Baada ya Kiapo, Rais Samia Atoa Ujumbe Mzito Kwa Ndejembi- (Video +Video)

Global Publishers
August 29, 2026
66 views
0 Comments

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amempa pole Deogratius John Ndejembi baada ya kuapishwa rasmi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Samia amesema Ndejembi sasa amebeba jukumu kubwa la kuwatumikia Watanzania, akitoa kauli hiyo leo Jumamosi, Agosti 29, 2026, katika Ikulu ya Chamwino, Dodoma, muda mfupi baada ya hafla ya kuapishwa kwake.

Ndejembi ameapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, George Mcheche Masaju, na kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Dkt. Emmanuel Nchimbi, aliyekuwa Makamu wa Rais kabla ya kutangaza kujiuzulu.

Uteuzi wa Ndejembi ulipata ridhaa ya Bunge jana Ijumaa, Agosti 28, 2026, baada ya jina lake kuwasilishwa na Rais Samia kwa ajili ya kuthibitishwa kuwa Makamu wa Rais.

Bunge lilimthibitisha Ndejembi kwa asilimia 100, hatua iliyofungua njia kwa ajili ya kuapishwa kwake na kuanza rasmi majukumu ya Makamu wa Rais.

Akizungumza baada ya kiapo hicho, Rais Samia amemtakia Ndejembi mafanikio katika kutekeleza majukumu yake mapya, huku akimueleza kuwa nafasi hiyo ni dhamana kubwa kwa taifa.

Ndejembi Aapishwa Kuwa Makamu wa Rais, Rais Samia Ashuhudia (Picha +Video)

Global Publishers
August 29, 2026
12 views
0 Comments

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameshuhudia kuapishwa kwa Deogratius John Ndejembi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ndejembi ameapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, George Mcheche Masaju, katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma, leo Agosti 29, 2026.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na viongozi wengine wa kitaifa, wakishuhudia hatua hiyo muhimu katika uongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kuapishwa kwa Ndejembi kunamuweka rasmi katika nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akianza kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.

Rais Samia amekuwa miongoni mwa viongozi walioshuhudia tukio hilo, huku picha za hafla hiyo zikionesha Rais akiwa pamoja na Jaji Mkuu Masaju na Makamu wa Rais aliyeapishwa, Ndejembi.

IAA YAZINDUA RASMI SHAHADA KAMPASI YA BABATI HOSTELI BURE KWA MWAKA WA KWANZA

Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kimeandika historia mpya mkoani Manyara kwa kuzindua rasmi utoaji wa programu Shahada (Degree) katika Kampasi ya Babati. 

Hafla hiyo ya uzinduzi wa ‘Bachelor of Accountancy with Information Technology’ na “Bachelor of Computer Science’ imeongozwa leo Agosti 24, 2026 na Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Daniel Sillo.

Mhe. Sillo amesema wahitimu wa programu hizo watakuwa sehemu ya kizazi kipya cha wabunifu watakaosadia kuimarisha matumizi ya Teknolojia katika sekta ya fedha, elimu, afya,biashara, kilimo, utalii, viwanda na utoaji wa huduma za serikali.

Mkuu wa Chuo IAA, Prof. Eliamani Sedoyeka amesema” hatua hii ni mkakati wa IAA kuunga mkono juhudi za Serikali kusogeza elimu bora kwa wananchi na kuhakikisha wanapata elimu inayokidhi mahitaji ya dunia ya sasa na baadaye”.

Aidha, Prof. Eliamani Sedoyeka ametangaza kuwa wanafunzi wote wa mwaka wa kwanza watapatiwa huduma ya hosteli bure  hatua inayolenga kupunguza gharama kwa wazazi na kuwawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira salama na tulivu.

Kampasi ya Babati ilianza mwaka 2014 ikiwa na wanafunzi 272, sasa ina wanafunzi 728 na IAA  inalenga kuongeza idadi ya wanafunzi Babati hadi 6,000 ifikapo mwaka 2031.

Aidha, IAA inaandaa mkakati wa kuanzisha programu za  elimu inayozingatia ujuzi (skills-based curriculum) katika maeneo kama Kilimo biashara, Uchakataji wa chakula,Uchakataji wa ngozi,Uhandisi wa uchomeleaji.Lengo ni kuwaandaa vijana wenye ujuzi wa vitendo, kuongeza fursa za kujiajiri na kuajiriwa, na kuendana na mahitaji ya soko la ajira.

