Kajala Afunguka Kuhusu Harmonize, Aunty na Irene Uwoya Wamshauri

Dar es Salaam – Mambo ya mapenzi yameendelea kuteka mjadala katika ulimwengu wa mastaa wa Bongo, safari hii baada ya Kajala Masanja kufunguka kuhusu uhusiano wake na mwanamuziki Harmonize, huku mastaa wenzake Irene Uwoya, Jacqueline Wolper na Aunty Ezekiel wakihusika katika mazungumzo hayo.

Kajala ameeleza kuwa changamoto zinazojitokeza mara kwa mara katika uhusiano wake na Harmonize hazimaanishi kwamba hana sehemu nyingine ya kwenda au kwamba hana mtu mwingine anayempenda.

Akizungumza mbele ya marafiki zake, Kajala amesema sababu kubwa inayomfanya aendelee kuwa na Harmonize ni namna anavyojisikia anapokuwa naye, akisisitiza kuwa moyo wake unapata hali ya furaha na utulivu akiwa pamoja na mwanamuziki huyo.

Jambo la kuvutia ni kwamba Harmonize alikuwa akisikiliza maelezo hayo moja kwa moja, hivyo alisikia mwenyewe namna Kajala alivyoeleza hisia zake kuhusu uhusiano wao.

Katika mazungumzo hayo, Irene Uwoya na Aunty Ezekiel walimweleza Harmonize kuwa baadhi ya matendo yake yamekuwa yakimkwaza Kajala, hasa kutokana na kuhusishwa na wanawake wengine kisha kurejea kwenye uhusiano wake.

Walimshauri mwanamuziki huyo kufanya maamuzi yatakayompa Kajala uhakika na usalama katika uhusiano wao, badala ya kuendelea na hali inayoweza kumfanya mwenza wake kuwa na mashaka.

Kwa mujibu wa ushauri huo, Harmonize anatakiwa kutulia na kuweka msimamo katika uhusiano wake ili kujenga mazingira yenye utulivu na kuondoa migogoro inayojitokeza mara kwa mara.

Katika sehemu nyingine ya mazungumzo hayo, Harmonize alionekana kushangazwa na mazingira ya kukaa pamoja na Jacqueline Wolper, ambaye aliwahi kuwa mpenzi wake, huku Wolper akiwa tayari na maisha yake ya sasa.

Harmonize alieleza kuwa si jambo la kawaida kwake kukaa sehemu moja na mtu ambaye waliwahi kuwa katika uhusiano wa kimapenzi, hasa wakati kila mmoja ana mwenza wake wa sasa.

Hali hiyo iliongeza mvuto wa mazungumzo hayo, kwa kuwa iliwakutanisha watu wenye historia mbalimbali za kimapenzi katika mazingira moja.

Kwa upande wake, Irene Uwoya alitoa mtazamo wake kuhusu wanaume wanaoingia kwenye mahusiano na wasanii wa kike.

Alisema mwanaume anayekuwa kwenye uhusiano na msanii anapaswa kuwa na uwezo wa kifedha, akisisitiza kuwa katika mahusiano hayo si suala la kutegemea umaarufu wa mwanamke pekee, bali pia mwanaume kuwa na uwezo wa kifedha na kusimama katika majukumu yake.

Mjadala huo umeibua mazungumzo kuhusu changamoto zinazowakabili mastaa katika mahusiano, hasa pale maisha yao binafsi yanapokuwa sehemu ya mijadala ya umma.

Kwa upande wa Kajala na Harmonize, kauli zilizotolewa katika mazungumzo hayo zimeonyesha namna ambavyo hisia, uaminifu na msimamo katika mahusiano vinavyoweza kuwa sehemu muhimu katika kudumisha uhusiano wa watu maarufu.

Kutoka SGR Hadi Wizara ya Ujenzi;- Masanja Kadogosa Ateuliwa Waziri -Video

Masanja Kungu Kadogosa ni Mbunge wa Jimbo la Bariadi Vijijini mkoani Simiyu, kupitia chama cha Chama cha Mapinduzi (CCM) ameteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Waziri wa Ujenzi, akichukua nafasi iliyoachwa na Abdallah Hamis Ulega, ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.

Uteuzi huo umetangazwa Jumapili, Septemba 27, 2026, kupitia taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka.

Kadogosa anaingia katika nafasi hiyo akiwa na uzoefu wa muda mrefu katika sekta ya miundombinu, hususan kwenye masuala ya reli na usafiri. Kabla ya kuingia katika siasa, aliwahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi katika sekta ya fedha na reli.

Kwa miaka kadhaa, Kadogosa alihudumu katika uongozi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), kipindi ambacho Tanzania ilikuwa ikitekeleza mradi mkubwa wa Reli ya Kisasa (SGR).

