MAGEREZA YAIPIGISHA KWATA POLISI BAMMATA 2026

Na Ssgt Mawazo Mtondo – MWANZA

Timu ya mpira wa pete ya Jeshi la Magereza imeendeleza kiwango chake kizuri katika Mashindano ya Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA) 2026, baada ya kuibuka na ushindi wa magoli 63–36 dhidi ya timu ya Polisi Tanzania katika mchezo uliochezwa leo, Septemba 28, 2026, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa, timu ya Magereza ilionyesha uwezo mzuri katika kujenga mashambulizi na kutumia vyema nafasi ilizopata, hali iliyoiwezesha kufunga magoli 63 na kuibuka na ushindi wa kishindo dhidi ya Polisi.

Ushindi huo unaendeleza mwendelezo mzuri wa Kanda ya Magereza katika mashindano hayo, baada ya awali kuifunga Kanda ya JKT Tanzania kwa magoli 46–43.

 

ENG. SAMAMBA ATOA MAELEKEZO KWA WAMILIKI WA MIGODI NA MAAFISA MADINI WAKAZI WA MIKOA

🔶Aagiza maboresho ya taratibu za migodi, ukaguzi wa maduara, mabwawa ya tope sumu na maandalizi ya dharura

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Eng. Yahya I. Samamba, amewaelekeza wachimbaji wadogo, wamiliki, mameneja na wakaguzi wa migodi nchini kuchukua hatua za haraka kujiandaa na kukabiliana na mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha kuanzia Oktoba hadi Desemba mwaka huu, ikiwemo kuongeza kasi ya ukaguzi wa maeneo ya uchimbaji (maduara), mabwawa ya kuhifadhia tope sumu na kuimarisha mipango ya dharura.

Eng. Samamba ametoa maelekezo hayo leo, Septemba 28, 2026, wilayani Kahama Mkoani Shinyanga wakati akifungua mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini kuhusu maandalizi ya kukabiliana na athari za mvua hizo, akisema tahadhari hiyo inazingatia taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu uwezekano wa mvua kubwa kuliko wastani katika kipindi hicho.

Amesema mvua hizo zinaweza kuathiri shughuli za uchimbaji na kusababisha madhara kwa watu, mazingira, miundombinu na uzalishaji iwapo hatua stahiki za tahadhari hazitachukuliwa mapema.

“Wamiliki, mameneja na wakaguzi wa migodi wanapaswa kuboresha taratibu za usalama ili ziakisi hali ya mvua kubwa, kuongeza ukaguzi wa maduara na mabwawa ya kuhifadhia tope sumu, pamoja na kuhakikisha kila mgodi una mpango wa dharura unaoeleweka na kutekelezeka,” amesema.

Amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa wachimbaji wadogo katika maendeleo ya sekta ya madini na uchumi wa Taifa, hivyo maandalizi hayo ni muhimu ili shughuli za uchimbaji ziendelee kwa usalama na tija.

Eng. Samamba amesema miongoni mwa hatari zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua kubwa ni kuporomoka kwa maduara na kuta za migodi kutokana na miamba kulainika na kupoteza uimara, mafuriko ndani ya migodi, kudhoofika kwa mihimili inayoshikilia miamba, pamoja na kufurika au kudhoofika kwa mabwawa ya kuhifadhia tope sumu.

Amesema pia mazingira yasiyo safi na maji yaliyotuama yanaweza kuongeza hatari za kiafya kwa wachimbaji na jamii zinazozunguka maeneo ya migodi.

 

Kwa mujibu wa Eng. Samamba, wamiliki, mameneja na wakaguzi wa migodi wanapaswa kuhakikisha hakuna mchimbaji anayeingia au kuendelea kufanya kazi chini ya ardhi wakati wa mvua kubwa au mara baada ya mvua kukatika iwapo hali ya eneo husika si salama.

 

Aidha, amewaagiza kuhakikisha maduara yanakaguliwa kila siku kabla ya kazi kuanza na sehemu zote dhaifu kuimarishwa kwa kutumia mihimili imara ya miti au chuma kulingana na mahitaji ya kiusalama.

 

Amesema mifereji inayozunguka midomo ya maduara na maeneo ya kazi inapaswa kujengwa na kusafishwa mara kwa mara, huku matuta, kingo, mawe na vifusi vikitumika katika maeneo yanayohitaji ulinzi ili kuzuia maji ya juu ya ardhi kuingia kwenye migodi.

