AFISA WA POLISI NA RAIA WAWILI WAFARIKI DUNIA KATIKA VURUGU ZA LINDA MWANANCHI, KENYA

 

Afisa mmoja na raia wawili wamefariki dunia, huku wengine wkijeruhiwa kutokana na ghasia za zilizokumba mkutano wa kisiasa wa Linda Mwananchi katika eneo la Homa Bay, nchini Kenya.

Afisa huyo ambaye alipigwa jiwe kichwani alikimbizwa katika hospitali moja katika Kaunti ya Kisumu, ambako alifariki dunia alipokuwa akipokea matibabu.

Polisi imetoa taarifa na kusema kuwa washukiwa 37 wamekamatwa baada ya kupatikana na silaha mbalimbali za kienyeji, zikiwemo mapanga, kamba, vyuma, visu, marungu, fimbo za polisi na tochi.

Kukamatwa kwao ni sehemu ya operesheni inayoendelea dhidi ya wahalifu na makundi ya vijana wanaosababisha vurugu nchini humo, wakiwemo wale wanaoshukiwa kuhusika na ghasia zilizoshuhudiwa Homa Bay siku ya Jumapili.

Katika taarifa iliyotiwa saini na Msemaji wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS), Muchiri Nyagah, alisema washukiwa hao watachukuliwa hatua za kisheria na kufikishwa mahakamani ili kujibu mashtaka yanayowakabili.

Aliongeza kuwa polisi wanamsaka Oliver Jaoko, anayejulikana kwa jina la “Olivetti,” ambaye ameelezwa kujisalimisha katika kituo cha polisi kilicho karibu ili kusaidia katika uchunguzi unaoendelea. Wakati huo huo, operesheni ya kumkamata yeye pamoja na watu wengine wote wanaoshukiwa kuhusika na vurugu hizo inaendelea.

Vurugu hizo zimezua taharuki kubwa kisiasa huku waandaaji wa vuguvugu la Linda Mwananchi wakiwatuhumu baadhi ya watu wasiotajwa majina katika siasa na usalama kwa kuhusika na kile wanachodai kuwa ni shambulio lililoratibiwa. Hata hivyo, madai hayo hayajathibitishwa kwa njia huru.

Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, vuguvugu hilo lilisema msafara wake ulikumbana na vizuizi barabarani kuanzia mpaka wa Kisumu na Homa Bay, kupitia barabara za Homa Bay–Migori na Migori–Kisii.

Vuguvugu hilo lilidai kuwa makundi yaliyokuwa yakishambulia msafara huo yalionekana kushirikiana na maafisa wa polisi.

Hichilema ashinda tena urais Zambia

Dar es Salaam. Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, ameshinda uchaguzi wa urais na kupata muhula wa pili wa miaka mitano, katika ushindi unaompa nafasi ya kuendeleza mpango wake wa kurekebisha uchumi uliokuwa ukikabiliwa na mzigo mkubwa wa madeni.

Tume ya Uchaguzi ya Zambia imemtangaza Hichilema kuwa mshindi baada ya kupata asilimia 61.4 ya kura, sawa na karibu kura milioni tatu.

Mpinzani wake mkuu, Brian Mundubile wa Tonse Alliance, amepata takriban asilimia 38, sawa na kura milioni 1.86.

Hichilema amewashukuru wananchi kwa kumpa tena dhamana ya kuongoza nchi hiyo na kuahidi uongozi unaojumuisha hata waliompigia kura mpinzani wake.

Ushindi huo unakuja baada ya uchaguzi iliofanyika Agosti 13,2026 ukiwa na mvutano, huku shughuli ya kuhesabu kura ikisimamishwa kwa muda kutokana na taarifa za madai ya kushambuliwa kwa baadhi ya watendaji wa uchaguzi na kuibwa kwa karatasi za kura katika baadhi ya maeneo.

 Upinzani pia umekosoa ushindi huo ukihoji mwenendo wa mchakato, ingawa mamlaka za Zambia zimekana madai ya kuingilia uchaguzi.

Safari ya Hichilema, kutoka mpinzani hadi kuingilia Ikulu

Hichilema, anayejulikana kwa jina la HH, aliingia madarakani mwaka 2021 baada ya kushindwa mara kadhaa katika mbio za urais.

Alikuwa kiongozi wa muda mrefu wa Chama cha United Party for National Development (UPND) kabla ya kumshinda Rais wa wakati huo, Edgar Lungu, katika uchaguzi wa 2021.

Kabla ya siasa, Hichilema alijijengea jina katika biashara na ujasiriamali, akiongoza kampuni kubwa za ushauri wa biashara nchini Zambia na baadaye kuwa mwekezaji katika sekta mbalimbali, ikiwamo kilimo na mifugo.

Alipoingia madarakani mwaka 2021, alikuta Zambia ikiwa imetoka katika mgogoro mkubwa wa madeni, ikiwamo kutolipa deni lake la taifa mwaka 2020.

Katika muhula wake wa kwanza, serikali yake iliongoza mchakato wa marekebisho ya deni la zaidi ya dola za Marekani bilioni 12 (Sh31.68 trilioni), ikaongeza ushirikiano na taasisi za fedha za kimataifa na kuvutia uwekezaji katika sekta ya madini, hasa shaba.

 Serikali pia ilipanua huduma za kijamii, ikiwamo elimu ya sekondari bila ada. Hata hivyo, mafanikio hayo ya kiuchumi hayajaondoa changamoto kwa wananchi wa kawaida.

 Gharama za chakula na nishati, ajira na umaskini bado ni miongoni mwa masuala yaliyotawala mjadala wa uchaguzi.

Kwa hiyo, ushindi wa Hichilema unaweka mbele yake mtihani wa kuhakikisha mafanikio ya uchumi wa taifa yanaonekana pia katika maisha ya wananchi.

Muhula wake wa pili pia utaangaliwa katika eneo la demokrasia kwani Serikali yake imekabiliwa na tuhuma kutoka kwa wapinzani na mashirika ya kiraia kuhusu kubanwa kwa upinzani na uhuru wa kisiasa, madai ambayo imekuwa ikiyakanusha.

Hivyo, ushindi wa Hichilema si mwisho wa safari yake ya kisiasa bali mwanzo wa miaka mingine mitano ambayo itaamua kama ahadi za mageuzi ya uchumi zitaendelea kubaki kwenye takwimu za Serikali pekee, au  kuwa mabadiliko yanayoonekana katika maisha ya Mzambia wa kawaida.

Kwa nini shahada yako si tiketi tena ya ajira

Dar es Salaam. Wakati maelfu ya vijana wa Tanzania wakijiandaa kuhitimu kutoka vyuo vikuu na taasisi za elimujuu mwaka huu, wataalamu wa elimu na wadau wa maendeleo ya vijana,  wameonya kuwa kuwa na shahada pekee hakutoshi tena kupata ajira katika soko la ajira linalozidi kuwa na ushindani mkubwa na kuendeshwa na maendeleo ya teknolojia.

