TAFORI KUTAFUTA SULUHISHO LA MOTO WA MISITU

Serikali imeitaka Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) kuipa kipaumbele tafiti za kubaini viashiria vya moto wa misitu mapema na kuboresha usimamizi wa moto katika maeneo ya hifadhi, ili kulinda misitu, bioanuai na shughuli za utalii.

Naibu waziri wa Maliasili na Utalii Hamad Hassan Chande ametoa agizo Septemba 21, 2026, wakati akizindua Bodi ya 13 ya Wakurugenzi ya TAFORI kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na utalii Dkt. Ashatu Kijaji  ambapo amesema tafiti zinapaswa kutoa majibu ya kisayansi kuhusu moto unaotumika kama sehemu ya usimamizi wa maeneo ya hifadhi, pamoja na njia za kuzuia moto usio wa lazima na kutoa tahadhari mapema.

Pia ameielekeza TAFORI kuongeza uwezo wa maabara za ndani kupima usalama na ubora wa asali, akisema Tanzania inalenga kutumia fursa ya masoko ya nje, ikiwamo Ulaya, bila kulazimika kupeleka sampuli nje ya nchi. Amesema uwezo huo utapunguza gharama za vipimo na kuongeza ushindani wa asali ya Tanzania.

Aidha ameitaka Bodi kusimamia Mpango Mkakati wa TAFORI wa miaka mitano, 2026/27–2030/31, unaolenga kuimarisha tafiti na matumizi ya matokeo yake katika uhifadhi na maendeleo ya sekta.

Amesema katika kipindi cha Bodi ya 12, TAFORI ilikamilisha tafiti 17, zikiwamo saba za kimkakati, zilizohusu maeneo kama umri wa uvunaji wa misindano na misaji, Alama ya Asali ya Tanzania (Honey Trademark), mchango wa misitu na nyuki katika pato la Taifa kupitia Green Accounting, pamoja na changamoto za ufugaji nyuki. Serikali pia imewezesha fedha kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya Makao Makuu, ujenzi wa Kituo cha Utafiti Tabora, uboreshaji wa maabara na ununuzi wa vitendea kazi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAFORI, Dkt. Revocatus Mushumbusi, amesema taasisi hiyo itatekeleza maelekezo ya Wizara na kuendelea kuimarisha tafiti zenye tija kwa uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu na nyuki. Amesema TAFORI pia itaendelea kujenga uwezo wa watafiti kupitia mafunzo ya juu na uzoefu ndani na nje ya nchi, huku ikiimarisha ushirikiano na taasisi za kitaifa na kimataifa katika tafiti za misitu na ufugaji nyuki.

Wakenya watawala km 21, Watanzania wang’ara km 10 katika Yas Zanzibar International Marathon 2026

Zanzibar, Septemba 20, 2026 – Wanariadha kutoka Kenya wametawala mbio za kilomita 21 za Yas Zanzibar International Marathon 2026, huku Watanzania wakifanya vizuri katika mbio za kilomita 10, katika msimu wa sita wa mashindano hayo yaliyofanyika Viwanja vya Maisara, Zanzibar.

Katika mbio za kilomita 21 kwa upande wa wanaume, Wakenya Justus Nyesya, Ransisi Kamito na Simon Kelenzyo walishika nafasi tatu za juu. Kwa upande wa wanawake, Valentine Chep na Rael Mitieka kutoka Kenya walimaliza nafasi ya kwanza na ya pili, huku Mtanzania Failuna Abdi akishika nafasi ya tatu.

Katika mbio za kilomita 10 kwa wanaume, Watanzania Shedrak Damas na Boay Maganga walishika nafasi mbili za juu, huku Duncan Kipchumba wa Kenya akimaliza katika nafasi ya tatu. Kwa upande wa wanawake, nafasi ya kwanza ilichukuliwa na Mkenya Faith Jeptum, akifuatiwa na Watanzania Anna Dolomong na Dorcas Boniface.

Akifunga mashindano hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hamza Hassan Juma, aliyemwakilisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, alisema mbio hizo zimeendelea kuwa jukwaa muhimu la kukuza michezo na kuitangaza Zanzibar kupitia utalii.