 

“Kila mgodi unapaswa kuwa na pampu za kuvuta maji pamoja na mafuta ya kutosha ili kuwezesha kuchukua hatua za haraka endapo maji yatajaa kwenye mashimo,” amesema.

 

Kuhusu mabwawa ya kuhifadhia tope sumu (TSF), Eng. Samamba amewataka waendeshaji wa migodi kuhakikisha mabwawa hayo yana nafasi na uimara wa kutosha kupokea ongezeko la maji wakati wa mvua, huku ukaguzi wa kingo, mifereji, kiwango cha maji, dalili za kuvuja na mmomonyoko ukifanyika kwa wakati.

 

Amesema hatua hizo ni muhimu katika kuzuia madhara kwa binadamu, wanyama, mimea na mazingira.

 

Eng. Samamba pia amesisitiza kuzingatiwa kwa taratibu za usalama wakati wa ulipuaji, akielekeza kuhakikisha watu wote wanatoka katika eneo la tukio na kufika umbali salama kabla ya ulipuaji, na kurejea baada ya muda uliowekwa kwa mujibu wa taratibu za usalama.

 

Amesema zamu za wachimbaji zinapaswa kusimamiwa kwa kuzingatia uwezo wa watendaji ili kuzuia uchovu unaoweza kuongeza uwezekano wa kutokea kwa ajali.

 

Aidha, amewaelekeza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kusimamia utekelezaji wa maelekezo hayo pamoja na Kanuni za Madini (Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira) za mwaka 2010, na kuchukua hatua stahiki pale ukiukwaji unapobainika.

Amesema ukaguzi wa mabwawa ya kuhifadhia tope sumu, maeneo ya kuhifadhi miamba taka na miundombinu mingine ya migodi unapaswa kuongezwa kabla na wakati wa mvua, huku kasoro zinazoweza kuhatarisha usalama zikishughulikiwa mara moja.

 

Amesisitiza kuwa kila mgodi unapaswa kuwa na mpango wa dharura unaoeleweka kwa watendaji, unaoainisha namna ya kutoa taarifa, kuokoa watu, kusimamisha shughuli pale inapobidi na kuwasiliana na mamlaka husika.

 

Aidha, amewataka viongozi wa vyama vya wachimbaji wa madini kutumia mitandao yao kutoa elimu kwa wanachama na kuwataka wachimbaji kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa na kuzitumia katika kupanga shughuli zao za kila siku.

 

“Kaeni na wachimbaji, wasikilizeni hoja zao na mzitatue kwa kushirikiana. Tusifanye kazi kwa maelekezo pekee, bali kwa ushirikiano,” amesema.

 

Amesema usalama haupaswi kuchukuliwa kuwa gharama inayopunguza uzalishaji, kwa kuwa ajali inaweza kusababisha kusimama kwa shughuli za uchimbaji, kuharibu miundombinu, kuathiri mazingira na jamii na kusababisha kupoteza maisha.

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wakaguzi wa Migodi Tanzania, Shija Mussa, amesema wachimbaji wadogo wanakabiliwa na changamoto ya maji kujaa kwenye mashimo wakati wa uchimbaji na kuiomba Serikali kusaidia upatikanaji wa mitambo mikubwa ya kunyonya maji (heavy-duty pumps) pamoja na vifaa vingine vya dharura.

 

Amesema mitambo hiyo inapaswa kuwekwa katika maeneo ya kimkakati ili iweze kutumika kwa haraka wakati wa dharura.

 

Awali, Mkurugenzi wa Leseni kutoka Tume ya Madini, Eng. Aziza Swedi, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Eng. Ramadhani Lwamo, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwapa wachimbaji wadogo

 elimu na uzoefu kuhusu namna ya kuchukua tahadhari dhidi ya athari za mvua kubwa.

 

Amesema Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Tume ya Madini imeamua kuchukua hatua mapema baada ya kutolewa kwa tahadhari ya mvua, ambapo wataalamu wanawasilisha mada kuhusu usalama wa migodi, mabwawa ya kuhifadhia tope sumu, maeneo ya kuhifadhi miamba taka, udhibiti wa mafuriko na mipango ya dharura.

