Yanga Yatikisa Afrika, Wachezaji 12 Waitwa Timu Za Taifa

Global Publishers
September 22, 2026
1,128 views
0 Comments

Yanga imeendelea kuthibitisha ukubwa wake barani Afrika baada ya wachezaji wake 12 kuitwa kuziwakilisha timu zao mbalimbali za taifa.

Hali hiyo inaonyesha ubora wa kikosi cha Wananchi pamoja na uwekezaji mkubwa uliofanywa na uongozi katika kusajili nyota wa kiwango cha kimataifa.

Wachezaji hao wameitwa kujiunga na vikosi vya mataifa yao kwa ajili ya michezo ya kalenda ya FIFA, ikihusisha mechi muhimu za kufuzu. Idadi hiyo kubwa inaiweka Yanga kwenye orodha ya klabu zinazoongoza kwa kutoa wachezaji wengi kwenye timu za taifa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.

Nyota hao 12 wanawakilisha mataifa mbalimbali, huku Taifa Stars ya Tanzania ikichukua fungu kubwa la wachezaji wazawa, akiwemo Dickson Job, Ibrahim Bacca, Mudathir Yahya na Clement Mzize, ambao wamekuwa sehemu muhimu ya kikosi cha taifa.

Kwa upande wa wachezaji wa kigeni, mlinda mlango mahiri Djigui Diarra anaendelea kuaminiwa kwenye kikosi cha timu yake ya taifa ya Mali, huku kiungo mshambuliaji Stephane Aziz Ki akijumuishwa kwenye kikosi cha Burkina Faso.

Wengine kutoka mataifa mbalimbali wamejiunga na timu zao za taifa kwa ajili ya kusaidia kupata matokeo mazuri.

Wakati mashabiki wa Yanga wakijivunia hatua hiyo, hali hii pia inaleta mtihani na changamoto ya kipekee kwa benchi la ufundi la klabu hiyo, kwani kocha mkuu analazimika kubaki na kikosi kidogo cha wachezaji ili kuendelea na programu za mazoezi.

Hata hivyo, faida kubwa ni kwamba wachezaji hao wanatarajiwa kurejea wakiwa wamepata uzoefu zaidi wa mechi za kimataifa, jambo linaloweza kuwa na manufaa kwa Yanga inaposhiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Sasa macho ya wapenzi wa soka nchini yanaelekezwa kuona jinsi nyota hao watakavyoiwakilisha vyema Yanga pamoja na mataifa yao katika mechi zijazo.

Na Peter Jinanai | GPL -TUDACO

Yanga Yatoa Pole Kufuatia Kifo cha Mama Fatma Karume

Global Publishers
September 22, 2026
0 views
0 Comments

Uongozi wa Young Africans Sports Club (YANGA) umetuma salamu za pole kufuatia kifo cha Mjumbe wa Baraza la Wadhamini wa klabu hiyo, Mama Fatma Karume, aliyefariki dunia Septemba 21, 2026.

Kupitia taarifa iliyotolewa Septemba 22, 2026, Uongozi wa YANGA umesema umepokea kwa huzuni kubwa taarifa za kifo cha Mama Fatma Karume, akielezwa kuwa mmoja wa viongozi waliokuwa na mchango mkubwa katika historia ya klabu hiyo.

“Huu ni msiba mkubwa kwetu. Tumepoteza Kiongozi mkubwa mwenye busara, hekima na mapenzi makubwa na Klabu yetu. Tutamkumbuka Mama yetu Fatma Karume kwa mengi mazuri aliyofanya ndani ya Klabu yetu, ikiwemo upatikanaji wa Ardhi ya jengo letu la Makao Makuu, Jangwani Jijini Dar es Salaam. Hakika, tumepoteza Mwanachama na moja ya nembo ya Klabu hii,” amesema Rais wa YANGA, Eng. Hersi Said.

Uongozi wa YANGA umetoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki pamoja na wadau wote wa michezo, huku ukiwaombea wafiwa nguvu na ustahimilivu katika kipindi hiki cha majonzi.

“Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi. Ameen.”

Taarifa hiyo imetolewa na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Young Africans Sports Club.