Safari yake ya kikazi ilianza katika sekta ya benki, ambako aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Mikopo katika Benki ya Maendeleo ya TIB. Mwaka 2016 aliteuliwa kuongoza kampuni ya Reli Tanzania (TRL).

Kadogosa ana shahada ya uzamili ya Utawala wa Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Umeå nchini Sweden, huku akiwa na uzoefu katika maeneo ya uhasibu, usimamizi wa fedha na benki.

Kisiasa, mwaka 2025 aliingia kwenye mchakato wa mchujo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kuwania nafasi ya ubunge, kabla ya sasa kuingia katika Serikali kama Waziri wa Ujenzi.

Akiwa Waziri wa Ujenzi, Kadogosa atakuwa na jukumu la kusimamia sekta inayohusisha ujenzi na maendeleo ya barabara, madaraja pamoja na miradi mbalimbali mikubwa ya miundombinu nchini.

Uteuzi wake unakuja wakati ambapo miradi ya miundombinu ikiendelea kuwa sehemu muhimu ya ajenda ya maendeleo ya Tanzania, hivyo utekelezaji na usimamizi wa miradi hiyo utakuwa miongoni mwa maeneo yatakayokuwa chini ya wizara hiyo.

Uapisho wa mawaziri walioteuliwa utafanyika katika tarehe itakayotangazwa baadaye.

Stori na  Mathna Simba | GPL -TUDACO

DKT. MWIGULU ATEMBELEA MAKTABA YA TAIFA YA QATAR

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Jumapili, Septemba 27, 2026, ametembelea Maktaba ya Taifa ya Qatar (Qatar National Library) jijini Doha, Qatar.

Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu amepokelewa na Rais wa Maktaba hiyo, Dkt. Mohamed Bin Ahmed Bin Twar Al Kuwari, na kupata fursa ya kufahamu shughuli mbalimbali zinazofanywa na taasisi hiyo katika kuhifadhi, kukuza na kuwezesha upatikanaji wa maarifa na urithi wa kiutamaduni.

Ziara hiyo ni sehemu ya ratiba ya Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba akiwa nchini Qatar kwa ziara ya kikazi.

 

Baba Akamatwa Kwa Tuhuma za Kuwatupa Watoto Wake Kutoka Ghorofa ya Sita Japan

Mwanaume mwenye umri wa miaka 25 amekamatwa nchini Japan kwa tuhuma za kujaribu kuwaua watoto wake wawili, baada ya kudaiwa kuwatupa kutoka kwenye roshani ya ghorofa ya sita ya jengo la makazi.

Tukio hilo lilitokea mapema Jumamosi, Septemba 26, katika mji wa Kakamigahara, mkoani Gifu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini Japan, mtuhumiwa huyo, Tomokazu Miura, alidaiwa kuwatupa watoto wake wawili, msichana mwenye umri wa mwaka mmoja na mwingine mwenye umri wa miaka minne, kutoka kwenye roshani ya nyumba yao.

Watoto hao walianguka kutoka urefu wa takribani ghorofa sita, lakini waliangukia kwenye mikeka iliyokuwa imeandaliwa chini na wahudumu wa dharura.

Wote wawili walinusurika na kupelekwa hospitalini. Ripoti zinasema walikuwa na fahamu wakati wakisafirishwa kwenda hospitali, huku majeraha yao yakielezwa kuwa hayakuwa ya kuhatarisha maisha.

Tukio hilo lilitokea saa 4:20 asubuhi, saa za Japan, muda mfupi baada ya polisi kufika katika nyumba hiyo kufuatia simu ya dharura iliyopigwa na mke wa mtuhumiwa usiku wa kuamkia tukio.

Majira ya saa 11:30 jioni siku ya Ijumaa, Septemba 25, mke huyo aliwapigia polisi na kuwaeleza kuwa mume wake alikuwa amemshika mkono wakati wa mabishano.

Polisi walifika katika eneo hilo na kuzungumza na mwanamke huyo nje ya nyumba. Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti, Miura alikataa kushirikiana na polisi na kujifungia ndani ya nyumba.

Inadaiwa kuwa wakati polisi walipokuwa wakijiandaa kuingia ndani, ndipo watoto hao walipotupwa kutoka kwenye roshani.

Kamera za usalama zilizokuwa karibu na eneo hilo zilinasa tukio hilo, huku picha zikionyesha vitu viwili visivyoeleweka vizuri vikianguka kutoka juu ya jengo.

Baada ya tukio hilo, Miura alikamatwa kwa tuhuma za kujaribu kuua. Vyombo vya habari nchini Japan vimeripoti kuwa alibaki kimya wakati akihojiwa na polisi.

