DKT. MWIGULU: TANZANIA NA QATAR BADO TUNA FURSA NYINGI ZA KIUCHUMI

_Apigia chapuo utekelezaji wa DIRA 2050_

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema bado kuna fursa nyingi za ushirikiano wa kiuchumi baina ya Taifa la Qatar na Tanzania ambazo zikitumiwa vizuri zitawanufaisha raia wa nchi zote mbili.

 

“Bado tuna fursa nyingi ambazo tunaweza tukanufaika nazo kama tutatekeleza baadhi ya shughuli za kiuzalishaji. Tanzania kama lango la Afrika Mashariki, Kusini na Kati na Qatar kama lango la Mashariki ya Kati na Umoja wa Nchi za Ghuba tulikubaliana kuwa tukichangamkia fursa zote zinazojitokeza, tutaongeza ushiriki wa wananchi wa nchi zote mbili,” alisema.

 

Alikuwa akizungumza na Rais na Mtendaji Mkuu wa Power International Holding (PIH), Bw. Ramez Al-Khayyat na baadhi ya viongozi wakuu wa taasisi hiyo kwenye makao makuu ya kampuni hiyo yaliyopo Lusail, jijini Doha.

 

Waziri Mkuu alimshukuru Rais na Mtendaji Mkuu wa PIH kwa kuonesha nia ya dhati ya kuwekeza katika sekta ambazo DIRA 2050 imeyaainisha kama maeneo ya kipaumbele.

 

“Tunashukuru kwamba hii kampuni imeonesha nia ya kuwekeza kwenye maeneo yaliyotajwa katika DIRA 2050 ambayo na sisi tumeyawekea kipaumbele. Wameonesha nia ya kushiriki DIRA yetu kupitia utekelezaji wa fursa zilizopo. Tumekubaliana kwamba mawaziri waliopo wakiongozwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mheshimiwa Kapinga wafuatilie kwa karibu ili utekelezaji uanze mara moja.”

 

Kwa upande wake, Rais na Mtendaji Mkuu wa PIH, Bw. Ramez Al-Khayyat alimweleza Waziri Mkuu kwamba Power International Holding ni kampuni kubwa ya kimataifa inayomilikiwa na watu binafsi ambayo inaendesha kampuni tanzu 400 zenye wafanyakazi 65,000 katika nchi 26.

 

Kati ya nchi 26, za Afrika ni Misri, Libya, Morocco, Algeria, Mauritania na Rwanda. Alisema wameshaingia makubaliano na Ethiopia (ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa) na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (ujenzi wa barabara yenye urefu wa km. 400).

 

“Utendaji kazi wa taasisi yetu umegawanyika katika makundi makubwa saba ya kibiashara yanayoendeshwa kimataifa na yenye kampuni tanzu 400 na wafanyakazi 65,000. Kwa sehemu kubwa, shughuli zetu zinajihusisha na madini, ujenzi wa miundombinu mikubwa, ujenzi wa majengo ya makazi pamoja na hoteli, kilimo na viwanda, utalii na utoaji huduma za mawasiliano,” alisema

 

Mapema, akitoa taarifa kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE, Bw. Ephraim Mafuru alisema kwa muda mrefu Tanzania ilikuwa ikisafirisha nyama ya mbuzi na kondoo kwenda nchi za Ghuba lakini kwa sasa inaweza kufanya vizuri zaidi endapo itaongeza mazao ya kilimo na madini hasa ya dhahabu.

 

“Tunalo soko kubwa la dhahabu ambalo kimsingi halijatumiwa. Tunajua soko liko hapa katika Ghuba. Lakini pia kuna fursa kubwa kwenye mchele ambao unaweza kutuingizia dola bilioni 3.9. Mwaka jana, tulizalisha tani milioni 3.4 za mchele na tukatumia tani milioni 1.8 tu. Maana yake ni kwamba tuna zaidi ya tani milioni 1.6 ambazo tunaweza kuzisambaza kwa watu milioni 3.4 waishio nchini Qatar.”

 

Akielezea kuhusu fursa za uwekezaji nchini Tanzania, Bw. Mafuru aliyataja maeneo hayo kuwa ni nishati, LNG, utalii, mbogamboga na matunda, maua, uzalishaji wa malisho ya mifugo pamoja na mazao yanayotokana na uchumi wa bluu.