Marekani Yatangaza Hatua Kali Dhidi ya Mashirika ya Ndege ya Iran

Global Publishers
September 22, 2026
0 views
0 Comments

Waziri wa Hazina wa Marekani, Scott Bessent.

NEW YORK, Marekani: Waziri wa Hazina wa Marekani, Scott Bessent, amesema mashirika ya ndege ya Iran yanatarajiwa kukabiliwa na vikwazo vikubwa vya kiuchumi duniani kuanzia Septemba 23, 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Rais Donald Trump kuongeza shinikizo kwa Tehran.

Akizungumza na kituo cha CNBC Jumatatu, Septemba 21, 2026, Bessent alisema mashirika yote ya ndege ya Iran yataathiriwa na hatua hizo, akidai kuwa yatazuiwa kupata huduma muhimu katika viwanja vya ndege duniani.

Bessent amesema ndege za Iran zitakapowasili katika viwanja vya ndege, watoa huduma watakabiliwa na vikwazo iwapo wataendelea kuwapatia mafuta, huduma za kutua na kuondoka, pamoja na kuuza tiketi.

Kwa mujibu wa Bessent, kampuni au taasisi zitakazokiuka masharti hayo zinaweza kupoteza uwezo wa kufanya miamala kupitia mfumo wa dola wa Marekani.

Hatua hiyo ni sehemu ya sera ya Marekani ya kutumia vikwazo vya kiuchumi kuongeza shinikizo dhidi ya Iran, huku ikilenga sekta ya usafiri wa anga ya nchi hiyo.

Mpigie Kura Godmuya, Kura Yako Ni Ushindi! – Tuzo za Samia Kalamu Awards 2026

Global Publishers
September 22, 2026
2,754 views
0 Comments

Mtangazaji wa @globaltvonline na @255globalradio, Godfrey Nathan @godmuya ameteuliwa kuwania tuzo za Samia Kalamu Awards 2026.

Sasa Godmuya anaomba support yako, mfuatiliaji wa Global TV, kwa kumpigia kura ili kufanikisha ushindi wake.

🗳️ MPIGIE KURA: GODFREY LUHILABAKE NATHAN
🔢 Kodi: 260246

Kura yako ni mchango mkubwa kwa Godmuya katika safari hii ya tuzo.

🙏 Piga kura, share na mwambie mwingine apige kura!

Fursa Mpya ya Ajira NEEC, Mwisho wa Maombi Oktoba 1, 2026

Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imetangaza nafasi moja ya Mtendaji Mkuu wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Kiuchumi (NEEC) kwa Watanzania wenye sifa zinazohitajika. Tangazo hilo limetolewa Septemba 18, 2026, kwa niaba ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

NEEC limeanzishwa chini ya Sheria ya Uwezeshaji Kiuchumi Na. 16 ya mwaka 2004 na lipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Majukumu yake ni pamoja na kusimamia, kuratibu, kuwezesha na kufuatilia shughuli za uwezeshaji kiuchumi nchini.

Sifa za mwombaji

Mwombaji anatakiwa kuwa na Shahada ya Uzamili katika mojawapo ya fani zifuatazo:

  • Utawala wa Umma
  • Ujasiriamali
  • Fedha
  • Uhasibu
  • Utawala wa Biashara
  • Biashara, akiwa amebobea katika Ujasiriamali, Masoko au Fedha
  • Uchumi
  • Uchumi wa Kilimo
  • Au sifa zinazolingana kutoka taasisi inayotambuliwa.

Shahada ya Uzamili inapaswa kuhusiana na Shahada ya Kwanza ya mwombaji.

Mwombaji anatakiwa pia kuwa na uzoefu wa kazi wa angalau miaka 12 katika maeneo yanayohusiana, ambapo angalau miaka mitatu iwe katika nafasi ya kiutawala. Uelewa wa masuala ya uwezeshaji kiuchumi umetajwa kuwa ni sifa ya ziada.

Majukumu ya Mtendaji Mkuu

Mtendaji Mkuu atawajibika kusimamia shughuli za kiutawala za Baraza na kuwa msemaji wake. Pia atasimamia utekelezaji wa majukumu ya Baraza, maandalizi ya mipango ya kimkakati na bajeti, taarifa za fedha na maendeleo, pamoja na utekelezaji wa maazimio na maelekezo ya Baraza.

