Wafanyabiashara Waikimbia Stendi ya Sh2.8 Bilioni Bariadi

BARIADI: Stendi ya malori iliyojengwa kwa zaidi ya Sh2.8 bilioni katika Mji wa Bariadi, Simiyu, imegeuka kuwa mradi usiotumika ipasavyo, huku wafanyabiashara, madereva na mawakala wa mizigo wakieleza kuwa umbali na ukosefu wa miundombinu muhimu ni miongoni mwa sababu zinazowafanya kuikwepa.

Stendi hiyo iliyobuniwa mwaka 2019 na Halmashauri ya Mji wa Bariadi ililenga kuhudumia malori makubwa ya mizigo yanayoingia na kutoka mjini, kupunguza msongamano wa magari na kuondoa utaratibu wa kupakia na kushusha mizigo katikati ya mji.

Ujenzi wake ulikamilika mwaka 2020 kwa gharama ya zaidi ya Sh2.8 bilioni, lakini takribani miaka sita baadaye, matumizi yake yameendelea kuwa madogo.

Uchunguzi umebaini kuwa ni malori kati ya matano na 10 pekee kwa mwezi yanayotumia stendi hiyo, huku takribani malori 150 kwa mwezi yakitajwa kuendelea kushusha na kupakia mizigo katika maeneo yasiyo rasmi katikati ya mji.

Madereva wanaokwepa stendi hiyo hutozwa faini ya Sh100,000 na Halmashauri, lakini hatua hiyo haijaonekana kuzuia ongezeko la malori yanayoendelea kutumia maeneo yasiyo rasmi.

CAG: Utafiti Haukuwa wa Kutosha

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2025/26 imeibua hoja kuhusu utekelezaji wa mradi huo, ikieleza kuwa utafiti wa kutosha haukufanyika kabla ya kuanzishwa kwa mradi.

Mkaguzi wa Nje wa Hesabu za Serikali Mkoa wa Simiyu, Fortunatus Donge, amesema Halmashauri ilipaswa kufanya utafiti wa kina kubaini kama mradi huo ungekuwa na manufaa kwa Serikali na wananchi.

“Katika ukaguzi tulichokibaini ni kuwa mradi haukufanyiwa utafiti wa kutosha, mradi umetumia fedha nyingi za umma, lakini hautumiki, malori hayataki kupaki,” amesema Donge.

Ameeleza kuwa kutotumika kwa stendi hiyo ni changamoto katika matumizi ya fedha za umma, huku akishauri Halmashauri kufanya tathmini na kuangalia uwezekano wa kubadilisha matumizi ya eneo hilo.

TAKUKURU Yabaini Wadau Hawakushirikishwa

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) nayo imebaini changamoto katika utekelezaji wa mradi huo.

Katika ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha 2023 hadi 2026, TAKUKURU Mkoa wa Simiyu ilibaini kuwa baadhi ya miradi ilitekelezwa bila ushirikishwaji wa kutosha wa wadau.

Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Simiyu, Aron Misanga, amesema stendi ya malori ni miongoni mwa miradi ambayo wadau hawakushirikishwa kikamilifu.

“Moja ya miradi ambao tulibaini wadau hawakushirikishwa ni stendi hiyo ya malori, tangu umekamilika ni muda mrefu, lakini haitumiki. Wenye magari wamegoma kutumia stendi hiyo,” amesema Misanga.

Umbali Wawalazimisha Wafanyabiashara Kuikwepa

Kwa wafanyabiashara wa Bariadi, umbali wa stendi hiyo ni moja ya sababu kubwa inayowafanya waendelee kushusha mizigo katikati ya mji.

Stendi hiyo ipo takribani kilomita saba kutoka katikati ya Bariadi, jambo linalowalazimisha wafanyabiashara kutumia gharama za ziada kusafirisha mizigo kutoka stendi hadi madukani.

Neema Shija, mfanyabiashara wa nafaka, amesema gharama hizo ni mzigo kwa wafanyabiashara wenye mitaji midogo.

“Ukiishushia humo ndani, unatakiwa kutafuta gari ndogo au bajaji kuleta mzigo hadi mjini na gharama zake ni kubwa,” amesema.