Onyo hilo linakuja wakati wahitimu wengi wanaingia kwenye soko la ajira wakiwa na matarajio yasiyoendana na uhalisia wa fursa zilizopo, huku wengine wanaojaribu kujipatia kipato kupitia biashara za mtandaoni na kazi za kujitegemea, wakikumbana na changamoto ya kujenga utambulisho imara wa kitaaluma.

Akizungumza katika mkutano wa mradi uitwao Career Development Project Summit 2026, ulioandaliwa na Save Youths Dreams Foundation hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Meneja wa mradi huo, Winny Kaaya, alisema kuna umuhimu mkubwa wa kuwapa wanafunzi nafasi ya kukutana na waajiri, wajasiriamali na wataalamu kabla ya kuhitimu masomo yao.

Alisema vijana wengi huhitimu vyuo vikuu wakiwa na uelewa mdogo kuhusu matarajio ya waajiri, umuhimu wa kujenga mitandao ya kitaaluma pamoja na fursa zilizopo nje ya ajira rasmi.

“Lengo la mkutano huu ni kuwapa wanafunzi na wahitimu maarifa ya vitendo kuhusu uwezo wa kuajirika, kujenga utambulisho wa kitaaluma na kutambua fursa zilizopo katika ujasiriamali, uchumi wa kidijitali na sekta binafsi,” alisema.

Kaaya aliongeza kuwa aina hiyo ya mafunzo huwasaidia vijana kufanya uamuzi sahihi kuhusu taaluma zao na kujenga mitandao itakayowawezesha kupata fursa hata baada ya kuhitimu.

Katika mkutano huo, umuhimu wa kujenga sifa njema na kuzingatia maadili binafsi pia vilisisitizwa. Kiongozi wa Mahusiano ya Umma na Mawasiliano ya Kimkakati wa taasisi ya Empower, Furahini Godlike, aliwataka vijana kuzingatia uadilifu, uwajibikaji na uaminifu kama nguzo muhimu za mafanikio katika taaluma zao.

Alisema waajiri na washirika wa biashara hawazingatii vyeti vya kitaaluma pekee, bali pia huangalia kiwango cha uaminifu, nidhamu na maadili ya mtu.

“Maadili yako yanaongoza uamuzi wako, na uamuzi wako ndiyo unaoamua jinsi watu watakavyokukumbuka,” alisema.

Majadiliano hayo pia yaligusia mustakabali wa ajira, ambapo maendeleo ya teknolojia yanaendelea kubadilisha ujuzi unaohitajika na waajiri.

Naye Ofisa Mawasiliano wa  taasisi ya African Leadership Initiative for Impact, Yusra Abdulbastwa, alisema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,  inalenga kujenga uchumi wenye ushindani unaotegemea ubunifu, mabadiliko ya kidijitali, viwanda na ujasiriamali.

Alisema moja ya vipaumbele vya dira hiyo ni kuweka mazingira yatakayowawezesha vijana kuanzisha biashara, kupata fursa za uwekezaji na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

“Serikali inataka vijana wasiishie kutafuta ajira pekee, bali pia wawe waajiri,” alisema.

Yusra  pia aliwahimiza wanafunzi kukumbatia matumizi ya akili unde  (AI), akieleza kuwa teknolojia hiyo haitachukua nafasi ya kila mtu, lakini wale watakaoshindwa kujifunza kuitumia wanaweza kupitwa na wenzao watakaoimudu.

Alisema stadi kama huruma, kufanya uamuzi wenye kuzingatia maadili, uongozi, maono na tabia njema zitaendelea kuwa muhimu kwa sababu ni vigumu kwa AI kuzifanikisha kikamilifu.

“Watu wanaojua kutumia AI watachukua nafasi ya wale wasioijua,” alisema.

Kwa upande wake, mhitimu wa kidato cha sita wa mwaka 2026, Buminganyikani Metson, alisema mkutano huo ulimfundisha umuhimu wa kujitokeza katika maeneo ambako fursa hutengenezwa.

Aliwahimiza vijana wenzake kuhudhuria semina, makongamano na matukio yanayowalenga vijana hata kama hayatoi malipo ya moja kwa moja.

“Huenda usilipwe kwa kuhudhuria tukio, lakini watu utakaokutana nao wanaweza kukufungulia milango ya fursa zinazoweza kubadilisha maisha yako,” alisema.

Kwa ujumla, washiriki wa mkutano huo walikubaliana kuwa mafanikio katika soko la ajira la sasa hayategemei tena vyeti vya kitaaluma pekee, bali yanahitaji pia ujuzi wa vitendo, mtandao mpana wa kitaaluma na uwezo wa kuendana na mabadiliko ya kasi ya uchumi na teknolojia.

VIJANA NA MAMA LISHE WANUFAIKA MKOPO IRAMBA, SINGIDA ‎

 

‎Na Elisante John, Matukiodaima Singida,

‎

‎Vijana wa Kijiji cha Makunda, Wilaya ya Iramba, wamepatiwa Sh263 milioni kwa ajili ya kuboresha kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji, ajira na thamani ya zao hilo katika eneo analotoka na kuzaliwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.

‎Fedha hizo ni sehemu ya Sh.363/- milioni zilizotolewa na Serikali kwa vijana na wanawake mkoani Singida, kupitia mpango wa mikopo unaotokana na Sh.200/- bilioni zilizotengwa kwa ajili ya kuwawezesha vijana nchini, kujikwamua kiuchumi.

‎Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya mikopo hiyo, uliofanyika Kijiji cha Makunda, wilaya ya Iramba, Waziri wa Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, amesema Sh.263/- milioni zilizotolewa kwa vijana wa Kijiji hicho, zitatumika kuboresha kiwanda hicho, ikiwemo kupatiwa mashine kubwa na ndogo za kuchakata alizeti, gari la tani saba na mtaji wa kununua zao hilo

 kutoka kwa wakulima.

‎Nanauka amesema gari hilo lina thamani ya zaidi ya Sh.97.6/- milioni na litatumika kusafirisha alizeti pamoja na kusambaza mafuta kwa haraka sokoni. Aidha, sehemu ya fedha hizo, Sh.100/- milioni zitatumika kama mtaji wa kununua alizeti shambani, hatua inayolenga kuhakikisha kiwanda kinapata malighafi ya kutosha kwa uzalishaji.

‎Amesema uwezeshaji huo utaongeza uwezo wa kiwanda kutoka kuchakata tani 2.5 za alizeti hadi tani 11 kwa siku, huku zaidi ya watu 60 wakitarajiwa kupata ajira katika mnyororo mzima wa thamani wa zao hilo, kuanzia uzalishaji shambani hadi uchakataji na usambazaji wa mafuta.