 

Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu alifuatana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga; Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ngwaru Maghembe, Katibu Wakuu (OR-Uwekezaji), Wakuu wa Mikoa ya Pwani na Dodoma, Wabunge Esther Matiko na Subira Mgallu na watendaji wengine wa Serikali.

TANZANIA NA UTURUKI KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA USIMAMIZI WA MAAFA

SERIKALI ya Tanzania imesema itaendelea kuimarisha ushirikiano na Mamlaka ya Usimamizi wa Maafa na Dharura ya Uturuki (AFAD), kwa lengo la kuimarisha uwezo wa nchi katika kuzuia na kupunguza athari za maafa, kujiandaa, kukabiliana na dharura na kurejesha hali baada ya maafa kutokea.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi, wakati wa kikao cha pamoja kati ya ujumbe wa Serikali ya Tanzania na uongozi wa AFAD kilichofanyika katika ofisi za taasisi hiyo mjini Ankara, Uturuki ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi nchini humo iliyolenga kuongeza ujuzi na maarifa ya kiufundi, kuimarisha uwezo wa kitaasisi, kujifunza uzoefu wa Uturuki katika kupunguza vihatarishi vya maafa, kujiandaa na kukabiliana na dharura, pamoja na kurejesha hali baada ya maafa kwa kutumia mbinu, mifumo na teknolojia za kisasa.

Dkt. Yonazi amesema Tanzania inathamini uzoefu na utaalamu wa AFAD katika usimamizi jumuishi wa maafa na kwamba Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano huo kwa manufaa ya Tanzania na Uturuki, hususan katika kuendeleza mifumo ya kisasa ya usimamizi wa maafa, teknolojia, mafunzo ya wataalam, utafutaji na uokoaji pamoja na uratibu wa hatua za mwitikio wakati wa dharura. 

“Tanzania itaendelea kujifunza na kushirikiana na taasisi mbalimbali zenye uzoefu katika usimamizi wa maafa, ikiwemo AFAD, ili kuimarisha uwezo wa kitaifa wa kuzuia na kupunguza athari za maafa, kujiandaa, kukabiliana na kurejesha hali pindi yanapotokea,” amesema Dkt. Yonazi.

Kwa upande wake, Mkuu wa AFAD nchini humo, Gavana Ali Hamza Pehlivan, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendeleza ushirikiano na Uturuki katika eneo la usimamizi wa maafa na kueleza kuwa AFAD ipo tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali ya kitaalamu.

Gavana Pehlivan amesema maeneo hayo ni pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa katika usimamizi wa maafa, mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ya vihatarishi na madhara ya maafa, maandalizi na mwitikio wa dharura, pamoja na uanzishaji, mafunzo na uendelevu wa timu maalumu za utafutaji na uokoaji na upatikanaji wa vifaa vinavyohitajika wakati wa maafa.

Ameeleza kuwa AFAD inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia dhana ya usimamizi jumuishi wa maafa, inayolenga kushughulikia hatua zote za mzingo wa usimamizi wa maafa, kuanzia katika kutambua na kutathmini vihatarishi, kuzuia na kupunguza uwezekano na athari za maafa, kujiandaa, kukabiliana na dharura hadi kurejesha hali pindi maafa yanapotokea. 

Vilevile, AFAD imejenga uwezo wa kuratibu timu za wataalam na vikosi vya utafutaji na uokoaji vinavyoshughulikia majanga mbalimbali, yakiwemo matetemeko ya ardhi, mafuriko na dharura nyingine, kwa lengo la kuokoa maisha na kulinda mali. Taasisi hiyo pia hushiriki katika uratibu wa utoaji wa misaada ya kibinadamu kwa waathirika wa maafa na kusaidia shughuli za kurejesha hali na makazi katika maeneo yaliyoathirika.

Katika eneo la kujenga uwezo wa rasilimali watu, AFAD inaendesha mafunzo na mazoezi ya vitendo kwa wataalam na timu za mwitikio wa maafa kupitia miundombinu yake ya mafunzo, ikiwemo Disaster and Emergency Training Centre (AFADEM). Mafunzo hayo yanalenga kuongeza ujuzi wa kitaalamu, uwezo wa kufanya kazi kwa pamoja na utayari wa kukabiliana na matukio ya dharura.

