
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imewekeza Sh1.8 bilioni katika ujenzi na uboreshaji wa jengo pamoja na miundombinu ya chumba cha kisasa cha upasuaji wa uzazi (Modular Theatre) kwa ajili ya huduma za mama na mtoto.
Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dkt. Delilah Kimambo, amesema uwekezaji huo umehusisha ujenzi na uboreshaji wa miundombinu pamoja na uwekaji wa vifaa tiba vya kisasa katika vyumba vya upasuaji kwa ajili ya wajawazito na watoto.
Akizungumza na Global TV, Dkt. Kimambo leo Oktoba 2, 2026 amesema uwekezaji huo unalenga kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto, kupunguza muda wa kusubiri huduma pamoja na kusaidia kupunguza vifo vya akina mama na watoto wachanga.
Amesema vyumba hivyo vimewekewa vifaa tiba vinavyokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa na ubobezi kwa wajawazito na watoto.

Mtoto Atatibiwa Akiwa Tumboni
Dkt. Kimambo amesema moja ya huduma mpya zitakazopatikana ni Fetal Maternal Medicine, inayowezesha mtoto kutambuliwa na kufuatiliwa akiwa bado tumboni mwa mama.
Kwa mujibu wa Dkt. Kimambo, huduma hiyo itawezesha wataalamu kubaini mapema matatizo mbalimbali yanayoweza kuhatarisha maisha ya mama na mtoto na kuchukua hatua kabla ya kujifungua.
“Chumba hiki kinaleta huduma mpya na ya kipekee nchini ambapo mtoto sasa anaweza kutambuliwa kama mgonjwa, kufuatiliwa, na kupata matibabu au upasuaji akiwa bado tumboni mwa mama yake kabla hajazaliwa,” amesema.
Ametaja baadhi ya hali zinazoweza kufuatiliwa kwa karibu kuwa ni pamoja na ujauzito unaohusisha kisukari, selimundu, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha changamoto za kiafya zinagundulika mapema na hatua stahiki zinachukuliwa ili kuokoa maisha ya mama na mtoto.
Mfumo Mpya wa Oksijeni
Mbali na huduma hizo, Dkt. Kimambo amesema MNH imeweka pia mfumo wa gesi ya oksijeni ambao utasaidia kupunguza utegemezi wa mitungi ya oksijeni katika baadhi ya maeneo ya hospitali.
Amesema mfumo huo utawezesha oksijeni kufikishwa moja kwa moja kwenye wodi na vyumba vya upasuaji, tofauti na utaratibu wa awali uliotegemea mitungi ya gesi.
Mradi huo ulizinduliwa rasmi Septemba 30, 2026, sambamba na uzinduzi wa Bodi ya Wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, ambaye alishiriki katika uzinduzi wa vyumba hivyo vya kisasa.
STORI NA ELVAN SITAMBULI | GPL





