Majukumu mengine ni kusimamia utekelezaji na tathmini ya mipango ya muda mfupi, wa kati na mrefu, kuendesha shughuli za kila siku za Sekretarieti, kuandaa mikakati ya kuongeza ufanisi, kusimamia uundaji na utekelezaji wa sera pamoja na kuongoza juhudi za kutafuta rasilimali za kifedha kwa ajili ya miradi ya Baraza.

Nafasi hiyo ni ya ajira ya kudumu na yenye mafao ya kustaafu, huku mshahara ukiwa kwa mujibu wa kiwango kilichoidhinishwa cha NEECS 13.

Waombaji wanatakiwa kuwa raia wa Tanzania na kwa ujumla wasizidi umri wa miaka 45, isipokuwa watumishi wa umma. Pia wanapaswa kuambatanisha CV, nakala zilizothibitishwa za vyeti vya elimu na taaluma, cheti cha kuzaliwa pamoja na picha ya pasipoti.

Mwisho wa kutuma maombi ni Oktoba 1, 2026. Maombi yanapaswa kutumwa kupitia Recruitment Portal ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

Mama Fatma Karume Afariki Dunia Nyumbani Kwake Zanzibar – Video

Global Publishers
September 22, 2026
0 views
0 Comments

Mama Fatma Karume, aliyekuwa mke wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, amefariki dunia akiwa nyumbani kwake Zanzibar.

Mama Fatma Karume amefariki dunia Septemba 21, 2026, huku taarifa zaidi kuhusu sababu ya kifo, ratiba ya mazishi na taratibu nyingine za msiba zikitarajiwa kutolewa na Serikali pamoja na familia.

Mama Fatma alikuwa mjane wa Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Kifo chake ni msiba mkubwa kwa familia, ndugu, jamaa na wananchi wa Zanzibar.

DKT. MWIGULU ATETA NA MKURUGENZI MKUU WA FAO

*_▪︎ Ataja umwagiliaji, zana za kisasa za kilimo, na uongezaji thamani kuwa maeneo ya kimkakati_*

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali imedhamiria kuongeza uwekezaji katika maeneo ya umwagiliaji, uzalishaji wa mbegu kwa wingi na matumizi ya zana za kilimo kisasa kama njia ya kuimarisha sekta ya kilimo.

Amesema hayo leo (Jumatatu, Septemba 21, 2026) wakati akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Dkt. Qu Dongyu kuhusu mageuzi ya mifumo ya chakula na kilimo nchini Tanzania, ambako anashiriki Mkutano wa Kimataifa wa Kujadili Afya Moja na Mifumo ya Chakula na Kilimo unaofanyika katika Makao Makuu ya FAO, jijini Roma, Italia.

Dkt. Mwigulu amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeongeza uwekezaji katika kilimo na kuelekeza nguvu katika miradi ya kimkakati, huku ikilenga kuhakikisha wakulima wanapata zana za kilimo na huduma bora zaidi katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Amesema Tanzania pia ina fursa kubwa ya kuongeza uzalishaji kutokana na uwepo wa ardhi nyingi na vyanzo vya maji, hivyo inataka kutumia rasilimali hizo kujenga mifumo ya kilimo inayostahimili mabadiliko ya tabianchi.

“Tanzania inalenga kuacha kuuza bidhaa ghafi, ambazo zimekuwa zikileta changamoto tunapokutana na misukosuko katika masoko ya dunia. Tunataka kuongeza thamani ya mazao na kuwa na masoko yenye ushindani,” amesema.

Waziri Mkuu amesema Tanzania pia inaendelea kutumia teknolojia za kidijitali katika kuwaandikisha wakulima na wasambazaji wa pembejeo, hatua inayosaidia kuboresha usambazaji wa zana za kilimo, mbolea na huduma nyingine kwa wakulima.

