CCM WAMFUTA UANACHAMA DKT NCHIMBI ,NDEJEMBE AMRITHI UMAKAMU

 

 

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Kimemfuta uanachama Dkt Emmanuel Nchimbi ambae juzi alitangaza kujiuzulu nafasi ya umakamu urais na kustaafu siasa na utumishi wa umma .


Pamoja na kujiuzulu CCM kimetangaza kumfuta uanachama wake ,katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro, ametangaza kuwa vikao vya Chama hicho vilivyokutana jana na leo jijini Dar es Salaam vimempitisha kwa kauli moja Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, kuwa mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dkt. Migiro amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya vikao husika vya CCM kujadili na kuridhia jina la Mhe. Ndejembi, ambaye ni mwanachama wa chama hicho, kwa ajili ya kujaza nafasi hiyo iliyo wazi kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Makamu wa Rais, Dkt. Emmanuel Nchimbi.

Amesema baada ya taratibu za ndani ya chama kukamilika, jina la Mhe. Ndejembi litawasilishwa Bungeni kwa ajili ya kuthibitishwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mhe. Ndejembi amekuwa Waziri wa Nishati, akisimamia masuala mbalimbali ya sekta ya nishati nchini, ikiwemo upanuzi wa uzalishaji na usambazaji wa umeme pamoja na utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya nishati.

Hatua hiyo sasa inaweka wazi mchakato wa kumpata Makamu wa Rais mpya, ambapo baada ya jina lake kuwasilishwa na kuthibitishwa na Bunge, taratibu nyingine za kikatiba zitafuatwa ili kukamilisha uteuzi huo.

WABUNGE WAMUUNGE MKONO NDEJEMBI KUWA MAKAMU WA RAIS

Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanayo nafasi ya kihistoria kumuidhinisha Mhe. Deogratius John Ndejembi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hii ni baada ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa kupitisha jina lake tarehe 26 Agosti 2026, hatua inayofuata inahitaji busara, umoja na uzalendo katika kutambua uwezo wa kiongozi huyu.

Mhe. Ndejembi amejenga uzoefu mpana katika utumishi wa umma, siasa na uongozi.

Amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, kabla ya kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Chamwino.

Aidha, amewahi kuwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (2021–2023), na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI (2023–2024).

Mwaka 2024 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), kisha Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi (2024–2025), ambako alisimamia masuala nyeti ya ardhi, mipango ya matumizi ya ardhi na makazi.

Tangu mwaka 2025 amekuwa Waziri wa Nishati, akisimamia sekta yenye umuhimu wa moja kwa moja kwa uchumi na maisha ya Watanzania.

Katika sekta ya Nishati, utendaji wake umeonekana katika kusukuma ajenda ya nishati safi ya kupikia, usafirishaji wa umeme na uwekezaji katika gesi.

Agosti 22, 2026, alishiriki katika uzinduzi rasmi wa kituo cha kuzalisha umeme cha Julius Nyerere (JNHPP) chenye uwezo wa MW 2,115 ambapo alieleza kuwa, uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme nchini umefikia takribani MW 4,075.

Kwa historia hii, Ndejembi anaunganisha uzoefu wa utawala wa wilaya, serikali za mitaa, utumishi wa umma, kazi na ajira, ardhi pamoja na nishati.

Hivyo, Waheshimiwa Wabunge wanaombwa kuangalia sifa, uzoefu, uwezo wa kuratibu taasisi na dhamira ya kuitumikia Jamhuri, na kumpa ridhaa yao. 

Kumuunga mkono Ndejembi ni kuamini katika uongozi wenye uzoefu, mwendelezo na uwezo wa kusimamia majukumu ya kitaifa.

KUMFUTA UANACHAMA NCHIMBI NI USHINDI WA TAASISI, KANUNI NA NIDHAMU NDANI YA CCM

Uamuzi wa vikao vya juu vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumvua uanachama Dkt. Emmanuel Nchimbi unapaswa kutazamwa kwanza kama ushindi wa taasisi, kanuni na nidhamu ya chama kuliko kutazamwa kama hatua dhidi ya mtu binafsi. CCM ni chama chenye Katiba, kanuni na taratibu zinazopaswa kuheshimiwa na kila mwanachama, bila kujali cheo alichowahi kushika. 

