Global Publishers September 26, 2026 1,092 views 0 Comments
Wasanii wakubwa kutoka Tanzania, Diamond Platnumz na Joel Lwaga, wameungana kwa mara ya kwanza katika wimbo mpya unaokwenda kwa jina la “Nikumbuke”, uliotoka rasmi Septemba 23, 2026.
Ushirikiano huo umekutanisha wasanii wawili wanaotoka katika mazingira tofauti ya muziki, huku Diamond Platnumz akijulikana zaidi kupitia Bongo Flava na Afropop, wakati Joel Lwaga akitambulika kwa kazi zake katika muziki wa Injili.
“Nikumbuke” umejengwa katika ujumbe wa imani, subira na matumaini, ukielezea hali ya mtu anayepitia changamoto lakini bado anaendelea kumtegemea Mungu na kusubiri majibu ya maombi yake.
Kupitia wimbo huo, wasanii hao wameleta ladha tofauti za muziki na kuunganisha mashabiki wa Bongo Flava pamoja na wale wanaopenda muziki wa Injili.
Kwa Diamond, ushirikiano huo unamuweka kwenye mazingira yenye ujumbe wa kiroho zaidi, huku Joel Lwaga akiendelea kusimamia aina ya muziki ambao amejijengea jina kwa miaka kadhaa.
Wimbo huo tayari umeanza kupata uangalizi kutoka kwa mashabiki kwenye majukwaa mbalimbali ya muziki na mitandao ya kijamii.
Taarifa zilizopo kwenye YouTube zinaonyesha kuwa lyric video ya “Nikumbuke” iliwekwa kwenye ukurasa wa Joel Lwaga Septemba 23, 2026, siku ambayo wimbo huo ulitolewa rasmi.
Ushirikiano wa Diamond na Joel Lwaga unaifanya “Nikumbuke” kuwa moja ya kazi zinazowakutanisha wasanii wenye mitazamo tofauti ya muziki, huku ujumbe wake ukilenga kuhamasisha watu kuendelea kuwa na matumaini, subira na imani hata wanapopitia nyakati ngumu.
AHSANTE KWA KUPIGIA KWA KUENDELEA KUTUPIGIA KURA MATUKIO DAIMA MEDIA ENDELEA KUTUPIGIA KURA KILA BAADA YA SAA 24 HADI SEPT 30 KASI YAKO YA KUPIGA KURA NDIO USHINDI .
Msanii wa Tanzania, Rayvanny, ametangazwa kuwa miongoni mwa wasanii watakaotumbuiza katika tamasha kubwa la Afro Nation Portugal 2027, nchini Ureno.
Jina la Rayvanny limeonekana katika orodha ya kwanza ya wasanii iliyotangazwa na waandaaji wa tamasha hilo Septemba 23, 2026, hatua inayomweka tena msanii huyo wa Tanzania kwenye jukwaa kubwa la muziki wa Afrika kimataifa.
Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika kuanzia Juni 9 hadi 11, 2027, katika ufukwe wa Praia da Rocha, Portimão, nchini Portugal, likiwa na lengo la kuunganisha muziki, utamaduni na burudani kutoka Afrika na maeneo mbalimbali duniani.
Rayvanny atashiriki jukwaa hilo pamoja na baadhi ya majina makubwa katika muziki wa Afrika na kimataifa, akiwemo Davido, Rema, Fally Ipupa, Omah Lay, Victony na Shenseea.
Davido, Rema na Fally Ipupa wametajwa miongoni mwa wasanii wakuu watakaotumbuiza katika tamasha hilo.
Kwa upande wa muziki wa Amapiano, jukwaa la Piano People Stage linatarajiwa kuwakutanisha wasanii mbalimbali, akiwemo Kabza De Small, TxC na Dlala Thukzin.
Waandaaji wa Afro Nation wamesema orodha hiyo bado haijakamilika, huku wasanii wengine wakitarajiwa kutangazwa katika awamu zijazo kuelekea tamasha hilo.