Gavana Pehlivan ameongeza kuwa AFAD pia hushiriki katika ushirikiano wa kimataifa wa usimamizi wa maafa kupitia Timu ya Kimataifa cha Utafutaji na Uokoaji (The International Search and Rescue Advisory Group – INSARAG) ambayo inasimamiwa na Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (UN-OCHA) katika kupeleka timu maalumu za utafutaji na uokoaji na kutoa msaada wa kibinadamu katika nchi mbalimbali pale kunapojitokeza maafa makubwa.

Tanzania na Uturuki zimeendelea kuwa na fursa ya kubadilishana uzoefu na utaalamu katika eneo la usimamizi wa maafa, hususan katika teknolojia, mifumo ya taarifa na tahadhari za mapema, mafunzo, utafutaji na uokoaji, uratibu wa mwitikio wa kukabili na urejeshaji wa hali, kwa lengo la kujenga jamii na taasisi zenye uwezo mkubwa wa usimamizi wa maafa.

=MWISHO=

GST NA GTK ZAFUNGUA UKURASA MPYA UTAFITI WA MADINI

• *GST na GTK zasaini MoU*

• *Kufanya Utafiti wa Kina wa madini*

• *Kuimarisha upatikanaji wa taarifa za madini*

*Pori, Finland*

Tanzania na Finland zimefungua ukurasa mpya wa ushirikiano katika utafiti wa madini baada ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Taasisi ya Utafiti wa Jiolojia ya Finland (GTK) kusaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) unaolenga kuimarisha utafiti wa jiolojia na upatikanaji wa taarifa sahihi za rasilimali za madini nchini.

Makubaliano hayo yaliyosainiwa Septemba 30, 2026, yanahusisha utekelezaji wa Utafiti wa Kijiolojia kwa kutumia ndege ( _Airborne Geophysical Survey)_ pamoja na kuwajengea uwezo wataalam wa GST katika Uhakiki wa Ubora wa Takwimu na Udhibiti wa Ubora.

Akizungumza wakati wa kusaini makubaliano hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, alisema kuwa, Serikali ya Tanzania inathamini ushirikiano huo kwa kuwa una fursa ya kuimarisha uwezo wa Tanzania katika kutambua, kuchambua ili kutambua kiwango cha rasilimali madini zilizopo nchini.

Aliongeza kuwa, taarifa sahihi za kijiolojia ni msingi muhimu katika kufanya tafiti, kupanga matumizi ya rasilimali na kuvutia uwekezaji katika Sekta ya Madini.

“ _Ushirikiano huu utaleta mabadiliko katika namna Tanzania inavyokusanya, kuchambua na kutumia taarifa za kijiolojia,”_ alisema Mbibo.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa GTK, Dkt. Saku Vuori, alisema utekelezaji wa programu ya kuwajengea uwezo wataalam wa GST tayari imeanza, huku wataalam wa GTK wakiendelea kufanya tathmini ya hatua nyingine za utekelezaji.

Dkt. Vuori alisema kuwa, GTK pia iko tayari kuiwezesha GST katika kuimarisha uwezo wa Maabara mpya inayojengwa Dodoma, ikiwemo upatikanaji wa vifaa vya teknolojia ya kisasa kwa ajili ya uchambuzi na upimaji wa sampuli za miamba na madini.

Hatua hiyo inalenga kuiwezesha Tanzania kupata taarifa za maabara zinazokidhi viwango vya kisasa, ambazo zinaweza kutumika katika utafiti, tathmini ya rasilimali madini na maamuzi ya uwekezaji.

Katika makubaliano hayo, Umoja wa Ulaya (EU) umeonesha nia ya kusaidia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuimarisha utekelezaji wa ushirikiano huo, hususan katika kuhakikisha taarifa na takwimu za kijiolojia zinazokusanywa zina ubora na sahihi kwa uwekezaji.