Cardi B Avamia Jalada la Vogue Arabia, Aonyesha Mvuto wa Kiarabu

Msanii wa kimataifa kutoka Marekani, Cardi B, amepewa nafasi ya kipekee kwenye jalada la toleo la Septemba 2026 la Vogue Arabia, katika picha iliyozua gumzo kutokana na mtindo wake wa kipekee wenye mguso wa utamaduni wa Kiarabu.

Jalada hilo, lililotolewa Agosti 27, 2026, linamuonyesha Cardi B akiwa amevalia vazi la kifahari lenye mchanganyiko wa rangi nyeusi na kijani, huku akiwa ameshikilia tufaha.

Kinachovutia zaidi ni ujumbe ulioandikwa kwenye jalada hilo, “Assalamu Alaikum, Cardi B”, ambao umeongeza mvuto wa picha hiyo na kuonyesha namna msanii huyo anavyoendelea kuhusishwa na utamaduni wa eneo la Arabia.

Katika toleo hilo, Vogue Arabia imemzungumzia Cardi B kwa upana, ikigusa safari yake ya muziki, mitindo, umaarufu pamoja na maisha yake nje ya jukwaa akiwa mama.

Jarida hilo limemuelezea kama msanii mwenye uwezo mkubwa wa kubadilika kimtindo bila kupoteza utambulisho wake.

Cardi B naye ameonyesha furaha yake kupitia mitandao ya kijamii, ambapo amewashukuru Vogue Arabia pamoja na mpiga picha na mkurugenzi wa ubunifu Szilveszter Makó kwa kazi hiyo.

Mwonekano wake umeendelea kuzungumziwa na mashabiki kwenye mitandao ya kijamii, wengi wakimpongeza kwa kuonekana tofauti na vile walivyozoea kumuona kwenye matukio mbalimbali.

Cardi B si mgeni katika eneo la Mashariki ya Kati. Amewahi kutembelea Saudi Arabia na kutumbuiza katika tamasha la MDLBEAST Soundstorm jijini Riyadh.

Safari hiyo pia ilimpa nafasi ya kueleza hisia zake kuhusu watu na utamaduni wa Saudi Arabia, huku akionyesha kuvutiwa na baadhi ya vipengele vya utamaduni huo.

Kwa jalada hili la Vogue Arabia, Cardi B anaendelea kuonyesha kuwa ushawishi wake hauishii kwenye muziki pekee, bali pia unaendelea kukua katika mitindo, utamaduni na burudani ya kimataifa.

Stori na Nasra Kassim | GPL – TUDACO

Exclusive: Saleh Ally Afichua Siri ya Safari Yake Katika Uandishi wa Habari za Michezo – Video

Global Publishers
August 29, 2026
1,128 views
0 Comments

Mwandishi mahiri wa habari za michezo nchini Tanzania, Saleh Ally (@salehjembefacts), amefanya mahojiano maalum (exclusive interview) na Global TV, ambapo amefunguka kwa kina kuhusu safari yake ya uandishi wa habari za michezo na mambo mbalimbali ambayo wengi hawakuyajua kuhusu maisha yake ya kikazi.

Katika mahojiano hayo, Saleh Ally amezungumzia kwa undani safari yake katika taaluma ya uandishi wa habari, changamoto alizokutana nazo pamoja na matukio yaliyokuwa na mchango mkubwa katika kujenga jina lake kwenye tasnia ya habari za michezo nchini.

Miongoni mwa mambo aliyoyafichua ni kuhusu mahojiano yake makubwa ya kwanza aliyowahi kufanya na mshambuliaji wa zamani wa Chelsea F.C. na Timu ya Taifa ya Ivory Coast, Didier Drogba.

Saleh Ally amesema mahojiano hayo na Drogba yalikuwa miongoni mwa matukio muhimu yaliyomfungulia milango katika safari yake ya kutimiza ndoto yake ya kuwa mwandishi mahiri wa habari za michezo.

Kwa mujibu wa Saleh Ally, fursa hiyo haikuwa tu mahojiano ya kawaida na nyota mkubwa wa soka, bali ilikuwa hatua muhimu iliyompa msukumo, kujiamini na kumfungulia njia ya mafanikio katika taaluma aliyokuwa akiipenda.

Katika mahojiano hayo na Global TV, Saleh Ally pia amegusia mambo mengine mengi kuhusu maisha yake, safari yake ya kikazi, namna alivyokutana na changamoto mbalimbali na matukio yaliyomsaidia kufika alipo leo.