‎Waziri huyo amesema Serikali inalenga kuongeza thamani ya mazao ya ndani na kupunguza utegemezi wa mafuta ya kula yanayoagizwa kutoka nje ya nchi. Ameongeza kuwa vijana wanapaswa kutumia fursa hizo kuanzisha na kukuza biashara pamoja na viwanda vitakavyoongeza ajira na kuchangia uchumi.

‎

‎Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Vijana, Dkt. Reginald Malima, amesema baada ya kutembelea vikundi mbalimbali vya vijana Iramba, na kujionea shughuli zinazofanyika, amesema juhudi hizo zinaweza kuwa mfano wa kuigwa na wilaya nyingine nchini, hiku pia akiitaka Serikali ya Wilaya ya Iramba kuwawezesha vijana kupata maeneo ya ardhi kwa ajili ya kuendeleza na kupanua shughuli zao, ikiwemo viwanda, ili waweze kutumia kikamilifu fursa za kiuchumi zilizopo katika wilaya hiyo.

‎Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda, amesema wilaya hiyo ina zaidi ya vikundi 246 vya vijana vilivyosajiliwa vinavyojishughulisha na ufundi, biashara na shughuli nyingine za kiuchumi, huku zao la alizeti likiwa miongoni mwa shughuli zinazotoa fursa nyingi kwa vijana. Katika hafla hiyo, Serikali pia ilikabidhi Sh.100/- milioni kwa wanawake wanaojishughulisha na biashara ya mama lishe katika Manispaa ya Singida, huku wanufaika akiwemo Janifa David na Orgenes Yindi, wakisema mikopo hiyo itasaidia kuongeza uzalishaji na kukuza shughuli zao.

‎Meneja Biashara wa CRDB Kanda ya Kati, Andrew Mheziwa, amesema benki hiyo imepewa jukumu la kusaidia mchakato wa kuwawezesha vijana, ikiwemo kuwachambua wanaokidhi vigezo na kuwapatia mafunzo ya biashara, ili kuweza kumudu shughuli zao za biashara.

‎MWISHO

Mama asimulia gharama za dialisisi zilivyokuwa mzigo kwa familia – 2

Singida/Dar. Nikiwa ndani ya Hospitali ya Makiungu, iliyopo Kijiji cha Makiungu, Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, macho yangu yanavutiwa na mwanamke wa makamo aliyeketi kimya kwenye benchi la wagonjwa wa nje.

Mama huyo, aliyevalia kilemba cheusi na khanga nyeupe, anaonekana kuchoka. Macho yake yamejaa huzuni, huku mikono yake ikiwa imekunjwa kana kwamba anajaribu kujizuia kulia.

Namsogelea na kujitambulisha. Kwa sauti ya chini anasema, “Nimekuja kutibiwa shinikizo la juu la damu (presha).”

Hata hivyo, kadiri mazungumzo yanavyoendelea, ninagundua tatizo haliko kwenye presha pekee, bali ni maumivu ambayo hayapimwi kwa kifaa chochote cha hospitali.

“Presha hii imenianza baada ya kumzika mwanangu,” anasema Christina Hamis (69), mkazi wa Kijiji cha Muhintiri, Kata ya Ihanja, Wilaya ya Ikungi, huku machozi yakianza kumtoka.

Miezi michache iliyopita alimzika mwanawe, Emmanuel Alute (35), aliyefariki dunia Mei 16, 2026, katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kutokana na ugonjwa sugu wa figo baada ya kupambana kwa zaidi ya miaka miwili na matibabu ya dialisisi.

Anasema hayo yote yalitokana na kukosekana kwa huduma za kibingwa ndani ya Mkoa wa Singida.

Hata hivyo, Christina anaamini kama huduma hizo zingepatikana karibu na makazi yake, huenda simulizi ingekuwa tofauti.

“Kama Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida ingekuwa na huduma hizi mapema, tusingekaa miaka miwili Dodoma tena ugenini kwa maji na chakula cha kununua, sahani ya chakula Sh9,000 kwa mlo mmoja wa mtu mmoja. Tusingeuza kila kitu. Huenda mwanangu angekuwa hai,” anaeleza.

Anasema kila safari ya mamia ya kilomita iliongeza gharama ambazo familia haikuweza kuzimudu. “Maskini anaumwa mara mbili. Mara ya kwanza ugonjwa, mara ya pili gharama.”

Christina, ambaye mwanawe alifariki dunia baada ya kukaa zaidi ya wiki moja katika chumba walichopanga bila kufanyiwa dialisisi baada ya kukosa Sh150,000, licha ya kulipia huduma hiyo kwa zaidi ya miaka miwili mfululizo katika Hospitali ya BMH jijini Dodoma, anasimulia:

“Nilimfuata mhusika, akanijibu, ‘Mama, katafute hela.’ Nilimuomba sana kwamba nimelipia zaidi ya miaka miwili, nimeuza kila kitu na sasa nimeishiwa. Alisisitiza lazima nichangie gharama.”

Anasema ilimbidi amuache mgonjwa peke yake na kurudi Ikungi kutafuta fedha, na siku tano baadaye alipigiwa simu na majirani kuwa hali ya mwanaye imebadilika.

Christina anasema aliporudi Dodoma, licha ya kuwa na fedha mkononi, alimkuta mwanawe anakoroma na kabla hajaita bajaji kumuwahisha kwenye mashine ya dialisisi, alifariki dunia.

Alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo za kuambiwa atafute hela, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Profesa Abel Makubi, anasema, “Sijawahi kuwa na hii taarifa kama sababu ya kifo. Ni kushindwa kulipia dialisisi, maana tuna mwongozo wa Wizara ya Afya ambao huwa tunautumia kutoa idhini ya kupata matibabu kwa waliothibitika hawajiwezi.”

Akitoa ufafanuzi zaidi Agosti 13, 2026, Profesa Makubi anasema mfumo wa msamaha wa gharama za matibabu upo kisera na unatekelezwa kwa kuzingatia miongozo ya Wizara ya Afya.

Anasema mwananchi anayeshindwa kumudu gharama hupewa fursa ya kufanyiwa tathmini ili kuthibitisha hali yake ya kiuchumi na kubaini kama anaangukia katika makundi yanayostahili msamaha.

Baada ya kuthibitishwa, mwananchi hupewa cheti cha msamaha na kuendelea kupata huduma kama kawaida hadi atakapotoka hospitalini. Mchakato huo unaweza kuchukua siku moja hadi tatu, kutegemea na tathmini.

Profesa Makubi anasema BMH husamehe gharama zinazofikia takriban Sh400 milioni kwa mwezi, zikiwamo dawa, vipimo na huduma za upasuaji.

Ugonjwa wa figo ulianza kwa ajali

Baada ya mazungumzo yangu na Christina, nilishawishika kufahamu zaidi, hivyo tukaongozana kutoka Makiungu mpaka katika kijiji anachoishi kwa lengo la kukutana na familia yake.