Jumanne Singibala, mfanyabiashara wa mbao, amesema umbali huo unawalazimisha kufanya safari nyingi za kusafirisha mizigo.

Amesema gharama ya gari ndogo kusafirisha mzigo kutoka stendi hadi mjini ni kati ya Sh40,000 na Sh50,000 kwa safari moja.

Mfanyabiashara mwingine, Manase Shingile, amesema amewahi kutumia stendi hiyo lakini gharama za kusafirisha mzigo kutoka eneo hilo hadi mjini zilikuwa kubwa.

Usalama wa Mizigo Nao Watajwa

Mbali na umbali, wafanyabiashara wameeleza ukosefu wa sehemu maalumu za kuhifadhi mizigo kuwa changamoto nyingine.

Henry Shabani amesema hali huwa mbaya zaidi wakati wa mvua kwa sababu hakuna ghala au eneo salama la kuhifadhi mizigo.

“Wakati stendi inaanza kufanya kazi, tulianza kushushia huko, lakini tulipata shida sana mvua zilipoanza kunyesha. Mizigo ya wafanyabiashara ilinyeshewa mvua na tukapata hasara kubwa,” amesema.

Mawakala wa mizigo nao wameeleza kuwa changamoto hizo zimefanya wafanyabiashara kutafuta maeneo mengine ya kushushia mizigo.

Jumanne Kiyumbi, mmoja wa mawakala, amesema hakuna mfanyabiashara aliye tayari kuongeza gharama kwa ajili ya usafirishaji wa mizigo kutoka stendi hiyo hadi mjini.

Stendi Bubu Yaibuka

Kwa mujibu wa Julius Mlangila, wakala wa mizigo, kutotumika kwa stendi rasmi kumesababisha kuibuka kwa maeneo yasiyo rasmi ya kushushia mizigo.

Amesema baadhi ya malori yanashusha mizigo katika maeneo hayo licha ya kutozwa Sh100,000 na Halmashauri.

“Kila gari linalofika kushusha mzigo kwenye eneo letu jipya, Halmashauri wanachukua ushuru (faini), kila gari linalipia Sh100,000 na wafanyabiashara wapo tayari kulipa hicho kiasi na siyo kushushia kwenye ile stendi,” amesema Mlangila.

Madereva Walalamikia Huduma

Madereva nao wamesema eneo hilo halina huduma muhimu zinazoweza kuwafanya wabaki hapo wakati wa kusubiri kupakia au kushusha mizigo.

Jafari Mohamed, dereva wa lori, amesema eneo hilo halina nyumba za kulala wageni wala migahawa ya kutosha.

“Hili eneo ni kama porini, hakuna nyumba ya kulala wageni au mgahawa wa chakula. Dereva unafika hapa umechoka, inakulazimu upaki gari humu ndani, kisha uchukue bodaboda kwa gharama ya Sh5,000 ndiyo upelekwe mjini,” amesema.

Halmashauri Yakiri Changamoto

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Idd Ndabhona, amekiri kuwa stendi hiyo haitumiki kwa kiwango kilichokusudiwa, lakini amesema uongozi unaendelea kufanyia kazi ushauri wa CAG na TAKUKURU.

Ndabhona amesema eneo hilo lilichaguliwa kutokana na matarajio ya ukuaji wa Mji wa Bariadi na nia ya kupunguza msongamano katikati ya mji.

“Kweli ni mbali, lakini huo ulikuwa ushauri wa kitaalamu ijengwe kule kutokana na mji kukua kila wakati. Tuliwaza mbele zaidi ili kupunguza msongamano mjini,” amesema.

Amesema Halmashauri imebaini changamoto zinazohusu usalama wa mizigo na matumizi ya stendi na inaendelea kufanya tathmini ya mradi huo.

“Watalaamu watakaa na kupitia changamoto zote, ufanisi wa mradi kama ambavyo tumeshauriwa, kisha tutakuja na jibu kama tuibadilishie matumizi au tufanye jambo gani,” amesema.