 

Eng. Swedi amesema mafanikio ya mafunzo hayo yataonekana kupitia utekelezaji wa vitendo katika maeneo ya uchimbaji, akiwataka washiriki kurejea katika maeneo yao ya kazi, kufanya tathmini, kubaini maeneo hatarishi na kurekebisha kasoro kabla ya madhara kutokea.

RC HAMDUN AWATAKA WATUMISHI KUFATA SHERIA, KANUNI NA TARATIBU

 .

NA CHAUSIKU SAID

MATUKIO DAIMA MWANZA

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, CP Salum Hamdun, amewataka watumishi wa umma katika Wilaya ya Kwimba kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu yao, akisisitiza kuwa hatakuwa na utani kwa watumishi watakaoshindwa kutekeleza maagizo na maelekezo ya Serikali.

CP Hamdun ametoa kauli hiyo kufatia hatua ya mkuu wa Wilaya ya Kwimba Ng’wilabuzu Ludigija kumwamuru Mkurugenzi wa halmashauri hiyo pamoja na wakuu idara wote kuripoti kwa mkuu wa polisi wa Wilaya (OCD) kufatia hatua yao ya kukaidi mara kadhaa agizo la kushiriki zoezi la usafi wa mazingira.

Maagizo hayo ameyatoa leo septemba 28, 2026 wakati akizungumza na viongozi na watumishi wa Wilaya ya Kwimba, ambapo amesisitiza umuhimu wa watumishi kutekeleza kikamilifu maelekezo yanayotolewa na viongozi katika ngazi mbalimbali kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.

Amesema watumishi wa umma, viongozi na watendaji katika kila ngazi wanapaswa kuhakikisha wanafata maagizo na maelekezo yanayotolewa na Serikali nakutekelezwa kwa wakati na kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

Akitolea mfano wa zoezi la usafi wa mazingira, CP Hamdun amesema agizo la kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi linatoka Serikalini na limekuwa likishushwa kutoka ngazi ya Taifa hadi mkoa na wilaya, hivyo hakuna sababu kwa watumishi kushindwa kulitekeleza.

Aidha amefafanua kuwa kutokuwepo kwa baadhi ya watumishi katika utekelezaji wa majukumu yaliyokubaliwa kunatoa taswira ya kutokuwepo kwa ushirikiano na uwajibikaji miongoni mwa watendaji wa Serikali.

“Hawezekani Mkuu wa Wilaya kufika kwenye zoezi ambalo tulikubaliana, halafu akitazama kulia na kushoto anajikuta yuko peke yake niwaombe watumishi wa umma na Mkurugenzi Mtendaji ambaye ni mamlaka ya nidhamu, pamoja na Baraza la Madiwani, kusimamia nidhamu ya watendaji wa halmashauri,” amesema CP Hamdun.

Amesema ni wajibu wa kila mtumishi wa umma kutenda kwa mujibu wa taratibu, akizingatia sheria za utumishi wa umma, maelekezo na miongozo ya Serikali pamoja na maadili ya viongozi na watendaji.

CP Hamdun amemtaka Katibu Tawala wa Wilaya kuhakikisha watumishi walio chini ya mamlaka yake wanafuata sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma, huku akisisitiza kuwa suala hilo halipaswi kufanyiwa mzaha.

“Sitakakuwa na utani na mtu yeyote yule. Katibu Tawala Mkoa, hakikisha jambo hili unalisimamia. Kama unaona huwezi kufanya kazi, una shughuli zako nyingine, andika notisi ya saa 24 kuacha kazi, maana tunao Watanzania vijana wengi wenye sifa na uwezo wa kuajiriwa,” amesema.

Aidha, amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, ambaye ni mamlaka ya nidhamu kwa watumishi, pamoja na Baraza la Madiwani kupitia uongozi wake, kuhakikisha nidhamu ya watendaji inasimamiwa na watumishi wanawajibika katika maeneo yao ya kazi

Hata hivyo ameeleza kuwa  utekelezaji wa maagizo ya Serikali unapaswa kuwa sehemu ya majukumu ya kila siku ya mtumishi wa umma, huku kila mmoja akitakiwa kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia sheria na taratibu bila kusubiri kusukumwa na viongozi.

