KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI YAPATIWA MAFUNZO KUHUSU MIKATABA YA MSAADA WA KIUFUNDI KATIKA SEKTA YA MADINI

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Subira Mgalu (Mb.) imepatiwa mafunzo kuhusu usimamizi wa mikataba ya msaada wa kiufundi katika Sekta ya Madini, ikiwa ni pamoja na masharti ya kisheria yanayohusu umiliki wa leseni ndogo za uchimbaji wa madini.

Akizungumza kupitia mafunzo hayo yaliyofanyika kwenye Ofisi za Makao Makuu ya Tume ya Madini jijini Dodoma mapema leo Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Tume ya Madini, Francis Kayichile, kwa Niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini amesisitiza kuwa mtu ambaye si raia wa Tanzania kupewa leseni ndogo ya uchimbaji madini ni kosa kwa mujibu wa Sheria ya Madini, Sura ya 123, kwa kuwa fursa ya kuomba na kumiliki leseni hizo imetengwa kwa Watanzania pekee.

Kayichile amesema Kifungu cha 64 kikisomwa pamoja na kifungu cha 9 (3) cha Sheria ya Madini, Sura ya 123, kinatoa fursa kwa Watanzania pekee kuwasilisha maombi ya leseni ndogo za uchimbaji madini, hivyo mtu asiye raia wa Tanzania hanufaiki na fursa hiyo.

Amesema pamoja na umiliki wa leseni kuwa kwa Watanzania, wamiliki wa leseni ndogo wanaweza kupata msaada wa kiufundi kutoka kwa wawezeshaji kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo.

Aidha ameeleza kuwa kwa mujibu wa kanuni hizo mwenye leseni yenye msaada wa kiufundi amepatiwa  asilimia 30 ya faida baada ya kuondoa tozo zote za Serikali, bila kuzingatia gharama za uendeshaji wa mradi alizobeba mwezeshaji.

Ameongeza kuwa usimamizi wa mgodi, uingizaji wa vifaa na mitambo pamoja na ulinzi wa eneo na mali ni majukumu ya pamoja ya wahusika wa mkataba.

Kayichile amesema mkataba wa msaada wa kiufundi huwa na muda wa awali wa miaka mitatu na unaweza kuhuishwa, lakini kwa jumla muda wake haupaswi kuzidi miaka 12 au uhai wa mgodi unapoisha.

“Mikataba hiyo husajiliwa na Tume ya Madini na wahusika wana haki ya kufanya marekebisho  wakati wowote na pindi kunapofanyika marekebisho ya sheria  yanayoathiri masharti ya mkataba au pale inapobainika uwepo wa madini mapya katika eneo lenye leseni yenye msaada wa kiufundi” amesema.

Amesema Tume ya Madini inaendelea kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa mikataba hiyo, huku akisisitiza kuwa ukiukwaji wa masharti unaweza kusababisha hatua kuchukuliwa kwa mujibu wa Kifungu cha 74 cha Sheria ya Madini, Sura ya 123, ikiwemo kusitishwa au kufutwa kwa leseni.

Aidha, Kayichile amesema Serikali imefanya marekebisho ya Kanuni za Haki Madini kwa lengo la kulinda haki za wenye maduara waliopo ndani ya maeneo yenye leseni ndogo za uchimbaji madini.

Amesema kupitia Kanuni za Madini (Msaada wa Kiufundi) za mwaka 2025, hususan Kanuni ya 8(1)(h), mwenye leseni analazimika, kabla ya kuingia mkataba wa msaada wa kiufundi, kufanya makubaliano na wenye maduara au kuwalipa fidia kwa uwekezaji walioufanya katika eneo lenye leseni hiyo.

Kwa mujibu wa Kayichile, hatua hiyo inalenga kuhakikisha haki za Watanzania wanaomiliki leseni na wenye maduara zinalindwa, huku ikiweka mazingira ya ushirikiano katika shughuli za uchimbaji madini yanayozingatia sheria na kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha Watanzania wote.

Kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu (Mb.) kimeshirikisha pia watendaji wa taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Madini.