Kinachopaswa kupongezwa zaidi ni msimamo wa CCM wa kutenganisha heshima ya mtu na wajibu wake kwa chama. Mwanachama anapokuwa katika nafasi ya juu, anakuwa na wajibu mkubwa zaidi wa kuilinda taasisi aliyokabidhiwa kuiongoza. Pamoja na hayo, uamuzi wa sasa haupaswi kutenganishwa na historia ya Nchimbi ndani ya CCM. 

Huyu si mwanasiasa mgeni; amepitia ngazi mbalimbali za chama na Serikali, amewahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM na baadaye akawa mgombea mwenza wa Rais Samia katika Uchaguzi Mkuu wa 2025. 

Agosti 2025, Nchimbi aliondoka kwenye nafasi ya Katibu Mkuu baada ya CCM kumteua Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro kushika nafasi hiyo, huku yeye akipewa jukumu la kuwa mgombea mwenza. Baada ya ushindi wa CCM, akaingia Ikulu kama Makamu wa Rais.

Safari hiyo ndefu ndiyo inayofanya hatua ya leo kuwa na uzito mkubwa zaidi. Nchimbi amewahi pia kukumbana na hatua za kinidhamu ndani ya CCM katika historia yake ya kisiasa, jambo linaloonesha kwamba suala la nidhamu kwake si jambo jipya. 

Kwa hiyo, kama NEC imefikia uamuzi wa kumvua uanachama baada ya kupitia taratibu zake, jambo la msingi si ukubwa wa jina la Nchimbi, bali kama chama kimefuata Katiba na kanuni zake katika kufikia uamuzi huo. 

Chama kinapoweka kanuni halafu kikashindwa kuzitekeleza dhidi ya viongozi wake wakubwa, kinadhoofisha mamlaka yake yenyewe; lakini kinapozitekeleza bila kujali cheo, kinaimarisha taasisi.

Uamuzi huu pia unatuma ujumbe muhimu kwa makada wengine wa CCM kwamba uanachama ni dhamana yenye masharti, si leseni ya kufanya kila jambo bila kuwajibika. 

CCM imekuwa ikijenga hoja ya chama chenye nidhamu, mshikamano na kuheshimu maamuzi ya vikao. 

Hivyo, pale mwanachama anapokiuka misingi hiyo, hatua ya kinidhamu haipaswi kutafsiriwa moja kwa moja kama chuki binafsi au kisasi cha kisiasa. Kinyume chake, inaweza kuwa sehemu ya utaratibu wa kujilinda kwa taasisi. 

Aidha, NEC inapaswa kupongezwa kwa kuonesha kwamba CCM ni kubwa kuliko mtu mmoja. 

Nchimbi ameitumikia Serikali kwa vipindi mbalimbali, amewahi kuwa Waziri, mwanadiplomasia na kiongozi wa juu wa chama kabla ya kufikia nafasi ya Makamu wa Rais. 

Lakini taasisi inayodumu haiwezi kujengwa kwa kumlinda mtu kwa sababu ya historia yake. Inajengwa kwa kuheshimu kanuni zilezile kwa viongozi wakubwa na wanachama wa kawaida. 

Hata kujiuzulu kwake kwa hiari kutoka nafasi ya Makamu wa Rais hakufuti wajibu wa chama kushughulikia mwenendo wake kama kuna ukiukaji wa kanuni za uanachama. Kujiuzulu kwenye nafasi ya Serikali na kuwajibika ndani ya chama ni mambo mawili tofauti. 

Kwa hiyo, hatua ya NEC inapaswa kuchukuliwa kama onyo la kisiasa na mafunzo ya kinidhamu kwa CCM nzima. Ni ujumbe kwamba uaminifu kwa chama haupimwi kwa ukubwa wa nafasi uliyowahi kushika, bali kwa namna unavyoheshimu Katiba, kanuni, maamuzi na maadili ya taasisi. 