Amesema usafi wa mazingira nao unapaswa kuwa sehemu ya utamaduni wa wananchi wa Wilaya ya Kwimba, ambapo pamoja na kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi, zoezi hilo linapaswa kwenda sambamba na upandaji miti na uanzishaji wa bustani za kupumzikia ili kuboresha mazingira ya miji na maeneo ya makazi.

RC HAMDUN, TUSHIRIKIANE KUTATUA CHANGAMOTO ZA MAJI, BARABARA KWIMBA

NA CHAUSIKU SAID

MATUKIO DAIMA MWANZA.

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, CP Salum Hamdun, amesema atahakikisha anashirikiana na wananchi wa Wilaya ya Kwimba katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto za maji na barabara zinazowakabili wakazi wa wilaya hiyo.

Amesema utatuzi wa changamoto hizo mbili ni miongoni mwa mambo muhimu yatakayosaidia kuleta tabasamu kwa wananchi wa Kwimba, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, viongozi na wananchi katika kuzitafutia ufumbuzi.

CP Hamduni ameyasema hayo leo Septemba 28, 2026, wakati wa ziara yake ya kujitambulisha kwa watumishi wa Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza, na kueleza kuwa barabara nyingi katika wilaya hiyo zinapitika, lakini bado zinahitaji maboresho ili kuwawezesha wananchi kupata huduma na kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa urahisi zaidi.

Ameeleza kuwa moja ya kilio kikubwa cha wananchi wa Kwimba ni wilaya hiyo  kutounganishwa kikamilifu kwa barabara ya lami na makao makuu ya Mkoa.

Aidha ameeleza, kuwa  Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 hadi Agosti 2026, Wilaya ya Kwimba imepokea zaidi ya Sh bilioni 17 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya barabara.

“Fedha hizo zimetumika katika kuboresha miundombinu ya barabara, hali ambayo imewezesha baadhi ya barabara katika wilaya hiyo kupitika kwa urahisi” Alisema Hamduni.

Aidha amefafanua kuwa katika mwaka wa fedha 2026/2027, wilaya hiyo imetengewa kiasi cha Sh bilioni 4 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya barabara katika maeneo mbalimbali, yakiwemo Kata za Sumve, Ngudu, Hungumalwa, Malya, Mwantale na Mwabomba.

Aidha ameeleza kuwa kwa upande wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), imeelezwa kuwa kuna miradi mbalimbali inayohusisha barabara muhimu katika Wilaya ya Kwimba, ikiwemo kipande cha barabara kutoka Ngudu hadi Mabuki chenye urefu wa kilomita 26, Ngudu hadi Malya kilomita 28, pamoja na barabara ya kiwango cha lami kutoka Hungumalwa hadi Magu yenye urefu wa kilomita 71.

Akisoma taarifa ya Wilaya ya Kwimba mbele ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya hiyo, Ng’wilabuzu Ludigija, alisema changamoto ya maji bado ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili wananchi kutokana na uchakavu wa bomba la maji linalohudumia wilaya hiyo.

Alisema bomba hilo lilianza kutumika tangu mwaka 1975 na kwa sasa limezeeka, hali inayochangia kuwepo kwa changamoto katika upatikanaji wa maji

Hata hivyo, alisema wananchi wanamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuelekeza hatua za kuchukuliwa, ikiwemo kuingia mkataba na mkandarasi kwa ajili ya kubadilisha bomba hilo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ukarabati wa mradi huo utakaogharimu kiasi cha  Sh milioni 6 na ukikamilika unatarajiwa kusaidia kuondoa changamoto ya maji inayowakabili wananchi wa Wilaya ya Kwimba.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kwimba, Cosmas Bulala, ameeleza kuwa Wilaya ya Kwimba ndiyo pekee ambayo haijaunganishwa kwa barabara ya lami na makao makuu ya Mkoa wa Mwanza, akieleza umuhimu wa suala hilo kushughulikiwa

Mzee Mpili Apumzishwa katika Makaburi ya Msikiti, Ikwiriri – (Picha + Video)

Global Publishers
September 28, 2026
54 views
0 Comments

MAZIKO ya Mwanachama wa Yanga, Haji Omari Ramadhani Mpili, yamefanyika leo Jumatatu, Septemba 28, 2026, katika Makaburi ya Msikiti Mkuu, Wilaya ya Ikwiriri, Mkoa wa Pwani.

