Benki ya Exim Tanzania Yashiriki CEO Golf Day 2026 Visiwani Zanzibar

Benki ya Exim Tanzania imeungana na viongozi wa taasisi, wafanyabiashara, washirika na wadau mbalimbali katika CEO Golf Day 2026, hafla iliyofanyika Septemba 26, 2026 katika Sea Cliff Golf Club, Zanzibar, na kuwakutanisha viongozi wa biashara, wanadiplomasia na wachezaji wa gofu kutoka Tanzania na nje ya nchi.

Hafla hiyo inalenga kutumia mchezo wa gofu kama jukwaa la kuwakutanisha viongozi na wadau wa biashara kutoka Tanzania na nje ya nchi, ikiwemo Kenya, Uganda, Zambia, Malawi, Afrika Kusini na Nigeria, na hivyo kutoa nafasi kwa washiriki kutoka masoko mbalimbali kukutana kujenga mahusiano na kuendeleza mazungumzo kuhusu fursa mbalimbali.

Benki ya Exim Tanzania imeshiriki katika hafla hiyo ikiwa ni mmoja wa wadhamini, hatua inayoakisi dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na jumuiya ya wafanyabiashara na wadau mbalimbali, kuimarisha mahusiano na kujenga fursa za pamoja zinazoweza kuchangia ukuaji wa biashara nchini.

Mbali na mchezo wa gofu, hafla hiyo ilitoa nafasi kwa viongozi na washiriki kuendelea na mazungumzo na kujenga mahusiano ya kikazi. Mashindano hayo yalihusisha mchezo wa gofu wa mashimo 18, kabla ya washiriki kuhitimisha siku kwa hafla ya chakula cha jioni.

Kwa Benki ya Exim Tanzania, ushiriki huo ni sehemu ya kuendelea kuwa karibu na jumuiya ya biashara na wadau wake, wakiwemo wateja.

Kwa jumla, dhumuni la siku hii ya kipekee ni kujenga mtandao wa kibiashara na ushirikiano wa kijamii, kuweka mazingira ambapo viongozi wa biashara na wadau wanaweza kuungana, kubadilishana mawazo na kuimarisha mahusiano nje ya mazingira ya kawaida ya kazi.

Trump Akataa Pendekezo la Iran la Kufungua Mlango wa Hormuz

WASHINGTON: Rais wa Marekani Donald Trump amekataa pendekezo la Iran la kufungua tena Mlango wa Hormuz na kusitisha mapigano yanayoendelea katika Mashariki ya Kati.

Iran iliwasilisha mpango huo wakati wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mjini New York, ikisema pendekezo hilo lilifikishwa kwa Marekani kupitia wapatanishi kutoka Qatar.

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, makubaliano hayo yangeweza kuwezesha kufunguliwa tena kwa Mlango wa Hormuz ndani ya siku saba, sambamba na kusitishwa kwa mapigano katika eneo hilo.

Hata hivyo, Trump amekataa mpango huo akisema Iran inataka kufunguliwa kwa haraka kwa njia hiyo kutokana na shinikizo la kiuchumi linaloikabili.

Trump alisema Iran imeathirika kwa sababu ya kupungua kwa shughuli za usafirishaji kupitia Hormuz, ambayo ni moja ya njia muhimu zaidi za usafirishaji wa nishati duniani.

“Nimekataa pendekezo lao,” Trump aliwaambia waandishi wa habari katika Ikulu ya White House kabla ya kuondoka kuelekea Tennessee.

Mlango wa Hormuz unaunganisha Ghuba ya Uajemi na Ghuba ya Oman na una umuhimu mkubwa katika biashara ya kimataifa, hasa kwa usafirishaji wa mafuta na bidhaa nyingine za nishati.

Marekani imeendelea kuweka shinikizo la kiuchumi dhidi ya Iran huku ikitaka Tehran kuondoa vizuizi katika Mlango wa Hormuz.

Iran yaweka wazi msimamo wake

Kwa upande wa Iran, Araqchi amesema Tehran iko tayari kufikia makubaliano iwapo Marekani itaonyesha utayari wa kufanya hivyo.

Alisema pendekezo hilo lingeanza kwa kufunguliwa kwa Hormuz ndani ya muda wa siku saba na kusitishwa kwa mapigano, kabla ya kuanza kwa mazungumzo mapana zaidi kati ya pande zinazohusika.

Mazungumzo hayo yanaweza pia kugusa suala la mpango wa nyuklia wa Iran.