“Mashindano haya yana mchango mkubwa katika kukuza michezo na kuitangaza Zanzibar kama moja ya maeneo muhimu ya utalii, huku yakifungua fursa katika sekta za hoteli, usafiri, biashara na huduma mbalimbali,” alisema Mhe. Juma.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Fedha wa Yas Tanzania, CPA Innocent Rwetabura, alisema katika kipindi cha miaka sita, mbio hizo zimekuwa sehemu muhimu ya kuitangaza Zanzibar, kuhamasisha mtindo bora wa maisha na kuchochea uchumi wa buluu.

Rwetabura alisema Yas imeendelea kuwekeza Zanzibar, ambapo mtandao wake umeenea kwa takribani asilimia 99 ya maeneo ya Zanzibar, huku zaidi ya minara 60 mipya ikikamilishwa mwaka huu kwa kushirikiana na Serikali na UCSAF. Kupitia Yas Fiber, kampuni hiyo pia imeingia makubaliano na ZICTIA kuwekeza zaidi ya Sh bilioni 300 katika miundombinu ya fiber.

Aliongeza kuwa kupitia Mixx, kampuni hiyo imeendelea kuimarisha huduma za fedha kidijitali Zanzibar, ikiwemo kurahisisha usajili na malipo ya mbio hizo kwa Watanzania. Pia imeendelea kurahisisha huduma kwa wakulima kupitia ushirikiano na ZSTC, huku ushirikiano na ZanBus ukisaidia kurahisisha malipo ya nauli kidijitali kwa wakazi wa Zanzibar.

Rwetabura alisema Mixx pia imeendelea kufanya ushirikiano mbalimbali na taasisi za Zanzibar, ikiwemo ushirikiano wa hivi karibuni na ZANGOF pamoja na ZMBF, unaolenga kupanua huduma za kidijitali kwa makundi mbalimbali, yakiwemo wakulima wa mwani.

Yas pia imeendelea na programu za kijamii Zanzibar, ikiwemo kutoa intaneti bila malipo katika shule zaidi ya 50 za Serikali, kuendesha kambi za huduma za macho na Kampeni ya Tumaini inayolenga kusaidia huduma za afya ya mama na mtoto.

Mashindano hayo yalihusisha mbio za kilomita 21, 10 na 5, na kuwakutanisha wanariadha kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali.

Moscow Yaonyesha Teknolojia na Fursa kwa Vijana 10,000 Katika Tamasha la Kimataifa

YEKATERINBURG, URUSI: Kuanzia Septemba 11 hadi 17, 2026, jiji la Yekaterinburg limekuwa mwenyeji wa International Youth Festival 2026, iliyowakutanisha washiriki 10,000 kutoka nchi 191.

Katika tamasha hilo, Moscow imewasilisha banda shirikishi lenye kaulimbiu “Moscow — City of the Future”, linalowawezesha wageni kufahamu historia ya jiji hilo, teknolojia za kisasa pamoja na shughuli mbalimbali za ubunifu.

Kupitia eneo la mradi wa “Youth of Moscow”, washiriki waliweza kutengeneza vikuku na mapambo maalum ya mifuko, huku wakipata taarifa kuhusu fursa zinazotolewa kwa ajili ya maendeleo yao binafsi na kitaaluma. Mradi huo pia huandaa mashindano ya ubunifu, majukwaa ya ajira na kozi za elimu bila malipo katika nyanja mbalimbali.

Banda hilo pia lina eneo maalum la chai, ambapo wageni wanaweza kufahamu utamaduni wa Moscow wa kunywa chai na kuonja bila malipo mchanganyiko maalum wa chai wa jiji hilo.

Kupitia ukumbi wa teknolojia ya uhalisia pepe (VR), wageni waliweza kupata uzoefu wa kutembelea kwa njia ya kidijitali baadhi ya maeneo maarufu ya Moscow. Paneli shirikishi pia zinawawezesha kufahamu huduma za kidijitali za jiji hilo na namna teknolojia inavyorahisisha maisha ya kila siku.

Wageni wanaweza pia kuchunguza nakala za kidijitali za Central Alley ya VDNH, Cosmos Pavilion na Pavilion No. 1 kupitia VDNH Metaverse.

Kwa upande wa ajira, wataalamu wenye sifa wanatoa ushauri wa mtu mmoja mmoja kuhusu fursa za ajira na maendeleo ya taaluma. Eneo la maudhui ya picha na video linaonyesha pia ubunifu wa hivi karibuni wa Moscow.