Baada ya safari ya takribani kilomita 40 kwa mwendo wa pikipiki kutoka Hospitali ya Makiungu hadi Kijiji cha Muhintiri, tunaketi na ananieleza kwa kina, akisema kifo cha Emmanuel hakikuua mtoto wake pekee, bali kilizika pia uchumi wa familia nzima.

“Nimeuza kila kitu. Mashamba, ng’ombe, kibanda, hata nyumba niliyokuwa najenga ilisimama kama unavyoona. Leo hii nimebaki sina kitu,” anasema.

Kisa cha Emmanuel hakikuanza na figo. Mwaka 2014, akiwa mchimbaji mdogo wa dhahabu huko Ikungi, alifukiwa na mawe mgodini na kuvunjika mgongo karibu na eneo la figo.

Baba yake, Yohana Alute, anasimulia kwamba walimkimbiza Hospitali ya Puma kabla ya kuhamishiwa Mtimaru na baadaye Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kilimanjaro (KCMC), Moshi, ambako alitibiwa kwa karibu mwaka mzima.

“Baada ya kurudi nyumbani alikuwa anatembea kwa magongo, baadaye kwa bakora. Polepole alianza kujitegemea tena,” anasimulia.

Familia iliingia gharama kubwa hata kabla ya ugonjwa wa figo kuanza. “Niliuza ng’ombe wengi ili kumtibu. Nilidhani tumeshamaliza matatizo.”

Lakini mwisho wa mwaka 2023, Emmanuel alianza kulalamika maumivu makali ya kifua na kushindwa kupumua. Alipelekwa Hospitali ya Makiungu. Familia ilipewa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

“Tuliondoka Makiungu kwa ambulensi akiwa anahema kwa shida. Hata daktari alisema hakuwa na uhakika kama angefika akiwa hai,” anasimulia baba yake. Kwa bahati nzuri walifika, lakini hapo ndipo safari ya mateso ilipoanza.

Miaka miwili ya kuishi hospitalini

Christina anasema tangu Machi 2023 maisha yake yalihamia Dodoma.

Kwa siku 10 za mwanzo, Emmanuel alikuwa Chumba cha Uangalizi Maalumu (ICU), huku gharama zikiongezeka kila siku; na baada ya kutoka ICU, alianza dialisisi mara tatu kwa wiki.

“Nikapanga chumba Ujasi Ng’ona. Kila Jumatatu, Jumatano na Ijumaa nilikuwa nampeleka dialisisi.

“Kila wiki tulilipia Sh750,000 kabla ya gharama kushuka. Gharama nyingine hazikuisha; bajaji ya kwenda na kurudi hospitalini ilikuwa Sh4,000 kwa siku. Mbali na chakula na maji, kulikuwa na kodi ya nyumba, vipimo, dawa, damu na gharama nyingine zisizokoma. “Niliishi asubuhi nikifikiria dialisisi, jioni nikifikiria nitapata wapi fedha ya wiki inayofuata,” anaelez amama huyo.

Christina anasema hata baada ya kukata bima ya afya aliyoshauriwa na madaktari, bado alibaki analipa kiasi kikubwa cha fedha. “Niliendelea kuuza mali moja baada ya nyingine. Mwisho nikabaki sina chochote,” anaeleza.

Anasimulia kuwa katika miezi ya mwanzo ndugu na watoto wengine walichangia fedha, lakini siku zilivyosonga, uwezo wao ukaisha.

“Mwanzoni walikuwa wanapiga simu kila siku. Baadaye simu zikaanza kuzimwa. Watu walikuwa wamechoka,” anasema, huku akisema hakuwalaumu. “Kila mtu ana maisha yake, lakini mzigo wote ukabaki mabegani kwangu. Nilibaki mimi na mwanangu.”

Mei 2026, bima ilimalizika muda wake, hospitali ilimtaka aanze tena kulipa gharama kubwa za dialisisi, Christina anasema aliomba msaada kwa viongozi wa hospitali.

“Niliwaambia sina tena kitu. Nimeuza kila nilichokuwa nacho.”

Anasema alipewa muda mfupi kutafuta fedha, akalazimika kurejea Singida kuuza chochote kilichokuwa kimebaki. Alipokuwa akihangaika kutafuta fedha, Emmanuel alimuacha peke yake katika chumba alichopanga. Anasema usiku wa Mei 15 alipigiwa simu kuwa hali yake imebadilika.

Asubuhi ya Mei 16 alirejea Dodoma. Alipomuona Emmanuel, alianza kumuita mama yake. “Mama, nakufa… niombee.” Christina anasema alipiga magoti pembeni mwa kitanda.

“Nikaanza kuomba. Nilipofumbua macho nikakuta anakoroma. Dakika chache baadaye alikuwa amefariki,” anasimulia, kwamba wanafunzi waliokuwa wamepanga nyumba hiyo walikuja baada ya kusikia kilio chake. Hata hivyo, alinyanyuka na kuanza kupambana kurudi na mwili wa mwanaye nyumbani (anaanza kulia kwa kwikwi).

Baba naye alibaki na majeraha. Alute naye hakuficha maumivu. Anasema zaidi ya ng’ombe 20 waliuzwa kugharamia matibabu ya mwanawe.

Nyumba aliyokuwa anajenga ilisimama, mifugo iliisha, uchumi ukaanguka. “Lakini bado hatukuweza kumuokoa.”

Anasema walipofikiria kumhamisha Emmanuel kutoka Dodoma kwenda Makiungu baada ya huduma za dialisisi kuanza kupatikana, gharama zilikuwa bado kubwa kiasi cha kushindwa kuanza upya mchakato wa matibabu. “Tuliona tubaki pale Dodoma hadi mwisho.”

Katika Kijiji cha Muhintiri, kwa waliomfahamu Emmanuel, alikuwa mchimbaji aliyewahi kuwapa nafasi vijana wengine kufanya kazi kwenye eneo lake la uchimbaji na hata alipopata jiwe lenye thamani ya Sh70 milioni alisaidia wengi.

“Alikuwa golikipa wa timu ya kijiji, kijana aliyependwa,” anasema mmoja wa vijana kijijini hapo.

Baada ya kifo chake, kijiji kilichanga fedha za mazishi, wakiwamo marafiki zake na wachimbaji wenzake pia. “Hakuwa na maadui, alikuwa mtu wa watu,” anasema mama yake.

Leo Christina anarudi Hospitali ya Makiungu kama mgonjwa. Anasema tangu alipompoteza mwanawe amepata shinikizo la damu, maumivu ya kichwa yasiyoisha na tatizo la kuona kwa jicho moja.

“Maumivu haya hayaishi. Kila nikikumbuka alivyoniambia, ‘Mama, nakufa, niombee,’ moyo unauma upya.”

Anatazama mbali, akisema mwanawe alikuwa anatoka kwenye mashine ya dialisisi akiwa amechoka baada ya saa tano za matibabu.

