CCWT YAIPA SERIKALI KIJANI, YATOA ONYO KWA WAFUGAJI DODOMA.

 

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

CHAMA Cha Wafugaji Nchini (CCWT) kimesema kufutwa kwa sheria iliyokuwa ikiruhusu mifugo kutaifishwa baada ya kuingia katika maeneo ya hifadhi ni hatua inayokwenda kuondoa hofu na kero iliyokuwa ikiwakabili wafugaji nchini.

Hata hivyo, chama hicho kimesisitiza kuwa mabadiliko hayo hayatoi ruhusa kwa wafugaji kuingiza mifugo katika maeneo ya hifadhi, kikieleza kuwa wafugaji wanapaswa kutumia nafasi hiyo kuimarisha ufugaji wao na kuzingatia sheria za uhifadhi.

Mwenyekiti wa CCWT, Mrida Mshota, amesema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari, akieleza kuwa wafugaji wamepokea hatua hiyo kwa matumaini makubwa kutokana na changamoto walizokuwa wakikabiliana nazo kutokana na utekelezaji wa sheria hiyo.

Amesema pamoja na kuondolewa kwa adhabu ya kutaifishwa mifugo, wafugaji bado wana wajibu wa kuhakikisha shughuli zao zinafanyika katika maeneo yanayotambuliwa kisheria na kuepuka migogoro na maeneo ya hifadhi.

Kwa mujibu wa Mshota, ufugaji wenye tija unahitaji wafugaji kuachana na mifumo ya zamani na kuelekea katika ufugaji wa kisasa unaozingatia matumizi bora ya ardhi, lishe bora ya mifugo na uzalishaji wenye tija.

Amesema hatua hiyo inaweza kusaidia kujenga mazingira mazuri zaidi kati ya wafugaji, Serikali na taasisi zinazohusika na uhifadhi, iwapo wafugaji wataendelea kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.

Katika hatua nyingine, CCWT imeitaka Serikali kuendelea kuboresha huduma za msingi kwa wafugaji, hasa kuhakikisha chanjo za mifugo zinapatikana na kutolewa kwa wakati katika maeneo mbalimbali nchini.

Mshota pia amesisitiza umuhimu wa kuharakisha utambuzi na usajili wa mifugo, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kuwezesha Serikali kuwa na takwimu sahihi za mifugo na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wafugaji.

Amesema uwepo wa mfumo mzuri wa utambuzi wa mifugo utasaidia pia katika kudhibiti magonjwa, kufuatilia mifugo na kuboresha mipango ya maendeleo katika sekta ya mifugo.

CCWT imesema ushirikiano kati ya Serikali na wafugaji ni muhimu katika kuhakikisha mabadiliko ya sera na sheria yanafikia malengo yaliyokusudiwa, huku wafugaji wakitakiwa kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia maslahi mapana ya taifa.

Marekebisho ya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori yaliyofuta utaifishaji wa mifugo inapoingia ndani ya hifadhi yameelezwa kuzingatia matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuwa utaratibu wa awali ulikuwa ukikiuka misingi ya Katiba.