Pamoja na mambo mengine, ujumbe wa Tanzania ulipata fursa ya kutembelea maabara ya kisasa ya GTK na kupata maelezo kuhusu matumizi ya teknolojia katika uchambuzi wa sampuli za miamba na madini pamoja na mifumo ya uhakiki na udhibiti wa ubora wa taarifa za kisayansi.

Ziara hiyo imehusisha wajumbe kutoka Wizara ya Madini, GST, Chemba ya Migodi Tanzania, kampuni za uchimbaji madini, Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden, Umoja wa Ulaya nchini Tanzania na Ubalozi wa Finland nchini Tanzania.

Ushirikiano wa Tanzania na Finland unatarajiwa kuongeza uwezo wa wataalam wa Tanzania na kuimarisha upatikanaji wa taarifa za kisayansi zitakazosaidia katika utafiti, uendelezaji na uongezaji thamani katika rasilimali madini nchini.

MUST Yatangaza Nafasi za Ajira kwa Wahitimu Wenye GPA 3.8

Global Publishers
October 1, 2026
930 views
0 Comments

Mbeya University of Science and Technology (MUST) imetangaza nafasi tano (5) za ajira kwa Watanzania wenye sifa, katika kada mbalimbali za Tutorial Assistant, ambapo nafasi zote zipo katika Kampasi Kuu ya Chuo.

Nafasi hizo ni:

  • Tutorial Assistant – Aquatic Science and Aquaculture Technology: Nafasi 1. Mwombaji anatakiwa kuwa na Shahada ya Sayansi katika Aquatic Sciences and Aquaculture Technologies, Aquaculture, Aquatic Science, Fisheries au Marine Science, akiwa na GPA isiyopungua 3.8/5.
  • Tutorial Assistant – Health Information Science: Nafasi 1, kwa mwenye Shahada ya Sayansi katika Health Information Systems na GPA isiyopungua 3.8/5.
  • Tutorial Assistant – Interior Design: Nafasi 2, kwa mwenye Shahada katika Interior Design Technology, Bachelor of Science in Interior Design au Bachelor of Interior Architecture, akiwa na GPA isiyopungua 3.8/5.
  • Tutorial Assistant – Inclusive Education: Nafasi 1, kwa mwenye Shahada ya Education in Special Needs and Inclusive Education na GPA isiyopungua 3.8/5.

Waombaji wote wanatakiwa kuwa raia wa Tanzania wenye umri usiozidi miaka 45. Watu wenye ulemavu wanahimizwa kuomba, huku watumishi walio katika utumishi wa umma wakielezwa kutoruhusiwa kuomba nafasi hizo.

Maombi yanapaswa kuwasilishwa kupitia Recruitment Portal ya Ajira, na waombaji wanatakiwa kuambatanisha vyeti vilivyoidhinishwa, transcripts, vyeti vya Form IV na Form VI, cheti cha kuzaliwa, picha ya passport na taarifa za wadhamini watatu.

Mwisho wa kutuma maombi ni tarehe 6 Oktoba 2026.

Soma zaidi bonyeza link chini

Wadau madini wasisitizwa kuzingatia viwango – HabariLeo

GEITA: SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wafanyabiashara wa madini, wachimbaji na wasindikaji kuanzisha mifumo ya usimamizi wa ubora, mazingira, matumizi ya nishati pamoja na afya na usalama mahali pa kazi, ili kuhakikisha shughuli zao zinaendeshwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.

Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa Magharibi, Joseph Makene, amesema hayo wakati akizungumza katika Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita, ambapo TBS inatoa elimu kwa wadau kuhusu viwango, ubora na usalama wa bidhaa.

Makene amesema TBS imekuwa ikishiriki maonesho hayo tangu yalipoanza Septemba 23 mwaka huu, ikitumia fursa hiyo kuwafikia wajasiriamali na wadau mbalimbali wa sekta ya madini na sekta nyingine.

Amesema mifumo inayosisitizwa ni pamoja na Mfumo wa Usimamizi wa Ubora (Quality Management System), Mfumo wa Usimamizi wa Nishati (Energy Management System), Mfumo wa Usimamizi wa Mazingira (Environmental Management System), pamoja na Mfumo wa Usimamizi wa Afya na Usalama Mahali pa Kazi.