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema nchi yake iko tayari kufanya mazungumzo kuhusu mpango wake wa nyuklia na masuala mengine, lakini haitakubali kile alichokiita vitisho, shinikizo au kulazimishwa.

Iran imekuwa ikisisitiza kuwa haitafuti vita, lakini itaendelea kujilinda dhidi ya mashambulizi na vitisho.

Mzozo kati ya Iran, Marekani na Israel umeendelea tangu Februari 28, kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

Tangu wakati huo, mapigano yamekuwa yakibadilika kati ya vipindi vya kusitisha mashambulizi na kurejea kwa mapigano, huku kukiwa na madhara kwa miundombinu na uchumi wa Iran.

Iran na washirika wake nao wamejibu kwa mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya maeneo mbalimbali katika Mashariki ya Kati.

Kwa sasa, kukataliwa kwa pendekezo la Iran na Trump kunaacha hatma ya kufunguliwa tena kwa Mlango wa Hormuz ikiwa haijulikani, huku juhudi za kidiplomasia za kusitisha mapigano zikiendelea kufuatiliwa kwa karibu.

CCM Iringa yamkabidhi Asas tuzo ya heshima – HabariLeo

IRINGA: KATIBU wa NEC Idara ya Oganaizesheni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Paul Matiko Chacha (MCC), amemkabidhi Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Salim Abri Asas, tuzo maalumu ya heshima iliyotolewa na CCM Mkoa wa Iringa kwa kutambua mchango wake katika ujenzi na uimarishaji wa Chama.

Tuzo hiyo imetolewa baada ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Iringa kuwasilisha hoja ya kumtambua Asas, ambayo ilipitishwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Mkoa wa Iringa uliofanyika katika Chuo cha UVCCM Ihemi.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Asas amesema viongozi wa sasa wanapaswa kufanya mambo yatakayobaki kuwa kumbukumbu ndani ya CCM, akisema kizazi kijacho kitakuja kuwauliza walifanya nini walipokuwa na dhamana ya uongozi.

“Kizazi kitakuja kutuuliza, mlilikifanyia nini CCM?” amesema Asas aliyekuwa akishangiliwa kwa nguvu na wajumbe wa Mkutano huo.

Amesema swali hilo limekuwa sehemu ya msukumo wake wa kushiriki katika ujenzi na uimarishaji wa miundombinu ya Chama, hususan ujenzi wa ofisi za CCM katika ngazi ya Kata.

Asas amesema ni jambo lisilofaa kwa CCM kufikisha miaka 50 huku baadhi ya Kata zikiwa hazina ofisi za Chama, miradi au makazi kwa ajili ya watumishi wake.

Amesema kutokana na msimamo huo, amejitolea kuhakikisha ifikapo CCM inatimiza miaka 50, kila Kata inakuwa na ofisi ya Chama, akieleza kuwa baadhi ya miradi hiyo tayari imekamilika huku mingine ikiendelea.

“Tumejiwekea msimamo kwamba itakuwa aibu kufikia miaka 50 ya CCM, halafu kuna Kata ambazo hazina ofisi za Chama,” amesema.

Amesema dhamira yake ya kuona ofisi hizo zinakamilika imefikia hatua ya kuiweka kazi hiyo kwenye wosia wake kwa wanafamilia, akieleza kuwa amewaeleza ndugu zake kwamba iwapo Mungu atamchukua kabla ya kukamilisha azma hiyo, wahakikishe fedha zinatengwa kutoka kwenye mali ya familia ili kukamilisha ujenzi wa ofisi hizo.

Kwa mujibu wa Asas, hatua hiyo inalenga kuhakikisha kazi aliyoianza inaendelea hata kama hatakuwepo, ili ofisi hizo zitumike na viongozi na wanachama wa CCM wa sasa na vizazi vijavyo.

Amesema anataka mchango wake ndani ya Chama usibaki kwenye maneno pekee, bali uonekane kupitia miradi na miundombinu itakayodumu na kuwa na manufaa kwa wanachama kwa muda mrefu.

Akimpongeza Asas kwa tuzo hiyo, Chacha, amewataka viongozi na wanachama kuendelea kujipanga na kuweka mikakati ya muda mrefu kuelekea miaka 50 ya chama hicho.

Chacha amesema CCM ilipoanzishwa iliweka malengo mbalimbali, likiwemo lengo la kushika dola, hivyo wanachama wanapaswa kuendelea kutafakari namna ya kukiendeleza chama hicho katika vipindi vijavyo.