Mkazi mmoja wa eneo hilo aliyedai kushuhudia polisi wakimchukua mtuhumiwa alisema kuwa Miura alidaiwa kusema kwamba alikuwa na nia ya kufa pamoja na watoto hao.

Hata hivyo, kauli hiyo ni madai ya shahidi yaliyoripotiwa na chombo cha habari na haijathibitishwa rasmi na polisi.

Polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo, huku watoto hao wakiendelea kupata matibabu hospitalini.

MAGEREZA YAWIKA BAMMATA 2026, JKT NA NGOME JWTZ ZAKUBALI KICHAPO

Na Ssgt Mawazo Mtondo – MWANZA

Timu ya mpira wa wavu wanaume ya Jeshi la Magereza imeendeleza ushindani katika Mashindano ya Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA) 2026, baada ya kuibuka na ushindi wa seti 3–1 dhidi ya Timu ya JKT Tanzania, katika mchezo mkali uliofanyika leo Septemba 27, 2026 katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Mchezo huo uliokuwa wa kusisimua na wenye mashambulizi makali kutoka pande zote mbili, uliwashuhudia wachezaji wa Magereza wakitumia vyema mipango ya ushambuliaji na kuweka ulinzi imara, hali iliyowawezesha kutawala mchezo na hatimaye kupata ushindi wa seti 3–1.

Ushindi huo umeongeza nguvu kwa timu hiyo katika mwendelezo wa mashindano hayo, huku Magereza ikiendelea kuonyesha ushindani mkubwa dhidi ya timu za majeshi na vyombo vya ulinzi na usalama vinavyoshiriki BAMMATA 2026.

Katika mchezo uliotangulia, Timu ya Kanda ya Magereza ilikutana na Timu ya Ngome ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambapo Magereza ilipata ushindi wa seti 3–2 katika mchezo uliokuwa wa ushindani mkubwa.

Matokeo hayo yanaendelea kuonyesha kiwango cha ushindani cha timu ya Magereza katika michuano hiyo, huku wachezaji wakiendelea kuweka nguvu na umakini katika michezo inayofuata.

 

Jazzma Kendrick Afichua Sababu ya Kuachana na Rick Ross

Global Publishers
September 28, 2026
0 views
0 Comments

Siku chache tangu mwanamitindo mashuhuri nchini Marekani, Jazzma Kendrick atangaze rasmi kuvunja uhusiano wake wa kimapenzi na rapa mkongwe Rick Ross, mapya yameibuka baada ya mrembo huyo kudai kuwa aliachana na rapa huyo kwa sababu alikuwa akimfanyia ukatili wa kimwili ikiwemo kumpiga.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Jazzma ameeleza kuwa alipigwa ngumi ya mdomo na msanii huyo, tukio lililomfanya afikie uamuzi wa kuondoka kwenye uhusiano huo.

Mwanamitindo huyo aliongeza kuwa shambulio hilo limemdhihirishia wazi kwamba Rick Ross hana upendo wa dhati kwake.

Tukio hilo limevuta hisia za watu wengi, ikiwa ni pamoja na rapa 50 Cent ambaye ameingilia kati suala hilo kwa kumsemea mbovu hasimu wake huyo wa muda mrefu.

Akizungumzia mkasa huo, 50 Cent alidai kuwa kitendo alichofanya Rick Ross kinatokana na msongo wa mawazo unaomkabili, baada ya albamu yake mpya ya ‘Set In Stone’ kubuma.

Uhusiano wa Jazzma Kendrick na Rick Ross ulianza kuwekwa wazi katikati ya mwaka 2025, ambapo wawili hao walianza kuonekana pamoja hadharani na kupost picha na video za kimapenzi kwenye mitandao ya kijamii.

Hata hivyo, uhusiano wao umekuwa wa kuingia na kutoka (on-and-off relationship), ukikumbwa na migogoro pamoja na kutengana kwa muda mfupi mara kadhaa kabla ya kuibuka kwa tuhuma hizi za hivi karibuni za shambulio la kimwili lililosababisha Jazzma kutangaza kuondoka jumla.

Hadi sasa, Rick Ross hajatoa tamko lolote au kujibu tuhuma hizo za shambulio zilizoelekezwa kwake.

Stori na Hasina Thabit | GPL

UDOM Yatangaza Nafasi Mpya za Kazi 15, Maombi Septemba 28, 2026

Global Publishers
September 28, 2026
1,374 views
0 Comments

Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimetangaza nafasi mbalimbali za ajira kwa Watanzania wenye sifa zinazohitajika, kwa ajili ya kujaza nafasi za kitaaluma. Tangazo hilo limetolewa Septemba 15, 2026.