Akielezea matarajio ya baadaye katika sekta ya kilimo, Waziri Mkuu amesema Tanzania inataka kuelekeza nguvu katika programu chache za kimkakati zitakazotoa matokeo makubwa na yanayopimika ikiwemo kuhamasisha uwekezaji na mitaji kwa ajili ya mageuzi ya sekta hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Dkt. Qu Dongyu, ameitaka serikali ya Tanzania iwekeze kwa wanasayansi na watafiti chipukizi ili waweze kufanya mageuzi makubwa.

“Wekezeni kwa wanasayansi chipukizi. Muwatajirishe kwa kuwawezesha kushiriki kwenye tafiti na bunifu mbalimbali,” alisisitiza na kuongeza kwamba: “Serbia ilifanya hivyo na ndani ya miaka miwili imefanikiwa kubadilika na kukua kiuchumi ndani ya miaka miwili tu.”

Alisema pamoja na mipango mizuri iliyopo kwenye kilimo, Serikali ya Tanzania isiache kuwashirikisha wakulima wadogo kwenye maamuzi kuhusu masuala yanayowahusu kwani wao ndiyo watekelezaji wakuu. 

Dkt. Dongyu amesema FAO pia inaendelea kuhimiza matumizi ya viwango katika uzalishaji na biashara ya mazao, pamoja na matumizi ya teknolojia kuwaunganisha wakulima wadogo na masoko, ili kuongeza ushindani na kunufaika na fursa za biashara.

Dkt. Mwigulu anamwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo wa kimataifa unaofanyika jijini Roma kuanzia Septemba 21 hadi 23, 2026.

WAZIRI MKUU AHIMIZA NCHI ZA AFRIKA ZIONGEZE MAPAMBANO DHIDI YA SOTOKA

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amezitaka nchi za Afrika na washirika wa kimataifa ziweke kipaumbele kwenye ajenda ya kutokomeza ugonjwa wa sotoka kwa mbuzi na kondoo (Peste des Petits Ruminants-PPR) kwa kuimarisha misaada ya kifedha na kiufundi.

“Mpango wa kutokomeza PPR si uwekezaji katika afya ya mifugo pekee, bali pia ni uwekezaji katika usalama wa chakula, kupunguza umaskini, kukuza biashara ya mifugo na kuimarisha ustahimilivu wa kiuchumi kwa wananchi. Tunatakiwa kuhakikisha ajenda hii inaendelea kupewa kipaumbele katika ngazi za kitaifa, kikanda na kimataifa ili kufikia lengo hili,” amesema.

Ametoa wito huo leo (Jumatatu, Septemba 21, 2026) wakati akitoa hotuba kuu kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi wa mkutano wa siku tatu wa Kimataifa wa Kujadili Afya Moja na Mifumo ya Chakula na Kilimo ulioanza leo katika Makao Makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), jijini Roma, Italia.

Akielezea mafanikio ya Tanzania katika kutokomeza ugonjwa wa sotoka, Waziri Mkuu amesema Serikali ililifanya suala hilo kuwa jambo kitaifa na inaendelea kutetea jitihada za kutokomeza ugonjwa huo barani Afrika.

“PPR si tu tatizo la afya ya wanyama. Kwa mamilioni ya kaya za wafugaji, hasa zile zinazotegemea kondoo na mbuzi, ni tishio kwa usalama wa chakula, mapato ya kaya, biashara na maisha,” amesema.

Katika mwaka wa fedha wa 2025/2026, Dkt. Mwigulu amesema Tanzania ilichanja kondoo na mbuzi milioni 16.8 dhidi ya sotoka na ilifanikiwa kufikia sehemu kubwa ya wanyama 17.2 waliolengwa kupata chanjo katika maeneo hatarishi. 

“Kwa mwaka 2026/2027, zaidi ya sh. bilioni 30.8 (takriban dola milioni 11.6) zimetengwa kuendeleza awamu ya pili ya kampeni. Uzoefu wetu umetupa somo rahisi kwamba sotoka haiwezi kuondolewa kwa chanjo pekee bali kunahitajika jitihada zaidi. Inahitaji uchunguzi, utambuzi na ufuatiliaji wa wanyama, huduma sahihi kwa mifugo, ushirikiano baina ya nchi na nchi, na ufadhili endelevu.”