CCM ikitaka kubaki imara, lazima kanuni ziwe juu ya watu; na uamuzi wa NEC kuhusu Nchimbi ni ukumbusho kwamba ndani ya chama, hakuna cheo kinachopaswa kuwa kinga dhidi ya uwajibikaji.

CCM Yampendekeza Ndejembi Kuwa Makamu wa Rais

Global Publishers
August 27, 2026
36 views
0 Comments

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro, ametangaza kuwa vikao vya Chama hicho vilivyokutana jana na leo jijini Dar es Salaam vimempitisha kwa kauli moja Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, kuwa mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dkt. Migiro amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya vikao husika vya CCM kujadili na kuridhia jina la Mhe. Ndejembi, ambaye ni mwanachama wa chama hicho, kwa ajili ya kujaza nafasi hiyo iliyo wazi kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Makamu wa Rais, Dkt. Emmanuel Nchimbi.

Amesema baada ya taratibu za ndani ya chama kukamilika, jina la Mhe. Ndejembi litawasilishwa Bungeni kwa ajili ya kuthibitishwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Samia Akutana na Kamati Kuu ya CCM Katika Kikao Maalum Dar

Global Publishers
August 26, 2026
42 views
0 Comments

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiongoza Kikao Maalum cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM kilichofanyika jijini Dar Es Salaam leo, Jumatano tarehe 26 Agosti 2026.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Jumatano, Agosti 26, 2026, ameongoza Kikao Maalum cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho maalum kimefanyika jijini Dar es Salaam huku kikiongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kikao hicho ni sehemu ya shughuli za chama zinazofanywa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa Chama.

Taarifa zaidi kuhusu ajenda na maazimio ya kikao hicho zitatolewa na CCM endapo kutakuwa na taarifa rasmi kuhusu yaliyofikiwa katika kikao hicho.

Kesi ya Uhaini: Lissu Akabiliana na Maswali ya Upande wa Jamhuri

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ameanza kukabiliana na maswali ya upande wa Jamhuri baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake mkuu katika kesi ya uhaini inayomkabili.

Dodoso hilo limeanza baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, kuahirisha mwenendo wa kesi kwa muda wa saa moja na nusu baada ya Lissu kukamilisha ushahidi wake wa msingi.

Mawakili wa upande wa Jamhuri, wakiongozwa katika hatua hiyo na Nassoro Katuga, wameanza kumuuliza Lissu maswali mbalimbali yanayohusu ushahidi alioutoa mbele ya jopo la majaji watatu.

Mwanzoni mwa dodoso hilo, Katuga alimpongeza Lissu kwa ushahidi mrefu alioutoa kabla ya kumtaka athibitishe kuwa anafahamu kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mchakato wa kisheria.

Lissu alikubaliana na kauli hiyo, akisisitiza kuwa yeye ni wakili wa Mahakama Kuu na ana uelewa wa sheria.

Nassoro Katuga: Shahidi pole na ushahidi mrefu

Lissu: Ahsante sana

Katuga: Kama nimekusikia vyema ulisema utatuacha sisi ndugu zako tukuulize maswali.

Lissu: Sahihi.

Katuga: Waambie majaji hiki tunachokifanya ni kitu cha kisheria na hakina nasaba nyingine yeyote.

Katuga: Uliiambia mahakama wewe ni wakili wa mahakama kuu na una ujuzi wa kisheria.

Lissu: Ndio

Katuga: Hebu waambie majaji Tanzania ilipata uhuru mwaka gani.

Lissu: 9/12/1961

Katuga: Kwa majibu hayo Tanzania ni nchi huru.

Lissu: Ndio

Katuga: Chombo cha mwisho cha kufanya maamuzi ya mwisho kwa mujibu wa kisheria ni ni kipi?

Lissu: Mahakama

Katuga: Mahakama haitakiwi kuingiliwa na mtu yeyote inapotoa maamuzi na pia mahakama hailazimishwi wala haipingwi na mtu au chombo chochote toka nje au ndani.

Lissu: Sahihi haipangiwi walakulazimishwa.

Katuga: Umetuambia wewe ni Mwenyekiti wa Chadema, Je katika utetezi wako umeimbia mahakama hii kuwa mwenyekiti wa Chadema ana kinga?