Ushauri wa Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha, amesema uchunguzi alioufanya awali ulibaini kuwa utafiti wa kutosha haukufanyika kabla ya mradi kutekelezwa.

Macha amesema sababu zilizotolewa na wafanyabiashara kuhusu umbali na usalama wa mizigo zina msingi.

Ameshauri Halmashauri kufanya tathmini upya ya mradi huo na kuangalia matumizi mengine yanayoweza kulifanya eneo hilo liwe na tija.

“Mimi nadhani ushauri wa CAG ufanyiwe kazi, mradi umekuwa hasara kwa Halmashauri. Fanyeni tathmini upya kuangalia ni mradi gani mwingine unaweza kutekelezwa pale na ukaleta ufanisi kwenye Halmashauri,” amesema Macha.

Kwa sasa, stendi hiyo bado inakabiliwa na changamoto ya kupata watumiaji, huku malori yakiendelea kushusha na kupakia mizigo katikati ya Bariadi licha ya kuwepo kwa miundombinu iliyogharimu mabilioni ya fedha za umma.

Stori na Derick Nilton | GPL -Bariadi

Tanzania Yaingia Top 8 Miss Grand International Kupitia Jihandi Mack

Global Publishers
September 30, 2026
12 views
0 Comments

Mrembo Jihandi Mack amewashukuru Watanzania kwa sapoti kubwa baada ya kuvuka kwa kishindo hatua ya pili ya kipengele cha Country’s Power of the Year katika mashindano ya Miss Grand International, na kuiweka Tanzania ndani ya Top 8.

Kupitia ujumbe wake, Jihandi amewashukuru Watanzania wote waliompa sapoti na kushiriki katika kumpigia kura hadi kufikia hatua hiyo.

Sasa ushindani unaingia katika hatua ya tatu, ambapo kura zinahitajika ili kumpata Top 4.

Upigaji kura unafanyika kupitia tovuti rasmi ya Miss Grand International, na zoezi hilo linatarajiwa kudumu kwa saa 24, kuanzia saa 2 usiku leo hadi kesho.

Watanzania wanaendelea kuhamasishwa kumpa sapoti Jihandi Mack ili Tanzania iweze kusonga mbele zaidi katika mashindano hayo.

MAMBA MIAMBA WAPATA ELIMU YA JIOLOJIA NA TAHADHARI ZA EL NIÑO

Na Ashrack Miraji Matukio Daima 

Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imetoa elimu kuhusu tahadhari za majanga ya asili, masuala ya jiolojia na El Niño kwa wakazi wa Kijiji cha Mamba Miamba, Jimbo la Same Mashariki, Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro.

Elimu hiyo ilitolewa katika kikao kilichofanyika Septemba 29, 2026, kilichowakutanisha viongozi wa Serikali ya Kijiji, Mtendaji wa Kijiji pamoja na wananchi, ambapo walijadili hatua mbalimbali za kuchukua ili kupunguza athari za majanga ya asili katika eneo hilo.

Kikao hicho kilifanyika kufuatia ombi la Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela, lililotolewa Septemba 28, 2026, mara baada ya semina iliyowakutanisha maafisa tarafa, madiwani na watendaji wa kata. Katika semina hiyo, pamoja na kutembelea baadhi ya maeneo hatarishi upande wa tambarare, mbunge huyo aliwaomba wataalamu kufika katika maeneo ya milimani kwa ajili ya kutoa elimu na ushauri wa kitaalamu.

Katika kikao hicho, wananchi walikubaliana kusitisha mara moja shughuli za kilimo katika eneo lililowahi kuathiriwa na maporomoko ya udongo mwaka 2009. Badala yake, walikubaliana kupanda miti katika eneo hilo ili kusaidia kurejesha uimara wa udongo na kupunguza mmomonyoko.

Aidha, wananchi waliiomba Serikali kuchukua hatua za kudhibiti athari za radi katika eneo hilo, ikiwemo kuweka mifumo au vifaa maalumu vya kinga dhidi ya radi, kutokana na eneo hilo kuwa na historia ya kukumbwa na matukio ya radi mara kwa mara.