“Wadau hawa wakiwa na mifumo hii, hasa mifumo inayokidhi viwango vya kimataifa, wataweza kufanya shughuli zao katika mazingira yanayozingatia viwango vya kimataifa,” amesema.

Aidha, amesema TBS hutoa elimu kuhusu namna ya kuanzisha na kusimamia mifumo hiyo, pamoja na kufanya uhakiki na kutoa vyeti vya mifumo ya usimamizi (Management System Certification) kwa taasisi zinazokidhi matakwa ya viwango husika.

Makene pia amewataka wafanyabiashara wenye maabara zinazotumika katika upimaji wa madini kutumia huduma za maabara ya metrology ya TBS kwa ajili ya uhakiki na urekebishaji (calibration) wa vifaa vyao, ili kuhakikisha vipimo vinavyofanyika vinakuwa sahihi.

Kwa upande wa waingizaji wa bidhaa zinazotumika katika shughuli za uchimbaji madini, amewataka kuhakikisha bidhaa hizo zinakaguliwa na kuthibitishwa ubora kabla ya kuziingiza nchini.

Amesema TBS ina mawakala wa ukaguzi wa bidhaa katika nchi mbalimbali ambao hufanya ukaguzi wa bidhaa kabla hazijasafirishwa kuja Tanzania.

Katika hatua nyingine, Makene amewataka wafanyabiashara wa vipodozi katika Kanda ya Ziwa Magharibi kuhakikisha wanauza bidhaa zinazokidhi viwango na zisizo na viambata sumu.

Ametaja maeneo yanayolengwa katika ukaguzi kuwa ni Geita, Katoro, Runzewe, Kahama, Shinyanga na Bukoba, akisema TBS itaendelea kutoa elimu na kufanya ukaguzi wa bidhaa hizo.

Amesema wafanyabiashara wanapaswa kuhakikisha vipodozi wanavyouza havina viambata vilivyopigwa marufuku, huku akiwataka kutumia taarifa zinazopatikana kupitia tovuti ya TBS kujua bidhaa ambazo haziruhusiwi.

“TBS Kanda ya Ziwa Magharibi imejipanga kufanya operesheni kubwa katika masoko ya maeneo ya Geita, Katoro, Kahama, Shinyanga na Bukoba, kuweza kuviondoa vipodozi vyote ambavyo vina viambata sumu na kuviteketeza kwa mujibu wa sheria,” amesema Makene.

Fahamu Mali za Kifahari Alizoacha Wicknell Chivayo Magari, Majumba, Ndege na Biashara

Mfanyabiashara wa Zimbabwe, Wicknell Chivayo, aliyefariki  Septemba 30, 2026 katika ajali ya helikopta pamoja na mkewe Lucy Muteke, alikuwa akijulikana kwa maisha ya kifahari, magari ya gharama kubwa, mali zisizohamishika na ndege binafsi.

Hata hivyo, hakuna taarifa rasmi inayothibitisha thamani ya jumla ya mali zote alizokuwa anamiliki. Chivayo mwenyewe aliwahi kujieleza kuwa utajiri wake ulikuwa zaidi ya dola milioni 100  sawa TSh 264,000,000,000 (bilioni 264), lakini vyombo vikuu vya habari vya fedha havijathibitisha kwa kujitegemea makadirio hayo.

Majumba ya kifahari

Moja ya mali zilizoripotiwa ni jumba kubwa jijini Harare, ambalo kwa mujibu wa News24 lilikuwa likimilikiwa na Chivayo na hapo awali lilikuwa la aliyekuwa Mkuu wa Polisi wa Zimbabwe, Augustine Chihuri. Thamani yake iliripotiwa kuwa karibu R130 milioni za Afrika Kusini (ni takribani TSh bilioni 20.9).

Mwaka 2026, Chivayo pia alionyesha hadharani nyumba nyingine ya kifahari katika eneo la Clifton, Cape Town, Afrika Kusini, aliyosema ilinunuliwa kwa takribani R160 milioni TSh bilioni 25.51. Nyumba hiyo ina ghorofa nne, lifti, gym na mandhari ya bahari na Robben Island.