Kwa Rayvanny ushiriki huo unampa nafasi ya kuwakilisha muziki wa Tanzania katika moja ya matukio ya kimataifa yanayolenga Afrobeats, Amapiano na muziki wa Afrika. Tamasha hilo limekuwa likifanyika Portugal tangu mwaka 2019 na limeendelea kuwaleta pamoja wasanii na mashabiki kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Serikali imeeleza kuwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umeendelea kuimarika na kuwa mfano katika utoaji wa huduma za hifadhi na kinga ya jamii nchini, huku thamani ya mfuko huo ikifikia Sh trilioni 16.96.
Akizungumza wakati wa Maonyesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika mkoani Geita, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amesema ameridhishwa na jitihada zinazofanywa na PSSSF katika kuhakikisha waajiri na wastaafu wanapata elimu kuhusu umuhimu wa hifadhi ya jamii na maandalizi ya maisha baada ya kustaafu.
Sangu amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza katika kuimarisha PSSF, hatua ambayo imechangia ongezeko kubwa la thamani ya mfuko huo.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, thamani ya PSSSF imeongezeka kutoka Sh trilioni 7.4 wakati Rais Samia alipoingia madarakani hadi kufikia Sh trilioni 16.96, ongezeko analolitaja kuwa ni hatua kubwa katika historia ya mfuko huo.
Amesema ukuaji huo umewezesha PSSSF kuboresha zaidi huduma kwa wastaafu, ikiwemo kuhakikisha wanapata pensheni zao kwa wakati.
“Tunalipa jana,” ni kaulimbiu ambayo, kwa mujibu wa Sangu, imeendelea kutekelezwa kwa vitendo, ambapo wastaafu hulipwa pensheni zao kila tarehe 25 ya mwezi bila kuchelewa.
Aidha, amesema kiwango cha chini cha pensheni kwa sasa kimefikia Sh 250,000, hatua inayolenga kuimarisha ustawi wa wastaafu baada ya kumaliza safari yao ya utumishi.
Waziri Sangu pia amepongeza uwekezaji mkubwa uliofanywa na PSSSF katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), akisema umeleta mabadiliko katika upatikanaji wa huduma kwa wastaafu.
Amesema hapo awali wastaafu walilazimika kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya uhakiki wa taarifa zao, lakini kwa sasa huduma hizo zimeboreshwa kupitia mifumo ya kidijitali, hivyo kupunguza usumbufu na kurahisisha upatikanaji wa huduma.
Ameeleza kuwa matumizi ya teknolojia yanaendelea kuwa sehemu muhimu katika kuboresha huduma za PSSSF na kuhakikisha wanachama na wastaafu wanapata huduma kwa urahisi, ufanisi na kwa wakati.
Nafasi za kazi kila siku Tanzania, Serikalini, Makampuni na Taasisi mbalimbali tembelea website yetu ya Global Publishers muda wote bonyeza hapa Publishers muda wote bonyeza hapa
MATUKIO DAIMA IMETEULIWA KUSHIRIKI TUZO ZA UMAHIRI WA VYOMBO VYA HABARI NA WANAHABARI TANZANIA TUZO HIZI ZIMETOLEWA NA TCRA NA TAMWA
MAARUFU KWA JINA LA SAMIA KALAMU AWARDS (SKA2026)
1:TUZO YA CHOMBO CHA HABARI -MATUKIO DAIMA MEDIA
2:TUZO YA JINSIA ,WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM
3:TUZO YA AFYA
4:TUZO YA MPIGA PICHA
AHSANTE KWA KUPIGIA KWA KUENDELEA KUTUPIGIA KURA MATUKIO DAIMA MEDIA ENDELEA KUTUPIGIA KURA KILA BAADA YA SAA 24 HADI SEPT 30 KASI YAKO YA KUPIGA KURA NDIO USHINDI .
TANGA; Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema kimeridhishwa na uhai na utekelezaji wa shughuli za chama Mkoa wa Tanga kutokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya chama na serikali umesaidia kurahisisha upelekaji wa maendeleo kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi katika ziara yake mkoani Tanga yenye lengo la kukagua uhai wa chama na utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2025-2030.