Lissu; Hapana na sina kinga hiyo

Katuga: Ndugu shahidi kama nilikupata vyema ulieleza sifa nyingi kukuhusu wala sizikatai iambie mahakama hizi tuzo ulizopewa ziko kwenye form gani kama maandishi au katika hali gani.

Lissu: Ziko katika hali ya maandishi, na ile alama yenyewe

Katuga: Ka object flani hivi.

Lissu: Ndio

Katuga: Embu iambie haya matuzo yote haya umeyaleta mahakamani

Lissu: Hapana na sina sababu ya kuyaleta.

Katuga: Twende pole pole tutakuwa na siku saba hapa.

Lissu: Hakuna neno

Katuga: Wewe umeleta nini hapa

Lissu: Maneno

Katuga: Sasa wewe uliposema mashahidi wa jamuhuri wameleta meneno ulimaanisha nini?

Lissu: Siwajibiki kufanya hivyo mimi nimeleta maneno sababu sina kesi ya kuthibitisha

Katuga: Sheria inasemaje?

Lissu: Sheria inataka mtu alete ushahidi pamoja na vithibitisho

Katuga: Unajua usilete ujuaji

Lissu: Yes mimi mjuaji

Katuga: Principles gani zinakutaka ulete maneno bila vithibitisho?

Lissu: Mimi sina wajibu wa kuthibitisha lolote.

Katuga: Unajua kifungu cha sheria kinasema yule anasema ana wajihi fulani anapaswa kuthibitisha.

Lissu: Ndio ninathibitisha

Katuga: Ulisema mahakama ni chombo huru wale uliosema wameelekeza uachiwe na unakubali mahakama ni chombo huru ndani ya nchi huru ya Tanzania?

Lissu: Ndio, Kamati ya haki za binadamu ya Umpja wa Mataifa

Katuga: Shahidi kuna mahali popote kwenye ushahdi wako kuna umekanusha maneno haya ya tunakwenda kukinukisha kweli kweli?

Lissu: Nimesema hivi maneno hayo ukitaka kuyaelewa unabidi usikilize hotuba yote.

Katuga: Mimi siwezi kukuuliza una akili timamu wewe ni kaka yangu

Lissu: Niulize tu

Katuga: Siwezi swali langu kuna mahali umekanusha maneno haya

Lissu: Hapana

Katuga: Kwa maana hiyo maneno haya huyakatai

Lissu: Siyakatai wala hayana shida.

Katuga: Nilitaka tu hicho

Lissu: Nimesema mara kadhaa.

Harmonize Afichua Wasanii Walio kwenye Albamu Yake Mpya “31”

Msanii wa Bongo Fleva, Harmonize, ameweka wazi orodha ya nyimbo zitakazopatikana katika albamu yake mpya inayokwenda kwa jina la “31”, ambayo inatarajiwa kutoka hivi karibuni.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Harmonize ameshirikisha mashabiki wake orodha ya nyimbo 14 zitakazounda albamu hiyo, huku akitangaza kuwa inatarajiwa rasmi kutoka Septemba 4, 2026.

Albamu hiyo imebeba ushirikiano mbalimbali kutoka kwa wasanii wakubwa ndani na nje ya Tanzania, akiwemo Marioo, Young Lunya, Jay Melody, Mayorkun, Darkoo, Yemi Alade, Rayvanny na Sofia Nzau, pamoja na wasanii wengine.

Kwa mujibu wa orodha hiyo, Harmonize anatarajiwa kuendelea kuonyesha uwezo wake wa kuunganisha muziki wa Bongo Fleva na ladha mbalimbali za kimataifa kupitia nyimbo zitakazopatikana kwenye albamu hiyo.

Harmonize, ambaye ni miongoni mwa wasanii waliofanikiwa kujenga jina kubwa katika muziki wa Tanzania, tayari ameachia albamu kadhaa zilizofanya vizuri, zikiwemo “Afro East” iliyotoka mwaka 2020, “High School” mwaka 2021 na “Made For Us” mwaka 2022.