Wataalamu wa GST pia waliwasisitiza wananchi kuendelea kufuatilia taarifa na tahadhari zinazotolewa na mamlaka husika kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na majanga ya asili, pamoja na kuchukua hatua mapema wanapoona dalili zinazoweza kuhatarisha usalama wa watu na mali.

GST imeendelea kutoa elimu kwa jamii katika maeneo mbalimbali nchini kuhusu masuala ya jiolojia, majanga ya asili na namna ya kuchukua tahadhari, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uelewa wa wananchi na kupunguza athari za majanga yanayoweza kujitokeza.

 

Mgomo wa Madereva: Katambi Aweka Wazi Hatua za Serikali, Leseni Zarejeshwa, VTS Yachunguzwa – Video

DAR ES SALAAM: Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, ametangaza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kufuatia maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kumaliza kero za madereva na mgomo uliodumu kwa siku mbili.

Akizungumza leo, Septemba 30, 2026, katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli, Mbezi jijini Dar es Salaam, Katambi amesema maagizo ya Rais yamepitishwa kwa Waziri Mkuu na kuanza kutekelezwa kwa haraka.

Miongoni mwa hatua hizo ni kurejeshwa kwa leseni za madereva, kuondolewa kwa vizuizi visivyo na sababu barabarani pamoja na kushughulikia miundombinu ya barabara, ikiwemo matengenezo ya maeneo yenye mashimo yanayoweza kusababisha ajali.

Kuhusu madereva ambao leseni zao zilikamatwa au kufungiwa kutokana na makosa madogomadogo, Katambi amesema wataweza kurejeshewa leseni zao kwa mujibu wa sheria kupitia Mamlaka ya Rufaa iliyo chini ya Waziri wa Mambo ya Ndani.

Amesema hatua hiyo haitawahusu madereva waliothibitika kuhusika na ajali mbaya zilizosababisha vifo na ambao kesi zao bado zinaendelea mahakamani.

Katambi pia amewataka madereva na wananchi kutafuta suluhisho la changamoto kupitia mazungumzo badala ya migogoro, akisisitiza umuhimu wa Serikali kusikiliza na kuwashirikisha wananchi katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.

Amesema amepewa mamlaka na Waziri Mkuu kushughulikia malalamiko ya madereva na kwamba changamoto zao sasa zitafanyiwa kazi.

Katika hatua nyingine, Katambi ametangaza kuwa wizara nne za Serikali zitakutana kuchambua na kutafuta suluhisho la changamoto zinazotokana na Mfumo wa Kufuatilia Magari (VTS).

Amesema mkutano huo utazihusisha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Uchukuzi pamoja na Wizara ya Kazi, Ajira na Mahusiano.

Hatua hiyo imekuja baada ya madereva kulalamikia tofauti za takwimu kati ya mfumo wa VTS na kamera za usalama barabarani.

Kwa mujibu wa Katambi, kuna maeneo ambayo kamera za usalama barabarani zinaweza kuonesha gari lilikuwa likisafiri kwa kasi ya kilomita 100 kwa saa, wakati mfumo wa VTS unaonesha kasi ya kilomita 130 kwa saa.

Amesema tofauti hizo zimekuwa zikisababisha madereva kupata adhabu na kuingia katika changamoto ambazo zinahitaji kufanyiwa tathmini.

Katambi amesema Serikali itakaa pamoja kuchambua changamoto hizo na kuweka utaratibu utakaokuwa na uwazi na haki zaidi kwa madereva.

Aidha, amesema mfumo wa VTS ni wa muda katika kipindi cha mpito, huku Serikali ikielekea kwenye mfumo wa kisasa wa kidijitali wa kudhibiti mwendo wa magari.

Kwa maelezo yake, mfumo huo mpya utakuwa na mfumo wa kamera huru zitakazorekodi makosa ya barabarani moja kwa moja bila kuhitaji udhibiti wa askari.

Katambi amefananisha mfumo huo na VAR inayotumika katika soka, akisema lengo ni kuhakikisha ushahidi wa kamera unatumika katika kuthibitisha makosa na kuongeza usawa katika utekelezaji wa sheria za usalama barabarani.