“Ni muhimu kwa viongozi wa sasa kuacha msingi ambao utakuwa na manufaa kwa vizazi vitakavyokuja na kuhakikisha chama kinaendelea kuwa na mipango madhubuti na muda mrefu,” alisema.

Aidha, amewataka wanachama kuendelea kujiandaa kwa uchaguzi wa chama unaokuja na kuhakikisha wanashiriki katika shughuli za chama kwa umoja na mshikamano.

DKT. HOMERA: SHERIA YA NDOA KUFANYIWA MAREKEBISHO, AIPONGEZA PLAN INTERNATIONAL TANZANIA

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, amesema Serikali ipo katika mashauriano ya kufanya marekebisho ya baadhi ya vifungu vya Sheria ya Ndoa, hususan vinavyohusiana na masuala ya elimu.

Ameyasema hayo Septemba 25, 2026, Mtumba jijini Dodoma, wakati akizungumza katika Programu Maalumu ya Sema na Waziri, ambapo amesema kuwa Serikali inaendelea kushughulikia suala la ndoa za utotoni.

Amesema kuwa Serikali haiwezi kubadilisha vifungu vyote vya Sheria ya Ndoa, bali kuna baadhi ya vifungu vinavyofanyiwa mashauriano kwa ajili ya marekebisho, ikiwemo kuangalia suala la elimu ya awali, msingi, sekondari hadi kidato cha sita.

Aidha, amebainisha kuwa Wizara ya Katiba na Sheria itaendelea kushirikiana na Plan International katika kuhakikisha mtoto wa kike anapata haki na fursa ya kutimiza ndoto zake, huku akiwataka kuendelea kushirikiana katika kuwasaidia mabinti wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali.

Pia ameongeza kuwa kuna umuhimu wa kwenda katika maeneo mbalimbali kujifunza changamoto zinazowakabili wanawake na mabinti wadogo, wakiwemo wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia, huku akisema kuwa mabinti wanaokumbwa na changamoto wanapaswa kuwezeshwa mitaji ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Naye, Mkurugenzi wa  Plan International  Tanzania, Jane Sembuche, amesema asilimia 29.1 ya wanawake wenye umri wa miaka 20–24 walioolewa waliingia kwenye ndoa kabla ya kufikisha miaka 18, hali inayoweza kuathiri elimu, afya na fursa za kiuchumi za wasichana. Amesisitiza umuhimu wa kufanyia marekebisho Sheria ya Ndoa ili kuweka miaka 18 kuwa umri wa chini wa ndoa kwa wote, hatua muhimu katika kufikia malengo ya Dira ya Tanzania 2050.

Kwa upande wake, Mkuu wa Sera, Mkakati na Ubora wa Plan International Tanzania, Christina Ruhinda, amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria, huku mabinti wakiendelea kushiriki katika shughuli mbalimbali zinazofanywa na wizara hiyo ili kujifunza uongozi, sheria na haki.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CAMFED Tanzania, Anna Sawaki, amepongeza hatua ya Serikali kuanza mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Ndoa, akisema kwa pamoja wanaweza kumwezesha mtoto wa kike. Amesema CAMFED inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo Plan International na mashirika ya kimataifa, kuhakikisha watoto wa kike wanaotolewa katika mazingira hatarishi wanapata elimu na kuwezeshwa kutimiza ndoto zao, ikiwemo kuwa viongozi. Aidha, amesema amefurahishwa na ushiriki wao katika kampeni ya Girls Takeover inayohamasisha wasichana kushiriki katika uongozi na kujenga uwezo wa kufikia matarajio yao.

Naye Veronica Kalenga, mnufaika wa Plan International Tanzania, amesema amefurahi kushiriki katika programu ya Girls Takeover 2026, ambapo alipata fursa ya kuchukua nafasi ya Waziri wa Katiba na Sheria wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kujifunza masuala ya uongozi, utendaji wa Serikali pamoja na namna ya kusikiliza na kushughulikia kero za wananchi.

Aidha, Jenipha Lucas, mkazi wa Geita na mnufaika wa Plan International Tanzania, amesema programu hiyo imempa fursa ya kujifunza na kushiriki katika masuala ya uongozi, huku akiishukuru Plan International Tanzania kwa kuwawezesha wasichana kupata nafasi za kujenga uwezo na kujiamini. Ameomba shirika hilo kuendelea kushughulikia changamoto zinazowakabili wasichana, ikiwemo ndoa za utotoni na mimba katika maeneo ya vijijini.