Katika kesi ya talaka kati yake na mke wake wa zamani, Sonja Madzikanda, nyaraka za mahakama pia zilitaja mali nyingine, zikiwemo nyumba na mali za Johannesburg.

Hata hivyo, madai hayo yalikuwa sehemu ya mchakato wa kisheria na hayapaswi kuchukuliwa kama orodha rasmi ya mali zote za Chivayo.

Mkusanyiko wa magari ya kifahari

Chivayo alikuwa maarufu kwa magari ya kifahari na pia kwa kutoa baadhi ya magari hayo kama zawadi.

Ripoti kuhusu mali zilizotajwa katika kesi ya familia ziliorodhesha magari kama Rolls-Royce Spectre, Rolls-Royce Ghost, Rolls-Royce Phantom, Range Rover, Mercedes-Benz V-Class, Mercedes-Maybach na Lexus SUV.

Chivayo alikuwa akipenda kuendesha Rolls-Royce nyeupe na alikuwa na magari mengine mengi ya kifahari. Baadhi ya magari aliyokuwa akinunua baadaye alikuwa akiyatoa kama zawadi kwa watu mbalimbali.

Kwa upande wa zawadi, ripoti ya Billionaires.Africa inaeleza kuwa Chivayo alitoa magari na fedha zenye thamani ya mamilioni ya dola kwa watu mbalimbali, wakiwemo wanamuziki, viongozi wa dini na watu wengine aliowachagua.

Ndege binafsi ya Gulfstream

Miongoni mwa mali zilizovutia zaidi ni Gulfstream G550. South African iliripoti mwaka 2026 kwamba Chivayo alitangaza kupata ndege hiyo yenye thamani ya takribani dola milioni 34 TSh 90,312,300,000, sawa na mamia ya mabilioni ya shilingi za Tanzania kutegemea kiwango cha ubadilishaji.

Ndege binafsi ilikuwa sehemu ya maisha yake ya kifahari ambayo mara kwa mara alikuwa akiyaonyesha kupitia mitandao ya kijamii.

Biashara na mikataba mikubwa

Utajiri wa Chivayo ulihusishwa kwa kiasi kikubwa na biashara na mikataba ya serikali. BBC iliripoti kuwa kampuni yake Intratrek Zimbabwe, kwa kushirikiana na kampuni ya China, ilipata mkataba wa takribani dola milioni 172.8 sawa na TSh bilioni 459 kwa mradi wa nishati ya jua wa Gwanda.

Billionaires Africa iliripoti kwamba kampuni zinazohusishwa na Chivayo ziliwahi kupata mikataba ya serikali yenye thamani inayokaribia dola bilioni 1, ikiwemo miradi ya nishati ya jua, ukarabati wa kituo cha umeme cha Munyati na mradi wa umeme wa Gairezi. Billionaires.Africa

kuhusu ukubwa wa utajiri wake, chanzo cha baadhi ya fedha zake na biashara zake, huku Chivayo mwenyewe akiwa amekanusha tuhuma mbalimbali zilizowahi kutolewa dhidi yake. The Times+1

WATAKIWA KUTUMIA MAMLAKA YA MKEMIA KWA MAFANIKIO YA KAZI ZAO

Wadau wa sekta ya Madini, Tiba Asili na Mbadala wametakiwa kutumia Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili kuwezesha usalama na mafanikio katika kazi zao wanazofanya.

Wito huo umetolewa leo kwenye kwenye Maonesho ya Tisa Kitaifa ya Teknolojia ya Madini Mkoani Geita na Meneja Mkuu wa Mamlaka ya Maabara ya Serikali Kanda ya Ziwa John Wanjala.

Alisema kuna umuhimu mkubwa wa kufanya uchunguzi wa shughuli hizo ili ziweze kuleta matokeo chanya kwenye jamii kwani madhara yanayoweza kuletelezwa na sekta hizo yaweza kuwa mabaya kwa wananchi.

Wanjala alisema Mamlaka hiyo inavyo vifaa vya kisasa kuwezesha ufanyaji wa utafiti wenye tija kwa sekta hizo zenye mchango katika kukuzanuchumi wa taifa.