Mgomo wa Madereva: Katambi Aweka Wazi Hatua za Serikali, Leseni Zarejeshwa, VTS Yachungwa – Video

DAR ES SALAAM: Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, ametangaza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kufuatia maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kumaliza kero za madereva na mgomo uliodumu kwa siku mbili.

Akizungumza leo, Septemba 30, 2026, katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli, Mbezi jijini Dar es Salaam, Katambi amesema maagizo ya Rais yamepitishwa kwa Waziri Mkuu na kuanza kutekelezwa kwa haraka.

Miongoni mwa hatua hizo ni kurejeshwa kwa leseni za madereva, kuondolewa kwa vizuizi visivyo na sababu barabarani pamoja na kushughulikia miundombinu ya barabara, ikiwemo matengenezo ya maeneo yenye mashimo yanayoweza kusababisha ajali.

Kuhusu madereva ambao leseni zao zilikamatwa au kufungiwa kutokana na makosa madogomadogo, Katambi amesema wataweza kurejeshewa leseni zao kwa mujibu wa sheria kupitia Mamlaka ya Rufaa iliyo chini ya Waziri wa Mambo ya Ndani.

Amesema hatua hiyo haitawahusu madereva waliothibitika kuhusika na ajali mbaya zilizosababisha vifo na ambao kesi zao bado zinaendelea mahakamani.

Katambi pia amewataka madereva na wananchi kutafuta suluhisho la changamoto kupitia mazungumzo badala ya migogoro, akisisitiza umuhimu wa Serikali kusikiliza na kuwashirikisha wananchi katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.

Amesema amepewa mamlaka na Waziri Mkuu kushughulikia malalamiko ya madereva na kwamba changamoto zao sasa zitafanyiwa kazi.

Katika hatua nyingine, Katambi ametangaza kuwa wizara nne za Serikali zitakutana kuchambua na kutafuta suluhisho la changamoto zinazotokana na Mfumo wa Kufuatilia Magari (VTS).

Amesema mkutano huo utazihusisha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Uchukuzi pamoja na Wizara ya Kazi, Ajira na Mahusiano.

Hatua hiyo imekuja baada ya madereva kulalamikia tofauti za takwimu kati ya mfumo wa VTS na kamera za usalama barabarani.

Kwa mujibu wa Katambi, kuna maeneo ambayo kamera za usalama barabarani zinaweza kuonesha gari lilikuwa likisafiri kwa kasi ya kilomita 100 kwa saa, wakati mfumo wa VTS unaonesha kasi ya kilomita 130 kwa saa.

Amesema tofauti hizo zimekuwa zikisababisha madereva kupata adhabu na kuingia katika changamoto ambazo zinahitaji kufanyiwa tathmini.

Katambi amesema Serikali itakaa pamoja kuchambua changamoto hizo na kuweka utaratibu utakaokuwa na uwazi na haki zaidi kwa madereva.

Aidha, amesema mfumo wa VTS ni wa muda katika kipindi cha mpito, huku Serikali ikielekea kwenye mfumo wa kisasa wa kidijitali wa kudhibiti mwendo wa magari.

Kwa maelezo yake, mfumo huo mpya utakuwa na mfumo wa kamera huru zitakazorekodi makosa ya barabarani moja kwa moja bila kuhitaji udhibiti wa askari.

Katambi amefananisha mfumo huo na VAR inayotumika katika soka, akisema lengo ni kuhakikisha ushahidi wa kamera unatumika katika kuthibitisha makosa na kuongeza usawa katika utekelezaji wa sheria za usalama barabarani.

SAME WATAKIWA KUTUMIA MVUA ZA EL NINO KUPANDA MITI

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Yusto Mapande, amewataka wananchi na watumishi wa umma kutumia mvua zinazotarajiwa kunyesha kutokana na hali ya El Niño kupanda miti kwa wingi katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Mapande ametoa wito huo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati akizungumza katika kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Same.

Amesema pamoja na tahadhari zinazotolewa kuhusu athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo, wananchi wanapaswa pia kuzitazama kama fursa ya kupanda miti, kwani unyevu wa mvua utasaidia miche kustawi vizuri.