Kwa sasa, Harmonize anaendelea kufanya vizuri kupitia wimbo wake “Beautiful”, ambao pia umejumuishwa katika albamu mpya ya “31”.

Albamu hiyo inatarajiwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya Harmonize kwa mwaka huu, huku mashabiki wakisubiri kwa hamu kuona namna atakavyowasilisha kazi hizo mpya pamoja na ushirikiano wa wasanii mbalimbali.

Stori na Na Didas Didas | GPL

Airtel Fursa Lab Yazinduliwa Upya, Zaidi ya Watu 5,800 Wanufaika

Dar es Salaam. Wanafunzi, walimu na vijana nchini Tanzania wamepata fursa mpya ya kujifunza na kuendeleza ubunifu wa kiteknolojia baada ya Airtel Africa Foundation kuzindua upya jengo la Airtel Fursa Lab lililopo katika Shule ya Sekondari Kijitonyama, Dar es Salaam.

Airtel Fursa Lab ilianzishwa mwaka 2020 kupitia ushirikiano kati ya Airtel Africa Foundation na Dar Teknohama Business Incubator (DTBi), ikiwa na lengo la kuwawezesha wanafunzi, walimu na vijana kupata ujuzi wa kidijitali, kufanya majaribio na kubuni suluhisho za changamoto zinazowakabili katika maisha ya kila siku.

Tangu kuanzishwa kwake, zaidi ya watu 5,800 wamenufaika na kituo hicho, wakiwemo wanafunzi, walimu, vijana, wajasiriamali na wanawake.

Kituo hicho pia kimekuwa kikitoa fursa kwa wanafunzi waliomaliza Darasa la Saba, Kidato cha Nne na Kidato cha Sita pamoja na wahitimu wa vyuo vikuu kupata ujuzi katika teknolojia, biashara, ubunifu na stadi nyingine za maisha.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa jengo hilo lililokarabatiwa, Mkuu wa Programu kutoka Airtel Africa Foundation, Esi Prah, alisema uwekezaji huo unalenga kuwapa vijana mazingira na zana zinazowawezesha kutumia teknolojia kwa vitendo.

“Tunaamini kuwa upatikanaji wa teknolojia na elimu ya kidijitali unaweza kubadilisha maisha ya vijana kwa kuwapatia maarifa, ujasiri na ujuzi wanaohitaji ili kutengeneza suluhu mbalimbali na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali,” alisema Prah.

Alisema Airtel Fursa Lab imejengwa katika dhana ya kuwapa vijana nafasi ya kujifunza, kufanya majaribio na kugeuza mawazo yao kuwa suluhisho zinazoweza kutumika katika jamii.

Katika kituo hicho, wanafunzi hupata mafunzo na kufanya mazoezi katika maeneo mbalimbali, yakiwemo sayansi ya kompyuta, programu za kompyuta, biashara, stadi za maisha, chakula na lishe pamoja na ushonaji na ubunifu.

Airtel Fursa Lab pia imewaunganisha wanafunzi na majukwaa mbalimbali ya kujifunzia kama ShuleDirect, Maktaba ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na WazoLearn, pamoja na maudhui yanayotumia teknolojia ya akili mnemba (AI).

Kwa miaka kadhaa, kituo hicho kimekuwa sehemu ya kukuza vipaji na ubunifu kwa wanafunzi, huku baadhi ya walionufaika wakifanikiwa kushiriki katika programu mbalimbali na kuwa Mabalozi wa UNICEF na Plan International, wabunifu wa Oky, wasanii wa kidijitali na wabunifu katika sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM).

Miongoni mwa miradi iliyobuniwa na wanafunzi ni programu ya kufuatilia mzunguko wa hedhi iliyolenga kuwasaidia wasichana kupata taarifa na kufuatilia mizunguko yao.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Beatrice Singano, alisema ufunguzi huo mpya unaonyesha dhamira ya kampuni hiyo ya kupanua fursa za elimu ya kidijitali kwa vijana nchini.

“Ukarabati na ufunguzi upya wa Airtel Fursa Lab unaakisi dhamira yetu ya kuhakikisha vijana wa Tanzania wanapata zana, maarifa na fursa wanazohitaji ili kufanikiwa katika dunia ya kidijitali,” alisema Singano.