Nafasi za Kazi kwa Wanawake – Wahudumu wa Maduka Mlimani City na Posta

Global Publishers
August 29, 2026
1,392 views
0 Comments

Nafasi za kazi zimetangazwa kwa wanawake pekee kwa ajili ya kufanya kazi kama Wahudumu wa Maduka katika maeneo ya Mlimani City na Posta, Dar es Salaam.

Mshahara: TSh 450,000 kwa mwezi.

Sifa za mwombaji:

  • Awe mwanamke.
  • Awe mchapakazi, mwaminifu na mwenye nidhamu.
  • Awe na uwezo mzuri wa kuwasiliana na wateja.
  • Uzoefu wa kazi ni faida.

Jinsi ya kuomba

Waombaji wanatakiwa kutuma maombi yao kupitia WhatsApp: 0747065803.

Kumbuka: Nafasi hizi ni kwa wanawake pekee na nafasi ni chache. Waombaji wanashauriwa kutuma maombi mapema.

‘Starrgirl’ Yafanya Makubwa Billboard, Ayra Starr Atoboa Top 4

Mwimbaji wa Nigeria, Ayra Starr.

Mwimbaji wa Nigeria, Ayra Starr, ameendelea kuonyesha nguvu ya muziki wa Afrika katika soko la kimataifa baada ya album yake mpya “Starrgirl” kuingia katika nafasi ya nne kwenye Billboard World Albums Chart.

Mafanikio hayo yanaifanya “Starrgirl” kuwa miongoni mwa miradi iliyofanya vizuri kwenye chati hiyo, huku Ayra Starr akiendelea kujenga jina lake katika soko la muziki duniani.

Hii ni mara ya kwanza kwa Ayra Starr kuingia kwenye Billboard World Albums Chart kupitia album yake kama msanii wa solo, hatua inayochukuliwa kuwa moja ya mafanikio makubwa katika safari yake ya muziki pamoja na kuongeza heshima kwa muziki wa Nigeria.

Album hiyo ilitolewa rasmi Agosti 14, 2026, kupitia Mavin Records na Republic Records, ikiwa ni album yake ya tatu ya studio.

“Starrgirl” inafuatia album zake mbili zilizotangulia, “19 & Dangerous” iliyotoka mwaka 2021 na “The Year I Turned 21” iliyotolewa mwaka 2024.

Album hiyo ina jumla ya nyimbo 16, huku Ayra Starr akiwashirikisha baadhi ya majina makubwa kutoka Nigeria na kimataifa, akiwemo Wizkid, Rema, ZAYN, Leon Thomas, kwn, Theodora na Danny Ocean.

Miongoni mwa nyimbo zinazopatikana kwenye album hiyo ni “Gimme Dat” akiwa na Wizkid, “Who’s Dat Girl” akiwa na Rema na “Heaven Baby” akiwa na ZAYN.

“Starrgirl” Yawa Mbele ya Album ya Tyla

Katika Billboard World Albums Chart, “Starrgirl” imeingia katika nafasi ya nne, ikiwa nyuma ya miradi mitatu ya K-pop.

Nafasi ya tano imechukuliwa na album “APOP” ya msanii wa Afrika Kusini, Tyla, hivyo Ayra Starr ameweka “Starrgirl” mbele ya album hiyo katika chati.

Mafanikio hayo yamekuja ndani ya muda mfupi tangu album hiyo itoke, jambo linaloendelea kuongeza uzito wa Ayra Starr katika muziki wa Afrobeats na soko la muziki la kimataifa.

Kwa kuingia katika nafasi ya nne kwenye Billboard, Ayra Starr anaendelea kuthibitisha kuwa wasanii wa Afrika wana uwezo wa kushindana katika majukwaa makubwa ya muziki duniani na kuvuka mipaka ya bara hilo.

Stori na Razaku Ramadhan | GPL – TUDACO

Baada ya Kimya, Mwijaku Amtaka Maua Sama Aachie Muziki Mpya

Mjadala kuhusu kurejea kwa msanii wa Bongo Fleva, Maua Sama, katika muziki umeibuka upya baada ya mwanahabari na mchambuzi wa burudani Mwijaku kumtaka msanii huyo kuanza kutoa kazi mpya.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram leo, Agosti 27, 2026, Mwijaku ametoa ujumbe mfupi lakini wenye uzito kwa Maua Sama, akisisitiza kuwa mashabiki wake bado wanahitaji kusikia muziki mpya kutoka kwake.

“Tunataka nyimbo mpya,” aliandika Mwijaku.

