Na Matukio Daima Media, Mbarali
Mbunge wa Jimbo la Mbarali, Bahati Ndingo, ameiomba Serikali kuwasaidia wakulima wadogo kupata maeneo rasmi ya kulima badala ya kukodisha mashamba kwa gharama kubwa.
Ndingo amesema hali hiyo inawaumiza wakulima kwenye uzalishaji na kuathiri maisha ya familia zao.
Alitoa ombi hilo wakati Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Deogratius Ndejembi, akiweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa Miji 28 Rujewa.
Alisema wakulima wengi wa Mbarali hawana mashamba ya kudumu na wanalazimika kukodisha kila msimu, jambo ambalo linapunguza faida yao.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais Dkt. Ndejembi amesema Serikali inatambua changamoto hizo na umuhimu wa kuwapatia wakulima mazingira bora ya kazi.
Dkt. Ndejembi alimpongeza Mbunge Ndingo kwa kuendelea kupigania maendeleo ya wakulima wa jimbo lake.
Alisema Serikali imejipanga kutafuta suluhisho la kudumu litakalowawezesha wakulima kumiliki maeneo ya kulima badala ya kukodisha.
Naye Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, alisema Serikali imeanza kutekeleza maelekezo ya Rais kuhusu suala hilo.
Chongolo alibainisha kuwa hatua za awali zimeanza kuchukuliwa ili kuhakikisha changamoto hiyo inapatiwa ufumbuzi.
Aidha, alisema kuna watu wanaotaka kujinufaisha kupitia mpango huo, na akasisitiza kuwa Serikali itahakikisha haki inatendeka kwa wananchi wanaostahili kupata maeneo hayo.