Maziko hayo yamefanyika majira ya saa 10:00 jioni, kufuatia kifo chake kilichotokea usiku wa Jumapili, Septemba 27, 2026, akiwa anapatiwa matibabu katika Kituo cha Afya cha Wilaya ya Ikwiriri.

Katika msiba huo, Msemaji wa Yanga, Ally Kamwe, amewasili nyumbani kwa marehemu Ikwiriri na kushiriki katika kutoa pole kwa familia pamoja na ndugu na jamaa.

Akizungumza wakati wa msiba, mtoto wa marehemu ametoa shukrani kwa Rais wa Yanga kwa namna alivyomhudumia baba yake wakati wa kipindi cha ugonjwa hadi alipofariki dunia.

Msiba huo umehudhuriwa na ndugu, jamaa, marafiki pamoja na baadhi ya wanachama na wapenzi wa Yanga waliofika kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu.

Uongozi wa Yanga uliwahi kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na wadau wa mpira kufuatia kifo cha Haji Omari Ramadhani Mpili.

Mzee Mpili Apumzishwa, Mwanaye Atoa Shukrani kwa Rais wa Yanga – Video

Global Publishers
September 28, 2026
24 views
0 Comments

MAZIKO ya Mwanachama wa Yanga, Haji Omari Ramadhani Mpili, yamefanyika leo Jumatatu, Septemba 28, 2026, katika Makaburi ya Msikiti Mkuu, Wilaya ya Ikwiriri, Mkoa wa Pwani.

Maziko hayo yamefanyika majira ya saa 10:00 jioni, kufuatia kifo chake kilichotokea usiku wa Jumapili, Septemba 27, 2026, akiwa anapatiwa matibabu katika Kituo cha Afya cha Wilaya ya Ikwiriri.

Katika msiba huo, Msemaji wa Yanga, Ally Kamwe, amewasili nyumbani kwa marehemu Ikwiriri na kushiriki katika kutoa pole kwa familia pamoja na ndugu na jamaa.

Akizungumza wakati wa msiba, mtoto wa marehemu ametoa shukrani kwa Rais wa Yanga kwa namna alivyomhudumia baba yake wakati wa kipindi cha ugonjwa hadi alipofariki dunia.

Msiba huo umehudhuriwa na ndugu, jamaa, marafiki pamoja na baadhi ya wanachama na wapenzi wa Yanga waliofika kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu.

Uongozi wa Yanga uliwahi kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na wadau wa mpira kufuatia kifo cha Haji Omari Ramadhani Mpili.

Ndejembi Aagiza Mashirika ya Umma Kutoa Fursa kwa Vijana 10,000

Global Publishers
September 28, 2026
36 views
0 Comments

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Deogratius Ndejembi ametoa wiki mbili kwa Wizara ya Mipango na Uwekezaji, Fedha na Kilimo kuandaa mpango wa mafunzo kwa Vitendo ambao utaanza kuchukua walau vijana 10,000 kupata uzoefu katika Taasisi, Mashirika ya Umma na Sekta binafsi ili kuandaa vijana watakaokuwa na uzoefu wa kujiajiri na kuajiriwa kama sehemu muhimu ya kutekeleza nguzo ya pili ya Dira ya Taifa 2050 na kusaidia maendeleo ya Nchi.

Makamu wa Rais ametoa maelekezo hayo wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwenye ufunguzi wa Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Mashirika ya Umma, kinachofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC).

Amewataka Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Mashirika ya Umma kubadili namna taasisi hizo zinavyofanya kazi na kuwa injini ya mageuzi ya uchumi kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku akielekeza kuanzishwa kwa mkakati huo utakaowapatia angalau wahitimu 10,000 nafasi za mafunzo kwa vitendo na kuwapatia fedha za kujikimu katika mashirika ya umma na wengine wasiopungua 20,000 katika sekta binafsi.

“ Kila mwaka kwa takribani vijana 62,570 wanahitimu elimu ya juu na hii ni takwimu ya mwaka Jana 2025 toka TCU, idadi hiyo haihusishi wale wanaomaliza VETA na Vyuo vya Kati.

Ukiangalia TAESA takwimu zao zinaonesha vijana 3,200 pekee walikuwa wamepitia programu za mafunzo internship, idadi hii ni ndogo sana kwa kulinganishwa na wahitimu 62,570 kutoka vyuo mbalimbali nchini.