Christina anataka simulizi yake iwe fundisho. “Asipatikane mama mwingine atakayelazimika kuuza kila kitu, kukesha hospitalini miaka miwili, halafu mwisho arudi nyumbani na jeneza la mwanawe.”

Ananyamaza kwa sekunde chache, kisha anasema, “Mimi nilipoteza mtoto, lakini sitaki familia nyingine ipitie njia niliyopita.”

WATOTO 774,459 WALIO CHINI YA MIAKA 10 KUPATIWA CHANJO YA POLIO MKOANI ARUSHA.

 

Na,Jusline Marco;Arusha

Serikali kupitia Wizara ya afya imeanza Kampeni kubwa kwaajili ya kuwakinga watoto dhidi ya Polio zoezi hilo likitekelezwa kwa awamu ya kwanza kwenye Mikoa 7 ya Arusha, Dar Es Salaam, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Manyara pamoja na Mara.

Hatua hiyo imekuja kufuatia kuwepo kwa visa vinavyojitokeza katika maeneo mbalimbali, vya karibuni zaidi vikitokea Mkoani Mwanza ambapo wadudu wa Polio walipatikana kwenye mfumo wa maji machafu licha ya juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kupambana na ugonjwa wa kupooza kwa watoto maarufu kama Polio.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wasimamizi wa zoezi hilo ngazi ya Mkoa na Halmashauri za Mkoa wa Arusha mapema wiki hii, Mwakilishi wa Meneja wa Mpango wa Taifa wa Chanjo Dkt. Majaliwa Mtoroki amesema walengwa katika kampeni hiyo ni watoto wote walio chini ya miaka 10.

Dkt. Mtoroki amesema mafunzo hayo ya kuwezeshana yatafanyika kwa siku mbili na baada ya hapo watatawanyika kuelekea ngazi ya Halmashauri ili kuendelea na mafunzo kwa watoaji wa chanzo, wachukua takwimu na wahamasishaji pamoja na kuandaa vikao vya kamati za msingi ngazi ya Halmashauri.

Katibu tawala Mkoa wa Arusha Dkt. Toba Nguvila akifunguaafunzo hayo kwa wasimamizi wa zoezi la Kampeni ya Chanjo dhidi ya Polio, ngazi ya Mkoa na Halmashauri za Mkoa wa Arusha, amebainisha kuwa serikali imeweka lengo la kufikiwa jumla ya watoto 774,459, zoezi litakaloendeshwa kupitia Vituo vyote vya kutolea huduma, Kliniki mkoba, shule za Msingi na kwenye ngazi ya Kaya.

Dkt. Nguvila amesisitiza umuhimu wa chanjo hiyo ya Polio, huku akibainisha kuwa chanjo hiyo pia ni suala la usalama kwani afya za watoto zikiimarika zitasaidia katika ujenzi wa Taifa bora la kesho, kuwanusuru watoto dhidi ya kupooza pamoja na kuipunguzia serikali gharama kubwa za matibabu kwa watu wenye ulemavu nchini.

 Sambamba na hayo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji wake wa zaidi ya Shilingi Bilioni 1.4 kwaajili ya uratibu wa Chanjo ya ugonjwa wa kupooza kwa watoto Chini ya miaka 10 maarufu kama Polio, na kusema kuwa ni wajibu wa kila Kiongozi na watendaji wa Mkoa wa Arusha kuhakikisha zoezi hilo linatekelezwa vyema na thamani ya fedha ionekane kwa kuhakikisha lengo la idadi ya watoto lililowekwa linafikiwa.

Mafunzo hayo ya siku mbili ambayo yamewezeshwa na wataalamu kutoka wizara ya afya yamewajumuisha Wataalamu wa afya ngazi ya Halmashauri, Waganga wakuu wa Wilaya pamoja na Maafisa Elimu ngazi ya Halmashauri.

Vyuo vikuu vinavyohitaji mfumo wa ‘Living Lab’ kwenye utafiti

Kwa muda mrefu, Wataalamu na watafiti wamekuwa wakiwaona wananchi wa vijijini kama watu wa kufanyiwa utafiti, badala ya kuwa washirika katika kutafuta suluhisho la changamoto zao.

Mfumo huo umezalisha maarifa muhimu ya kitaaluma, lakini pia umeacha pengo kubwa kati ya kile watafiti wanachogundua katika maabara, na kile ambacho jamii zinahitaji katika maisha yao ya kila siku.

Kupuuza maarifa ya asili ya jamii, watalamu wanasema, kumesababisha gharama kwa Taifa.

Kwa mfano, hatua za kukabiliana na changamoto za mazingira zinaposhindwa kuzingatia uhusiano wa kina uliopo kati ya watu na ardhi yao, huwa zinakosa uhalisia wa kitamaduni unaohitajika ili ziwe endelevu kwa muda mrefu.

Kwa jamii za wafugaji, mfano, maarifa hayahifadhiwi kwenye vitabu, kanzidata au machapisho ya kitaaluma pekee.

Yamejikita katika uzoefu wa muda mrefu wa kutazama mvua, malisho, tabia za mifugo, vyanzo vya maji, magonjwa, uoto wa asili na mifumo ya kijamii inayoamua namna jamii inavyokabiliana na uhaba wa rasilimali.

Kwa mzee wa Kimaasai na mhifadhi wa maarifa ya asili, Ole Morind, maisha ya jamii yake yamejengwa juu ya nguzo tatu; rasilimali za asili, mifugo na jamii.

“Watafiti wanaposhindwa kuelewa namna nguzo hizi zinavyohusiana, wanakosa kutambua kuwa kupambana na umaskini bila kushughulikia mabadiliko ya tabianchi, ni kazi isiyoweza kufanikiwa,”anasema.

Hapa ndipo uzoefu wa Kituo cha Utafiti na mazingira kilichopo Arusha (Arusha Climate and Environmental Research Centre (ACERC) cha Aga Khan University (AKU) unapokuwa na  umuhimu mkubwa unaoweza kubadilisha namna kazi za kitafiti zinavyoweza kufanywa nchini.

Katika kituo hicho, mfumo tofauti umeanzishwa; ni mfumo unaotazama mazingira na watu wanaoishi ndani yake si kama watafitiwa pekee, bali kama sehemu kuu ya kuendesha ubunifu na kutafuta suluhisho la pamoja.

AKU-ACER imekuwa ikijenga mazingira ya utafiti yanayofanana na maabara hai, ambako wanafunzi, watafiti na jamii hujifunza na kutafuta suluhisho kwa changamoto halisi za mazingira.

Falsafa ya ‘Macho Mawili’

Chini ya uongozi wa Dk Emmanuel Sulle, ACERC inaendeleza mfumo unaoelezwa kama “Macho Mawili”, unaolenga kuunganisha maarifa ya kisayansi na maarifa ya asili.

“Falsafa hii inawawezesha watafiti kuuona ulimwengu kwa kutumia jicho la sayansi na jicho la maarifa ya asili kwa wakati mmoja, huku wakitambua kwamba si elimu yote inayopatikana darasani,” anasema Dk Sulle.