Alisema mojawapo ya majukumu yao ni kutoa elimu kuhusiana na namna ya kuweza kufanya shughuli za uchenjuaji wa madini kwa kutumia kemikali bila ya kuleta madhara ya kimazingira na kwa afya ya binadamu.

“Kunapokuwa na uelewa ndani ya jamii juu ya kutumia mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali huwezesha wadau kwenye sekta hiyo kuepuka hasara katika kazi zao” alisema Wanjala.

Wajala alisema kupitia uchunguzi wanaofanya wanawezesha wachimbaji kufahamu juu ya uwepo wa madini hivyo wadau hao kuwa na uhakika wa shughuli wanazofanya katika maeneo yao.

Alisema vilevile mamlaka hiyo inalo jukumu la kusimamia mchakato wa sheria zinazoendesha matumizi ya kemikali katika shughuli wanazofanya wadau wa sekta hizo hapa nchini.

Mfahamu Rubani Aliyepongezwa Baada ya Tukio la Ndege ya Dubai–Israel

Global Publishers
October 1, 2026
0 views
0 Comments

Kapteni Smit Machhar, rubani raia wa India wa shirika la ndege la Flydubai.

Kapteni Smit Machhar, rubani raia wa India wa shirika la ndege la Flydubai, ameibua gumzo duniani baada ya tukio lililotokea ndani ya ndege iliyokuwa ikisafiri kutoka Dubai kuelekea Israel.

Machhar amepokea pongezi kutoka kwa viongozi mbalimbali, akiwemo Rais wa Marekani Donald Trump na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, kutokana na hatua alizochukua wakati wa tukio hilo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa, Machhar alikuwa rubani wa ndege ya Flydubai, FZ1073, iliyokuwa ikielekea Israel, ambapo alishambuliwa kwa kisu ndani ya ndege.

Inadaiwa kuwa licha ya kujeruhiwa, Machhar alifanikiwa kufungua mlango wa chumba cha marubani kabla ya kupoteza fahamu kutokana na majeraha aliyoyapata.

Hatua hiyo ilitajwa kuwa muhimu katika kuhakikisha tahadhari zinaendelea kuchukuliwa wakati ndege ikiwa angani, katika mazingira yaliyokuwa magumu.

Taarifa kuhusu tukio hilo zilitolewa na Yaniv Hayun, abiria raia wa Israel aliyekuwa ndani ya ndege hiyo. Hayun alisimulia yaliyotokea wakati akizungumza na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, katika Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion Jumatano, Septemba 30.

Kabla ya kujiunga na Flydubai, Machhar alikuwa akifanya kazi katika shirika la ndege la India SpiceJet, ambako alitumikia kwa zaidi ya muongo mmoja.

Tukio hilo limemfanya Kapteni Smit Machhar kuwa gumzo, huku hatua zake wakati wa tukio zikielezwa kama mfano wa ujasiri na utulivu katika mazingira ya hatari.

Serikali yaimarisha huduma za afya Nkasi – HabariLeo

RUKWA: Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkansi, Manispaa ya Sumbawanga na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Rukwa,  Jacqueline Mzindakaya,  wamefurahishwa na jitihada za Serikali za kuimarisha huduma za afya, huduma za uchunguzi na matibabu.

Hatua hiyo itasaidia kupunguza vifo vya wanawake wajawazito na watoto, baada ya Zahanati za Chala na King’ombe kupatiwa na Serikali vifaa tiba vyenye thamani ya jumla ya Sh milioni 312.

Vifaa tiba vyenye thamani ya Sh milioni 267 vimetolewa katika Zahanati ya Chala, Nkansi, na vyenye thamani ya Sh milioni 45 vimetolewa katika Zahanati ya King’ombe, Manispaa ya Sumbawanga, kwa lengo la kuongeza uwezo wa vituo hivyo kutoa huduma bora na salama za afya, ikiwepo huduma za afya ya mama na mtoto.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa wananchi kwa niaba ya Serikali, Septemba 30, 2026, Mhe. Mzindakaya amesema uwepo wa vifaa hivyo utaboresha huduma za uchunguzi na matibabu, kuimarisha mazingira ya kazi kwa watumishi wa afya na kuongeza uwezo wa zahanati hizo kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.