“Kuthibitisha hilo, Tanzania ilikuwa mwenyeji mkutano wa kikanda kuhusu masuala ya sotoka uliofanyika jijini Dar es Salaam tangu tarehe 14 hadi 16 Septemba 2026, na kuzikutanisha nchi saba kutoka Kusini, Kati na Mashariki mwa Afrika ili kuimarisha hatua za kudhibiti na kutokomezwa kwake. 

Amesema mkutano huo ni matokeo ya mazungumzo ya awali ya kikanda, ikiwa ni pamoja na warsha ya sotoka iliyofanyika Arusha Aprili, 2026 ambayo ililenga kuwianisha mbinu zinazozingatia mfumo wa ikolojia katika ukanda wa Maziwa Makuu.

Waziri Mkuu amesema mada ya mkutano huo: “Afya Moja katika Mifumo ya Kilimo ni afya ya kila mtu, ni wajibu wa kila mmoja wetu, na inahitaji hatua za kila mmoja wetu,” inabainisha ukweli kwamba afya ya watu, wanyama, mimea na mifumo ya ikolojia haiwezi kutenganishwa.

“Kwa Tanzania, Afya Moja siyo tu ni dhana ya kisera bali ni wito wa kuchukua hatua. Inamaanisha kuwekeza katika mifumo inayozuia magonjwa kabla hayajawa majanga, kulinda chakula na maliasili zetu, kudumisha maisha na kuimarisha uthabiti wa jamii na uchumi wetu,” amesisitiza.

Awali, akiwakaribisha washiriki kwenye mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Bw. Qu Dongyu alisema Afya Moja huanzia shambani, ghalani, msituni, kwenye mito na bahari na popote pale ambapo wanyama, mimea, na watu hushiriki pamoja kuvuta hewa, kutumia udongo na maji. “Afya Moja huanzia pale maisha yanapounganishwa na hakuna mahali ambapo hilo linaonekana zaidi kuliko katika mifumo yetu ya chakula cha kilimo,” alisema.

Alisema udongo unapoharibiwa, mazao na malisho hudhoofika, mifumo ya ikolojia, watu na wanyama huwa hatarini zaidi, hivyo basi kuhatarisha lishe na maisha. Uduni wa maji hubeba vimelea vya magonjwa kati ya wanyama na watu, na hivyo kuongeza utegemezi wa dawa za kuua viini, jambo ambalo husababisha upinzani wa vimelea.

“Tunahitaji kufanya kazi kwa ukamilifu. Kinga na utayari ni muhimu – kuanzia mimea yenye afya, wanyama wenye afya nzuri, maji salama na udongo wenye afya. Miunganisho hiyo hiyo hupitia mazao yetu, misitu, uvuvi na bahari. Tunahitaji suluhu zilizounganishwa yaani Suluhu za Afya Moja,” amesisitiza.

Mapema, Rais wa Uswisi, Waziri Mkuu wa Serbia, Mawaziri wa Afya, Kilimo, Chakula na Mazingira kutoka Bangladesh, Ufaransa, Ireland, Tunisia na Jamhuri ya Korea walizungumza kwenye ufunguzi huo na kusisitiza kuwa utekelezaji wa dhana ya Afya Moja haupaswi kubaki kuwa jukumu la sekta ya afya pekee na badala yake, unahitaji ushiriki na uwajibikaji wa kila mdau yaani serikali, sekta binafsi, wakulima, wafugaji, watafiti, vijana, jamii za asili, asasi za kiraia, taasisi za fedha na wananchi kwa ujumla.

MAMA FATMA KARUME AFARIKI DUNIA LEO

 

Na Matukio Daima Media 

Mama Fatma Karume, aliyekuwa mke wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, amefariki dunia leo, Septemba 21, 2026.

Taarifa za kifo chake zimefika wakati akiwa nyumbani kwa mmoja wa watoto wake huko Zanzibar.

Mama Fatma Karume alikuwa mjane wa Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar, ambaye aliiongoza Zanzibar baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Kifo chake ni msiba mkubwa kwa familia, ndugu, jamaa na wananchi wa Zanzibar. Taarifa zaidi kuhusu mazishi na ratiba nyingine za msiba zinatarajiwa kutolewa na Serikali.

Mama Fatma Karume amefariki akiwa na umri wa miaka 97.