Kihongosi afunika mkutano CCM Tanga – HabariLeo

TANGA; WANANCHI wa Tanga wamejitokeza kwa wingi jioni ya leo Septemba 26, 2026 kwenye mkutano wa hadhara wa Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi uliofanyika Viwanja vya Lamore Wilaya ya Tanga.
–
Mkutano huo ni hitimisho la ziara yake ya siku mbili aliyoianza jana mkoani Tanga kwa kutembelea Wilaya ya Mkinga kwa lengo la kukagua uhai wa chama na utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2025-2030.

Mapema leo Kihongosi alitembelea kukagua maendeleo ya ujenzi na ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Tanga, ambao ujenzi wake utagharimu Sh Bilioni 78.8 utakapokamilika.

Akizungumza kwenye ziara hiyo alisema kukamilika kwa mradi huo kutafungua fursa mpya za kiuchumi, kuongeza uwekezaji na kuboresha huduma za usafiri wa anga Mkoa wa Tanga na maeneo ya jirani.

 

Alisema tayari Bandari ya Tanga imeboreshwa na inatoa huduma vizuri, Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani, Tanga umeiva na sasa ujenzi na ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Tanga nao unaendelea, huku ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Tanga kwenda Musoma mkoani Mara nao uko kwenye mchakato.

TBS, WMA NA FCC WATINGA NJOMBE, WABAINI KASORO KATIKA BIDHAA

   Na Mwandishi Wetu.

Kikosi kazi cha Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Wakala wa Vipimo (WMA) na Tume ya Ushindani (FCC), kimehitimisha zoezi la ukaguzi na utoaji elimu kwa wafanyabiashara na wananchi mkoani Njombe, lililofanyika kwa siku tano kuanzia Septemba 19 hadi Septemba 25, 2026, likilenga kuimarisha usalama wa mlaji, ubora wa bidhaa na uadilifu katika biashara.

Zoezi hilo limekuwa sehemu ya juhudi za taasisi hizo katika kuhakikisha bidhaa zinazofika kwa wananchi zinakidhi matakwa ya viwango, vipimo na sheria za ushindani, huku wafanyabiashara wakipatiwa elimu kuhusu wajibu wao katika kulinda afya, usalama na maslahi ya watumiaji.

Katika ukaguzi huo, kikosi kazi hicho kimebaini kasoro mbalimbali katika baadhi ya bidhaa zinazouzwa kwenye maduka na maghala, ikiwemo pembejeo za kilimo, vipodozi, vifaa vya ujenzi na vyakula.

Meneja wa TBS Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Rodney Alananga, amesema ukaguzi huo umebaini changamoto zinazohitaji hatua stahiki, huku akisisitiza kuwa matumizi na uuzaji wa bidhaa zisizokidhi matakwa ya sheria unaweza kuwa na madhara kwa watumiaji na biashara kwa ujumla.

Alananga amesema TBS itaendelea kushirikiana na taasisi nyingine katika kutoa elimu na kufanya ukaguzi ili kuhakikisha wafanyabiashara wanazingatia viwango na wananchi wanapata bidhaa salama na zenye ubora unaostahili.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Njombe, Shabani Kingu, amesema moja ya changamoto iliyobainika ni uwepo wa mifuko ya mbolea yenye ujazo pungufu, hali inayoweza kumuathiri mkulima anayenunua bidhaa hiyo kwa kutegemea kiasi kilichoainishwa kwenye kifungashio.

Amesema WMA itaendelea kusimamia usahihi wa vipimo katika biashara ili kuhakikisha mlaji anapata kiasi cha bidhaa anacholipia na wafanyabiashara wanaendesha shughuli zao kwa kuzingatia sheria.

Naye Kaimu Meneja wa FCC Kanda ya Mbeya, Anderson Lwiza, amesema baadhi ya wafanyabiashara waliobainika kutumia au kunakili nembo za bidhaa za wazalishaji wengine wamechukuliwa hatua za kisheria.

Lwiza amesema hatua hizo ni sehemu ya utekelezaji wa sheria zinazolenga kulinda ushindani wa haki katika soko, pamoja na kuhakikisha wazalishaji halali na watumiaji wanalindwa dhidi ya vitendo vinavyoweza kupotosha soko.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara, Neema Michael, mfanyabiashara wa vipodozi mkoani Njombe, amesema ukaguzi unaofanywa na taasisi hizo umekuwa na umuhimu mkubwa katika kuwasaidia wafanyabiashara kuelewa matakwa ya kisheria na kuhakikisha bidhaa wanazouza ni salama kwa watumiaji.