Katika kituo cha Russian Post, washiriki waliweza kutuma kadi za posta kwenda sehemu mbalimbali duniani.

Aidha, eneo la mapumziko lina vituo vya kompyuta kibao vinavyowawezesha wageni kufahamu RUSSPASS, huduma ya kidijitali ya utalii ya Moscow. Kupitia Route Planner, wageni wanaweza kupanga ratiba binafsi za safari na kupata njia zinazolingana na maeneo wanayopendelea.

Timu ya Moscow pia imeandaa mkusanyiko maalum wa pini za chuma zenye alama maarufu za jiji hilo, zilizotengenezwa mahsusi kwa ajili ya washiriki wa tamasha.

Wageni waliweza pia kupiga picha katika eneo la “Katyusha the Panda”, sanamu ya kisanii iliyopewa msukumo na mmoja wa wanyama maarufu wa Moscow Zoo.

Aidha, chapa 35 kutoka Moscow zinaonyeshwa katika Art.Molodost International Design and Merchandise Market, ikiwa na bidhaa kutoka katika sekta mbalimbali. Washiriki na wageni pia wana fursa ya kufahamu zaidi kuhusu sekta ya filamu ya Moscow.

Banda la “Moscow — City of the Future” limeandaliwa na “Youth of Moscow”, mradi wa Moscow Committee for Public Relations and Youth Policy.

Zaidi ya watu 230 waliojitolea kutoka Moscow walishiriki katika uendeshaji wa tamasha hilo kupitia maeneo 17 ya kazi. Majukumu yao yalijumuisha usajili na usafirishaji, kusaidia ujumbe wa Urusi na kimataifa pamoja na wataalamu, kuwasaidia washiriki wenye uhitaji wa msaada wa uhamaji, kutoa huduma za ukalimani, kuandaa ziara za kuongozwa na kutengeneza maudhui kwa ajili ya mitandao ya kijamii.

Wajitolea hao pia waliwasaidia wageni kufahamu maeneo mbalimbali ya tamasha, kushughulikia masuala ya kiutawala na kuchangia katika kuhakikisha washiriki wanapata mazingira mazuri na yenye ukarimu katika maeneo yote ya tamasha.

Waziri Mkuu Ahimiza Nchi Za Afrika Ziongeze Mapambano Dhidi Ya Sotoka

Global Publishers
September 21, 2026
0 views
0 Comments

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amezitaka nchi za Afrika na washirika wa kimataifa ziweke kipaumbele kwenye ajenda ya kutokomeza ugonjwa wa sotoka kwa mbuzi na kondoo (Peste des Petits Ruminants-PPR) kwa kuimarisha misaada ya kifedha na ya kiufundi.

“Mpango wa kutokomeza PPR si uwekezaji katika afya ya mifugo pekee, bali pia ni uwekezaji katika usalama wa chakula, kupunguza umaskini, kukuza biashara ya mifugo na kuimarisha ustahimilivu wa kiuchumi kwa wananchi. Tunatakiwa kuhakikisha ajenda hii inaendelea kupewa kipaumbele katika ngazi za kitaifa, kikanda na kimataifa ili kufikia lengo hili,” amesema.

Ametoa wito huo leo (Jumatatu, Septemba 21, 2026) wakati akitoa hotuba kuu kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi wa mkutano wa siku tatu wa Kimataifa wa Kujadili Afya Moja na Mifumo ya Chakula na Kilimo ulioanza leo katika Makao Makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), jijini Roma, Italia.

Akielezea mafanikio ya Tanzania katika kutokomeza ugonjwa wa sotoka, Waziri Mkuu amesema Serikali ililifanya suala hilo kuwa jambo kitaifa na inaendelea kutetea jitihada za kutokomeza ugonjwa huo barani Afrika.

“PPR si tu tatizo la afya ya wanyama. Kwa mamilioni ya kaya za wafugaji, hasa zile zinazotegemea kondoo na mbuzi, ni tishio kwa usalama wa chakula, mapato ya kaya, biashara na maisha,” amesema.

Katika mwaka wa fedha 2025/2026, Dkt. Mwigulu amesema Tanzania ilichanja kondoo na mbuzi milioni 16.8 dhidi ya sotoka na ilifanikiwa kufikia sehemu kubwa ya wanyama 17.2 waliolengwa kupata chanjo katika maeneo hatarishi.