“Tumepata vifaa tiba vitakavyotusaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi pamoja na kupunguza vifo vya wanawake wajawazito na watoto. Ujio wa vifaa hivi unatokana na dhamira ya dhati ya Mhe. Rais Dk Samia Suluhu Hassan ya kutokomeza vifo vya wanawake wajawazito na watoto nchini,” amesema Mhe. Mzindakaya.

Mzindakaya amefafanua kuwa lengo la Serikali kupeleka vifaa hivyo ni kuimarisha upatikanaji wa vifaa muhimu katika vituo vya afya, kuboresha ubora wa huduma, kuimarisha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi wa afya na kupunguza changamoto zinazotokana na upungufu wa vifaa tiba, hivyo ameishukuru Serikali kwa kutoa vifaa hivyo kwa ajili ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Nkansi na Manispaa ya Sumbawanga.

Miongoni mwa vifaa tiba vilivyotolewa na Serikali kupitia mgao wa Mradi wa TCHMP ni mashine za kupima shinikizo la damu za kidijitali, vifaa vya kupima mapigo ya moyo wa mtoto tumboni, mashine ya kufuatilia hali ya mgonjwa, mashine ya kufuatilia hali ya mgonjwa, seti za vifaa vya kusaidia kujifungua kwa kutumia uvutaji, viti vya magurudumu kwa wagonjwa, friji za kuhifadhia bidhaa za dawa pamoja na vitanda vya kujifungulia.

Utoaji wa vifaa hivyo unaongeza uwezo wa Zahanati za Chala na King’ombe kutoa huduma kwa ufanisi zaidi na kuweka mazingira bora na salama kwa wananchi wanaohitaji huduma za afya, wakiwepo wanawake wajawazito na watoto.

Madini kupewa chapa ya ‘Made in Tanzania’ – HabariLeo

GEITA: MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) imepanga kusimamia kampeni ya usajili na uwekaji wa chapa ya ‘Made in Tanzania’ katika madini yanayozalishwa nchini.

Mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni ya matumizi ya chapa ya Made in Tanzania katika bidhaa zote zinazozalishwa nchini ikiwa ni sehemu ya utambulisho wa taifa nje ya nchi.

Meneja Ukuzaji Biashara wa TANTRADE, Deo Shayo ametoa taarifa hiyo wakati akizungumza katika kongamano la Made in Tanzania katika Maonyesho ya Teknolojia ya Madini mjini Geita.

Amesema kusudi la TANTRADE ni kuona madini yanayozalishwa Tanzania yanatambulika kimataifa, kuipa nguvu chapa ya Tanzania, kuimarisha uchumi na kuchochea uwekezaji na uzalishaji.

“Tunakusudia kuwaambia wazalishaji na wafanyabiashara wa madini wajisikie fahari kuyauza yakiwa na ile chapa ya Made in Tanzania.

“Itakuwa ni jambo la aibu kama kuna wajanja wanafanya uzalishaji hapa harafu wanakubali kuuza madini nje ya nchi yakiwa na utambulisho wa nchi zingine”, amesema Deo.

Deo amesema madini adhimu ya Tanzanite yanayozalishwa Tanzania pekee pamoja na madini mengine yanayozalishwa kwa uwingi ni miongoni mwa madini yatakayopewa kipaumbele.

Aidha amewaomba wafanyabiashara kuchangamukia usajili wa bidhaa zao kwa chapa ya made in Tanzania kwani mpaka sasa takribani asilimia 85 ya huduma ya Tantrade zinatolewa mtandaoni.

Amesema kwa kipindi cha miezi 10 iliyopita takribani aina ya bidhaa 120 zimesajiliwa kwenye chapa ya taifa nah atua zaidi zinaendelea kuongeza mwamko na mwitikio katika kampeni hiyo.

“TANTRADE tutahakikisha tunaendelea kuwa mstari wa mbele tunatoa fursa za maonyesho kwa kila aliyejisajili na Made in Tanzania tunatangaza bidhaa zao kupitia Kanzi Data yetu.

“Pia TANTRADE itafungua kituo cha kimataifa cha biashara pale Ubungo, kwa kila aliyejisajili atapewa nafasi ya kutangaza sampuli ya bidhaa zake pale”, amesema Deo.