Ili kuufanya mfumo huo kuwa sehemu ya taasisi, kituo hicho kimechukua hatua ya kumshirikisha Ole Morind kama mhadhiri msaidizi, akisaidia kuziba pengo kati ya maarifa ya jadi na yale ya kisayansi.

Dk Sulle anaeleza kuwa wazee ni kama miti kwa sababu wamekusanya utajiri wa uzoefu ambao vitabu pekee haviwezi kuutoa.

“Kwa kuishirikisha jamii katika kubuni na kutekeleza utafiti kwa pamoja, kituo kinahakikisha maarifa yanayozalishwa yanajibu mahitaji halisi badala ya kubaki katika maswali ya kitaaluma yasiyogusa maisha ya watu,” anasema.

Mtazamo huo unapata nguvu kutokana na tafiti nyingine zilizofanyika Tanzania.

Utafiti wa mwaka 2023 uliochapishwa katika Tanzania Journal of Development Studies, uliotathmini namna jamii ya Wamasai katika Tarafa ya Ngerengere, Morogoro, inavyokabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ulibaini kuwa wafugaji wanatumia mbinu mbalimbali, ikiwamo kuhamisha mifugo kutafuta malisho, ufugaji unaochanganywa na kilimo na kupunguza idadi ya mifugo wakati wa changamoto.

Watafiti walihitimisha kuwa uwezo wa jamii kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,  unahitaji kutambua na kutumia mifumo ya maarifa ya asili na jadi ya wafugaji.

Utafiti mwingine wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam uliofanyika katika Kijiji cha Parakuyo, pia ulionyesha umuhimu wa maarifa ya asili katika usimamizi wa malisho na mifugo wakati mazingira yanapobadilika.

Ushahidi huo unapinga dhana ya zamani kwamba maarifa huwa na uhalali pale tu yanapozalishwa ndani ya chuo kikuu.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Aga Khan, Dk Tania Bubela, anasema falsafa ya kituo hicho ya kufanya kazi kwa kushirikiana na jamii, ni muhimu katika kipindi ambacho taarifa potofu zinaongezeka.

Kwa mtazamo wake, ushirikiano huo unasaidia kujenga upya imani kati ya wataalamu na wananchi kupitia uwazi katika kuweka ajenda za utafiti na kuweka malengo yanayoshirikishwa.

Kurejesha uhai wa ardhi iliyoharibika

Matokeo ya ushirikiano huo tayari yanaonekana katika mazingira ya Arusha, ambako eneo la kituo limeendelea kuwa na uoto wa kijani hata wakati maeneo yanayokizunguka yakikabiliwa na ukame.

Hali hiyo imewafanya baadhi ya wananchi kujiuliza kituo hicho kinatumia “maajabu” gani, wakati kinachofanyika ni matumizi ya mbinu rahisi zilizobuniwa kwa ushirikiano, ikiwamo kilimo kisichogeuza udongo na urejeshaji wa ardhi iliyoharibika.

Dk Sulle anasema mafanikio makubwa ni pamoja na majaribio na usambazaji wa nyasi aina ya Bana, chakula chenye virutubisho kwa mifugo kinachosaidia kukabiliana kwa wakati mmoja na uhaba wa malisho na uharibifu wa ardhi.

“Kila asubuhi, wanawake wa eneo hili hufika katika ardhi ya kituo, ambayo sasa imekuwa chanzo cha nyasi wanazozihitaji kwa haraka ili kuendeleza maisha yao na mifugo wao,” anasema Dk Sulle.

Ushirikiano huo pia umewasaidia wafugaji kama Ole Morind, ambaye alipoteza asilimia 75 ya mifugo yake kutokana na ukame ndani ya miaka miwili, kubadili na kuanza kufuga mifugo yenye uwezo mkubwa wa kustahimili mazingira magumu.

Hata hivyo, funzo hapa si kwamba maarifa ya jadi yanapaswa kuchukua nafasi ya sayansi ya kisasa.

Badala yake, uzoefu huo unaonyesha umuhimu wa mifumo hiyo miwili kufanya kazi kwa pamoja.

Utafiti wa mwaka 2024 kuhusu wafugaji Wamasai katika Wilaya ya Longido, ulibaini kuwa jamii inatambua kuwa mabadiliko ya tabianchi yanazidi kuwa magumu kutabirika, na kwamba maarifa yao ya jadi pekee yanaanza kushindwa kutoa majibu ya kutosha.

Muhimu zaidi, watafiti walilinganisha mitazamo ya jamii na takwimu za muda mrefu za mvua na joto.

Hili ni fundisho muhimu linaloonyesha kuwa maarifa ya asili hayapaswi kutukuzwa kupita kiasi wala kupuuzwa. Mabadiliko ya tabianchi yenyewe yanabadilisha mazingira ambayo vizazi vilivyopita vilitumia kujenga maarifa hayo.

Kwa hiyo, utafiti imara zaidi ni ule unaoruhusu uchunguzi wa wananchi na vipimo vya kisayansi kujaribiana, kukamilishana na kutoa picha pana zaidi ya tatizo.

Sayansi kueleweka kwa lugha ya jamii

Ushirikishwaji wa jamii unaofanywa na kituo hicho hauishii kwenye kilimo pekee, bali unaingia pia katika afya na mawasiliano.

Kwa kutambua kuwa wafugaji wengi hawajui kusoma na kuandika, ACERC imefanya kazi na viongozi wa jamii, kurahisisha taarifa tata za kisayansi kwa kuzigeuza kuwa alama na michoro inayoweza kueleweka kwa urahisi.

Mfumo huo umetumika pia katika kushughulikia magonjwa ya kitropiki yaliyopuuzwa, ambapo watafiti na wazee wa jamii, wamebuni kwa pamoja alama na misimbo inayotokana na taarifa za Kiingereza na Kiswahili na kutafsiriwa katika Kimasai. Zana hizo zinawawezesha wananchi kutambua dalili za magonjwa na kupata matibabu bila kujali kiwango chao cha elimu.

“Mtazamo huu unahakikisha matokeo ya utafiti mkubwa hayabaki kwenye majarida ya kitaaluma pekee, bali yanatafsiriwa katika lugha rahisi inayoweza kubadilisha maisha na kuwafikia watu waliotengwa na ambao mara nyingi hawana sauti,” anasema Dk Sulle.

Kwa maelezo yake, lugha si suala la mawasiliano pekee; ni suala la utafiti pia.

Anasema, ikiwa jamii haiwezi kueleza uzoefu wake kwa lugha yake, watafiti wanaweza kupoteza maana muhimu wakati wa kukusanya taarifa.

Vilevile, “matokeo yanaporejeshwa kwa jamii kwa Kiingereza cha kitaalamu pekee, wananchi wanaweza kutengwa na uelewa wa utafiti unaohusu maisha yao wenyewe.”

