Zaanza kwa Kishindo UEFA Halland Akitupia Mawili

Global Publishers
September 9, 2026
0 views
0 Comments

Mzunguko wa kwanza wa hatua ya ligi ya UEFA Champions League msimu wa 2026/27 umeanza kwa michezo yenye ushindani mkubwa, huku baadhi ya vigogo wa soka barani Ulaya wakianza kampeni zao kwa ushindi.

Katika michezo iliyochezwa jana usiku, Manchester City ilianza kwa ushindi wa 2–0 dhidi ya Porto, huku mshambuliaji wake Erling Haaland akifunga mabao yote mawili.

Real Madrid nayo ilianza kampeni kwa ushindi wa 2–1 dhidi ya Inter Milan, wakati Borussia Dortmund ikiibuka na ushindi wa 3–1 dhidi ya Villarreal.

Aston Villa ilipata ushindi wa 3–2 ugenini dhidi ya Club Brugge, huku AEK Athens ikiifunga LASK kwa bao 1–0. Katika mchezo mwingine, Lille na Real Betis zilitoka sare ya mabao 2–2.

Matokeo kamili ni:

  • Club Brugge 2–3 Aston Villa
  • AEK Athens 1–0 LASK
  • Real Madrid 2–1 Inter Milan
  • Borussia Dortmund 3–1 Villarreal
  • Porto 0–2 Manchester City
  • Lille 2–2 Real Betis

Mzunguko huo utaendelea leo, Septemba 9, 2026, ukiwa na michezo mingine mikali ikiwemo Barcelona dhidi ya Feyenoord, Liverpool dhidi ya Atlético Madrid, Paris Saint-Germain dhidi ya Slovan Bratislava na Napoli dhidi ya Arsenal.

Macho ya mashabiki wa soka yataelekezwa zaidi kwenye michezo hiyo, huku vigogo hao wakisaka kuanza vyema katika mbio za kutwaa ubingwa wa Ulaya.

Lamata Village Yampa Pole Rais Samia Kufuatia Kifo Cha Mumewe

Global Publishers
September 9, 2026
66 views
0 Comments

LAMATA VILLAGE Septemba 8, 2026 walifika kumpa pole Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kufuatia kufiwa na Mume wake Marehemu Maalim Hafidh Ameir Hassan aliyefariki dunia katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Emilio Mzena Zanzibar, tarehe 07 Sept, 2026.

Kupitia ujumbe wao, LAMATA VILLAGE imesema imepata nafasi ya kumtembelea Rais Samia na kumpa pole, huku ikimuombea Mungu aendelee kumpa nguvu na kumsimamia katika kipindi hiki kigumu.

Aidha, wamewatoa pole ndugu, jamaa pamoja na wote walioguswa na msiba huo, wakisisitiza mshikamano na faraja katika kipindi hiki cha majonzi.

Ajira Mpya 678 Zatangazwa Serikalini, Madaktari na Walimu Watajwa

Dodoma, Septemba 3, 2026 — Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma (PSRS), kwa niaba ya

Tangazo hilo lenye Kumb. Na. JA.9/16/01/56, limetolewa Septemba 3, 2026, likiwa na nafasi katika kada mbalimbali kuanzia madaktari, wauguzi, walimu, wataalamu wa mifugo hadi watumishi wa ofisi.

Nafasi zilizotangazwa

1. Daktari Daraja la II – Nafasi 115

Waombaji wanatakiwa kuwa na Shahada ya Udaktari kutoka chuo kinachotambuliwa na Serikali, wawe wamekamilisha mafunzo ya Internship na kupata usajili kutoka Baraza la Madaktari Tanganyika.

Majukumu yanahusisha kutoa huduma za matibabu, elimu ya afya, kuzuia milipuko ya magonjwa, kutunza takwimu za afya, kusimamia watumishi na kushiriki katika kuboresha ubora wa huduma za afya.

Mshahara: TGHS E

2. Afisa Muuguzi Msaidizi Daraja la II – Nafasi 128

Nafasi hizi ni kwa wenye Stashahada ya Uuguzi ya muda usiopungua miaka miwili kutoka chuo kinachotambuliwa na Serikali.

Mwombaji anatakiwa pia kuwa amesajiliwa na Baraza la Wauguzi na Wakunga Tanzania.

Mshahara: TGHS B3. Afisa Mifugo Daraja la II – Nafasi 39

Waombaji wanatakiwa kuwa na Shahada ya Sayansi ya Wanyama (Animal Science) au Shahada ya Sayansi ya Kilimo aliyebobea katika Sayansi ya Wanyama kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine au sifa inayolingana kutoka chuo kinachotambuliwa na Serikali.

Majukumu yanahusisha kupanga na kusimamia uzalishaji wa mifugo, kutoa mafunzo kwa wafugaji, kuratibu miradi ya mifugo, kukusanya takwimu na kushiriki katika kudhibiti changamoto zinazohusiana na mifugo na mazingira.

Mshahara: TGS D

4. Tabibu wa Kinywa na Meno Daraja la II – Nafasi 17

Waombaji wanatakiwa kuwa na Stashahada ya Tabibu wa Meno (Diploma in Clinical Dentistry) kutoka chuo kinachotambuliwa na Serikali na wawe wamesajiliwa na Baraza la Madaktari.