Mlitazame hili kama uwekezaji wa kimkakati katika nguvu kazi ya Taifa kwa kubana matumizi ya kawaida, na hapa mtakuwa mmetekeza kwa Vitendo nguzo ya pili ya Dira 2050” alisisitiza

Mhe. Ndejembi, amesema dhamana ya Watendaji, Wakuu wa Mashirika na Wenyeviti wa Bodi ni kubwa, na hivyo wanatakiwa kutekeleza majukumu yao kwa ustadi na umakini mkubwa na kwa wakati sahihi katika kujenga uchumi, kuibua fursa mpya na kuinua maisha ya watanzania.

MABAHARIA WA TANZANIA WAGEUKA MABALOZI WA UTALII, NGORONGORO YAWAPA SABABU YA KUHAMASISHA DUNIA

Na Matukio Daima Media, Arusha

KATIBU wa Jumuiya ya Mabaharia Tanzania (Old Navy), Daniel Masele, amewataka Watanzania kuacha kuangalia hifadhi na vivutio vya utalii kama vitu vya wageni pekee, akisema safari yao katika Bonde la Ngorongoro imewapa fursa ya kushuhudia kwa macho yao utajiri wa asili ambao Tanzania imejaaliwa.

Masele amesema mabaharia hao, ambao wamekuwa wakisafiri katika maeneo mbalimbali duniani, wamekutana na mambo mengi katika safari zao, lakini baadhi ya yale waliyoyaona, Tanzania ni ya kipekee na hawajawahi kuyaona katika maeneo mengine waliyofika..

Amesema walipokuwa Ngorongoro walishuhudia wanyama mbalimbali wanaoishi ndani ya kreta, jambo alilolitaja kuwa sehemu ya maajabu yanayopaswa kuwafanya Watanzania wenyewe kuwa sehemu ya kwanza ya kutembelea na kuitangaza nchi yao.

Kwa mujibu wa Masele, Tanzania imekuwa ikipata mapato kupitia utalii, huku sehemu kubwa ya wageni wanaotembelea vivutio hivyo wakitoka nje ya nchi, hivyo Watanzania wanapaswa kutumia fursa hiyo kuvifahamu vivutio vyao na kuwa mabalozi wa utalii wanapokwenda maeneo mbalimbali.

Kauli hiyo imeungwa mkono na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Mohamed Said Ngamba, ambaye amesema wazo la kuanzisha Old Navy lilitokana pia na kutambua nafasi waliyonayo mabaharia kuitangaza Tanzania kutokana na mazingira yao ya kazi yanayowapeleka katika nchi na maeneo mbalimbali duniani.

Ngamba amesema wakiwa safarini baharini walikuwa wakifuatilia juhudi mbalimbali za kuitangaza Tanzania, ikiwemo kupitia Royal Tour, na kuona kuwa nao wana wajibu wa kushiriki katika kuitangaza nchi yao na kumuunga Mkono Rais  Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa kueleza kwa watu wanaokutana nao kuhusu vivutio vilivyopo Tanzania.

Amesema mabaharia ni sehemu ya wawakilishi wanaokutana na watu kutoka mataifa mbalimbali, hivyo Jumuiya yao imeamua kutumia nafasi hiyo kuhamasisha utalii kwa ushuhuda wa maeneo wanayoyatembelea wenyewe.

“Hatupaswi kukaa kimya wakati nchi yetu ina vivutio vingi. Kama tunasafiri na kukutana na watu kutoka sehemu mbalimbali duniani, tunapaswa kuwaambia Tanzania ina nini na kuwaalika waje kuona wenyewe,” amesema Ngamba.

Ameeleza kuwa ziara ya Ngorongoro ni sehemu ya mpango wao wa kutembelea vivutio mbalimbali nchini, wakianza na Mikumi na baadaye kutembelea maeneo mengine, ikiwemo Mlima Kilimanjaro, ili wanapozungumza kuhusu utalii wa Tanzania wawe wameviona vivutio hivyo kwa macho yao.

Amesema katika ziara hiyo amevutiwa na mandhari ya Ngorongoro pamoja na wanyama mbalimbali aliowaona, akiwemo Simba, Faru, Pundamilia na Kiboko, na kwamba uzoefu huo utawapa nguvu zaidi katika kuwahamasisha wengine kutembelea Tanzania.