Mtazamo huu unazidi kutambuliwa kimataifa, likiwamo Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu na Sayansi (Unesco), ambalo limekuwa likisisitiza sera za tabianchi na mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya mazingira, inayotumia ushahidi wa kisayansi pamoja na maarifa ya jamii za wenyeji.

Jamii hizo zimejenga kwa vizazi vingi maarifa ya kina kuhusu maeneo yao kupitia uchunguzi wa mvua, joto, bioanuwai na mabadiliko ya ikolojia.

Kwa hiyo, mjadala si kuhusu kuchagua kati ya maarifa ya “kisasa” na “jadi”. Ni kuhusu kujenga msingi mpana na kamili zaidi wa ushahidi.

Mwongozo wa kujenga ustahimilivu wa taifa

Tanzania imeweka lengo la kupunguza uzalishaji wa gesi zinazochangia ongezeko la joto duniani kwa kati ya asilimia 30 na 35 ifikapo mwaka 2030, ikilinganishwa na hali ya kawaida ya shughuli za kiuchumi.

Mpango huo unatambua kilimo, mifugo, misitu, maji na sekta nyingine kama maeneo muhimu ya kujenga uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kazi inayofanywa ACERC inatoa mfano muhimu wa namna Tanzania inavyoweza kubadilisha ahadi hizo kuwa hatua ambazo jamii inaweza kuzimiliki na kuzitekeleza.

Dk Sulle anasema kituo hicho tayari kinafanya jitihada kubwa za kufyonza hewa ukaa kupitia upandaji wa miti na urejeshaji wa mazingira.

Lakini ili mipango hiyo ikue na kufikia maeneo mengi zaidi, taasisi nyingine za utafiti zinapaswa kujifunza kuoanisha mikakati yao na hali halisi ya jamii wanazozihudumia.

Dk Bubela anashauri vyuo vikuu kuwa kiungo kinachounganisha vipaji vya ndani na washirika wa kimataifa, ili kujenga msingi wa ushahidi utakaosaidia utungaji wa sera unaowajibika.

“Kwa kutowachukulia wenyeji kama ‘watu wa porini’, bali kama watu wenye akili na utamaduni uliojengeka kwa kina, kituo kinaonyesha kuwa mifumo ya maisha ya jadi inaweza kutoa somo muhimu kuhusu namna ya kuishi katika mazingira yenye changamoto kubwa,” anasema.

Mtazamo huu pia unavipa vyuo vikuu changamoto ya kutafakari upya maana ya utaalamu katika utafiti.

Mzee anayeweza kutambua mabadiliko ya malisho, tabia za mifugo, upatikanaji wa maji au mabadiliko ya misimu, huenda asiwe na shahada ya kitaaluma, lakini hilo halimaanishi kwamba maarifa yake hayana thamani.

Mtafiti na mtaalamu wa utamaduni, Dk Mrisho Jonas, anasema changamoto ni kujenga mifumo ya utafiti yenye maadili ambayo inaweza kurekodi, kupima na kulinda maarifa hayo bila kuyachukua kutoka kwa jamii au kuwafanya wananchi kuwa vyanzo vya taarifa za bure.

“Jamii inapaswa kuwa na nafasi ya kuamua maswali yanayoulizwa, maarifa yanayoweza kushirikishwa, namna yanavyotafsiriwa na jinsi manufaa yanayotokana na utafiti yanavyogawanywa,” anaeleza.

Anaongeza: “Hapo ndipo utafiti unaweza kuwa na uhalisia wa kweli wa eneo husika.”

Mafanikio ya kituo cha Arusha, yanatoa somo pana kwa mfumo wa elimu ya juu nchini Tanzania.

“Utafiti huwa na uaminifu zaidi pale unapoweza kupita katika uchambuzi mkali wa kisayansi huku ukiendelea kuhusishwa na maisha halisi ya watu ambao unalenga kuyaboresha,” anasema Dk Jonas.

Mbinu za kuvunja ukimya wa wanafunzi darasani

Dodoma. Mwalimu anaingia darasani. Anaandika swali ubaoni. Anageuka na kuwauliza wanafunzi: “Nani anaweza kujibu swali hili?”  Kimya.

Anaangalia upande wa kushoto. Kimya. Anaangalia upande wa kulia. Bado kimya. Wanafunzi wanatazamana, wengine wanaangalia chini, na wachache wanatabasamu kwa aibu. Mwalimu anaishia kusema: “Hivi kweli hakuna anayejua?”

Lakini pengine tatizo si kwamba wanafunzi hawajui. Tatizo linaweza kuwa tumewazoesha kukaa kimya.

Tukirudi nyuma kidogo katika maisha yetu ya utotoni, wengi wetu tulikulia katika mazingira ambayo mtoto alifundishwa kusikiliza zaidi kuliko kuzungumza.

Watu wazima wanapozungumza, mtoto alitakiwa kukaa kimya. Ukijaribu kuingilia mazungumzo, unaweza kusikia: “Kaa kimya! Unaongea nini wewe?” Au, “Funga mdomo, watu wazima wanaongea.”

Ujumbe huu unapojirudia mara nyingi, mtoto hujifunza jambo moja muhimu: kuongea mbele ya watu wazima kunaweza kuwa hatari.

Mtoto anakua. Anaingia shule. Anaendelea na sekondari. Anafika chuo kikuu. Lakini ile hofu ya kuzungumza mbele ya mwenye mamlaka wakati mwingine inasafiri naye.

Darasani, mwalimu anaonekana kuwa ndiye mwenye maarifa yote. Mwanafunzi anaingia akiwa na mtazamo kwamba yeye amekuja kupokea ‘madini’ kutoka kwa mwalimu. Mwalimu anajua; mwanafunzi anapaswa kusikiliza.

Matokeo yake ni darasa ambalo mwalimu anaweza kuzungumza kwa dakika 60, huku wanafunzi 60 wakiwa wasikilizaji.

Lakini elimu ya kisasa inataka zaidi ya kusikiliza. Inahitaji mwanafunzi afikiri, aulize, ajadili, apinge, aeleze na ajenge maarifa pamoja na wengine.

Hapo ndipo mbinu maarufu kwa Kiingereza ijulikanayo kwa jina la ‘Think–Pair–Share’ inapoweza kuwa muhimu.

Ni mbinu rahisi, lakini yenye nguvu. Mwalimu anauliza swali. Badala ya kumtaka mwanafunzi ajibu mara moja mbele ya darasa, anampa muda wa kwanza kufikiri mwenyewe (think), kisha  azungumze na mwanafunzi mwenzake (pair) na mwisho mawazo yanashirikishwa na darasa zima (share).

Kwa nini mbinu hii inaweza kufanya kazi vizuri katika mazingira yetu? Kwa sababu mwanafunzi anaweza kuwa na ujasiri mkubwa zaidi wa kuzungumza na mwanafunzi mwenzake kuliko kuzungumza moja kwa moja mbele ya mwalimu na darasa zima.