“Kwa mwaka 2026/2027, zaidi ya sh. bilioni 30.8 (takriban dola milioni 11.6) zimetengwa kuendeleza awamu ya pili ya kampeni. Uzoefu wetu umetupa somo rahisi kwamba sotoka haiwezi kuondolewa kwa chanjo pekee bali kunahitajika jitihada zaidi. Inahitaji uchunguzi, utambuzi na ufuatiliaji wa wanyama, huduma sahihi kwa mifugo, ushirikiano baina ya nchi na nchi, na ufadhili endelevu.”

Taifa Stars Yajifua Gymkhana Kuelekea Mechi Za Kimataifa

Global Publishers
September 21, 2026
6 views
0 Comments

Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imeendelea na maandalizi yake katika Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam, chini ya Kocha Mkuu Miguel Ángel Gamondi. Kambi hiyo ilianza Septemba 19, 2026.

Taifa Stars inajiandaa kwa michezo dhidi ya Guinea-Bissau na Madagascar katika ratiba ya kimataifa ya Septemba. Tanzania itacheza dhidi ya Guinea-Bissau Septemba 25, 2026, katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Baada ya mchezo huo, Taifa Stars inatarajiwa kuelekea Casablanca, Morocco, kwa ajili ya mchezo dhidi ya Madagascar utakaochezwa Septemba 29, 2026. Aidha, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepanga mchezo wa kirafiki dhidi ya Ghana Oktoba 4, 2026.

TFF pia imetangaza kufanyika kwa Mashabiki Day Septemba 23, ambapo mashabiki watapata nafasi ya kushuhudia mazoezi pamoja na kupiga picha na wachezaji na benchi la ufundi. Waandishi wa habari wamepangiwa Septemba 21 kwa ajili ya kufanya mahojiano na timu.

Maandalizi hayo yanaendelea huku benchi la ufundi likitumia kambi hiyo kuimarisha kikosi kabla ya michezo hiyo ya kimataifa.

Na Anifa Mwegelo | GPL -TUDACO

Simba 10 Wakutwa Wamekufa Ngorongoro, Chanzo Chachunguzwa

Global Publishers
September 21, 2026
12 views
0 Comments

Simba 10 wamekutwa wamekufa katika eneo la Ndutu, ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, mkoani Arusha, huku mamlaka zikianzisha uchunguzi wa kitaalamu kubaini chanzo cha vifo hivyo na iwapo kuna wahusika.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), mizoga ya simba hao iligunduliwa Septemba 18, 2026, katika eneo la Ndutu, Kata ya Endulen.

Uchunguzi wa awali umeonyesha uwezekano wa simba hao kufa baada ya kula au kuingiza sumu mwilini. Hata hivyo, mamlaka zinaendelea na uchunguzi ili kuthibitisha chanzo halisi cha vifo hivyo na kubaini iwapo kuna waliohusika.

NCAA imesema taarifa zaidi kuhusu tukio hilo zitatolewa baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa kitaalamu.

Tukio hilo limeibua wasiwasi kuhusu usalama wa wanyamapori katika eneo la Ngorongoro, ambalo ni miongoni mwa maeneo muhimu ya uhifadhi wa wanyamapori nchini Tanzania.

Na Haika Urio | GPL -TUDACO

Yanga Yatikisa Afrika, Wachezaji 12 Waitwa Timu Za Taifa

Global Publishers
September 21, 2026
0 views
0 Comments

Yanga imeendelea kuthibitisha ukubwa wake barani Afrika baada ya wachezaji wake 12 kuitwa kuziwakilisha timu zao mbalimbali za taifa.

Hali hiyo inaonyesha ubora wa kikosi cha Wananchi pamoja na uwekezaji mkubwa uliofanywa na uongozi katika kusajili nyota wa kiwango cha kimataifa.

Wachezaji hao wameitwa kujiunga na vikosi vya mataifa yao kwa ajili ya michezo ya kalenda ya FIFA, ikihusisha mechi muhimu za kufuzu. Idadi hiyo kubwa inaiweka Yanga kwenye orodha ya klabu zinazoongoza kwa kutoa wachezaji wengi kwenye timu za taifa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.