Amesema upandaji wa miti kwa wingi utasaidia kulinda mazingira, ikiwamo kupunguza mmomonyoko wa udongo, huku akiwataka wananchi kuanza zoezi hilo mapema kabla na wakati wa mvua.

“Pamoja na tahadhari tunazotoa kuhusu mvua hizi, tutumie pia fursa hii kupanda miti kwa wingi. Miti ikipata mvua kwa wakati itastawi vizuri na baadaye itasaidia katika kulinda mazingira na kupunguza mmomonyoko wa udongo,” amesema.

Aidha, amewataka madiwani kwenda kutoa elimu katika kata zao na mashuleni kuhusu umuhimu wa upandaji miti, akisisitiza kuwa wananchi wapande miti ya kawaida pamoja na miti ya matunda.

Amesema hatua hiyo itaunga mkono kampeni ya Mkuu wa Wilaya ya Same, Kaslida Mgeni, ya kuifanya Same kuwa wilaya ya kijani, hivyo amewataka wananchi kuanza utekelezaji wake mapema.

Katika hatua nyingine, Mapande amemtaka Mkuu wa Idara ya Kilimo kuanzisha hamasa ya kilimo cha mazao ya kimkakati, hususan zao la parachichi, ili wananchi wanufaike na fursa hiyo.

Amesema baada ya kipindi cha El Niño, idara hiyo inapaswa kuandaa taarifa itakayoonyesha idadi ya miche ya parachichi iliyopandwa pamoja na kata ambazo zimefanikiwa katika kilimo hicho.

“Baada ya miaka mitatu tunahitaji kujua tumefikia wapi. Tuwe na kumbukumbu ya idadi ya miparachichi iliyopandwa, kata gani imefanya vizuri na ni matokeo gani tunayotarajia baada ya mvua hizi,” amesema.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Same Mamndolwa Gembe amesema wananchi hawapaswi kuzitazama mvua hizo kwa upande wa madhara pekee, bali wazitumie pia kama fursa ya kupanda miche ya mazao  

 

Dkt. Mwigulu Akutana na Viongozi wa Madereva, Mgomo Wasitishwa

Global Publishers
September 30, 2026
18 views
0 Comments

DAR ES SALAAM: Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa madereva wa mabasi na malori nchini, hatua iliyofuatia makubaliano ya kusitisha mgomo wa madereva uliodumu kwa siku mbili.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo, Septemba 30, 2026, katika Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Baada ya mazungumzo hayo, viongozi wa madereva wamekubali kusitisha mgomo huo, hivyo kuwezesha huduma za usafiri kuendelea kama kawaida nchini.

Serikali pia imeeleza utayari wake wa kusikiliza na kufanyia kazi changamoto zinazowakabili madereva, kwa lengo la kutafuta suluhisho la masuala yaliyosababisha mgomo huo.

Hatua hiyo inatarajiwa kurejesha huduma za usafiri huku Serikali na wadau wa sekta ya usafirishaji wakiendelea na majadiliano kuhusu changamoto zinazowakabili madereva.

Makubaliano hayo yamekuja baada ya mgomo wa siku mbili ambao uliathiri huduma za usafiri katika maeneo mbalimbali nchini.

DKT. MWIGULU AKUTANA NA VIONGOZI WA MADEREVA, MGOMO WASITISHWA

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Septemba 30, 2026, amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa madereva wa mabasi na malori nchini, katika Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wamekubali kusitisha mgomo wa madereva uliodumu kwa siku mbili, hatua inayowezesha huduma za usafiri kuendelea kama kawaida.

Aidha, Serikali imeeleza utayari wake wa kusikiliza na kufanyia kazi changamoto zinazowakabili madereva, kwa lengo la kupata suluhisho la masuala yaliyosababisha mgomo huo.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha huduma za usafiri zinaendelea kutolewa huku majadiliano kuhusu changamoto za madereva yakiendelea kati ya Serikali na wadau husika.