Fikiria mwanafunzi ameulizwa swali mbele ya wanafunzi 80. Anajua jibu, lakini anaogopa. Anafikiri, “Nikisema vibaya watanicheka.” Anaogopa mwalimu kusema hajui. Anaogopa wenzake kumwona hajui.

Lakini mwalimu akisema: “Kaa na mwenzako kwa dakika mbili, jadilini swali hili,” mazingira yanabadilika.

Mwanafunzi anamwambia mwenzake, “Mimi nimeelewa hivi…”

Mwenzake anajibu, “Mimi nimeona hivi…”

Wanalinganisha mawazo. Wanarekebishana. Wanajenga jibu.

Baada ya hapo mwalimu anaweza kusema: “Sasa niambieni, mwenzako amekuambia nini?”

Hapa kuna ujanja mkubwa wa kisaikolojia.

Mwanafunzi hatakiwi tena kusema, “Jibu langu ni hili.” Anaweza kusema, “Mwenzangu amesema…”

Hii inapunguza hofu ya kukosea. Ni rahisi zaidi kueleza wazo ambalo umesikia kutoka kwa mwenzako kuliko kusimama mbele ya watu na kutangaza kwamba “hili ndilo jibu langu.”

Hivyo hatua hii ndogo inaweza kuwa mwanzo wa kujenga ujasiri wa kitaaluma.

Baada ya muda, mwanafunzi ambaye jana aliogopa kusema neno moja mbele ya darasa, anaweza kuanza kuzungumza. Leo anazungumza na mwenzake. Kesho anashiriki katika kikundi baadaye anainua mkono. Hatimaye anaweza kusimama mbele ya darasa na kueleza wazo lake mwenyewe.

Kwa hiyo, Think–Pair–Share si tu mbinu ya kufanya wanafunzi washiriki somo. Inaweza kuwa daraja la kumtoa mwanafunzi kwenye utamaduni wa ukimya na kumuingiza katika utamaduni wa mazungumzo na ujenzi wa maarifa.

Hata hivyo, kuna jambo muhimu ambalo walimu tunapaswa kulielewa: ukimya si lazima uwe ujinga.

Mwanafunzi anayekaa kimya anaweza kuwa anajua. Anaweza kuwa na wazo zuri. Anaweza hata kuwa na jibu sahihi kabisa. Lakini anaweza kukosa ujasiri wa kulisema.

Kwa hiyo, kabla hatujasema “wanafunzi wetu hawajui”, tujiulize: Je, tumewajengea mazingira ya kuwaambia wanachojua?

Darasa halipaswi kuwa mahali ambapo mwalimu pekee ndiye mwenye haki ya kuzungumza. Mwalimu anaweza kuwa mwezeshaji wa maarifa, lakini wanafunzi pia wana uzoefu, mawazo, maswali na mitazamo inayoweza kulifanya darasa liwe hai.

Labda tunahitaji kubadilisha kidogo ujumbe tuliokulia nao. Badala ya mtoto kuambiwa kila mara: “Kaa kimya, watu wazima wanaongea.” Darasani tumwambie: “Fikiri, zungumza na mwenzako. Sikiliza. Kisha shiriki.”

Hii ni kwa sababu wakati mwingine, mwanafunzi hahitaji kushinikizwa kuzungumza mbele ya watu 60. Anahitaji tu kupewa mtu mmoja wa kwanza wa kuzungumza naye.

Hapo ndipo Think–Pair–Share inapoanzia. Na pengine, hapo ndipo safari ya kuvunja ukimya wa mwanafunzi wa Kitanzania inaweza kuanzia.

BIDHAA ZA CHAKULA ZISIZOKIDHI MATAKWA YA VIWANGO ZATEKETEZWA .

 Na Mwandishi Wetu.

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeendelea kuonesha dhamira yake ya kulinda afya za wananchi baada ya kuteketeza tani 39 za bidhaa za chakula ambazo hazikukidhi matakwa ya viwango, zenye thamani ya takribani Shilingi milioni 149.

Zoezi hilo la uteketezaji lililofanyika leo, Agosti 17, 2026, katika eneo la Mbezi Gongoni, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, ni sehemu ya juhudi za TBS katika kuhakikisha bidhaa zinazopatikana sokoni zinakuwa salama kwa matumizi ya binadamu.

Kwa mujibu wa Meneja wa TBS Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Bi. Noor Meghji, bidhaa hizo zilikamatwa kupitia ukaguzi wa mara kwa mara uliofanywa na wakaguzi wa shirika hilo katika kipindi cha Julai hadi Agosti mwaka huu.

Amesema ukaguzi huo umebaini kuwa baadhi ya bidhaa za chakula zinazouzwa katika masoko mbalimbali hazikuzingatia matakwa ya viwango, jambo ambalo linaweza kuhatarisha afya za watumiaji.

Bi. Meghji alieleza kuwa changamoto kubwa iliyobainika ni uwepo wa bidhaa nyingi ambazo hazikuwa na alama ya ubora pamoja na kukosa maelezo sahihi kwenye vifungashio.

Alifafanua kuwa baadhi ya bidhaa hizo hazikuwa na taarifa zilizoandikwa kwa lugha ya Kiswahili au Kiingereza, kinyume na matakwa ya Sheria ya Viwango nchini inayotaka maelezo ya bidhaa yawe wazi ili kumwezesha mtumiaji kuelewa bidhaa anayotumia na viambata vilivyomo.

“Ni muhimu kwa watumiaji kusoma maelezo yote yaliyopo kwenye vifungashio kabla ya kutumia bidhaa yoyote. Hii itawasaidia kufahamu bidhaa wanazonunua pamoja na kuhakikisha zinakidhi viwango vinavyotakiwa,” alisema Bi. Meghji.

Aidha, aliwataka wafanyabiashara kuzingatia sheria na kuhakikisha bidhaa wanazoziingiza au kuziuza zinakidhi viwango vilivyowekwa na mamlaka husika.

Hatua ya TBS kuendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara sokoni imeendelea kupongezwa na wadau mbalimbali kutokana na mchango wake katika kulinda afya za wananchi pamoja na kuimarisha mazingira salama ya biashara.

Kupitia ukaguzi huo, bidhaa ambazo hazikidhi viwango huondolewa sokoni mapema kabla hazijasambazwa kwa watumiaji, jambo ambalo limeendelea kusaidia kupunguza hatari ya matumizi ya bidhaa zisizo salama.

Hatua hiyo inaonesha wazi kuwa TBS, inaendelea kutekeleza wajibu wake wa kulinda afya ya jamii kwa vitendo kupitia ukaguzi endelevu unaosaidia kuhakikisha bidhaa zinazofika kwa watumiaji zinakuwa salama, zenye ubora na zinazokidhi matakwa ya sheria za nchi.