Amesema elimu inayotolewa wakati wa ukaguzi imekuwa chachu ya kuwajengea wafanyabiashara uelewa kuhusu ubora wa bidhaa na namna ya kuendesha biashara kwa kuzingatia sheria.

Kwa ujumla, zoezi hilo limeonesha umuhimu wa ushirikiano wa taasisi za udhibiti katika kulinda maslahi ya mlaji, kuimarisha uaminifu katika soko na kuwawezesha wafanyabiashara kufahamu na kuzingatia matakwa ya sheria.

TBS, WMA na FCC zimesisitiza kuwa ukaguzi na utoaji elimu kwa wafanyabiashara na wananchi ni mchakato endelevu, unaolenga kujenga soko lenye bidhaa salama, vipimo sahihi na ushindani unaozingatia haki.

TBS YASHIRIKI KONGAMANO LA WAFANYABIASHARA NDOGO NDOGO TEMEKE , YATOA ELIMU YA USALAMA WA BIDHAA .

  Na Mwandishi Wetu.

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kuimarisha juhudi za kulinda afya za wananchi na kukuza biashara zenye kuzingatia viwango kwa kutoa elimu kwa wafanyabiashara wadogo wadogo kuhusu umuhimu wa usalama wa chakula, ubora wa bidhaa na uzingatiaji wa matakwa ya kisheria katika shughuli zao za kila siku.

Elimu hiyo imetolewa leo, Septemba 26, 2026, wakati TBS iliposhiriki Kongamano la Wafanyabiashara Ndogo Ndogo lililofanyika katika Viwanja vya TEFA, Temeke, jijini Dar es Salaam, lililobeba kaulimbiu isemayo “Maendeleo Yangu, Mtaa Wangu, Urasimishaji ndio Uchumi wa Sasa.”

Kupitia kongamano hilo, TBS imekutana na makundi mbalimbali ya wafanyabiashara, wakiwemo Mama Lishe, Baba Lishe na wafanyabiashara wa nguo za mitumba maarufu kama Machinga, kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango na kulinda afya za watumiaji wa bidhaa na huduma zao.

Akizungumza na wafanyabiashara katika kongamano hilo, Meneja wa Tathmini ya Vihatarishi katika Chakula wa TBS, Bi. Immaculatha Justin Tarimo, amesema shirika hilo limetumia fursa hiyo kutoa elimu kwa wafanyabiashara wa chakula, hususan Mama Lishe na Baba Lishe wanaofanya shughuli zao katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu, ikiwemo masoko, stendi na maeneo mengine ya biashara.

Amesema elimu hiyo imelenga kuwahimiza wafanyabiashara hao kuandaa na kuhifadhi chakula katika mazingira safi na salama, ili kulinda afya za wateja wao na kuhakikisha kuwa chakula kinachouzwa kwa walaji kinakuwa salama kwa matumizi ya binadamu.

Bi. Tarimo amesisitiza kuwa kuzingatia usafi katika maandalizi na uhifadhi wa chakula ni jambo muhimu katika kuzuia vihatarishi vinavyoweza kusababisha madhara kwa afya za walaji, hivyo ni wajibu wa kila mfanyabiashara wa chakula kuhakikisha anazingatia maelekezo yanayotolewa na mamlaka husika.

Aidha, amesema wafanyabiashara hao wamekumbushwa kuhusu umuhimu wa kusajili majengo wanayotumia katika shughuli zao za biashara ya chakula, hatua inayochangia kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika katika mazingira yanayokidhi matakwa ya usalama na viwango vinavyohitajika.

Katika hatua nyingine, TBS imetoa elimu kwa wafanyabiashara wa nguo za mitumba kuhusu udhibiti wa uuzaji wa nguo za ndani zilizotumika, zikiwemo nguo za ndani za wanawake na wanaume, mataulo pamoja na nguo nyingine zinazovaliwa katika maeneo nyeti ya mwili wa binadamu.

Wafanyabiashara hao wameelezwa kuwa kwa mujibu wa matakwa ya kisheria, bidhaa hizo zilizotumika haziruhusiwi kuuzwa, kutokana na hatari zinazoweza kujitokeza kwa afya za watumiaji, ikiwemo uwezekano wa kuathiriwa na maradhi kutokana na matumizi ya nguo hizo na watu wengine.

Elimu hiyo inalenga kuongeza uelewa kwa wafanyabiashara kuhusu bidhaa ambazo haziruhusiwi kuuzwa, huku ikiwahimiza kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa katika biashara ya nguo za mitumba, kwa maslahi ya afya ya jamii.