Kihongosi amesema changamoto kubwa inayowakabili wananchi wa Mkinga ni suala la upatikanaji wa maji, lakini Rais Dk Samia Suluhu Hassan ametoa Sh bilioni 35 kwa ajili ya mradi wa maji.
“Changamoto kubwa inayowakabili hapa ni changamoto ya maji lakini hapa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameletea bilioni 35 za mradi wa maji,” amesema Kihongosi.
Akizungumza wakati akizindua Shina Namba 6 lililopo Mbuyuni, Kata ya Manza, Kihongosi amesema wananchi wamekuwa wakipata changamoto za maji, afya, elimu na nyinginezo lakini serikali inayoongozwa na CCM chini ya Rais Samia imekuwa macho kuhakikisha inawaletea wananchi maendeleo. –
Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) imehitimisha mafunzo ya mradi wa majaribio wa kuwawezesha vijana kutumia teknolojia ya kidigitali katika kujitangaza, kujiajiri na kuongeza fursa za ajira, huku vijana 48 ( kwa upande wa DIT ) waliohitimu mafunzo hayo wakikabidhiwa vyeti vya utambuzi wa ushiriki wao.
Hafla fupi ya kufunga mafunzo hayo imefanyika leo, Septemba 25, 2026, ikiwa ni hatua muhimu katika juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia za kuwawezesha vijana nchini kutumia ujuzi wa kidigitali kujiletea maendeleo na kuchangamkia fursa zinazotokana na ukuaji wa uchumi wa kidigitali.
Mafunzo hayo ni sehemu ya mradi wa majaribio unaolenga kuimarisha uwezo wa vijana wa elimu ya juu katika matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), hususan katika kutangaza ujuzi, ubunifu, bidhaa na huduma zao kupitia majukwaa ya kidigitali.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Prof. Ezekiel Amri, amewapongeza vijana hao kwa kuhitimu mafunzo hayo na kuwataka kutumia maarifa na ujuzi walioupata kwa malengo chanya yatakayowasaidia kujiajiri au kuongeza uwezekano wa kuajiriwa.
Prof. Amri amesisitiza kuwa teknolojia ya kidigitali inapaswa kuwa nyenzo ya maendeleo kwa vijana, hivyo kuwataka kuitumia kwa ubunifu na tija katika shughuli zao za kiuchumi na kijamii, badala ya kuitumia kwa mambo yasiyokuwa na manufaa.
Aidha, amewahimiza wahitimu hao kuendeleza mshikamano na ushirikiano walioanzisha wakati wa mafunzo, akieleza kuwa kuendelea kubadilishana maarifa, uzoefu na fursa kutawasaidia kukua zaidi katika shughuli zao za kitaaluma na kibiashara.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Umahiri wa TEHAMA cha DIT, kinachofahamika kama India–Tanzania Centre of Excellence in ICT, Bw. Finian Mwalongo, amesema vijana hao wamepata ujuzi muhimu wa kidigitali utakaowasaidia kujitangaza kitaalamu, kukuza biashara zao na kuongeza fursa za kupata ajira.
Amesema mafunzo hayo yamewajengea vijana uwezo wa kutumia majukwaa ya kidigitali kuwasilisha ujuzi na huduma zao kwa namna itakayorahisisha kufikiwa na wateja, waajiri na wadau wengine wanaohitaji huduma zao.
Bw. Mwalongo amebainisha kuwa DIT itaendelea kutoa mafunzo hayo kwa vijana wengine kupitia awamu ya pili, ikiwalenga zaidi wale walioomba kushiriki katika awamu ya kwanza lakini hawakupata nafasi kutokana na idadi ya nafasi zilizokuwepo.
“Mafunzo haya kwa hapa DIT ni ya awamu ya kwanza. Tutakuwa na mafunzo ya awamu ya pili kwa kundi la vijana, hasa wale walioomba lakini nafasi hazikutosha. Wiki ijayo tutaanza mafunzo mengine kwa vijana wengine.