 

VIVUTIO VYA UTALII KUTANGAZWA NCHINI INDIA

Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini India, imewapokea jumla ya mawakala wa utalii 13 kutoka India kwa ajili ya ziara maalum ya utangazaji utalii (Familiarization Trip) itakayofanyika nchini kuanzia tarehe 28 Septemba 2026 hadi 04 Oktoba, 2026.

Lengo kuu la ziara hii ni kuwapa fursa mawakala hao kujionea vivutio vya utalii vilivyopo nchini, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati yao na wadau wa utalii wa Tanzania.

Akizungumza kuwakaribisha nchini Mawakala hao, Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Mbega ambaye ameongozana na ujumbe huo, amesema Ubalozi utaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa utalii kutoka India katika kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini ili kukuza sekta hiyo na kuchangia Uchumi wa nchi na kwamba ziara ya mawakala hao ni moja ya jitihada za Ubalozi huo katika kuhakikisha vivutio vya utalii vinatangazwa nchini India kupitia mawakala hao.

Kwa upande wake, kiongozi wa ujumbe wa Mawakala hao ambaye pia ni Rais na Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha shughuli za Utalii cha India, Bw. Himanshu Patil amesema kuwa lengo la ziara yao hapa nchini ni kujionea vivutio vya utalii na kuzungumza na wadau muhimu katika sekta hiyo ili hatimaye kuwawezesha kushirikiana na Tanzania katika kuwafikia watalii kutoka India kuja nchini.

Kabla ya kuanza kwa ziara hiyo, mawakala hao walipata fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo ya kibiashara (B2B) na kundi la waendesha shughuli za utalii (Tour Operators) kutoka Tanzania. Mkutano huo ulilenga kujenga mahusiano ya kibiashara ya moja kwa moja na kufungua fursa mpya za kukuza idadi ya watalii kutoka soko la India.

Ziara hii ni sehemu ya mkakati endelevu wa Bodi ya Utalii Tanzania wa kukuza soko la India ambalo kwa sasa ni miongoni mwa masoko sita yanayoongoza kwa kuleta watalii nchini. 

Wakiwa nchini Mawakala hao watatembelea maeneo mbalimbali ya utalii yakiwemo Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Zanzibar.

 

Waajiri watakiwa kutatua changamoto za watumishi – HabariLeo

SIMANJIRO. Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Qwaray, amewataka waajiri na Mamlaka za Ajira na Nidhamu kuhakikisha changamoto za kiutumishi zinashughulikiwa kwa wakati ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Qwaray ametoa agizo hilo wakati wa kikao kazi cha kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili Watumishi wa Umma katika Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro.

Amesema waajiri wanapaswa kuhakikisha stahiki za watumishi, ikiwemo kupandishwa vyeo, uhamisho, malimbikizo ya mishahara na mafao, zinashughulikiwa kwa wakati kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.

Aidha, amesisitiza kuwa madai ya watumishi yanapaswa kuhakikiwa na kuwasilishwa yakiwa yameambatanishwa na nyaraka muhimu ili kurahisisha utatuzi wa changamoto hizo.

Qwaray amezitaka Mamlaka za Ajira na Nidhamu kusimamia haki na wajibu wa watumishi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma, akisisitiza umuhimu wa kuacha utendaji wa mazoea.

Amesema mambo yaliyo ndani ya uwezo wa waajiri na Mamlaka za Ajira na Nidhamu yanapaswa kushughulikiwa katika ngazi hizo badala ya kuendelea kuwasilishwa Ofisi ya Rais.

Kuhusu maadili ya utumishi wa umma, Qwaray amewataka watumishi kuyafahamu na kuyatekeleza kwa kuzingatia Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma.

“Watumishi wanaokiuka maadili au kutotekeleza majukumu yao ipasavyo wanapaswa kuchukuliwa hatua stahiki za kinidhamu kwa wakati,” amesema.

Aidha, amewataka waajiri na Mamlaka za Ajira na Nidhamu kushirikiana na Tume ya Utumishi wa Umma katika ukaguzi wa utekelezaji wa sheria, kanuni na taratibu za kiutumishi na kuhakikisha mapungufu yatakayobainika yanarekebishwa kwa wakati.