MBUNGE KIGOMA KASKAZINI AOMBWA KUBORESHA VIWANJA VYA MICHEZO

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

WAPENZI wa soka katika jimbo la Kigoma Kaskazini mkoani Kigoma wamemuomba mbunge wa jimbo hilo Kiza Mayeye  kuboresha viwanja vya soka katika jimbo hilo ikiwemo kuzungumzia uzio ili kuwezesha michezo kufanya kwa usalama na kulata tija katika kuibua vipaji.

Wito huo wa wapenzi wa soka wa jimbo hilo umetolewa katika uzinduzi wa ligi ya mpira wa miguu inayoandaliwa na Mbunge wa jimbo la Kigoma Kaskazini, Kiza Mayeye inayojumuisha jumla ya timu 32 ikijulikana kama Mayeye Cup.

Mmoja wa wapenzi hao wa soka Hussein Suleiman wa Mwandiga alisema kuwa jimbo hilo lina wapenzi wengi wa soka lakini viwanja vingi haviko kweny hali nzuri akitolea mfano Uwanja wa Tarafa kwenye mji mdogo wa Mwandiga maarufu kwa mashindano mbalimbali lakini uwanja huo hauna uzio na magari,pikipiki, baiskeli zimekuwa zikipita sambamba na kuwa na mifereji mikubwa wakati wa mvua.

Hoja hiyo imeunga mkono na Shaban Mambo Mshauri wa mbunge wa jimbo hilo Kigoma Kaskazini ambaye alisema kuwa amepokea maombi mengi ya vijana ya kutaka kuboreshwa kwa viwanja vyao ukiwemo uwanja maarufu wa Tarafa Mwandiga ambao umekuwa ukitumika kwa michezo mbalimbali.

Mambo alisema kuwa binafsi ameshafikisha suala hilo kwa mbunge na kwa kuanza kwa ligi hiyo ni wazi atatekeeleza ombi hilo ili kuwezesha michezo kufanyika mahali pazuri, salama na kuleta tija kwenye suala la michezo kuwa ajira.

 Akizungumza katika uzinduzi huo kwa niaba ya Mbunge wa jimbo hilo Katibu wa Mbunge,Ilaki Issa  alisema kuwa kufanyika kwa mashindano hayo kunatokana na maombi ya vijana wengi kuomba kufanyika kwa mashindano ambayo yatashirikisha timu mbalimbali za jimbo hilo na kwamba ametimiza ahadi hiyo.

 Issa alisema kuwa Mshindi wa kwanza atapata Zawadi ya pesa taslim shilingi milioni mbili na jezi seti moja, Mshindi wa pili atanyakua pesa taslim shilingi milioni moja na seti moja ya jezi ambapo mshindi wa tatu ataondoka na jezi Seti mbili huku kukiwa pia na zawadi kwa Mchezaji bora, mfungaji bora na golikipa bora.