Nafasi zilizotangazwa

  1. Tutorial Assistant – Fine Arts and Design – Nafasi 1
  2. Tutorial Assistant – International Relations – Nafasi 1
  3. Tutorial Assistant – History – Nafasi 1
  4. Tutorial Assistant – Chinese Language – Nafasi 1
  5. Tutorial Assistant – Biotechnology and Bioinformatics – Nafasi 1
  6. Tutorial Assistant – Applied Entomology – Nafasi 1
  7. Tutorial Assistant – Biomedical Engineering – Nafasi 1
  8. Tutorial Assistant – Psychiatry and Mental Health – Nafasi 1
  9. Tutorial Assistant – Pathology – Nafasi 1
  10. Tutorial Assistant – Physics Teaching Methods – Nafasi 1
  11. Tutorial Assistant – Biology Teaching Methods – Nafasi 2
  12. Tutorial Assistant – Nursing Nephrology – Nafasi 2
  13. Tutorial Assistant – Health Information Science – Nafasi 1

Kwa nafasi nyingi za Tutorial Assistant, mwombaji anatakiwa kuwa na shahada husika yenye GPA ya angalau 3.8 kati ya 5, ingawa sifa zinatofautiana kulingana na nafasi.

Masharti muhimu

Waombaji wote wanapaswa kuwa raia wa Tanzania na wasiwe na umri zaidi ya miaka 45. Pia wanatakiwa kuambatanisha CV yenye mawasiliano sahihi pamoja na nakala zilizothibitishwa za vyeti vya elimu, transcripts, vyeti vya Form IV na Form VI, vyeti vya usajili wa kitaaluma pale inapohitajika, pamoja na cheti cha kuzaliwa.

Waombaji walio katika Utumishi wa Umma hawaruhusiwi kuomba nafasi hizi, kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa kwenye tangazo.

Mwisho wa kutuma maombi ni Septemba 28, 2026. Maombi yote yanatakiwa kutumwa kupitia Recruitment Portal ya Ajira iliyoainishwa kwenye tangazo.

Mwanachama wa Yanga Haji Omari Ramadhani Mpili Afariki Dunia

Global Publishers
September 28, 2026
12 views
0 Comments

Mwanachama wa Yanga, Haji Omari Ramadhani Mpili, amefariki dunia usiku wa Septemba 27, 2026, akiwa anapatiwa matibabu katika Kituo cha Afya cha Wilaya ya Ikwiriri, Mkoa wa Pwani.

Kwa mujibu wa taarifa ya Uongozi wa Yanga, marehemu anatarajiwa ku =zikwa leo Jumatatu, Septemba 28, 2026, saa 10:00 jioni, katika Makaburi ya Msikiti Mkuu, Wilaya ya Ikwiriri, Mkoa wa Pwani.

Uongozi wa Yanga umetuma salamu za pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na wadau wa mpira kwa msiba huo, huku ukiwaomba kuwa na subira na utulivu katika kipindi hiki kigumu.

Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.

TMDA YAPIGA MARUFUKU MATANGAZO YA DAWA ZA KUACHA POMBE

 

 

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), imepiga marufuku matangazo yote yanayohamasisha matumizi ya dawa za kupunguza au kuacha unywaji wa pombe zikiwamo Naltrexone, Acamprosate na Disulfiram.

Taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt Adam Fimbo iliyotoelewa leo Jumapili, Septemba 27,2026, imesema kuwa mamlaka imebaini baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii vimekuwa vikirusha matangazo ya dawa hizo ambazo kisheria ni dawa zinazotolewa kwa cheti cha daktari pekee (Prescription-Only Medicines – POM).

TMDA imesema matumizi ya dawa hizo bila ushauri wa mtaalamu wa afya yanaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo kifo, hasa zinapotumiwa pamoja na pombe au dawa nyingine.

“Kifungu cha 52 cha Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba, Sura ya 219, kinakataza kutangaza kwa umma dawa yoyote inayotolewa kwa cheti cha daktari. Dawa hizo zinaruhusiwa kutangazwa kwa wataalamu wa afya pekee kupitia majarida ya kitaalamu,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Kutokana na hali hiyo, TMDA imewaelekeza wafanyabiashara, watoa huduma za afya, wamiliki wa vyombo vya habari na waendesha mitandao ya kijamii kuacha mara moja kuandaa, kurusha na kuchapisha matangazo hayo na kuwataka wananchi kutoa taarifa wanapobaini watu, vituo au vyombo vinavyotangaza dawa hizo kupitia ofisi za TMDA zilizopo maeneo mbalimbali nchini.