Mshahara: TGHS B

5. Mteknolojia Maabara Daraja la II – Nafasi 25

Nafasi hizi ni kwa wenye Stashahada katika Uteknolojia wa Maabara za Afya kutoka chuo kinachotambuliwa na Serikali.

Mwombaji anatakiwa pia kuwa amesajiliwa na Baraza la Wataalamu wa Maabara.

Mshahara: TGHS B

6. Mwandishi Mwendesha Ofisi Daraja la II – Nafasi 74

Waombaji wanatakiwa kuwa na elimu ya Kidato cha Nne au Kidato cha Sita, pamoja na Stashahada ya Uhazili (NTA Level 6).

Wanapaswa pia kuwa wamefaulu somo la Hatimkato ya Kiswahili na Kiingereza kwa kasi ya maneno 100 kwa dakika moja na kuwa na ujuzi wa programu za kompyuta za ofisi kama Word, Excel, PowerPoint, Internet, E-mail na Publisher.

Mshahara: TGS C

7. Mwalimu Daraja la III C – Fizikia – Nafasi 55

Waombaji wanatakiwa kuwa na Shahada ya Elimu/Bachelor of Education yenye somo la Fizikia au shahada isiyo ya ualimu yenye Fizikia kama somo la kufundishia pamoja na Stashahada ya Uzamili ya Elimu (PGDE).

Mshahara: TGTS D

8. Mwalimu Daraja la III C – Hisabati – Nafasi 67

Waombaji wanatakiwa kuwa na Shahada ya Elimu/Bachelor of Education yenye Hisabati kama somo la kufundishia, au shahada isiyo ya ualimu yenye Hisabati pamoja na PGDE.

Mshahara: TGTS D

9. Mwalimu Daraja la III B – Fizikia – Nafasi 43

Nafasi hizi ni kwa wahitimu wenye Cheti cha Kidato cha Sita waliofaulu masomo mawili au zaidi yanayofundishwa shuleni na wenye Stashahada ya Ualimu ya miaka miwili yenye Fizikia kama somo la kufundishia.

Mshahara: TGTS C

10. Mwalimu Daraja la III B – Hisabati – Nafasi 48

Waombaji wanatakiwa kuwa na Cheti cha Kidato cha Sita, wakiwa wamefaulu masomo mawili au zaidi yanayofundishwa shuleni, pamoja na Stashahada ya Ualimu ya miaka miwili yenye Hisabati kama somo la kufundishia.

Mshahara: TGTS C

11. Afisa Misitu Msaidizi Daraja la II – Nafasi 28

Waombaji wanatakiwa kuwa na Stashahada katika fani kama Forestry, Agroforestry, Forest Resources Assessment and Management, Forest Biology, Forest Economics, Forest Engineering au fani inayohusiana.

Majukumu ni pamoja na kusimamia ukusanyaji wa mbegu na bustani za miti, kukusanya takwimu za misitu, kusimamia upandaji na utunzaji wa miti, kupima mazao ya misitu na kufanya doria.

Mshahara: TGS C

12. Afisa Afya Mazingira Msaidizi Daraja la II – Nafasi 26

Waombaji wanatakiwa kuwa na Stashahada ya Sayansi ya Afya ya Mazingira kutoka chuo kinachotambuliwa na Serikali na wawe wamesajiliwa na Bodi ya Wataalamu wa Afya Mazingira.

Majukumu yanahusisha kudhibiti milipuko ya magonjwa, kutoa elimu ya afya ya mazingira, kukagua usalama wa maeneo ya chakula, kusimamia sheria za afya ya mazingira na kuhamasisha jamii kuhusu usafi na afya.

Mshahara: TGHS B

13. Mwalimu Daraja la III C – Fasihi ya Kiingereza – Nafasi 13

Waombaji wanatakiwa kuwa na Shahada ya Elimu/Bachelor of Education yenye Fasihi ya Kiingereza kama somo la kufundishia, au shahada isiyo ya ualimu yenye somo hilo pamoja na PGDE.

Mshahara: TGTS D

Masharti muhimu ya maombi

Waombaji wote wanatakiwa kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wasizidi umri wa miaka 45.

Waombaji wenye ulemavu wanahamasishwa kutuma maombi na wanapaswa kuainisha aina ya ulemavu wao kwenye mfumo wa maombi.

Mwombaji anatakiwa kuambatisha cheti cha kuzaliwa kilichothibitishwa na Mwanasheria/Wakili, pamoja na vyeti vya elimu na vyeti vya kitaaluma vinavyohitajika kwa nafasi husika.

Sekretarieti ya Ajira imesisitiza kuwa Testimonials, Provisional Results, Statement of Results pamoja na Result Slips za Kidato cha Nne na Kidato cha Sita hazitakubaliwa.

Waombaji waliosoma nje ya Tanzania wanapaswa kuhakikisha vyeti vyao vimethibitishwa na mamlaka husika kama TCU, NECTA au NACTVET, kulingana na sifa husika.