Alisema lengo ni kuhakikisha teknolojia inatumika kama nyenzo ya elimu, ubunifu na kujenga fursa za kiuchumi, badala ya kubaki kuwa chombo cha mawasiliano pekee.

“Kupitia ushirikiano wetu, Airtel sasa imeunga mkono zaidi ya shule tano, na tutaendelea kufanya kazi na washirika wetu kuwafikia vijana na jamii nyingi zaidi,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Kijitonyama, Halima Juma, alisema Airtel Fursa Lab imekuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya shule hiyo katika TEHAMA na ubunifu.

“Tangu mwaka 2020, Fursa Lab imewawezesha wanafunzi na walimu wetu kupata ujuzi wa kidijitali, mafunzo ya vitendo na fursa za ubunifu,” alisema Juma.

Alisema kituo hicho kimepanua wigo wa shule kwa kuwapa vijana kutoka nje ya shule hiyo nafasi ya kupata maarifa na ujuzi wa kidijitali.

Matokeo ya uwekezaji huo yanaonekana pia katika mafanikio ya Shule ya Sekondari Kijitonyama, ambayo imeorodheshwa katika nafasi ya 10 kitaifa katika TEHAMA kwa miaka mitatu mfululizo.

Aidha, wanafunzi wa shule hiyo wameshinda tuzo tatu katika mashindano ya Girls in ICT, yanayolenga kuhamasisha ushiriki wa wasichana katika teknolojia.

Miongoni mwa wanafunzi walionufaika na Fursa Lab ni Angel Swai, ambaye amebuni suluhisho la taa za kuongozea magari linalotumia akili mnemba (AI).

Angel alisema Fursa Lab imemsaidia kwenda zaidi ya nadharia anayojifunza darasani na kupata nafasi ya kufanya majaribio ya mawazo yake.

“Airtel Fursa Lab imenipa nafasi ya kujifunza, kufanya majaribio na kubadilisha mawazo yangu kuwa kitu cha vitendo,” alisema.

Alisema mazingira na rasilimali zinazopatikana katika kituo hicho zimemsaidia kuelewa namna teknolojia na AI zinavyoweza kutumika kutatua changamoto halisi katika jamii.

“Ubunifu wangu ni mfano wa kile ambacho vijana wanaweza kufanikisha wanapopewa zana na fursa zinazofaa,” alisema.

Ukarabati wa Airtel Fursa Lab unatarajiwa kuendelea kutoa nafasi kwa wanafunzi, walimu na vijana wengine kujifunza ujuzi wa kidijitali, kufanya majaribio na kukuza ubunifu.

Shule ya Sekondari Kijitonyama imeishukuru Airtel Africa Foundation, Airtel Money, DTBi na Serikali ya Tanzania kwa kuunga mkono mpango huo na kuongeza fursa za elimu ya kidijitali kwa wanafunzi, walimu na jamii kwa ujumla.

TAMASHA LA KITAIFA LA UTAMADUNI LAIMARISHA UMOJA NA URITHI×

Na Lilian Kasenene, Morogoro 

Matukio DaimaApp

Tanzania inaendelea kuhamasisha mshikamano, umoja na utaifa, kulinda maadili, kuhifadhi mila na desturi pamoja na kuendeleza urithi wa kitamaduni, kupitia Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni linaloendelea mkoani Morogoro.

Tamasha hilo, linalofanyika huku vikundi vya ngoma kutoka mikoa 27 ya Tanzania vikishiriki, limekuwa jukwaa la kuonesha utajiri wa mila, desturi na tamaduni za maeneo mbalimbali nchini.

Kupitia ngoma, sanaa na maonesho mbalimbali, washiriki wamewasilisha jumbe zenye umuhimu kwa jamii, ikiwemo kuhamasisha mshikamano, umoja na utaifa, kulinda maadili, kuhifadhi mila na desturi pamoja na kuendeleza urithi wa kitamaduni kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Tamasha hilo pia limekuwa fursa ya kuibua, kukuza na kutangaza vipaji vya wasanii na vikundi vya sanaa za asili, huku wananchi wakipata nafasi ya kujifunza na kuthamini tamaduni za makabila na maeneo mbalimbali ya Tanzania.