Mabaharia wengine walioshiriki ziara hiyo, Omary Said Kipelele, Siwatu Hassan Sembi, Fahad Mohamed na Miraji Omary, wamesema watatumia fursa walizonazo kuwahamasisha ndugu, marafiki na watu wanaokutana nao nje ya Tanzania kutembelea nchi hiyo na kushuhudia vivutio vilivyopo.

Wamesema wanatambua umuhimu wa juhudi zinazofanywa na Serikali katika kukuza sekta ya utalii, huku wakimshukuru Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt Mahmoud Thabit Kombo, kwa kusaidia kuwezesha safari zao za kutembelea hifadhi za Taifa ili waweze kupata uzoefu wa moja kwa moja wa vivutio wanavyotaka kuvitangaza.

Kwa upande wake, mdau wa utalii kutoka Kampuni ya Utalii ya Mbapari, Isaya John, amesema Watanzania wanapaswa kutumia fursa hiyo kutembelea hifadhi kwa kuwa gharama za kuingia kwa raia wa Tanzania zimewekwa katika viwango vinavyoweza kumudu, hivyo wananchi hawapaswi kuziacha fursa hizo na kuwaachia wageni pekee.

Wito huo umejitokeza pia wakati zaidi ya watu 1,700 waliokuwa wakishiriki Wiki ya Kitaifa ya Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza (MEL Week 2026), iliyofanyika Ngurdoto Mountain Lodge, Arusha, baadhi yao walipopata fursa ya kutembelea Ngorongoro na wengine vivutio vingine Jijini humo.

Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Yasin Msangi, amesema washiriki hao walikuwa wamekutana Arusha kwa ajili ya wiki hiyo iliyofanyika Septemba 22 hadi 26, 2026, na kuvutiwa kutumia nafasi hiyo ambapo watu zaidi ya 1000 wakiwa na magari zaidi ya 100 kutoka nchi mbalimbali za Afrika wakaamua kutembelea Ngorongoro na kujionea vivutio vilivyopo.

Msangi amesema ziara hiyo imewapa washiriki fursa ya kuona kwa vitendo kile ambacho mara nyingi hukisikia au kukisoma, huku akiwataka Watanzania wengine kujenga utamaduni wa kutembelea hifadhi na vivutio vya ndani

Kwa upande wao, Mabaharia wa Tanzania wamesema safari yao haitakuwa ya mara moja, bali wanatarajia kuendelea kutembelea maeneo mengine ya utalii nchini na kutumia uzoefu huo kuwaeleza wengine, hasa wanaokutana nao katika safari zao za kimataifa, kuhusu uzuri na utajiri wa Tanzania.

Lissu Aibua Mapungufu Katika Kesi ya Uhaini, Amtaja ACP Bagyemu

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ameiambia Mahakama kuwa kesi ya uhaini inayomkabili ina mapungufu kadhaa, akidai kuwa mchakato wa kuanzisha upelelezi wa kesi hiyo ulifanywa na mtu mmoja au watu wachache bila kuwashirikisha baadhi ya mamlaka husika.

Lissu ametoa hoja hizo leo, Jumatatu, Septemba 28, 2026, wakati akiendelea kuwasilisha hoja zake za mwisho mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru.

Katika hoja zake, Lissu amemtaja Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) George Bagyemu, anayehudumu kama Naibu Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, akidai kuwa ndiye aliyeamua kwamba maneno yaliyokuwa kwenye video yanaunda kosa la uhaini.

Lissu amesema kwa mujibu wa rekodi ya mahakama katika ukurasa wa 145 na 146, tukio hilo lilihusisha hatua zilizochukuliwa Aprili 8, 2025, siku nne baada ya video hiyo kuonekana.

Amedai kuwa baada ya Bagyemu kuipata video hiyo, alifungua faili la uchunguzi wa uhaini bila kuwashirikisha baadhi ya wakuu wake wa kazi, akiwamo Mkuu wa Polisi Kanda Maalum (ZPC) na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).

Kwa mujibu wa Lissu, Bagyemu aliwafahamisha viongozi hao baada ya faili hilo kufunguliwa.

Lissu pia amedai kuwa Bagyemu hakutafuta ushauri wa kisheria kabla au baada ya kufungua faili hilo. Akirejea ukurasa wa 159 wa rekodi ya ushahidi, amesema suala hilo lilithibitishwa katika ushahidi wa Bagyemu.