“Lakini pia, kama DIT, tutaendelea kuwa na hawa vijana, kuwaongoza na kuhakikisha mafunzo haya waliyoyapata na ambayo wataendelea kuyapata yanawanufaisha kama ambavyo Serikali yetu ililenga,” amesema Bw. Mwalongo.
Amesema DIT itaendelea kushirikiana na vijana hao kwa kuwapa mwongozo na kuwawezesha kutumia maarifa waliyojifunza katika mazingira halisi ya kazi na biashara, ili mafunzo hayo yawe na matokeo yanayoonekana katika maisha yao.
Kauli hiyo inaonesha dhamira ya DIT ya kutekeleza jukumu lake la kuendeleza ujuzi wa kiteknolojia kwa vitendo, sambamba na kuwaunganisha vijana na fursa zinazoweza kuchochea ubunifu, ujasiriamali na ajira.
Naye Nayfath Mohammed Abdallah, mmoja wa vijana walionufaika na mafunzo hayo, ameipongeza Serikali kwa kuanzisha programu hiyo, akisema imewapa vijana fursa ya kujifunza namna ya kutumia teknolojia ya kidigitali kutangaza na kukuza shughuli zao.
Nayfath amesema licha ya muda wa mafunzo kuwa siku tano pekee, washiriki wamejifunza mambo mengi yenye manufaa, huku baadhi yao wakianza kuona matokeo ya moja kwa moja kupitia upatikanaji wa wateja wa biashara zao kwenye majukwaa ya mtandaoni.
Ameomba mafunzo hayo yaendelee kutolewa kwa vijana wengine, huku akishauri muda wa mafunzo uongezwe ili washiriki wapate nafasi ya kujifunza kwa kina zaidi na kumudu stadi nyingi zaidi za kidigitali.
Amesema mafunzo hayo yamekuwa chachu ya kuwapa uelewa mpana kuhusu namna ya kutumia teknolojia kujitangaza, kufikia wateja wengi zaidi na kupanua wigo wa shughuli zao za kiuchumi.
Global Publishers September 25, 2026 24 views 0 Comments
Tanzania leo, Septemba 25, 2026, imeanza vibaya safari ya kufuzu AFCON 2027 baada ya kupoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Guinea-Bissau katika Uwanja wa New Amaan Complex, uliopo Unguja, Zanzibar.
Guinea-Bissau ilipata bao la kwanza dakika ya 33 kupitia Franculino Djú, aliyefunga baada ya kupokea pasi ya Beto.
Dakika ya 58, Mama Baldé aliifungia Guinea-Bissau bao la pili akimalizia pasi ya Dalcio na kuifanya Tanzania kuwa nyuma kwa mabao 2-0.
Matokeo hayo yanaifanya Taifa Stars kuhitaji kujipanga upya kuelekea mchezo wake wa pili wa kufuzu AFCON 2027 dhidi ya Madagascar, utakaochezwa Septemba 29, 2026.
NEW YORK, Marekani — Septemba 25, 2026 Viongozi na wadau wa afya duniani wameahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za Tanzania katika kuimarisha afya ya mama na mtoto, huku wakisisitiza umuhimu wa wanawake kushirikishwa zaidi katika uongozi na maamuzi ya mifumo ya afya.
Rais wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndeitwah, amesema dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kulinda afya na utu wa wanawake na watoto ina umuhimu mkubwa kwa mustakabali wa Afrika.
Akizungumza katika mkutano wa ngazi ya juu wenye kaulimbiu “Advocacy for a New Era: Women Leading Maternal and Child Health for All”, maarufu kama SHE RISES, Rais Nandi-Ndeitwah amesema uwekezaji katika afya ya mama na mtoto haupaswi kuonekana kama matumizi ya kawaida, bali ni uwekezaji katika watu, uchumi na maendeleo endelevu.
Mkutano huo umeandaliwa na Rais Samia, ambaye anahudumu kama Kinara wa Umoja wa Afrika katika Afya ya Mama na Mtoto, pembezoni mwa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaofanyika New York, Marekani.