Aidha, tamasha hilo limefungua fursa za kiuchumi kupitia bidhaa za sanaa na ubunifu, kazi za mikono, vyakula vya asili na shughuli nyingine zinazohusiana na sekta ya utamaduni, zinazowawezesha wasanii, wajasiriamali na wananchi kuongeza kipato.

Mbali na burudani, tamasha hilo linaimarisha mawasiliano na mshikamano miongoni mwa jamii, huku likihamasisha matumizi ya sanaa katika kuelimisha jamii na kukuza kizazi kinachotambua na kuthamini historia, mila na desturi za Tanzania.

Vilevile, tamasha hilo linachangia kuitangaza Tanzania kupitia utamaduni, sanaa na ubunifu, pamoja na kuchochea utalii wa kitamaduni kwa kuvutia wageni kutoka ndani na nje ya nchi.

Kwa ujumla, Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni ni sehemu muhimu ya juhudi za kulinda na kuendeleza urithi wa kitamaduni, kukuza vipaji, kuimarisha umoja na utaifa na kuchochea shughuli za kiuchumi, huku likihakikisha utajiri wa tamaduni za Tanzania unaendelea kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Mwisho.

Tundu Lissu Amaliza Kujitetea, Mahakama Yapumzika kabla ya Dodoso

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, leo Jumatano, Agosti 26, 2026, amehitimisha sehemu ya kwanza ya ushahidi wake katika kesi ya uhaini inayomkabili Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.

Lissu ametoa ushahidi wake mbele ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiwa na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.

Katika ushahidi wake, Lissu ameelekeza sehemu kubwa ya maelezo yake katika kuichambua hoja na ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka, akidai kuwa kuna mapungufu ambayo, kwa mtazamo wake, yanashindwa kuthibitisha shtaka linalomkabili kwa kiwango kinachotakiwa kisheria.

Lissu amesema upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi 17 kati ya 30 waliokuwa wameorodheshwa awali, akiwemo maafisa wa polisi pamoja na mashahidi waliolindwa ambao utambulisho wao haukuwekwa wazi kwa umma.

Katika hatua nyingine ya ushahidi wake, Lissu amepinga uzito wa ushahidi wa baadhi ya mashahidi wa upande wa mashtaka, akidai kuwa baadhi yao walikuwa wamewahi kukamatwa na polisi na baadaye kuachiwa baada ya kukubali kutoa ushahidi dhidi yake.

Pia amerejea baadhi ya vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani, akiwemo maelezo ya onyo ya baadhi ya mashahidi wa upande wa mashtaka, huku akisisitiza kuwa vielelezo hivyo vinapaswa kutumika katika kutathmini kama mashtaka dhidi yake yamethibitishwa.

Awali, katika siku zake za kwanza za kutoa ushahidi, Lissu alieleza historia yake ya muda mrefu katika harakati za demokrasia, utawala bora na mageuzi ya mfumo wa uchaguzi nchini Tanzania. Pia alikanusha kuwa alikuwa na nia ya kufanya uhaini kupitia kauli alizotoa katika mkutano wa CHADEMA wa Aprili 3, 2025, ambao ndio unaohusishwa na shtaka linalomkabili.

Baada ya Lissu kumaliza ushahidi wake mkuu, mwenendo wa kesi umeahirishwa kwa muda wa saa moja na nusu, huku ikitarajiwa kurejea saa 8:30 mchana kwa hatua inayofuata ya dodoso kutoka upande wa mashtaka.

Katika hatua hiyo, Lissu anatarajiwa kuhojiwa na mawakili wa upande wa mashtaka kuhusu ushahidi alioutoa katika utetezi wake. Endapo muda utaruhusu, mashahidi wengine wa upande wa utetezi wanaweza kuanza kutoa ushahidi wao.

Kesi hiyo ni Criminal Session Case No. 19605/2025, Jamhuri dhidi ya Tundu Lissu, na inaendelea mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu ya Tanzania.