Kauli hiyo imeibua hisia mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii, huku baadhi ya mashabiki wakionyesha hamu ya kumuona Maua Sama akirejea studio na kuendelea na safari yake ya muziki.

Maua Sama ni miongoni mwa wasanii wa kike waliowahi kufanya vizuri katika muziki wa Bongo Fleva na Afro-Pop nchini Tanzania.

Alijenga jina kupitia nyimbo mbalimbali zilizopokelewa na mashabiki, ikiwemo “Iokote”, ambayo ilichangia kuongeza umaarufu wake katika tasnia ya muziki.

Kwa kipindi cha hivi karibuni, mashabiki wamekuwa wakisubiri kusikia kazi mpya kutoka kwa msanii huyo, huku maisha yake binafsi yakionekana kuchukua sehemu kubwa ya muda wake.

Ujumbe wa Mwijaku umeongeza matarajio kwa mashabiki wanaotamani kumuona Maua Sama akirudi kwenye muziki.

Kwa kuwa tayari ana historia na msingi wa mashabiki katika tasnia hiyo, kurejea kwake kwa kazi mpya kunaweza kuongeza ushindani katika muziki wa kike na kutoa hamasa mpya kwa mashabiki wa Bongo Fleva.

Kwa sasa, bado haijafahamika iwapo Maua Sama amepanga kutoa kazi mpya, lakini ujumbe wa Mwijaku umeweka wazi jambo moja mashabiki bado wanaisubiri sauti yake.

Stori na Nasra Kassim | GPL -TUDACO

Jux Atoa Tamko Kuhusu Madai ya Mtoto “Sheria Kuchukua Mkondo”

Msanii Juma Jux ametoa tamko kwa umma akikanusha madai yanayosambaa yakimuhusisha kuwa baba wa mtoto wa mtu fulani, akisema taarifa hizo hazina ukweli na sasa suala hilo limefikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Kupitia tamko hilo, Jux amesema amekuwa akifuatilia suala hilo kwa utulivu bila kulipa uzito, kwa kuwa awali aliona halina msingi wala halistahili kupewa nafasi, lakini ameamua kulizungumzia baada ya madai hayo kuendelea kuhusisha jina lake, familia yake, biashara zake na taswira aliyoijenga kwa miaka mingi kwa jasho na kazi kubwa.

Jux amesema suala hilo liliwahi kujitokeza hapo nyuma, ambapo kwa kutaka kujiridhisha kuhusu chanzo cha madai hayo, alichukua hatua ya kumtafuta mhusika mwenyewe ili kufahamu ni kwanini alikuwa akisema alichokuwa amekisema hapo awali.

Kwa mujibu wa Jux, mhusika huyo alithibitisha kwa maneno na kwa sauti yake kuwa hakuwahi kukutana naye kimwili wala kuwa na mahusiano ya kimapenzi naye.

Aidha, Jux amesema mhusika huyo alimuomba asilipe uzito suala hilo, akieleza kuwa madai hayo yalitokana na maoni ya baadhi ya mashabiki waliokuwa wakimfananisha mtoto huyo na Jux, jambo lililopelekea baadhi yao kuanza kumhusisha kuwa baba wa mtoto.

Hata hivyo, Jux amesema madai hayo yameibuka tena na sasa yamechukua mwelekeo tofauti, hali iliyomfanya kuchukua hatua za kisheria.

Amesema suala hilo kwa sasa lipo mikononi mwa vyombo vya sheria, huku akieleza kuwa hatua zaidi zitachukuliwa dhidi ya mhusika.

Jux pia ametoa rai kwa vyombo vya habari na watu mbalimbali kuepuka kusambaza taarifa za kupotosha bila kuwa na uhakika wa ukweli wake, akisisitiza kuwa taarifa zisizo na ukweli zinaweza kuathiri jina, familia na biashara ya mtu.

Katika tamko lake, Jux amesema amejenga jina lake, brand na biashara zake kwa miaka mingi kupitia kazi, nidhamu na kujituma, hivyo mtu yeyote anayechagua kuhusisha jina lake, familia yake au biashara zake na madai yasiyo ya kweli, atalazimika kuwajibika kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake, Jux amesema amechagua kubaki katika utulivu na kusimamia ukweli, huku akiacha hatua zaidi zichukuliwe kupitia njia sahihi za kisheria.

“Kwa upande wangu, nimechagua utulivu, ukweli na hatua sahihi za kisheria,” Jux amesema katika tamko lake.

STORI NA Na DIDAS DIDAS | GPL -TUDACO