Wakizungumza katika kongamano hilo, wafanyabiashara walioshiriki wameishukuru TBS kwa kuwafikishia elimu hiyo, wakieleza kuwa imewasaidia kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango, kulinda afya za wananchi na kufanya biashara kwa kuzingatia matakwa ya kisheria.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wa nguo za mitumba, Bw. Salehe Omary, mfanyabiashara wa nguo za mitumba katika Soko la Tandika, amesema wameipokea elimu hiyo na kuahidi kuwafikishia wafanyabiashara wengine ili kuongeza uelewa kuhusu bidhaa zisizoruhusiwa kuuzwa na umuhimu wa kulinda afya za watanzania.

Amesema ushirikiano kati ya TBS na wafanyabiashara ni muhimu katika kuhakikisha elimu ya viwango inawafikia wadau wengi zaidi, hususan wafanyabiashara wadogo wanaohudumia wananchi katika masoko na maeneo mbalimbali ya biashara.

Kwa upande wake, Bi. Elizabeth Mfugale, ambaye ni mfanyabiashara wa chakula maarufu kama Mama Lishe, ameishukuru TBS kwa elimu waliyoipata na kuahidi kuyatekeleza maelekezo waliyopewa, hususan katika kuhakikisha chakula kinaandaliwa na kuhifadhiwa katika mazingira safi na salama.

Amesema elimu hiyo ni muhimu kwao kama watoa huduma za chakula, kwani inawasaidia kutambua wajibu wao katika kulinda afya za wateja na kuhakikisha wanapata chakula salama.

Ushiriki wa TBS katika kongamano hilo ni sehemu ya jitihada za kuendelea kuwaelimisha wafanyabiashara kuhusu viwango, usalama wa bidhaa na uzingatiaji wa sheria, huku ukichochea ujenzi wa mazingira bora ya biashara yanayolinda afya za wananchi na kuchangia maendeleo ya uchumi.

Kupitia elimu hiyo, TBS inaendelea kusisitiza umuhimu wa wafanyabiashara kuwa mabalozi wa usalama na ubora wa bidhaa wanazouza, ili kuhakikisha kuwa maendeleo ya biashara yanaenda sambamba na ulinzi wa afya za walaji na ustawi wa jamii.

WAISLAM KIGOMA WAJITOKEZA KUPIMA AFYA, KUCHAGIA DAMU

 

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

WAUMINI wa kiislam Zaidi ya 200 wamejitokeza kupima afya huku uniti 61 za damu zikikusanywa kutoka kwa waumini wa kiislam waliohudhuria Hauli ya kumbukumbu ya miaka 70 ya kifo cha Mwanazuoni na Mwalim Mkubwa wa dini mkoani Kigoma Marehemu Shekhe Mohamed Ibrahim Kabeka iliyofanyika Ujiji mjini Kigoma.

Kiongozi wa timu ya Madaktari waliokuwa wakisimamia zoezi hilo, Shaban Magorwa alisema kuwa zoezi hilo liliendeshwa kwa siku mbili katika msikiti wa Kabondo Ujiji Mjini Kigoma na kwamba zoezi hilo limekuwa na mafanikio makubwa.

Magorwa alisema kuwa mikusanyiko ya kidini na shughuli nyingine za kijamii ni vizuri zikafanyika na kufanyika kwa matukio hayo ya uchangiaji damu na kupima afya hasa kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo Presha na kisukari.

Akizungumza kufanyika kwa maadhimisho hayo kwa niaba ya Familia ya Shekhe Ibrahim kabeke, Shekhe wa mkoa Mwanza, Hassan Kabeke alisema kuwa maadhimisho hayo (Hauli) imefanyika miaka yote tangu kifo cha Mwanzuoni huyo na kwamba hilo linafanyika kuenzi mchango wake mkubwa katika mafundisho ya dini ambayo yametoa wahadhiri, walimu wa dini na Mashekhe mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Pamoja na kupima afya, kuchangia damu, dua na shughuli mbalimbali za kidini pia Shekhe Kabeke alisema kuwa kumefanyika makongamano ya kufundisha elimu ya ujasiliamali na masuala ya uchumi na biashara sambamba na kufundisha elimu ya kujikinga na magonjwa ikiwemo magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Akitoa mada ya elimu ya fedha na ujasiliamali katika maadhimisho hayo Imam wa Masjidi Maamur Upanga jijini Dar es Salaam na Mjumbe wa baraza la Ulamaa Taifa la Baraza kuu la Waisalm Tanzania (BAKWATA), Shekhe Issa Othman amewataka waumin wa dini ya kiislam nchini kujifunza masuala ya elimu ya fedha na biashara na kuanzisha shughuli za ujasiliamali kwani zina mchango mkubwa katika kuendesha maisha yao ya kila siku na kuwaondoa kwenye kashfa ya kuwa ombaomba.