Nyota hao 12 wanawakilisha mataifa mbalimbali, huku Taifa Stars ya Tanzania ikichukua fungu kubwa la wachezaji wazawa, akiwemo Dickson Job, Ibrahim Bacca, Mudathir Yahya na Clement Mzize, ambao wamekuwa sehemu muhimu ya kikosi cha taifa.

Kwa upande wa wachezaji wa kigeni, mlinda mlango mahiri Djigui Diarra anaendelea kuaminiwa kwenye kikosi cha timu yake ya taifa ya Mali, huku kiungo mshambuliaji Stephane Aziz Ki akijumuishwa kwenye kikosi cha Burkina Faso.

Wengine kutoka mataifa mbalimbali wamejiunga na timu zao za taifa kwa ajili ya kusaidia kupata matokeo mazuri.

Wakati mashabiki wa Yanga wakijivunia hatua hiyo, hali hii pia inaleta mtihani na changamoto ya kipekee kwa benchi la ufundi la klabu hiyo, kwani kocha mkuu analazimika kubaki na kikosi kidogo cha wachezaji ili kuendelea na programu za mazoezi.

Hata hivyo, faida kubwa ni kwamba wachezaji hao wanatarajiwa kurejea wakiwa wamepata uzoefu zaidi wa mechi za kimataifa, jambo linaloweza kuwa na manufaa kwa Yanga inaposhiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Sasa macho ya wapenzi wa soka nchini yanaelekezwa kuona jinsi nyota hao watakavyoiwakilisha vyema Yanga pamoja na mataifa yao katika mechi zijazo.

Na Peter Jinanai | GPL -TUDACO

Sheikh Ahmed Bin Rashid Al Maktoum Afariki Dunia, Dubai Yatangaza Siku 10 Za Maombolezo

Global Publishers
September 21, 2026
6 views
0 Comments

Sheikh Ahmed bin Rashid Al Maktoum, mdogo wa Mtawala wa Dubai, Sheikh Mohammed bin Rashid Al Maktoum, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 76, kwa mujibu wa taarifa ya Mahakama ya Mtawala wa Dubai iliyotolewa Jumatatu, Septemba 21, 2026.

Kufuatia kifo hicho, Dubai imetangaza siku 10 za maombolezo rasmi kuanzia Septemba 21, ambapo bendera zitapeperushwa nusu mlingoti katika kipindi hicho.

Sheikh Ahmed alikuwa mwanachama wa familia inayotawala Dubai na alishikilia nyadhifa mbalimbali katika sekta za usalama na kijeshi, ikiwemo nafasi ya Naibu Mwenyekiti wa Polisi na Usalama wa Dubai. Pia aliwahi kuwa Naibu Mtawala wa pili wa Dubai.

 

Watu 12 Wafariki Ajali ya Lori na Gari la Jeshi la Polisi Singida

Watu 12 wamefariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyohusisha lori na gari la Jeshi la Polisi Tanzania, iliyotokea Septemba 21, 2026 majira ya saa moja na dakika 30 asubuhi katika Barabara ya Singida–Nzega, eneo la Milima Sekenke, Kijiji cha Misigiri, Kata ya Ulemo, Wilaya ya Iramba mkoani Singida.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida, ajali hiyo ilihusisha lori lenye namba za usajili RAF 243X/TRL 4255 mali ya Kampuni ya YYUSSA ya Kigali, Rwanda, na Toyota Land Cruiser yenye namba PT 1982 mali ya Jeshi la Polisi Tanzania.

Lori hilo lilikuwa likiendeshwa na Ndanarasa Christian Alfonse, raia wa Rwanda, likitokea Dar es Salaam kuelekea nchini Rwanda, ambapo lililigonga gari la Jeshi la Polisi aina ya Toyota Land Cruiser lililokuwa likiendeshwa na Stafu Sajenti (S/SGT) Ussi Hassan. Gari hilo lilikuwa likitokea Kituo cha Polisi Shelui kuelekea Kiomboi kwa ajili ya kuwapeleka mahabusu mahakamani.

Waliofariki katika ajali hiyo ni askari watano wa Jeshi la Polisi, ambao ni SP Frank Lazima Mwasapili, aliyekuwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Shelui; S/SGT Ussi Hassan; SGT Paulo Silivin Gabriel; PC Ashraf Salumu Kheri na PC Nangida Ramadhani Mushi.