Aidha, Lissu amesema hata Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hakujulishwa kuhusu suala hilo wakati huo.

Ameongeza kuwa licha ya Bagyemu kuwafahamisha baadhi ya viongozi kuhusu hatua alizochukua, hakuna hata mmoja kati yao aliyefika mahakamani kutoa ushahidi kuhusu suala hilo.

Lissu pia amedai kuwa Bagyemu hakuhusisha wala kutoa taarifa kwa mamlaka nyingine za uchunguzi au taasisi nyingine za Serikali kuhusu hatua hizo.

Katika hatua hiyo ya hoja zake za mwisho, Lissu amesisitiza kuwa jukumu la kuthibitisha mashtaka linabaki upande wa mashtaka, akidai kuwa ushahidi uliowasilishwa mahakamani haujafikia kiwango cha uthibitisho kinachotakiwa kisheria.

FAIDA KUU YA LISHE BORA

 

 

NA BIBI MAENDELEO IRENE SAMORA

Lishe bora ni msingi muhimu katika ukuaji, afya na maendeleo ya mtoto, huku jamii ikihimizwa kuhakikisha watoto wanapata mlo kamili wenye virutubisho muhimu kwa ajili ya kuimarisha afya ya mwili na akili.

Akizungumza katika kipindi cha Bibi Maendeleo, kinachorushwa na Matukio Daima TV, Bibi Maendeleo Irene Samora amesema jamii inapaswa kuwa na uelewa mpana kuhusu umuhimu wa lishe bora, hususan kwa watoto, ili kusaidia kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na ukosefu wa lishe sahihi.

Irene amesema watoto wanapaswa kula mlo wenye mchanganyiko wa vyakula kutoka katika makundi mbalimbali, ili miili yao iweze kupata virutubisho vinavyohitajika kwa ajili ya ukuaji na maendeleo.

Amesema mlo bora unapaswa kuzingatia makundi mbalimbali ya vyakula, ikiwemo vyakula vya wanga, protini, mboga za majani na mboga nyingine, matunda pamoja na mafuta kwa kiasi kinachofaa.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa virutubisho kama vitamini A, vitamini C na madini ya zinki, ambavyo vina mchango muhimu katika kuimarisha afya na kinga ya mwili. Virutubisho hivyo vinaweza kupatikana kupitia ulaji wa vyakula mbalimbali, ikiwemo matunda na mboga.

Kwa upande wa wazazi na walezi, Irene amewataka kuhakikisha watoto wanapata mlo kamili na wenye mchanganyiko wa vyakula, huku wakizingatia pia usafi na usalama wa chakula kinachotayarishwa na kutolewa kwa watoto.

Ameongeza kuwa maziwa ya mama yana umuhimu mkubwa kwa mtoto, hasa katika hatua za mwanzo za maisha, kutokana na kuwa chanzo muhimu cha virutubisho vinavyohitajika kwa ukuaji na kinga ya mtoto.

Katika hatua nyingine, amesema ulaji wa lishe bora unahitaji pia matumizi yenye kiasi ya mafuta, chumvi na sukari, huku wazazi wakitakiwa kudhibiti matumizi ya vyakula vyenye chumvi na sukari nyingi.

Aidha, watoto wanapaswa kupewa maji ya kutosha na kuhamasishwa kula matunda pamoja na mboga mbalimbali ili kupata vitamini na madini muhimu kwa afya ya mwili.

Irene amesisitiza pia umuhimu wa wazazi na walezi kufuatilia ukuaji na maendeleo ya watoto, kuhakikisha wanapata chakula chenye virutubisho mbalimbali na kuzingatia usafi katika maandalizi, uhifadhi na utoaji wa chakula.TAZAMA KIPINDI HAPA

Amesema jamii ikiwa na uelewa sahihi kuhusu lishe na kuwajibika katika kuhakikisha watoto wanapata chakula bora, itaweza kuchangia katika kupunguza changamoto za utapiamlo na kuwezesha watoto kukua wakiwa na afya bora.

Bibi Maendeleo Irene Samora ametoa wito kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuendelea kuipa kipaumbele lishe ya watoto, kwa kuwa mtoto mwenye lishe bora ana nafasi kubwa ya kukua, kujifunza na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kila siku.