Shekhe Othman alisema kuwa mkoa Kigoma umepata bahati ya kuteuliwa na serikali kuwa mkoa wa kimkakati wa masuala ya uchumi na biashara hivyo waumin wa kiislam wanapaswa kutumia fursa hiyo kuchukua maeneo kuanzisha shughuli za kiuchumi ambazo kwa sasa zinatija kubwa mkoani humo.

BRELA YATOA WITO KWA WAFANYABIASHARA GEITA KUSAJILI BIASHARA KUEPUKA MIGOGORO YA MAJINA

 

Na Matukio Daima  Geita

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umewataka wafanyabiashara na wachimbaji madini mkoani Geita kutumia fursa ya maonesho ya madini kutembelea banda la BRELA na kupata elimu kuhusu umuhimu wa kusajili biashara na kampuni zao.

Wito huo umetolewa wakati BRELA ikishiriki katika Maonesho ya Tisa ya Madini mkoani Geita, ambapo wananchi wanapata fursa ya kujifunza kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo, ikiwemo usajili wa majina ya biashara na kampuni.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Geita, Afisa kutoka  BRELA Athumani Makuka  amewataka wafanyabiashara, wachimbaji na wajasiriamali kuhakikisha wanasajili majina ya biashara zao na kampuni ili kuepuka changamoto na migogoro inayoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya jina moja la biashara na watu tofauti.

Amesema usajili wa jina la biashara ni hatua muhimu kwa mfanyabiashara, kwani humsaidia kutambulika kisheria na kulinda jina alilolijenga kupitia shughuli zake za biashara.

Kwa mujibu wa BRELA, baadhi ya wafanyabiashara huanza kutumia majina ya biashara bila kuyasajili, na baadaye mfanyabiashara mwingine anaweza kusajili jina hilo na kuanza kulitumia kisheria, jambo ambalo linaweza kusababisha migogoro na changamoto kwa mwanzilishi wa biashara hiyo.

“Ni muhimu mfanyabiashara kuhakikisha jina la biashara limesajiliwa mapema ili kulinda utambulisho wa biashara yake na kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza baadaye,” amesisitiza.

Aidha, BRELA imesema inatumia maonesho hayo kuwaelimisha wananchi kuhusu huduma zake pamoja na kuwafikishia huduma karibu na maeneo yao.

Katika maonesho hayo, BRELA pia inatoa baadhi ya huduma bila malipo, ikiwemo huduma zinazohusiana na usajili wa biashara, leseni pamoja na huduma kwa viwanda vidogo na vya kati.

BRELA imewahimiza wananchi wanaoshiriki maonesho hayo, hususan wafanyabiashara na wachimbaji madini, kutumia fursa hiyo kutembelea banda la taasisi hiyo na kupata elimu pamoja na ufafanuzi kuhusu taratibu za usajili wa biashara na kampuni.

Maonesho hayo yanaendelea mkoani Geita yakilenga, miongoni mwa mambo mengine, kuwaunganisha wadau wa sekta ya madini, wafanyabiashara na taasisi mbalimbali za serikali ili kutoa elimu na huduma zinazohusiana na shughuli za kiuchumi.

Leo ni Siku ya Vita Uwanjani: Vigogo wa Ulaya na Afrika Kwenye Kivumbi

Viwanja mbalimbali kuwaka moto leo kuanzia hapa Afrika mpaka Kule Ulaya kuhudia mechi za Kimataifa yaani Afcon na Uefa Nations Leagu. Je nani kuibuka mbabe?

Michuano ya UEFA Nations League inaendelea na Czechia atakiwasha dhidi ya  Croatia katika dimba la Fortuna Arena mjini Prague ambapo huu ni moja ya mchezo ambapo utatazamwa sana.

Lakini Czechia wao wana faida zaidi kwani watakuwa nyumbani hivyo uwepo wa mashabiki zao unawapa hamasa ya kupambana zaidi, lakini wanaenda kukutana na Croatia ambayo ina uzoefu mkubwa kwenye mechi kubwa za Kimataifa.