Aidha, mahabusu saba waliokuwa kwenye gari hilo pia wamefariki. Wao ni Timotheo Lazaro Kimaro na Cassian Hassan, wakazi wa Doromoni; Fred Musuguli Mzoa, Wilfred Marko Amos na Mariam Hamis Kasijao, wakazi wa Mingela, pamoja na Vivian Saidi, mke wa Nsusu, na Hussen Hussein Kea, mke wa Tulya.

Majeruhi wawili wametajwa kuwa ni Petro Organes Nkana, mke wa Mingela, pamoja na Ndanarasa Christian Alfonse, dereva wa lori lililosababisha ajali hiyo. Wanaendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Iramba, Kiomboi, huku miili ya marehemu ikihifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mandewa, Singida.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha ajali hiyo kuwa uzembe wa dereva wa lori, ambaye alishindwa kumudu gari lake na kuhamia upande wa kulia kisha kuligonga gari la Jeshi la Polisi na kusababisha magari yote mawili kutumbukia korongoni.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida limetoa wito kwa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani, ikiwemo hali ya hewa na miundombinu ya barabara, ili kuchukua tahadhari na kuepuka ajali zinazoweza kusababisha vifo, majeruhi na hasara kwa Taifa.

Michezo ya Majeshi yafunguliwa Mwanza – HabariLeo

MWANZA; Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,  Hemed Suleiman Abdulla, amefungua rasmi mashindano ya Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA)  leo Septemba 21, 2026 Uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza.

Mashindano hayo yanayoshirikisha timu za majeshi na vyombo vya ulinzi na usalama kutoka kanda saba, yataendelea hadi Oktoba 5, mwaka huu, yakiwa na kaulimbiu, ‘Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kudumisha amani.’

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Abdulla amesema dhamira ya mashindano hayo si kuimarisha ushindani wa michezo pekee, bali pia kujenga umoja, mshikamano, urafiki na uhusiano meema miongoni mwa vyombo vya ulinzi na usalama.

Amewapongeza viongozi wa vyombo hivyo kwa kuendelea kuthamini michezo kama nyenzo muhimu ya kujenga nidhamu, upendo na mshikamano.

“Natoa wito kwa wananchi tuendelee kuwa wazalendo na kulinda tunu ya amani ya nchi yetu ili kukuza utalii na maendeleo ya sekta mbalimbali zinazogusa maisha ya watu wetu,” amesema.

Amesisitiza umuhimu wa kufanya mazoezi na kuzingatia lishe bora, akieleza kuwa afya ni mtaji muhimu katika kufikia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.

“Mashindano haya yanapaswa kuwa mahali pa kuonesha vipaji, nidhamu na uwezo wa kushindana kwa haki. Nawasihi washiriki na waamuzi kuzingatia kanuni na sheria,” amesema.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Rhimo Nyansaho, amesema mashindano hayo yanaonesha namna serikali inavyoupa umuhimu michezo katika kujenga afya, nidhamu, umoja na mshikamano.

Mkuu wa Majeshi (CD)F Jacob Mkunda, amesema michezo ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama si burudani pekee, bali ni sehemu ya maandalizi ya askari katika kutekeleza majukumu yao.

“Michezo siyo burudani tu bali ni maandalizi ya askari katika kuimarisha ulinzi. Ndani ya jeshi sisi kwetu michezo ni sehemu ya kazi,” amesema.

Awali, Mwenyekiti wa BAMMATA, Meja Jenerali Said Hamis Said, amesema wanamichezo watashindana katika michezo mbalimbali ikiwemo soka, mpira wa mikono, kikapu, wavu, riadha, vishale, kulenga shabaha na netiboli.

Amesema washiriki wanatoka kanda saba ambazo ni Ngome, JKT, Magereza, Uhamiaji, Polisi, Zimamoto na Uokoaji, pamoja na Kikosi Maalum cha SMZ.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, CP Salum Hamduni, amesema mashindano hayo yameleta manufaa mbalimbali ikiwemo burudani, kuongeza mzunguko wa fedha, kujenga mshikamano na kukuza utalii wa michezo, huku akiomba Mwanza ipewe nafasi ya kuandaa mashindano hayo mwaka 2027.