Rais wa Namibia amezitaka nchi za Afrika kuongeza uwezo wao wa ndani wa kugharamia huduma za afya ya mama na mtoto badala ya kutegemea zaidi misaada kutoka nje.
Amesema maendeleo ya Bara la Afrika hayawezi kutenganishwa na afya ya wananchi wake, huku Namibia ikiahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa ajenda hiyo ya Umoja wa Afrika.
Tanzania Yaonyesha Mafanikio
Akiwasilisha uzoefu wa Tanzania, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, amesema uwekezaji katika sekta ya afya umeanza kuonyesha matokeo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa katika mkutano huo, kati ya mwaka 2015 na 2022, vifo vya uzazi vilipungua kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000, huku vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano vikishuka kutoka 67 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1,000.
Aidha, bajeti ya afya imeongezeka kutoka takribani Sh bilioni 780 mwaka 2015 hadi Sh trilioni 1.8 katika mwaka wa fedha 2026/27.
Mfumo wa M-Mama, kwa upande mwingine, umewezesha zaidi ya rufaa 150,000 za dharura kwa akina mama na watoto wachanga hadi Agosti 2026.
Ndejembi amesema hatua hizo zinaonyesha umuhimu wa kuunganisha utashi wa kisiasa, rasilimali na utekelezaji katika kuboresha maisha ya wananchi.
Ajenda ya “SHE RISES”
Katika ngazi ya Bara la Afrika, Ndejembi amesema Rais Samia anaendelea kutumia nafasi yake kama Kinara wa Umoja wa Afrika katika Afya ya Mama na Mtoto kusukuma utekelezaji wa mpango wa Umoja wa Afrika kuhusu afya ya mama, mtoto mchanga, watoto na vijana balehe.
Ajenda hiyo pia inahusisha dhana ya “sifuri tatu”, inayolenga kuondoa kujifungulia nyumbani, kupunguza vifo vya mama na watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika pamoja na kuhakikisha watoto wanapata chanjo.
Kupitia SHE RISES, Tanzania pia inasisitiza umuhimu wa wanawake kutokuwa wapokeaji wa huduma za afya pekee, bali kushiriki katika uongozi na maamuzi yanayounda mifumo ya afya.
UNFPA na WHO Zapongeza Juhudi
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi (UNFPA), Diene Keita, amepongeza uongozi wa Rais Samia na nafasi ya Tanzania katika kuiweka afya ya mama na mtoto kwenye ajenda ya kisiasa ya Afrika.
Keita amesema mafanikio katika eneo hilo yanahitaji utashi wa kisiasa unaoonekana kupitia bajeti, uwekezaji katika huduma za afya ya uzazi na kuimarishwa kwa nafasi ya wakunga.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Dkt. Mohamed Janabi, amesema dhamira ya kisiasa inapounganishwa na uwekezaji, uwajibikaji na vitendo, maisha ya mama na mtoto yanaweza kuendelea kuokolewa.
Janabi amesisitiza pia umuhimu wa wanawake katika mifumo ya afya, akisema wanawake wanachangia sehemu kubwa ya utoaji wa huduma za afya barani Afrika.
Kwa mujibu wa takwimu alizowasilisha, wanawake ni takribani asilimia 70 ya watendaji katika sekta ya afya barani Afrika, lakini bado wanawakilisha takribani asilimia 25 katika nafasi za kufanya maamuzi.
Amesema SHE RISES inalenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika kutunga sera, kupanga bajeti, kuweka vipaumbele na kushika nafasi za uongozi katika sekta ya afya.
Mkutano huo pia umehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Afrika na nje ya bara hilo, viongozi wakuu wastaafu akiwemo Rais wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete, wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, wadau wa afya duniani pamoja na watunga sera.
Kwa Tanzania, ujumbe wa SHE RISES unaunganisha afya ya mama na mtoto na masuala ya uongozi, rasilimali, uwajibikaji na ushiriki wa wanawake katika kufanya maamuzi yanayohusu mifumo ya afya.
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais 25 Septemba 2026 New York, Marekani