Jambo muhimu kwa Czechia litakuwa kutokaa nyuma kupita kiasi. Timu hiyo ikiwa itapewa muda wa kumiliki mpira, inaweza kuanza kuzungusha mpira hadi ipate nafasi ya kupenya.

Croatia ina kikosi chenye mchanganyiko wa wachezaji wenye uzoefu na kizazi kipya. Luka Modric na Mateo Kovacic bado ni muhimu kwenye kiungo, huku Joško Gvardiol, Martin Baturina, Petar Sucic na Andrej Kramarić wakiongeza ubora katika maeneo mengine. Kikosi rasmi cha Croatia kinajumuisha pia Perisic, Budimir na Musa.

Mechi kali na ya kibabe ambayo itakuwa inasubiriwa itakuwa ni hii ya Uingereza ambao watakuwa wenyeji wa Hispania kwenye uwanja wa Wembley. Hispania wanaingia kama mabingwa wapya wa dunia wakati vijana wa Thomas wakiazamiwa kufanya vyema kwenye mchezo huu.

Kwa Uingereza, hii ni nafasi kubwa ya kuonyesha kama wamepunguza pengo dhidi ya timu bora za Ulaya. Thomas Tuchel ameuita mchezo huu mwanzo mpya, na kikosi kina vipaji vingi katika maeneo ya kiungo na ushambuliaji.

Hata hivyo, The Lions watakuwa na changamoto kubwa kutokana na kukosekana kwa Declan Rice, Cole Palmer, Marcus Rashford, Tino Livramento na Kobbie Mainoo kutokana na majeraha.

Faida yao kubwa ni kuchezea Wembley. Kucheza mbele ya mashabiki wao kunaweza kuwapa nguvu hasa katika mwanzo wa mchezo.

Hispania wanaingia kwenye mchezo huu wakiwa na kujiamini zaidi baada ya kushinda Kombe la Dunia 2026, sasa wanataka kuendeleza utawala wao kwenye Nations League.

Nguvu yao kubwa ni umiliki wa mpira na uwezo wa kuzungusha mpira kwa kasi, huku wakitumia wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kucheza katika maeneo madogo.

Macho yataelekezwa kwa Lamine Yamal, ambaye anaweza kuwa tatizo kubwa kwa upande wa kushoto wa ulinzi wa Uingereza. Hispania pia wana uwezo wa kubadilisha kasi ya mchezo ghafla kutoka possession ya taratibu kwenda mashambulizi ya haraka.

Kule AFCON pia kuna mechi za pesa lakini tutajikita kwenye mechi ya Afrika Kusini dhidi ya Guinea mchezo wa Kundi D wa kufuzu michuano hii mikubwa Afrika. Mchezo huu una umuhimu mkubwa kwa sababu Kenya, ambayo ipo kwenye kundi hilo, tayari imepata tiketi ya AFCON kama mwenyeji hivyo Afrika Kusini, Guinea na Eritrea zinapigania nafasi iliyobaki.

Ni mchezo wa kwanza wa ushindani kwa Pitso Mosimane tangu arejee kwenye benchi la Bafana Bafana kwa mara ya tatu. Hivyo, kuna presha ya kuanza vizuri, hasa kwa kucheza nyumbani.

Afrika Kusini ina mchanganyiko wa wachezaji wenye uzoefu kutoka Mamelodi Sundowns na Orlando Pirates, jambo ambalo Mosimane amelitaja kama moja ya nguvu za kikosi chake. Pia, Bafana wana nafasi nzuri ya kutumia kasi ya wachezaji wao wa pembeni na uwezo wa kutawala mpira katikati ya uwanja.

Lakini kwa upande wa Guinea si timu rahisi. Ingawa iko chini ya Afrika Kusini kwenye viwango vya FIFA, imekuwa mpinzani mgumu katika mikutano yao iliyopita. Rekodi ya hivi karibuni inaonyesha Afrika Kusini ina ushindi mmoja dhidi ya Guinea na sare moja katika mechi mbili zilizopita.

Nguvu kubwa ya Guinea inaweza kuwa kwenye mipira ya juu na nguvu za mshambuliaji Serhou Guirassy, ambaye Mosimane amemtaja kama tishio kubwa kutokana na uwezo wake wa kucheza kama namba tisa na kutumia mipira ya juu.

Mechi ya mwisho kukutana Afrika Kusini waliondoka na ushindi, hivyo hii ni nafasi ya Guinea kulipa kisasi. Je wataweza huku nafasi ya kuondoka na ushindi ikiwa kwenye timu ambayo imejiandaa.