WATAALAMU WA UCHUMI WA BULUU KUKUTANA DAR

Wataalamu, watafiti, wanasayansi, watunga sera na wadau wa Uchumi wa Buluu kutoka Tanzania, Afrika na mataifa mbalimbali duniani wanatarajiwa kukutana jijini Dar es Salaam katika Kongamano la Tano la Kimataifa la Uchumi wa Buluu.

Kongamano hilo litafanyika Septemba 7 hadi 9, 2026 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), huku Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam, Tumaini Gurumo, amesema kongamano hilo litatoa fursa kwa wadau kujadili namna rasilimali za maji zinavyoweza kutumika kuongeza ukuaji wa uchumi na kuchochea maendeleo endelevu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Septemba 3, 2026, Gurumo amesema washiriki watawasilisha tafiti na mawasilisho ya kitaalamu yatakayosaidia kubaini changamoto zinazoikabili sekta hiyo na kutafuta suluhisho.

“Lengo ni kuwakutanisha wabobezi wa masuala ya Uchumi wa Buluu pamoja na wadau mbalimbali, wakiwemo wale wenye uelewa mkubwa wa sekta hii na wale wanaotaka kujifunza zaidi,” amesema.

Amesema majadiliano yatahusisha fursa zinazopatikana kupitia bahari, mito, maziwa na rasilimali nyingine za maji, pamoja na namna ya kuzitumia kukuza ubunifu, ajira na shughuli za kiuchumi kwa kuzingatia matumizi endelevu.

Kwa mujibu wa Gurumo, kongamano hilo linaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika, ambazo zinasisitiza matumizi endelevu ya rasilimali katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Amesema washiriki kutoka nchi mbalimbali tayari wamethibitisha kushiriki, wakiwemo kutoka Kenya, Ghana, Afrika Kusini, Comoro, Seychelles na Uganda.

Kwa upande wa nje ya Afrika, amesema washiriki wanatarajiwa kutoka Japan, Sweden, Urusi na nchi nyingine, huku mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini Tanzania, taasisi za kitaifa na kimataifa, viongozi wa Serikali na sekta binafsi, wanasayansi na watafiti wakitarajiwa kuhudhuria.

Mbali na wataalamu na wadau wa sekta hiyo, waandaaji wamewaalika vijana kutoka vyuo vikuu, shule za sekondari na shule za msingi kushiriki katika kongamano hilo.

Gurumo amesema ushiriki wa vijana ni muhimu katika kuwajengea uelewa kuhusu Uchumi wa Buluu na fursa zilizopo, ili waweze kuwa sehemu ya kizazi kitakachobeba na kuendeleza ajenda hiyo.

Amesema vijana wanapaswa kutambua nafasi yao katika kutumia fursa zinazotokana na rasilimali za maji, hususan katika maeneo ya ubunifu, utafiti, ajira na shughuli za ujasiriamali.

Amewataka Watanzania kutumia fursa hiyo kushiriki na kuongeza uelewa kuhusu Uchumi wa Buluu, pamoja na namna bahari, mito, maziwa na vyanzo vingine vya maji vinavyoweza kutumika kuchochea maendeleo endelevu nchini na barani Afrika.