Aidha, waombaji waliostaafishwa katika Utumishi wa Umma hawaruhusiwi kuomba isipokuwa wawe na kibali cha Katibu Mkuu Kiongozi.

Mwisho wa kutuma maombi

Mwisho wa kutuma maombi ya nafasi hizi ni Septemba 17, 2026.

Maombi yote yanatakiwa kutumwa kwa njia ya kielektroniki kupitia Recruitment Portal ya Sekretarieti ya Ajira.

Barua ya maombi iliyosainiwa inapaswa kuambatishwa pamoja na vyeti vinavyohitajika na ielekezwe kwa:

KATIBU,
OFISI YA RAIS,
SEKRETARIETI YA AJIRA KATIKA UTUMISHI WA UMMA,
Mtaa wa Mahakama, Tambukareli,
S.L.P. 2320,
DODOMA.

Sekretarieti ya Ajira imeonya kuwa maombi yatakayowasilishwa nje ya utaratibu uliowekwa hayatafikiriwa.

Aidha, waombaji wamekumbushwa kuwa ni marufuku kutoa au kupokea rushwa kwa lengo la kupata ajira au kupangiwa kituo cha kazi. Mchakato wa ajira unapaswa kuzingatia misingi ya haki, usawa na uwazi.

Limetolewa na:
KATIBU
SEKRETARIETI YA AJIRA KATIKA UTUMISHI WA UMMA

Dereva wa Basi la SATCO Afariki Baada Ya Kugonga Lori Dodoma

Global Publishers
September 9, 2026
0 views
0 Comments

Mtu mmoja amefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa kufuatia ajali ya basi la kampuni ya SATCO iliyotokea katika kijiji cha Msembeta, Wilaya ya Dodoma, mkoani Dodoma.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma iliyotolewa Septemba 8, 2026, ajali hiyo ilitokea majira ya saa 12:20 asubuhi kwenye barabara ya Singida baada ya basi lenye namba za usajili T 115 EQD lililokuwa likitokea Bukoba kuelekea Dodoma kugongana na lori la kampuni ya Triples lenye namba T 834 EEE na T 161 CUX Semi Trailer aina ya DAF.

Polisi imeeleza kuwa basi hilo lilikuwa likiendeshwa na Juma Mohamed (40), mkazi wa Dodoma, ambaye alipoteza maisha katika ajali hiyo baada ya gari alilokuwa akiendesha kuligonga lori hilo na kisha kuacha njia kwenda kugonga mti.

Watu watatu walijeruhiwa katika ajali hiyo, ambao ni Sostenes Kusara Sengo, mkazi wa Kahama; Marco Makenzi, mkazi wa Nzega; pamoja na Koplo Korombia Ngonyani, askari wa Polisi wa Kahama.

Majeruhi wote wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, huku mwili wa marehemu ukihifadhiwa hospitalini hapo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa basi kushindwa kulimudu gari hilo.

Jeshi la Polisi limetoa wito kwa madereva na watumiaji wote wa barabara kuzingatia sheria za usalama barabarani, kuendesha kwa tahadhari na kuheshimu watumiaji wengine wa barabara ili kuepusha ajali zinazoweza kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.

Polisi Dar Yamshikilia Conrad Kayoza Kwa Kumshambulia Askari Wa Usalama Barabarani

Global Publishers
September 9, 2026
54 views
0 Comments

Jeshi la Polisi Mkoa wa Dar es Salaam linamshikilia mtu mmoja, Conrad Agonza Kayoza, mwenye umri wa miaka 35, mkazi wa Lugalo na Mloganzila, Dar es Salaam, kwa tuhuma za kumshambulia askari wa usalama barabarani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, tukio hilo limetokea Septemba 8, 2026 majira ya saa 1:30 asubuhi eneo la Lugalo, Kinondoni, kwenye barabara ya Bagamoyo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa askari mwenye namba F.8886 SGT Andrew, wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kinondoni, akiwa kazini na akitekeleza majukumu yake, alishambuliwa kwa ngumi na mateke na mtuhumiwa huyo.

Inadaiwa kuwa kabla ya tukio hilo, askari huyo alikuwa kazini na alizuia kisheria magari yaliyokuwa yakipita pembezoni mwa barabara katika eneo la “Service Road” nje ya utaratibu uliokuwepo, ikiwemo gari la mtuhumiwa aina ya Toyota Runx lenye namba za usajili T 455 EER.

Kwa mujibu wa Polisi, mtuhumiwa alishuka kwenye gari na kuanza kumshambulia askari kabla ya yeye mwenyewe kushambuliwa na wananchi waliokuwa wamechukizwa na kitendo hicho.

Conrad Agonza Kayoza alipelekwa hospitalini kwa matibabu baada ya kujeruhiwa na amepewa nafuu. Polisi imeeleza kuwa atahojiwa kwa kina ili hatua za kisheria zichukuliwe na mamlaka husika.

Polisi Dar es Salaam imetoa tahadhari kwa wananchi, ikisisitiza kuwa haitavumilia wala kusita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu yeyote au kundi litakalomshambulia polisi wakati wanatekeleza majukumu yao ya kisheria.